Home Habari Mauaji ya albino yapungua nchini

Mauaji ya albino yapungua nchini

1044
0
SHARE

BENJAMIN MASESE NA CLARA MATIMO-MWANZA

SERIKALI imepongezwa na Shirika la Under The Same Sun kwa namna ilivyoshiriki kupunguza mauaji na ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi tangu mwaka 2008 hadi mwaka 2018 ambapo matukio yamepungua kutoka 40 kwa mwaka na kufikia nane.

Shirika hilo limesema licha ya mauaji kupungua kwa asilimia 90 bado kundi hilo linakumbwa na vitendo vya unyanyapaa na kutopewa nafasi ya ajira ambapo jamii imekuwa ikiwaita majina mbalimbali ya kebehi yakiwamo ya wanyama.

Akizugumza na waandishi wa habari jana katika kambi ya wiki moja iliyowekwa katika Chuo cha Walimu Butimba jijini Mwanza iliyopewa jina la ‘Summer Camp 2019’, Muasisi wa Shirika hilo kutoka Canada, Peter Ash alisema ni mafanikio makubwa kwa shirika na Serikali kufikia hatua ya albino kuisha bila hofu.

“Mauaji au matukio yamepungua sana, mfano tangu mwaka 2008  matukio yalikuwa 40 kwa mwaka lakini yameendelea kupungua hadi kufikia nane mwaka jana, mpaka tunavyozungumza sasa kwa mwaka huu wa 2019, matukio yameripotiwa mawili tu.

“Jambo ambalo bado linaendelea ni unyanyapaa na kutopatiwa fursa ya ajira, wapo watu wanawaita majina ya wanyama kama mbuzi, nguruwe na majina mengine ya kikabila lakini tunaendelea kutoa elimu kwa jamii.

“Pia vitendo vya baba kutelekeza familia kutokana na mama kujifungua mtoto mwenye ulemavu wa ngozi vimepungua na sasa wanawalea.

“Hapo awali kulikuwa na mtazamo kwamba watu wenye ualbino hawafariki bali wanapotea tu, vile vile mitazamo ya jamii ilikuwa kwamba ukimgusa ni kosa hivyo hivyo ilionekakana mama akijifungua mtoto wa namna hiyo ni mkosi lakini leo wanashirikiana kwa kula na kulala pamoja, jambo ambalo tunalisisitiza kupewa ajira, inaweza kutokea kuna nafasi lakini ni ngumu kupewa licha ya kuwa na vigezo,”alisema.

Ash alisema shirika hilo liliamua kuja nchini kutokana na  vitendo vilivyokuwa vikifanyika vya ukataji viungo vya albino kutokana na imani za kishirikiana ambapo kutokana na jitihada walizozifanya za utoaji elimu kwa jamii, wanajisikia faraja kuona ahueni imepatikana.

Alisema mpaka sasa kuna watu wenye ualbino 400 wanaolelewa na shirika hilo  ambapo wale wanaosoma wanalipiwa ada, vifaa vya shule na kuwakatia kadi za afya kutoka Mfuko wa Taifa wa Afya (NIHF) huku akiwataka jamii kuelewa kuwa ualbino ni hali ya kawaida ya kurithi inayotoka kwa baba na mama.

Ash alisema kwa kipindi  cha miaka 10 sasa amegundua kwmaba watu wenye ulemavu wa ngozi wana akili kubwa na ujuzi  hivyo aliiomba Serikali  na mashirika binafsi inapotokea fursa ya ajira kundi hilo litazamwe ili waweze kuwa sehemu ya viongozi.

Naye Mkurugenzi wa  Shirika la Under The Same Sun-Tanzania, Berthasia Ladislaus alisema kambi hiyo yenye watoto 180 kutoka mikoa yote Tanzania bara watakuwepo hapo  kwa lengo la kujifunza na kuonyesha vipaji.

“Watoto hawa wametoka mikoa yote na tumechukua 180 ingawa shirika linalea 400, hapa watafundishwa mambo mengi na kuonyesha vipaji, tumekuja hapa na wachungaji, wataalamu wa mambo mbalimbali.

“Jambo ambalo tunasisitiza kwa jamii, mashirika ya binafsi na Serikali ni kwamba tunao vijana waliofikia vyuo vikuu na wanafanya vizuri sana, hivyo wapewe fursa inapojitokeza ili na wao wawe viongozi katika ngazi za juu,”alisema.