Home Habari kuu MAUAJI YA WATOTO NJOMBE: Mganga tiba asiliaibua jambo jipya

MAUAJI YA WATOTO NJOMBE: Mganga tiba asiliaibua jambo jipya

465
0
SHARE

*Msitu wa Nundu watajwa kuwa hatari

NA ELIZABETH KILINDI, NJOMBE.

MGANGA wa tiba asili, Antony Mwandulami mkazi wa kata ya Mtwango wilayani Njombe, ameibua fikra tofauti juu ya sababu za mauaji ya watoto mkoani Njombe.

Mwandulami ameweka wazi kuwa  fikra zake anaamini kuwa visasi ni sehemu kubwa ya sababu za mauaji hayo ya watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitano na 11.

Kwa zaidi ya wiki moja sasa, kumekuwa na sintofamu ya mauaji hayo huku sababu kadha wa kadha zikitajwa zikiwamo za kishirikina zinazowahusisha wafanyabiashara wanaousaka utajiri kwa njia na namna zisizo halali.

Tayari jeshi la Polisi chini ya kikosi maalumu cha Operesheni kutoa Makao Makuu ya jeshi hilo, kimeshawatia nguvuni washukiwa zaidi ya 20 na uchunguzi zaidi unaendelea ili kujua kiini cha tukio hilo lililohusisha vifo vya watoto saba.

Tangu kuanza kuripotiwa kwa mauaji hayo, watu wa kada mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni, mawazo na fikra zao juu ya suala hilo ambalo linatishia usalama wa watoto mkoani Njombe haza katika Halmashauri ya Mji wa Njombe na Halmashauri ya wilaya ya Njombe.

Kutokana na uzito wa tukio hilo RAI lilifanya jitihada za kuwasaka baadhi ya waganga wa asili na wale wa jadi ili kupata ufafanuzi wa ni kwanini mauaji hayo yanahusishwa na imani za kishirikina.

Wapo waliokuwa na utayari wa kuisemea dhana hiyo, huku baadhi yao wakikataa kuzungumza kwa hofu kuwa huenda nao wakajikuta matatani ingawa hawahusiki kwa namna yoyote na jambo hilo.

Mganga wa tiba za asili, Antony Mwandulami amepata ujasiri wa kulizungumzia suala hilo na kuibua fikra mpya, ambayo haikuwahi kupewa nguvu kama ilivyo kwa ushirikina.

Mwandulami, alisema kuwa anachokijua na kukiamini ni kwamba  hakuna utajiri unaosababishwa na viungo vya binadamu na  kama upo basi unafanywa na watu ambao si waganga wa kweli.

Fikra mpya aliyoiibua Mwandulami ni huenda mauaji hayo yanasababishwa kwa kiasi kikubwa na uwapo wa visasi kati ya wauaji na wazazi ama walezi wa watoto.

 “Nikwambie mwandishi, hakuna utajiri unaosababishwa na utoaji wa viungo vya binadamu,  mambo haya yanatokea kutokana na visasi.

“Na kama utajiri wa namna hiyo upo basi sidhani kama unagusa damu tofauti. Ninavyojua hapo zamani mtu alikuwa akiambiwa atoe damu yake yaani mtoto wake au mkewe, lakini damu ya mtu mwengine hiyo hapana.’’

Katika kuhakikisha utatuzi wa kudumu wa jambo hilo unapatikana Mwandulami alitoa wito kwa jeshi la polisi kushirikiana kikamilifu na waganga wa jadi.

“Katika mkoa wetu huu wa Njombe hakujawahi kutokea mauaji ya kutisha ya namna hii, yaani mimi linanishangaza sana na inawezekana linafanywa na waganga ambao sio waaminifu’’ anasema Mwandulami.

Baadhi ya mashuhuda wa miili ya watoto waliouawa kwa nyakati tofauti waliliambia RAI kwa sharti la kutotaja majina yao, kuwa wanaamini mauaji hayo yanagusa moja kwa moja imani za kishirikina kwani wameshuhudia mwili wa mtoto ukiwa umenyofolewa baadhi ya viungo.

“Tumekuta mwili umetupwa katika msitu ukiwa hauna viganja vya mikono, macho  pamoja na kukatwa koromeo na wahusika pia walimpasua tumbo’.

“Inashangaza kama nia ni kutaka utajiri, huo utajiri utakuwa ni namna gani…unyama huu hauwezi kuvumilika hata kidogo..mimi na baadhi ya wenzangu tumeona kwa macho yetu viungo hivyo havipo,’’ alisema.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alifika mkoani hapa na kupatiwa tathmini ya matukio hayo.

Mbali ya kupewa tathmini lakini pia alishiriki katika msiba wa watoto watatu wa familia moja ambao wanadaiwa kuuawa na kaka yao.

Katika kuhakikisha wahusika wanapatikana Masauni aliagiza kupelekwe kikosi maalumu cha upelelezi, ambacho tayari kimeshaanza kazi chini ya Kamishna wa

Operesheni Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani.

WAFANYABIASHARA

Katika kuhakikisha hakuna muhusika wa matukio hayo anasalia salama, Mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka awali aliagiza kukamatwa kwa wafanyabiashara wakubwa ambao wanadaiwa kuhusika na matukio hayo.

“Hili jambo linasababishwa na mambo matatu, Vijana, wafanyabiashara wakubwa pamoja na waganga,  naomba tuanze na hawa wafanyabiasha wao watasaidia jeshi la polisi,’’ alinukuliwa  Ole Sendeka.

MSITU WA NUNDU

RAI limeelezwa kuwa miongoni mwa maeneo ambayo miili ya watoto waliouawa imekutwa ni msitu wa Nundu pamoja na mto Agafilo.

Miongoni mwa miili iliyokutwa huko ni ile iliyowahusisha watoto watatu wa familia moja wakazi wa kijiji cha Ikando ambao mwili mmoja ulikutwa msitu wa Nundu uliopo katika kata ya Yakobi huku mwingine ulikutwa mto wa Agafilo kata ya mji Mwema.

FAMILIA

Familia nyingine ambayo imekutwa na tukio hilo ni wakazi wa Mfereke kata ya Utelingolo Halmashauri ya mji Njombe ambayo imempoteza mtoto Oliver Ng’ahala (5) aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya msingi Kambarage ambaye alipotea wakati akirudi kutoka nyumbani kutoka shule.

Mtoto huyo alipatikana siku ya pili akiwa ameuawa kwa kunyongwa shingoni na kuchomwa kitu chenye ncha kali sehemu za siri ambapo mwili wake ulikutwa umetupwa katika msitu wa miti ya kupandwa.

Matukio hayo yameibua hofu kwa kiasi kikubwa kwa wananchi wa Njombe

HOJA YA VISASI

Hoja ya kuwapo kwa visasi inapea nguvu na tukio lililowahusisha watoto watatu wa familia moja Godliva Mwenda(11), Gaspa Nziku(8) na Giliad Nziku (5) ambao walichukuliwa na kaka yao Joel Nziku na kuwapakia kwenye fuso yenye namba ya usajili T563 AWJ na baadaye kupatikana wakiwa wamefariki.

Baba mzazi wa watoto hao watatu Danfod Nziku alisema kuwa alikuwa na ugomvi na mtoto wa marehemu kaka yake juu ya mashamba.

“Alikuwa akinilazimisha nimpe mashamba aliyoyaacha baba yake.. nilimpa nikamwambia haya sasa ni ya watoto wangu…alikua akinitishia kuniua pia alinambia eti mimi namroga ili asifanikiwe’’ alisema Nziku.

Alisema kaka yao huyo pia alikuwa akidai kuwa wadogo zake hao ambao wamefariki walikua wakitumiwa kumroga.

“Alikuwa na sababu nyingi wakati mwingine alikuwa ananiambia eti

tujiunge na freemason, mara nawatumia hawa watoto kumroga yeye,’’ anasema Nziku.

Katika kijiji hicho cha Ikando, mtoto mwengine wa kiume Emanuel Kiombo alipotea January 6 mwaka huu katika mazingira ya kutatanisha ambapo mpaka sasa hajulikani alipo.

Hali hiyo imesababisha hofu kwa kiasi kikubwa kutokana na mauaji hayo kuhusishwa na imani za kishirikina katika kujitafutia utajiri.

Hofu hiyo imesababisha wazazi kushindwa kutekeleza kikamilifu majuku ya kusaka kipato ili kuwalinda watoto wao.

IMANI ZA KISHIRIKINA

RAI limeelezwa kuwa wapo watu wanaoutaka utajiri kutokana na kuchoshwa na umasikini na njia pekee ya kufanikisha hilo ni kutekeleza mauaji hayo na kuzipeleka kwa waganga zana walizotumia kutekeleza mauaji hayo.

 “Hawa wauaji wanatumwa lakini kuna matajiri ambao wanawatuma na unakuta mganga amemwambia tafuta damu changa uilete na baada ya kuleta utafanikiwa katika biashara yao’’ anasema mzee Mgaya na kuongeza kuwa;

“Iliwahi kutokea katika haya maeneo yetu kuna kijana alikuwa na wenzake wanafanya biashara ya mkaa wakatumwa na mganga watafute damu ya binti bikra ili biashara iwe na mafanikio makubwa’’ anasema.