Home Makala MAVUJI WANAMTAKA MWEKEZAJI MWENYE TIJA

MAVUJI WANAMTAKA MWEKEZAJI MWENYE TIJA

400
0
SHARE

NA JIMMY CHARLES, LINDI


IPO dhana ya hovyo iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya viongozi kuwa wananchi wanaotetea ardhi yao anayopewa mwekezaji kwa hila eti, hawaitakii mema nchi!

Hizi ni fikra hasi ambazo mara nyingi huibua vuguvugu la kudai haki kwa njia ya heri na shari.

Tumeshuhudia haya yakitokea kwenye maeneo kadhaa nchini, wananchi wamekuwa wakidai haki zao za msingi kutoka kwa mwekezaji, lakini baadhi ya watu waliopewa dhamana wamekuwa wakiwaona wananchi hao ni kama waasi wa maendeleo.

Utamaduni huu wa hovyo umekuwa ni kama mshali unaochoma mioyo ya wadai haki na matokeo yake ni kuacha matundu ya chuki na hasira kwenye vifua vya watawaliwa.

Ukweli wa hili unadhihirishwa na kauli ya Mwenyekiti wa zamani wa kijiji hicho Yusum Kiranda ‘Tangi’ zenye nia ya kuhalalisha ubaya kuwa uzuri dhidi ya  sakata zima la ugawaji na umilikishwaji wa ardhi kubwa yenye misitu minene iliyopo kwenye kijiji cha Mavuji, wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Zaidi ya ekari 15,000 za kijiji hiki kwa sasa ziko mikononi mwa kampuni ya kigeni ya BioShape ambaye ilitua nchini mwaka 2006 kwa nia ya kuanzisha kilimo cha mibono.

Nia kuu ilikuwa ni mbegu za mibono hiyo kutumika kuzalisha mafuta. Uzalishaji huo ulitajwa kuwa salama kwa mazingira.

Ujio wa kampuni hiyo ulitajwa kuwa na tija kubwa kwa wanakijiji, wilaya, mkoa na nchi kwa ujumla wake.

Baadhi ya wanakijiji cha Mavuji wanakiri kuziona tija hizo kwa mtu mmoja mmoja mwanzoni kabisa mwa mradi huo.

Wengi walipata ajira za kudumu na wengine walipata za muda mfupi, maisha yalikuwa burudani kwao, vijana walisahau kilimo kuwa ndio muhimili wao pekee.

Wengi wakatelekeza mashamba yao na kujitupa BioShape ili kwenda kulima mibodo, Kijiji kikaridhia kutoa ekari 1,000,  za ziada ili kampuni hiyo ilitumie eneo hilo kama shamba la mfano.

Kwa nia njema au ovu, kampuni hiyo ikazitumia ekari hizo 1000 ambazo ni nje ya zile nyingi walizomilikishwa. Wakavuna miti na kila kilichokuwamo kwenye ekari hizo ambazo zilitawaliwa na msitu wenye miti mingi ya mbao ya aina tofauti tofauti.

Wazungu wakavuta mamia kwa maelfu ya tani za mbao, wakasafirisha kote wanakojua wao, vijana wakatumikishwa kuikata misitu yao kwa kurambishwa posho na mishahara isiyotosha mifukoni.

Wakafurahia maisha, wakaamini BioShape ndie mkombozi wao, hawakutaka kusikia la mwazini wala la mnadi swala, hakuna aliyelalamikia kampuni hiyo na hawakutaka kusikia inalalamikiwa.

Mavuji kikawa kijiji kilichonoga na kupendeza, baadhi ya waliokuwa viongozi wa kijiji kwa kujua wanachokifanya wakahalalisha ujenzi wa soko la hovyohovyo ambalo sasa halitumiki kabisa ili kuwapofusha wenye vilimilimi.

Wajanja wakawa na safari za kila siku za kwenda Dar es Salaam na kurudi Mavuji, mambo yalikuwa mazuri.

Masikini wanakijiji hawakujua kama raha ile ilikuwa ni ya muda mfupi na ingewagharimu kwa miaka mingi ijayo. Halikuwa kosa lao kutokujua kwa sababu hakukuwa na wa kuwajuza, waliopaswa kuwajuza ndio walikuwa wakiwaangamiza.

Waliokuwa wakijua waliwarubuni na kuwaingiza mkenge na kujikuta wakikabidhi maelfu ya ardhi yao kwa Bioshape kwa kupatiwa raha za muda mfupi.

Sasa raha zimekwisha, wameachiwa ghadhabu, sononeko na uchovu war aha walizozipata ndani ya kipindi cha miezi sita tu.

Wanakijiji wa Mavuji wengi wao wanalia, hawana ardhi ya karibu inayowatosha kuendesha shughuli zao za kila siku wanalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata ardhi ili kuendesha shughuli zao za kilimo.

Jafari Mgudo ambaye ni mwanakijiji lakini pia ni mjumbe wa Serikali ya Kijiji, aliiambia timu ya Waandishi wa Habari waliofika kijijini hapo chini ya mwavuli wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), kuwa kama wangejua yatawafika haya yanayowafika sasa, kamwe wasingekubali kutoa ardhi yao.

Anasema wanalazimika kuzihama kaya zao kwa muda mrefu ili kufuata mashamba ambayo yako mbali na kijiji, hali hiyo inatokana na hatua yao ya kukubali yaliyokuwa mashamba yao kumilikishwa mwekezaji.

Mgudo anabainisha kuwa kwa sasa idadi ya watu wenye rika la kushiriki shughuli za uzalishaji kijijini kwao wameongezeka, hali hiyo inawalazimisha kunyang’anyana maeneo machache ya kilimo yaliyopo.

Anasema kamwe wao hawana ugomvi na wawekezaji, wako tayari kushirikiana na mwekezaji yoyote atakayefika kijijini hapo na kwamba hata BioShape kama atarejea wao wako tayari kumpokea, hata hivyo hawako tayari kumpokea mwekezaji ambaye hana tija na wao.

“Kwa sasa tunalazimika kulilia ardhi yetu kwa sababu mwekezaji alieopo ameishikilia ardhi yetu kubwa na hana chochote anachoifanyia na sisi haturuhusiwi hata kukanyaga kwenye maeneo hayo, hii si sawa, tunalazimika kwenda mbali kusaka ardhi.

“Sasa ni kwanini Serikali isiione haja ya kuirejesha ardhi yetu ili tuitumie kwa manufaa na kama Serikali inataka ardhi hiyo iendelee kuwa ya uwekezaji basi watuletee mwekezaji mwenye tija na sisi,”alisema Mgudo.

Kauli ya Mgudo inaungwa mkono na Pili Saidi mama wa wanne. Pili anasema wanachokutana nacho sasa ni mateso,  wanalazimika kwenda mbali kufuata mashamba yao huku wakishuhudia mashamba yao ya karibu yakiwa mikononi mwa mwekezaji.

Pili anasema wanalazimika kwenda kwenye kijiji cha Machenjele kufuata mashamba, hali hiyo inawafanya nyakati nyingine kuhamia huko kwa zaidi ya miezi miwili ili kulinda mazao yao.

Wakati wanakijiji wakilalamikia utaratibu uliotumika kugawa mashamba yao kuwa haukuwa na ushirikishwaji, kwa upande wake Tangi anaonekana kuwa tofauti na wenzake.

Tangi anawaita wanakijiji wenzake waliopata kumchagua kuwa Mwenyekiti wa Serikali yao ya Kijiji kuwa ni waongo na wanania ya kumchafua mwekezaji.

Nasema hivyo kwa hoja kuwa wanakijiji hao wengi wao walilipwa fidia na waliiridhia na kwamba hawapaswi kurudishiwa ardhi yao hata kama haitumiki kwani ni mali ya BioShape.

Hoja ya Mtangi inapingwa na Mwenyekiti wa sasa wa kijiji hicho, Seleman Chaola, ambaye yeye anasema waohawana ugomvi na BioShape na hawatakuwa na ugomvi na mwekezaji yoyote, badala yake wanachohitaji wao ni kurudishiwa ardhi ili waitumie na pale atakapopatikana mwekezaji mwenye tija watakuwa radhi kushirikina nae kama walivyofanya kwa huyu wa sasa.