Home Habari kuu MAWAZIRI 7 WAINGIA MTEGONI

MAWAZIRI 7 WAINGIA MTEGONI

3146
0
SHARE
Rais Dk. John Magufuli
GABRIEL MUSHI NA JOHANES RESPICHIUS    |  

HADI sasa tayari jumla ya mawaziri saba wameshaingia kwenye mtego wa hatari ya kuenguliwa kutokana na kulalamikiwa na Rais Dk. John Magufuli hadharani. RAI linachambua.

Tangu aingie rasmi madarakani, Novemba 5, mwaka jana Rais Magufuli amekuwa na kasi ya utendaji isiyokwisha hali inayomsukuma kutamani hata wateule wake na watendaji wengine ndani ya Serikali kwenda na kasi hiyo.

Hata hivyo, katika kipindi chote hicho bado kumeonekana kuwepo kwa utendaji wa kimazoea kwa baadhi ya wateule na watendaji wengine ndani ya Serikali.

Hali hiyo inaonekana kumsukuma Rais Magufuli, kutoona haya kuwakosoa hadharani baadhi ya mawaziri wake ambao utendaji wao unampa shaka kama wanamuelewa.

Ukweli wa hilo unadhihirishwa na kauli yake aliyoitoa mwanzoni mwa wiki hii dhidi ya mawaziri wawili na makatibu wakuu wao, ambao hawakuhudhuria kwenye mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC).

Katika mkutano huo Rais Magufuli alionesha wazi kutofurahishwa na kitendo cha Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kutoshiriki kwenye mkutano huo.

Kutofika kwao kwenye mkutano huo kulimfanya Rais kuhoji kama walipewa taarifa ama la na papo hapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alimweleza kuwa mawaziri hao walikuwa na taarifa, lakini walishindwa kutuma hata wawakilishi wao katika mkutano huo uliobeba maudhui ya ‘Tanzania ya Viwanda na Ushiriki wa Sekta Binafsi nchini’.

Kitendo hicho kilimkwaza Rais Magufuli ambaye pia ndie Mwenyekiti wa Baraza hilo na kuweka wazi kuwa mawaziri wa namna hiyo hawawezi kuujua uchungu wa watu wanaotaka kuwekeza na kwamba ni afadhali amepata watu wa kuwauliza maswali baadae.

Katika kuonesha kukwazwa kwake Rais Magufuli alisema anasikitika kuona baadhi ya watu aliowateua hawajaelewa anataka nini, pia inashangaza kuona wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali nchini wamekutana na serikali kuzungumza masuala mbalimbali yakiwamo ya kilimo na mifugo lakini mawaziri wa sekta hizo hawapo.

“Kwa hiyo yale mliyoyazungumza itabidi Waziri Mkuu achukue ‘notes’ akayashughulikie mwenyewe. Hii ndio Tanzania, linaumiza si kwamba ninawachukia, lakini wamenikwaza, najua hata ninyi mmekwazika, nasema uongo?”alihoji.

“Jamani yote mmezungumza ya mang’ombe, ya maninii, kumbe hakuna mtu anayesikiliza, itabidi tuchukue notes sisi, atajuaje uchungu wa watu hawa ambao wanataka kuwekeza kwenye mambo haya, nasema ndugu zangu tunachangamoto kubwa.”

MAWAZIRI HUSIKA

Juzi mawaziri hao wawili kila mmoja kwa wakati wake walisema kuwa hawako tayari kuzungumzia chochote badala yake wanafuatilia kwa karibu kujua nini kimetokea.

Mpina, alisema kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo, bali anafuatilia kwa ukaribu kujua nini kimetokea katika mawasiliano hayo.

Kwa upande wake Dk. Tizeba, aligoma kuzungumza lolote kuhusiana na kile kilichotokea huku akisema kuwa alikuwa kwenye kikao.

Hata hivyo, zipo taarifa kuwa mmoja wa mawaziri hao hakuwa na taarifa yoyote inayohusiana na mkutano huo na kwamba kamwe asingeacha kuhudhuria.

Kauli ya Rais dhidi ya mawaziri hao wawili kutomuelewa inawagusa pia mawaziri wengine watano ambao kwa nyakati tofauti walikutana na kauli kama hizo.

Mawaziri hao ni Angela Kairuki (Madini), Charles Mwijage (Viwanda, Biashara na Uwekezaji) Prof. Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) Dk. Philip Mpango (Fedha na Mipango) na Mhandisi Gerson Lwenge (Maji na Umwagiliaji)

KAIRUKI

Januari 8 mwaka huu Rais Magufuli aliweka bayana udhaifu wa mawaziri wa madini na kilimo, manaibu na watendaji wao na kuwapa wiki moja kutekeleza maagizo yake huku akiweka wazi kuwa kuna baadhi ya wateule wake bado hawajamuelewa anataka nini.

Rais Magufuli alitoa dukuduku hilo wakati akimuapisha Dotto Biteko kuwa Naibu waziri wa madini akisema labda ataenda kuamsha waliolala kwenye wizara hiyo.

“Wizara ya madini ina changamoto nyingi na hata sasa hivi bado ina changamoto nyingi na niseme tu, ukiacha mambo machache machache bado wizara ya madini haifanyi kazi vizuri sana, unajua nikizungumza kwa kupamba nitakuwa mnafiki.

“Nasema hivi kwa uchungu mkubwa kwa sababu baadhi ninaowateua bado hawajanielewa na inawezekana bado hawajaelewa Bunge na Watanzania wanataka nini. Ndio maana nikaona labda ngoja niongeze naibu waziri aliyekuwa kwenye kamati ya madini ili ushauri uliokuwa unatolewa na Bunge, ili haya mapendekezo yaliyopelekwa bungeni kupitia kamati yao labda ataweza kutoa changamoto kwa watu waliolala ambao bado wamelala ndani ya serikali.

“Sifahamu wizara ya madini ina ugonjwa gani. Mtu unamteua pale, lakini sioni ile shughuli ninayoitaka huu ni ukweli, ni kweli kuna hela na madhahabu haya ni kama mapepo tu, inawezekana yanawaharibu akili halafu hamchukui maamuzi,” alisema.

MWIJAGE

Agosti 6 mwaka jana, Rais Magufuli alieleza kukasirishwa na kitendo cha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage cha kutovirejesha serikalini viwanda ambavyo vilibinafsishwa lakini haviendelezwi.

Rais Magufuli alikuwa akizindua kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro kilichopo mjini Tanga ambapo pamoja na mambo mengine alimuonya waziri huyo.

“Sasa wewe waziri usiangalire sura za marafiki wa wenzako waliotangulia, wewe wakung’ute kisawasawa, hicho ndicho ninachotaka ukafanye wewe na makatibu wakuu wako, nataka kuona kiwanda kimefutwa, atakayejidai anakwenda mahakamani ninajua tuta-deal naye vipi najua sheria zipo.

“Waziri nakuomba nimezungumza mara nyingi, sitaki kukaa narudia kila siku, si vizuri kulizungumzia hili hapa Tanga lakini napenda nizungumze, nisingezungumza ningeondoka na moyo unauma nataka muelewe,” alisema Magufuli

TIZEBA

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Charles Tizeba ambaye sasa ni waziri wa Kilimo ni mmoja wa mawaziri ambao wameonywa na Rais Magufuli mara nyingi jambo linaloonesha kukasirishwa na utendaji wake ikiwamo kutofuatilia majukumu yake kwa umakini.

Hayo yalijiri Agosti 6 mwaka jana wakati akiwa ziarani mkoani Tanga ambapo pamoja na mambo mengine Rais Dk. Magufuli alimpa siku saba Dk.Tizeba kwenda kwenye kiwanda cha Tanga Fresh kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya kiwanda hicho.

Rais alitoa maagizo hayo baada ya kupokea taarifa ya Mwenyekiti wa Bodi wa kiwanda hicho, Hamis Mzee ambaye alisema wamekwama kutoa maziwa  kwa wingi pamoja na kupanua kiwanda kutokana na kuwa na deni kubwa la kodi  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Wakati mwingine huwa nakwamishwa na watendaji wangu serikalini, unawapa wizara kushughulikia matatizo yaliyopo, waziri anayehusika hatambui changamoto zilizopo.

“Sasa nampa siku saba Waziri wa Kilimo na Mifugo aje hapa atatue changamoto hizi. Kuhusu suala la hati nitawapatia mara moja,” alisema.

Dk. Tizeba alionywa mara ya pili Januari 8 mwaka huu ambapo Rais Magufuli alimnyooshea kidole wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Naibu Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko.

Rais Magufuli alionesha kukasirishwa kutokana na ucheleweshwaji wa usambazaji wa mbole katika baadhi ya mikoa, ikiwamo inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula, kushindwa kupata mbolea, huku yeye yupo bila kuchukua hatua.

“Ninapozungumza hapa ndugu zangu, ipo mikoa haijapelekewa mbolea, ikiwamo mikoa ya Rukwa sijui na mkoa gani. Wakati tunaizungumzia kama ‘the big four’ kwa ‘production’ ya chakula, mbolea bado haijapelekwa, lakini Waziri wa Kilimo yupo.

“Nimempa maagizo Waziri Mkuu mbolea isipofika huko ndani ya wiki hii, huyo anayehusika na kupeleka mbolea aachie kazi, labda tukianza kukimbizana tutajifunza, nilishasema wale wote ninaowateua mimi wasifikiri mchezo, wanakuja kufanya kazi,” alisema Rais Magufuli.

PROF. MBARAWA, DK. MPANGO, MHANDISI LWENGE

Mawaziri hao kwa pamoja Rais Magufuli aliwaambiwa wazi kutoridhishwa na utendaji wao wakati akiwa katika uzinduzi mwingine wa mradi wa matenki ya kuhifadhia mafuta uliofanywa na Kampuni ya GBP ambapo, Rais Magufuli alikumbushia kutokuwapo  mashine maalumu ya kupima wingi wa mafuta yanayoingia kutoka nje (Flow meter).

Alisema huenda kuna njama za rushwa kuhakikisha mashine hiyo haifungwi na kusababisha Serikali kukosa mapato yake.

“Ni mwaka (miwili) sasa tangu Waziri Mkuu pale Dar es Salaam aagize watangaze tenda za flow meter na ifungwe pale bandarini, lakini cha ajabu hata kandarasi hajapatikana, anatafutwa kwa ujanja ujanja.

“Hata matatizo mengine yanashindwa kutatuliwa kutokana  na visheria vya ovyo na vya kijinga. Mawaziri mlioko hapa mpelekeeni salamu Waziri Mbarawa.

“Suala hili ukitaka kulitatua inabidi uhusishe Wizara ya Fedha na Mipango, Nishati na Madini, Maji, Viwanda na Biashara. Ni bahati mbaya  hawa watu mara nyingi hawawasiliani na kusababisha mambo mengi kukwama.

“Haingii akilini msimamizi wa Mamlaka ya Maji na Nishati (Ewura),hausiki na suala la umeme…kwa mfano, mafuta ya GBP kwenda mikoa jirani wanapanga bei kana kwamba mafuta hayo yametoka Dar es Salaam,” alisema.

Katika maagizo hayo, Rais alizitaka wizara zote zinazohusika kwa namna moja au nyingine na suala la mafuta, zikae pamoja kuhakikisha flow metre inapatiwa ufumbuzi wake.

“Hili ni la Profesa Mbarawa… hili mfikishieni ujumbe… kila kitu kinafanywa kwa ujanja ujanja, wale watakaokumbwa na huu mkumbo wakae wajiandae.

“Mawaziri wengine ni wapumbavu hawataki kufanyakazi maana hakuna njia nyingine za kupima mafuta zaidi ya flow meters.

KAULI ZA WADAU

Akizungumza na RAI, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Profesa Mwesigwa Baregu alisema hali hiyo ya kutomuelewa Rais inawezekana ni kutokana na kutoelewana kwenye Baraza la Mawaziri.

Alisema kuwa inaonyesha kuwa kuna ubovu fulani na kutoelewana katika Baraza la Mawaziri ambao unatokana na mawasiliano dhaifu kwamba mpaka swali linaulizwa na Rais kumtafuta waziri wake kwahiyo hakujua idadi ya mawaziri walioudhuria.

“Waziri Mkuu anapaswa kujua mawaziri ambao wapo na wasiokuwapo kwani kama kweli serikali inafanya kazi, waziri akiwa nje ya kituo chake cha kazi ni suala linalojulikana kuwa hayupo na sehemu aliko.

“Nilishangaa Rais hakujua mawaziri wake wako wapi, hiyo inajenga taswira kwamba viongozi hao ni watoro… huu ni udhaifu mkubwa katika serikali, sijui kama ni kutoelewana ndani ya Baraza la Mawaziri au inamaanisha hawakulipa uzito suala hilo.

“Sasa kama una mawaziri watoro ina maana wewe mwenyewe ‘you’re not in charge, you’re not in control’. Rais alipaswa kupata ‘Situation analysis’ ambayo ndiyo inaainisha nani wawepo kimkakati,” alisema Profesa Baregu.

Alisema pamoja na yote inaonesha kuna mkanganyiko ndani ya Serikali ya Dk Magufuli na kwamba imefika wakati wa wale ambao wanaona hawawezi kukubaliana na hawana uwezo wa kumudu kile anachokifanya Rais kukaa kando. Hivyo ifike wakati Watanzania waache uoga, unafiki na ulafi wa kimadaraka.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema inawezekana mawaziri hao hawakupata taarifa za mkutano huo au taarifa ziliwafikia zikiwa zimechelewa.

“Inawezekana walipata taarifa wakiwa wamechelewa na saa nyingine labda walikuwa kwenye ziara huko mikoani au ni hizo ‘ logistics’. Au wanaweza kuwa waliogopa maana hata mimi ningekuwa Waziri ningeogopa kwa sababu unaweza kufika pale ukasimamishwa ukaanza kuulizwa maswali ya papo hapo halafu ukashushuliwa mbele za watu hiyo pia inaweza kuwa inawatisha.

“Maana kama walikuwa na taarifa halafu wakashindwa kwenda! Wanaweza kuwa na hofu kwani staili ya utawala uliopo, mnaitwa hapo… ‘Aya waziri wa viwanda ebu twambie hapa eneo hili limekaaje usipojibu vizuri manbo yanakuwa magumu’.

“Hali hii watu wanajisikia vibaya mambo ya kuumbuana mbele ya hadhara, inawezekana ukaamua bora kutokwenda uje ujibu kwanini hujaenda maana utakuwa peke yako. Hawa nao ni binadamu, ni watu wazima wana watoto, ndugu hivyo kwenda kumdhalilisha mbele za watu namna ile haifai,” alisema Dk Bisimba.

Wakati Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema mawaziri hao ni wachapa kazi na wamethibitika kuwa na nidhamu inawezekana walikuwa na sababu maalum kutokuwapo kwenye mkutano huo.

“Naamini walikuwa na sababu za kuridhisha kwani mawaziri hao ni ‘Royal’ nimeshawasikia mara nyingi kwa matamko yao. Na hata Rais alipogusia suala la mbolea Waziri Tizeba alihangaika, suala la uvuvi haramu, Waziri Mpina anashugulika vyema kwahiyo wote ni watendaji ambao wamethibitika kuwa na nidhamu.

“Kama hawakuwapo kwenye mkutano bila sababu ule labda wameshajifuta uwaziri maana Rais hawezi kuitisha mkutano halafu wewe msaidizi wake usionekane inazua maswali mengi,” alisema Dk Bana.

Alisema kama ilifikia hatua ya Rais kuwaita kwenye hadhara ile viongozi hao lazima wajieleze na kama maelezo hayatamridhisha Rais anaweza kuwaonyesha mlango wa kutoka nje.

Katika mkutano huo zaidi uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam, mawaziri zaidi ya 10 walihudhuria.