Home Makala MASWALI KWA WAZIRI MKUU BUNGENI: SPIKA ASIWE ANAMCHAGULIA MASWALI YA KUJIBU

MASWALI KWA WAZIRI MKUU BUNGENI: SPIKA ASIWE ANAMCHAGULIA MASWALI YA KUJIBU

587
0
SHARE
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akijibu swali bungeni wakati wa kipindi cha ‘Maswali kwa Waziri Mkuu’.

NA HILAL K. SUED


Leo ni siku ambayo shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano Dodoma zinaanza kwa kipindi cha ‘Maswali kwa Waziri Mkuu.’

Utaratibu huu ni kwa Waziri Mkuu ambaye ndiye Mkuu wa shughuli za Serikali bungeni, kuwekwa ‘kiti moto’  yaani husimama peke yake na wabunge kumuuliza maswali ya papo kwa papo, maswali ambayo huwa hapewi kabla ili atayarishe majibu.

Kipindi hiki cha Maswali kwa Waziri Mkuu (Kiingereza Prime Minister’s Questions) cha kila Alhamisi wakati Bunge linapoketi, ni utaratibu mpya katika historia ya Bunge letu, ulianzishwa mapema mwaka 2008, ikiwa ni miaka tisa tu iliyopita.

Ni utaratibu uliyoigwa kutoka Bunge la Uingereza (House of Commons) lililopo Westminster katika Jiji la London ambalo kihistoria limetokea kuitwa ‘Bunge Mama’.

Hutajwa kwa jina hilo si tu kwa sababu ndilo lililozaa takriban mabunge mengi katika nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth), nchi ambazo zilikuwa makoloni ya Uingereza, lakini pia kimfumo na uendeshaji wake limeigwa na mabunge mengi mengine duniani.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba miaka 56 tangu uhuru wetu ni mambo machache sana yaliyobakia ambayo bado yanafanana na ‘Bunge Mama’ la London. Machache hayo ni pamoja na kuwepo kwa Askari wa Bunge (Sergeant at Arms), Siwa (Mace), Katibu wa Bunge na wanadhimu wa vyama (Whips), ingawa hili la mwisho limeanzia baada ya ujio wa mfumo wa demokrasia wa vyama vingi robo karne iliyopita.

Huko Uingereza kipindi hicho (kilichoanzishwa mwaka 1959), huwa ni kila Jumatano na ni cha nusu saa wakati wa vikao vya Bunge hilo. Ni kipindi ambacho katika utamaduni wa kisiasa kimejengeka kuwa muhimu na maarufu katika shughuli za kibunge nchini humo na huangaliwa mubashara na mamilioni ya watu kupitia runinga na redio zao.

Aidha, siku hiyo tiketi za kukaa katika majukwaa ya wageni (public gallery) hufukuziwa sana na huuzwa na kumalizika siku kadhaa kabla.

Lakini bado haijafahamika kwanini hapa Tanzania hiki kipindi cha Maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kilikuja miaka 16 baada ya ujio wa vyama vingi, ingawa wengi wanasema uamuzi ulitokana na umahiri wa aliyekuwa Spika wakati ule Samuel Sitta (Mungu amrehemu) aliyejulikana kama ‘Spika wa Viwango na Kasi’ (Of standard and speed).

Kuna baadhi wanadai Spika Sitta aliweka msukumo wa kuanzisha kipindi hicho ili ‘kumkomoa’ aliyedaiwa kuwa hasimu wake, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, wakati wa lile sakata la kashfa ya Richmond. Yaani Waziri Mkuu huyo awe anababaika kwa kuulizwa maswali magumu ya papo kwa papo kutoka kwa Wabunge.

Hata hivyo, Lowassa alijiuzulu siku chache kabla ya kuanza rasmi kwa kipindi hicho kipya cha Bunge na mrithi wake Mizengo Pinda ndiye aliyeanza nacho.

Kuanzia hapo na katika kipindi chote cha uwaziri mkuu wa Mizengo Pinda (2008 – 2015), kwa kiasi kikubwa mambo yalikwenda vyema lakini kuanzia Bunge hili la 11 mambo kidogo yamekuwa hayaendi kwa unyofu kama zamani. Si mara moja au mara mbili, Spika  hususan Naibu Spika, amekuwa akiingilia na kumkataza (kumzuia) Waziri Mkuu asijibu maswali fulani fulani kutoka kwa wabunge; hasa wale wa Upinzani.

Mfano mmoja ni wakati wa kikao cha Bunge Septemba mwaka jana, Naibu Spika, Dr Tulia Ackson Mwansasu alipomzuia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kujibu swali kutoka kwa kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka maelezo kutoka serikalini kuhusu wabunge wa CCM aliodai wamehongwa Sh 10 milioni kila mmoja na chama chao ili kuupitisha muswada  mpya wa habari uliokuwa na utata.

Lakini Naibu Spika alikataa katakata Waziri Mkuu kulijibu swali la Mbowe kuhusu tuhuma hizo za wabunge wa CCM kupewa fedha ili wasiibane Serikali kwenye muswada ule wa sheria uliokuwa uwasilishwe siku iliyofuata.

Katika maelezo yake, Naibu Spika alisema swali hilo lilikuwa halihusu sera ingawa Mbowe alidai lilihusu sera kwa kuwa ni suala la rushwa kwa wabunge. Kwa maana nyingine ni kwamba kupambana na ufisadi ni kuweka mambo yote wazi kwa wananchi, hivyo Serikali ilipaswa kutoa kauli yake (yoyote ile) kuhusu madai yale, la sivyo vita yote dhidi ya ufisadi inaweza kuwa kiini macho.

Aidha, kuizuia Serikali bungeni kutoa ufafanuzi kuhusu suala linaloigusa jamii na siku zote kupigiwa kelele na jamii hiyo, kunaondoa maana nzima ya uwajibikaji kwa Serikali bungeni kupitia kipindi hicho cha Maswali kwa Waziri Mkuu.

Kwa upande mwingine, kumzuia Waziri Mkuu kuitetea Serikali yake kunawafanya wananchi wasiujue vyema umahiri wa kiongozi mkuu huyo wa Serikali bungeni katika kupangua hoja za wabunge wa upinzani na hata wale wa upande wa Serikali yenyewe. Na ndiyo maana yeye ndiye aliyeonekana anafaa kushika nafasi hiyo kuliko wabunge wengine wa kutoka chama chake.

Ikumbukwe kwamba waziri mkuu anayeteuliwa na rais sharti awe na sifa za kiwango cha juu katika utendaji na awe na uzoefu mkubwa katika kuzungumza na kujenga hoja kwa ufasaha mkubwa. Ni lazima aonyeshe kwa wananchi kwamba siku zote yuko tayari kuitetea Serikali ambayo wao (wananchi) hawakukosea kuichagua.

Na hata katika vikao vya kawaida vya Bunge pamoja na wakati wa maswali ya kawaida kwa mawaziri, Waziri Mkuu anapaswa kusimama na kufafanua jambo pale anapoona waziri wake ameshindwa kufafanua, hakueleweka au kakosea.

Ni matarajio kwamba Kiti cha Spika kiwe kinamwachia Waziri Mkuu kujibu maswali ya wabunge katika kipindi hicho kila Alhamisi bila ya kumzuia au kumbughudhi.