Home Makala Matukio yaliyobadili mtiririko wa mustakabali wa Zanzibar

Matukio yaliyobadili mtiririko wa mustakabali wa Zanzibar

2928
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Kwa kiasi fulani upo ukweli ule usemi kwamba historia ina tabia ya kujirudia, ingawa mimi nasema hujirudia kwa namna tofauti na ile ya awali. Na ni ukweli pia kwamba binadamu wengi wana hulka ya kupenda kuona mtiririko tofauti wa mambo iwapo tukio fulani lingejirudia, kuliko mtiririko wa ilivyokuwa awali.

Ni vyema nikalieleza hili kwa kutoa mfano wa tukio lilitokea Ulaya zaidi ya miaka 100 iliyopita, tukio ambalo lilisukuma kutokea Vita Kuu ya Kwanza ambayo zaidi ya watu milioni 16 walikufa, wakiwemo wazalendo wa nchi hii ambayo sasa inaitwa Tanzania.

Tukio lililoanzisha vita ile ni kuuawa kwa kupigwa risasi kwa Archduke Franz Ferdinand, mtawala wa Sarajevo (sasa mji mkuu wa Bosnia-Herzegovina) tarehe 28 June 1914. Mtawala huyo asingeuawa yumkini kusingetokea vita kwa namna ilivyokuwa.

Au chukulia mfano huu mwingine huko huko Ulaya. Mwaka 1929, wakati wa harakati zake za kisiasa na kabla ya kutwaa madaraka nchini Ujerumani, Adolf Hitler alinusurika kuuawa na mtu mmoja aliyetumwa na mahasimu wake wa kisiasa katika ukumbi mmoja aliokuwa akihutubia huyo dikteta mtarajiwa wa Ujereumani.

Mtu huyo ilikuwa amlenge Hitler na kumpiga risasi halafu akimbie. Lakini kabla ya kufanya hivyo alishikwa na haja ndogo na aliona ni vyema kwanza aende msalani amalize haja yake. Lakini aliporudi ukumbini akakuta Hitler kamaliza hotuba yake na alikuwa anaondoka ukumbni.

Hebu fikiria – watu wapatao milion 50 duniani kote waliteketea katika Vita ya Pili vya Dunia (1939 – 1945) iliyoanzishwa na Hitler kwa sababu mtu mmoja alishikwa haja wakati mbaya. Ukweli ni kwamba Hitler angeuawa siku ile, kusingotokea Vita hiyo yenye maafa makubwa kuliko yote katika historia ya dunia.

Hapa kwetu upo mfano kama huo, na ni matukio mawili kuhusu Zanzibar, ingawa matukio yote hayakutiririkia kwenye maafa makubwa ya vita. Hata hivyo moja – lile la awali lilisababisha mapinduzi ya umwagaji damu kwa kiasi kidogo.

Kwanza- mwaka 1963 katika harakati za kujipatia uhuru kutoka Uingereza ambayo Zanzibar ilikuwa chini ya himaya/ulinzi (protectorate) yake tangu 1896 kulikuwapo vyama vitatu vikuu vya kisiasa vikigombea kuunda serikali baada ya uhuru: Afro-Shirazi Party (ASP), Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba Peoples’ Party (ZPPP).

Katika uchaguzi wa mwisho kabla ya uhuru ASP iliongoza kwa kiti kimoja katika Baraza la Kutunga Sheria (Bunge) lakini haikuweza kuunda serikali kutokana na uamuzi wa chama cha ZPPP (ambacho kiliibuka cha tatu kwa idadi ya viti) chini ya kiongozi wake Mohamed Shamte kuungana na ZNP kilichokuwa kikiongozwa na Ali Muhsin Baruani na hivyo yeye (Shamte) kupewa jukumu la kuunda serikali na kuwa Waziri Mkuu wake wa kwanza.

Haya yalikuwa kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa baina ya ZPPP na ZNP na lengo ni kukipiku na kukiacha nje chama cha wazalendo – ASP cha Abeid Aman Karume.

Hili halikuonekana kukaa sawa kwa sababu ZNP kilikuwa kinaungwa mkono na utawala wa Kisultani ambao kulikuwapo kila dalili kuendelea kuwapo kwake, pamoja na Visiwa hivyo kupata ‘uhuru’ kutoka Uingereza. Hivyo mwaka 1964 yakatokea mapinduzi yaliyoongozwa na ASP na kubadilisha historia nzima ya Visiwa hivyo – angalau kwa kipindi cha miaka minane iliyofuata.

Laiti ZPP ingeungana na ASP, historia ingekwenda kivingine na wengi wanasema kusingekuwapo sababu ya mapinduzi. Demokrasia ingeweza kushamiri na nchi kupiha hatua kubwa za kimaendeleo hadi leo. Iwapo kisiwa cha Mauritius kiliweza kufanya hivyo, Zanzibar pia ingeweza.

Tukio jingine lilitokea baada ya kuuawa kwa Abeid Aman Karume, muasisi wa mapinduzi ya 1964 na rais wa kwanza wa Zanzibar, tukio ambalo kwa mara nyingine lilibadilisha mtiririko wa kihistoria wa visiwa hivyo hadi leo. Na iwapo angenusurika katika tukio lile la mauaji, bila shaka historia ya visiwa hivyo ingekwenda kivingine kuliko ilivyokuwa – na wengi wanasema hata tukio lile la mwaka 1977 la kuungana kwa TANU na ASP huenda lisingetokea.

Hivyo basi hali ya sasa hivi ya Visiwa vya Zanzibar – kisiasa, kiuchumi na hata kijamii unatokana na mtiririko wa historia tangu kuuawa kwa Karume. Karume alirithiwa na Aboud Jumbe ambaye kusema kweli ndiye aliyesababisha hali hii ya Zanzibar ya hivi kuwa ilivyo sasa.

Aboud Jumbe anahusishwa katika kuvisalimisha na ‘kuvifunga’ moja kwa moja Visiwa hivyo kwa mamlaka ya Bara. Bila shaka alifanya hivyo kwa kutojua athari yake miongo ya baadaye kwa watu wa Zanzibar. Yeye ndiye alitoa msukumo mkubwa katika kuviunganisha vyama vya TANU na ASP na kuundwa chama kimoja cha CCM mwaka 1977. Kuna wanaosema kwamba laiti Mzee Karume angekuwa hai, asingekubali kamwe kitu kama hicho kutokea.

Hata hivyo Jumbe alikuja kujutia sana hatua yake ile ya ‘kulikabidhi’ taifa la Zanzibar kwa Bara na jitihada zake, miaka 7 baadaye za kujaribu ‘kuifuta’ ilimgharimu sana kisiasa. Sote twafahamu yaliyotokea.

Na hata hivyo, Kwa Zanzibar, athari za kuviunganisha vyama hivyo viwili ilianza kuonekana baada ya ujio wa vyama vingi, mapema miaka ya 90. Ilionekana kama vile TANU ndiyo ilikuwa imeimeza ASP. Viongozi wa CCM wa upande wa Zanzibar, polepole wakajikuta wanapoteza uhuru, na hata pia mamlaka zao kimaamuzi kwani masuala muhimu ya chama hicho yalikuwa yakifanyika makao makuu yake yaliyopo Dodoma ambako katika vikao wajumbe wa Zanzibar huzidiwa akidi.

Si mara moja, tumeona hili likijitokeza sana katika mchakato wa uteuzi wa mgombea wa urais wa Zanzibar – yule aliyependekezwa na vikao vya Zanzibar vya chama hicho hutenguliwa na kikao cha juu vya uteuzi pale Dodoma. Matokeo ni kwamba wafuasi wa CCM wa Zanzibar husalimisha kwa wafuasi wa CCM wa Bara mamlaka ya kuteua mgombea wa kiti cha urais wa Zanzibar.

Lakini hili la ‘uporaji’ wa mamlaka ya kuteua mgombea polepole limekuwa likiendelea hadi imefikia mahali ambapo wenyewe Wazanzibari kupitia chama chao tawala hawawezi kutoa msimamo wa kuhusu chochote kinachohusu mustakabali wao.

Zanzibar yenyewe ikaamua kupiga zumari la pili (play second fiddle) na jinsi miaka ilivyokuwa ikiendelea ndiyo akili za viongozi wa chama hicho huko Zanzibar zilivyozidi kujiweka kisaikolojia katika kuiafiki hali hiyo.

Kwa mfano wakati wa uchaguzi wa 2015 kulikuwa hakuna kiongozi yoyote wa CCM kule Zanzibar aliyeonyesha nia ya kugombea urais wa Muungano. Wazanzibari wanaonekana hawana haja na kitu hicho. Hili linashangaza sana kwani kwa hali ya kawaida huwa ni fahari sana kwa sehemu ndogo ya Muungano kutoa rais wa Muungano. Imetokea mara moja tu (kwa Ali Hassan Mwinyi chini ya mfumo wa chama kimoja), na sidhani kama itajirudia tena.

Mwaka 2005 Zanzibar walikuwa na mgombea mwenye nguvu ya kushinda urais wa Jamhuri bila wasiwasi wowote lakini wenyewe viongozi wa CCM wa Zanzibar walimkataa kwa sababu ninazoweza kusema siyo za msingi, na hasa hasa zilikuwa za kitoto. Kwa maneno mengine viongozi wa CCM Zanzibar walionekana kuwaambia wenzao wa Bara kwamba “Huyo sie hatumtaki, endeleeni tu huko Bara kutoa marais wa Jamhuri.” Mambo ya kushangaza kweli kweli haya!

Amani Karume, mwanaye mrehemu Mzee Karume hususan katika kipindi chake cha pili cha utawala alijaribu kufuata nyao za baba yake kwa kufufua kifikra ‘uhuru’ wa Wazanzibari kupitia CCM kujiamulia mambo yao wenyewe hasa katika kuchagua viongozi, lakini mwishowe alionekana kukwama kwani mara kwa kulitokea misuguano wa kisirisiri baina yake na viongozi wa vikao vya juu vya chama chake upande wa Bara.

Katika mfumo huu wa vyama vingi ambapo upinzani kule Visiwani umetokea kuwa mkubwa sana, CCM Bara imekuwa ikihaha kuwapo kule aina ya viongozi ambao hatimaye wasije wakadai uhuru kamili. Na pia hapa tusisahau kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyeitoa mapema miaka ya 60 kwamba angekuwa na uwezo, visiwa hivyo angevikokota na kuvihamishia mbali, kiasi cha maili 1,000 nje ya Bahari ya Hindi. Alikuwa ana maana yake.

Na hata katika ule mchakato wa kuandika katiba mpya wa mwaka 2014, ule “msimamo” wa kipamoja uliowekwa na Baraza la Wawakilishi kuhusu mustakabali wa Zanzibar katika katiba mpya uliporomoka kule Dodoma baada ya kukunjiwa uso na CCM-Bara.

Viongozi wa wa Zanzibar wanaoheshimika walilazimika kujipindua chini juu na hatimaye kuukumbatia waraka uliondaliwa na CCM-Bara wa serikali mbili. Ninathubutu kusema kwamba iwapo Mzee Karume angenusurika kifo mwaka 1972 hali hii isingekuwapo.