Home Habari kuu Matukio 20 yaliyogeuza upepo wa siasa 2019

Matukio 20 yaliyogeuza upepo wa siasa 2019

578
0
SHARE

Na LEONARD MANG’OHA

ZIKIWA zimesalia siku tano kabla ya kuuaga mwaka 2019, matukio makubwa 20 ya kisiasa yaliyotokea Tanzania yatabaki kwenye kumbukumbu za wengi, huku Taifa likijindaa kwa Uchaguzi Mkuu baadae mwaka huu.

Matukio hayo si tu kwamba yaligusa siasa za ndani, bali mengine yaligusa siasa za nje, na kulitangaza vema Taifa letu kama mdau muhimu wa maendeleo, ulinzi na mahusiano ya kimataifa barani Afrika. 

Mkutano wa SADC:

Miongoni mwa matukio hayo ni kufanyika Mkutano wa 39wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika nchini Agosti 17 na 18.

Licha ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo, pia ilishawishi kupitiswa kwa lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi itakayokuwa ikitumika katika shughuli za jumuiya hiyo, jambo ambalo lilifanikiwa.

Rais Dk. John Magufuli aliyepokea uenyekiti wa SADC katika mkutano huo, alisema kuwa kitendo cha kukifanya Kiwashili kuwa lugha rasmi ya jumuiya hiyo ni heshima kubwa hasa kwa Mwasisi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alishiriki kwa namna mbalimbali kukuza lugha ya Kiswahili.

Lowassa kurejea CCM:

Machi Mosi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alitangaza kurudi rasmi Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kuwa nje ya chama hicho karibu miaka minne baada ya kujiunga na chama kikuu cha upinzani nchini Chadema.

Lowassa aliondoka CCM baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kupitisha mgombea urais wa hicho mwaka 2015, ambapo Rais Dk. John Magufuli alichaguliwa kuwa mgombe wa CCM, na baadae alishinda katika Uchaguzi Mkuu na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sumaye ajitoa Chadema:

Desemba 4, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alifikia uamuzi wa kujitoa Chadema, chama alichojiunga mwaka 2015 akitokea CCM.

Uamuzi wa Sumaye kujitoa Chadema ulikuja wakati ambapo kulikuwa na minong’ono mingi kuhusu kutozingatiwa kwa demokrasia katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa chama hicho uliofanyika hivi karibuni, huku akidai kufedheheshwa na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho.

Hatua hiyo ilikuja muda mfupi baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, ambapo licha ya kuwa mgombea pekee katika uchaguzi huo aliambulia kura 28 za ndiyo dhidi ya 49 za hapana.

Sumaye alifikia uamuzi huo akiwa miongoni mwa wagombea watatu waliokuwa wamerejesha fomu za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Chadema, ambapo wengine walikuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe.

Waraka wa Kinana na Mzee Makamba:

Julai 14, makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, walimwandikia barua Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, Pius Msekwa, wakilalamika kudhalilishwa kwa tuhuma za uongo na mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Makamba na Kinana kupitia waraka wao walieleza kuwa walizingatia Katiba ya CCM toleo la mwaka 2017, Ibara ya 122 na kwamba wamewasilisha maombi yao wakiwasihi wazee wa chama watumie busara zao katika kushughulikia jambo hilo ambalo walidai kuwa linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani na nje ya chama.

Katika waraka huo uliosambaa kwenye mitandano ya kijamii, walieleza kuwa baada ya kutafakari walipata majibu mtu huyo anatumwa na kutumiwa na watu wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na taasisi yoyote wala mtu yeyote.

Katika kipindi hicho hicho kwa nyakati tofauti, sauti zinazodaiwa kuwa ni za wabungei, January Makamba (Bumbuli), Nape Nnauye (Mtama) na makatibu wakuu hao wastaafu zilisambaa katika mitandao wakizungumzia kuandaa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwa Makamba na Kinana, kisha ikafuata sauti inayodaiwa kuwa ni mawasiliano Nape na Mbunge wa Sengerema, Wiliam Ngeleja na baadaye ikafuata sauti inayodaiwa kuwa ni ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Katibu Kata wa Kijiji cha Rondo mkoani Lindi.

January na Ngeleja na Nape kwa nyakati tofatuti walimwomba radhi Rais kutokana na vitendo hivyo.

Uchaguzi Serikali za Mitaa:

Vyama sita vyenye ushawishi katika siasa za upinzani vya Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, UPDP na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), vilisusia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24.

Vyama hivyo vilifikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa mchakato wa uchaguzi, baada ya idadi kubwa ya wagombea wake kuondolewa kwa madai ya kutokuwa na sifa.

Katika matokeo ya uchaguzi huo wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji CCM ilijipatia ushindi mwepesi kwa zaidi ya asilimia 99, huku mikoa ya Tanga, Katavi, Ruvuma na Njombe wagombea wote wa CCM wakipita bila kupingwa.

Ziara ya Rais Kenyatta Chato:

Mwezi Julai Tanzania ilimpokea Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta, katika ziaza ya kindugu alimpomtembelea Rais mwenzake Dk. John Magufuli aliyekuwa mapumzikoni nyumbani kwake Kilimani, Chato mkoani Geita.

Katika ziara hiyo pamoja na mambo mengine wawili hao walihimiza kuendelea kushirikiana na kulinda uhusiano wenye historia kubwa baina ya nchi hizo, na kuwataka wananchi wa mataifa hayo kutokubali kulaghaiwa na kupotoshwa kwa maneno yasiyofaa yanayolenga kuwatenganisha.

Ziara ya Rais Tshisekedi: 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, alifanya ziara ya siku mbili nchini ikiwa na lengo la kuzungumza na Rais Dk. Magufuli kuhusu kupatikana amani ya kudumu nchini DRC, ambapo Dk. Magufuli alimuhakikishia kuwa Tanzania itayaondoa majeshi yake yanayolinda amani nchini humo pale tu amani ya kudumu itakapopatikana.

Sherehe za Uhuru Mwanza:

Kwa mara ya kwanza Serikali ilifanya sherehe za maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika (Tanzania Bara) jijini Mwanza, sherehe ambazo zilihudhuriwa na idadi kubwa ya watu.

Kivutiuo kikuu katika sherehe hizo ni kitendo cha viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa walijvyojitokeza kushuhudia tukio hilo, wakiwamo viongozi wa Chadema walioongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ikiwa ni mara yao ya kwanza kufanya hivyo tangu kuingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano mwaka 2015.

Mkutano mawaziri wa mambo ya nje Afrika na nchi za Nordic:

Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 34 zikiwamo nchi tano zinazounda jumuiya ya Nordic inayojumuisha Sweden, Norway, Finland, Denmark na Iceland, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika barani Afrika.

Katika mkutano huo nchi hizo zijadili namna ya kuimarisha uhusiano wenye tija kwa maendeleo ya nchi washiriki, hususani katika sekta za biashara na uwekezaji kwa maendeleo pamoja na kukuza ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama.

Ziara ya Rais Ramaphosa:

Agosti 14 na 15, Tanzania ilimpokea Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, aliyekuja nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kwa mwaliko wa mwemyeji wake Rais Dk. John Magufuli. 

Ziara hiyo ya Ramaphosa nchini ililenga kukuza ushirikiano katika masuala uya uchumi, siasa, utamaduni na kijamii katika ya nchi hizo.

Rais Ramaphosa baadae alihudhuria mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika nchini siku tatu baadaye. 

Sakata la CAG na Ndugai: 

Mwezi Aprili Tanzania ilishuhudia mgogoro wa kiutendaji kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, na aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Musa Assad, baada ya kiongozi huyo wa Bunge kumtuhumu CAG kukidharau chombo hicho kwa kukiita kuwa ni dhaifu.

Kutokana na kauli hiyo, Spika Ndugai alimtaka CAG ajiuzulu hali iliyoibua hisia tofauti miongoni mwa wadau na kuzua taharuki katika mitandao ya kijamii, huku suala hilo likionekana kuchukua nafasi kubwa katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.

Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ilimwita CAG bungeni kuhojiwa kuhusu kauli hiyo, kisha ikapitisha azimio la kutofanya kazi naye baada ya kumtia hatiani kwa madai kuwa kauli yake ililenga kulidhalilisha Bunge. 

Spika Ndugai na Masele:

Spika Ndugai alijikuta katika mgogoro na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele, akisema sababu ni utovu wa nidhamu wa kiongozi huyo na kugonganisha mihimili, ambapo alitangaza kusitisha kwa muda uwakilishi wa Masele. 

Ndugai alimtuhumu Masele kuwa alikuwa akipeleka maneno ya uongo kwenye viongozi wa ngazi ya serikalini na kwamba Bunge lilikuwa likimuita Masele arejee nchini kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, lakini alikaidi. 

Baadae Ndugai alimwandikia barua Rais wa PAP, Roger Dang, kumweleza juu ya kusitisha kwa muda uwakilishi Masele katika Bunge hilo ili arudi kujibu tuhuma zilizokuwa zikimkabili.

Lissu, Nassari wavuliwa ubunge:

Machi 14, Ndugai alitangaza kuvuliwa ubunge kwa Mbunge ya Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, baada ya kupoteza sifa ya kuwa mbunge, hatua ambayo ilifikiwa huku mbunge huyo akiwa katika ziara ya kutekeleza majukumu ya kibunge kupitia Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyokuwa Chuo cha Mweka mkoani Kilimanjaro.

Katika tukio jingine, Ndugai alitangaza kumvua ubunge aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kwa madai ya kutohudhuria vikao vya bunge bila taarifa na kutowasilisha taarifa rasmi kuhusu mali na madeni, ambapo aliitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuandaa uchaguzi katika jimbo hilo.

Katika uchaguzi huu wa marudio ulioitishwa Julai, mgombea wa CCM, Miraji Mtaturu, alipitishwa kama mshindi kutokana na kuwa mgombea pekee aliyerejesha fomu za kuwania nafasi hiyo kati ya wagombea 13 waliojitokeza.

Uchaguzi Chadema:

Mwezi huu, Chadema ilifanya uchaguzi wa viongozi wake wakuu huku Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, akitetea nafasi yake akimshinda Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe.

Katika uchaguzi huo, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, aliteuliwa kuwa katibu Mkuu wa Chadema akichukua nafasi ya Dk. Vicent Mashinji. 

Pia kanda nane za chama hicho zilipata viongozi wake isipokuwa Kanda ya Pwani ambayo uchaguzi utarudiwa baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wake, Frederick Sumaye, kushindwa, ambao alikuwa mgombea pekee.

Kinana, Makamba na Membe kuhojiwa:

Mapema mwezi huu, Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliagiza makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba pamoja na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, waitwe na kuhojiwa na Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho kuhusu sakata la sauti zao kusambaa katika mitandao wakizungumzia mpasuko ndani ya chama hicho.

Pia watahojiwa kuhusu waraka wao waliouwasilisha katika Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM wakidai uongozi wa chama umeshindwa kuwalinda dhidi ya mtu ambaye amekuwa akiwadhalilisha, huku akilindwa na watu wenye mamlaka na kinga kisheria.

Hata hivyo kikao cha Halshauri Kuu hiyo kilichokaa Desemba 13, jijini Mwanza kiliwasamehe na kuwaonya wabunge watatu, January Makamba (Bumbuli), William Ngeleja (Sengerema) na Nape Nnauye (Mtama), ambao walihusishwa katika sakata hilo kutokana na uamuzi wao wa kumwomba msamaha Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli.

Maalim Seif ahamia ACT:

Mwaka 2019, mwanasiasa mwenye ushawishi katika siasa za upinzani Visiwani Zanzibar na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, alikihama chama hicho na kujiunga na chama cha ACT Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe.

Hatua ya Maalim Seif kuachana na CUF ilitokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliompa ushindi Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kutokana na mgogoro wa kiuongozi baina ya viongozi hao uliodumu tangu mwaka 2016, baada ya Profesa Lipumba kurejea CUF ambako alijitoa wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2015, akipinga uamuzi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumsimamisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa mgombea wao.

Utumbuaji waendelea: 

Mwaka 2019 pia ulishuhudia Rais Dk. John Magufuli akiendelea kuwatumbua na kutwateua baadhi ya mawaziri ambao hakuridhishwa na utendaji wao na kuwaingiza wengine kwenye Baraza la Mawaziri. 

Aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba, alimpisha George Simbachawene aliyekuwa nje ya uwaziri kwa zaidi ya miaka miwili.

Innocent Bashungwa aliteuliwa kuchukua nafasi ya Waziri wa Viwanda na Biashara akimrithi Joseph Kakunda ambaye uteuzi wake ulitenguliwa akiwa amehudumu katika nafasi hiyo chini ya mwaka mmoja. 

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, alipata nafasi ya kuhudumu kama Naibu Waziri wa Kilimo.

Pia mwaka huu ukielekea mwishoni imeshuhudiwa Rais akifanya mabadiliko makubwa katika idara mbalimbali na nyeti iliwamo Idara ya Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Ziara za Waziri Mkuu:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Ziara za Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ziligeuka mwiba mchungu kwa baadhi ya viongozi walionekana kutofuata maagizo na kushindwa kutekeleza vema majukumu yao, ambapo akiwa mkoani Morogoro alionesha kukerwa na hali ya kutoelewana kati ya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi (DC), Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo (DED), Mussa Mnyeti, jambo lililomfanya amwagize CAG na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwenda kuchunguza weledi wa wateule hao.

Hata hivyo kabla ya kuchukuliwa kwa hatua hizo, Dk. Magufuli alitengua uteuzi wao na kisha akafanya mabadiliko makubwa katika mkoa huo kwa kumwondoa Mkuu wa Mkoa huo, Stephen Kebwe.

Viongozi Chadema mahakamani:

Katika hatua nyingine Chadema imeendelea kuonja shubiri kutokana na viongozi wake wakuu wakiongozwa na Mwenyekiti Mbowe kuendelea kusota mahakamani wakikabiliwa na mashitaka 13, likiwamo la kula njama na kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri ya polisi kuwataka kutawanyika.