Home Uchambuzi Afrika MATAIFA YA KIGENI YANAPANDIKIZA ‘MAJIGAMBO’ KWA WAPINZANI AFRIKA?

MATAIFA YA KIGENI YANAPANDIKIZA ‘MAJIGAMBO’ KWA WAPINZANI AFRIKA?

3689
0
SHARE

Bobi Wine (kulia) akiwa na Mwanasheria wake kutoka Marekani, Robert Amsterdam.

WAKATI upinzani ukizidi kushika hatamu katika baadhi ya nchi za Bara la Afrika, viongozi walio madarakani, wamekuwa wakiyalaumu mataifa ya kigeni, hasusani, Bara la Ulaya na Amerika Kaskazini kwa madai kuwa yanaingilia siasa na mambo ya nchi husika.

Wimbi hili limekuwa likijitokeza katika kipindi ambacho anguko la viongozi walio madarakani, linapoonekana kujitokeza, au mtikisiko kutoka kwa wapinzani ambao kwa namna moja au nyingine, malengo yao nao ni kushika madaraka.

Aidha, hoja kubwa inayoonekana kubeba agenda za majigambo hayo kutoka kwa wapinzani, ni ufadhili wa shughuli zao za kisiasa ambao kwa tasfiri halisi, inaashiria kuunga mkono juhudi za kuwaong’oa madarakani viongozi waliopo.

Rwanda

Wiki iliyopita, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, aliliambia Bunge jipya la nchi hiyo, kuwa jeuri ya wanasiasa aliowataja kuwa na mienendo isiyofaa, inatokana na mataifa ya kigeni yanayowarubuni wapinzani.

Kagame alitoa kauli hiyo huku akitishia kumrejesha gerezani mpinzani wake mkuu Victoire Ingabire, aliyeachiwa huru hivi karibuni, endapo hatoacha majigambo kwamba hakuomba msamaha wa kuachiwa huru.

Alimuonya Ingabire, ambaye ni kiongozi wa Chama cha Upinzani (FDU-Inkingi), aliyeachiwa huru kwa msamaha wa rais, kwamba huenda angelirejeshwa tena jela ikiwa angeliendelea na kile Rais Kagame alichokitaja kuwa ni “mienendo ya kujigamba” kwamba kamwe hakuomba msamaha.

Ingabire aliachiwa huru baada ya kutumikia miaka saba ya kifungo cha miaka 15 alichohukumiwa kwa hatia za uhaini, lakini yeye akisema kesi yake ilikuwa ya kisiasa.

Kuachiwa huru kwa mwanasiasa huyu, kulichukuliwa na wengi kama shinikizo la wanaharakati na mataifa ya nje, lakini Rais Kagame aliukejeli mtazamo huo akisema serikali yake haifanyi kazi chini ya kivuli cha mtu yeyote.

Uganda

Katika siku za karibuni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ambaye amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 30, amepata mtikisiko wa kipekee kutoka kwa Mbunge wa upinzani nchini humo na mwanamuziki wa kizazi kipya Bobi Wine, ambaye amekuwa mkosoaji kwa muda mrefu.

Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi (36), alikuwa Marekani kwa ajili ya matibabu ya majeraha aliyopata baada ya kupigwa na wanajeshi alipokamatwa mnamo Agosti 14, mwaka huu.

Bobi Wine, Wabunge wengine wane, na wafuasi wake 30, walikamatwa mwezi uliopita baada ya maandamano kufanyika wakati wa shughuli za kampeni za uchaguzi mdogo.

Aidha, licha ya kutibiwa Marekani, Bunge la Umoja wa Ulaya (EU), nalo hivi karibuni lilikemea uovu huo uliotendekea nchini humo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, baadhi ya maamuzi kati ya 14 yaliyotolewa na Bunge hilo, yameitaka serikali ya Uganda, kuheshimu uhuru wa Bunge, kuheshimu haki za kibinadamu, na kufuta mashtaka ya uhaini dhidi ya Robert Kyagulanyi na wabunge wenzake, likisema kwamba mashtaka hayo ni ya kupandikiza.

Hata hivyo, serikali ya Uganda imelionya Bunge hilo la EU, kuacha kuingilia masuala ya uongozi wake pamoja na kuacha kutoa masharti kwa viongozi wa Uganda juu ya haki za binadamu.

Utawala wa Uganda unadai kwamba Bunge la EU, limekasirishwa na msimamo mkali wa Uganda dhidi ya ushoga, na kuongeza kwamba haitatatizwa na vitisho vya kutopewa msaada wa kifedha wala silaha.

Msemaji wa serikali ya Uganda, Ofwono Opondo, alisema kwamba Uganda haiogopi kuharibu uhusiano wake na Umoja wa Ulaya na kwamba ipo tayari kwa vita ilivyovitaja kama vita vya haki.

Vilevile, Rais Museveni aliyalaumu mataifa ya kigeni kwa kuingilia masuala ya nchi hiyo yakifahamu kuwa ina inakaribia  kuwa na uchumi na usalama imara.

Museveni amesema kwamba serikali yake, inaendelea kuimarisha usalama, lakini inatatizwa na makundi ya watu wasioitakia mema Uganda mema yakiwemo mashirika yasio ya kiserikali, vyombo vya habari, na watu wengine ambao wanawachochea wananchi kujenga chuki dhidi ya utawala wake.

Kenya

Licha ya kufanyika mazungumzo ya amani na kumaliza uhasama wa kisiasa nchini Kenya, haitosahaulika kuwa Rais Uhuru Kenyatta naye aliyashutumu mataifa ya kigeni kuwa yanatumia fedha kufadhili mashirika ya kiraia kwa lengo la kuingilia siasa za nchi hiyo.

Mwaka 2016, wakati akilihutubia taifa katika maadhimisho ya miaka 53 ya Jamhuri, Kenyatta alisema ikiwa mataifa hayo ya kigeni ambayo hakuyataja, yanataka kuisaidia Kenya, yaitumie Tume ya Uchaguzi.

Mpinzani mkuu wa Kenyatta katika kipindi chote alichokaa madarakani, ni kiongozi mkuu wa Umoja wa wapinzani (NASA) Raila Odinga.