Home Habari MAWAZIRI ZAIDI KUTUMBULIWA

MAWAZIRI ZAIDI KUTUMBULIWA

4996
0
SHARE

 

NA MWANDISHI WETU


KAULI ya Rais Dk. John Magufuli kuwa wapo baadhi ya mawaziri hawayajui  majukumu yao inaashiria uwezekano mkubwa wa mawaziri zaidi kutumbuliwa kabla ya kumalizika kwa muhula wa kwanza wa uongozi wake.

Mapema mwezi huu, akiwa katika hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu, manaibu katibu wakuu, wakuu wa mikoa na maofisa tawala mikoa, Rais Magufuli aliwataka mawaziri wasioyajua majukumu yao kuhakikisha wanatekeleza wao ipasavyo.

“Wakati mwingine kuna mambo ya kushangaza. Kulikuwa na mkubwa mmoja alifanya mambo ya hovyo tu katika wizara fulani, nikamuuliza waziri sitaki kumtaja, kwamba huyo mtu si yuko chini yako na amefanya ya hovyo? Akasema wa kutengua ni wewe, nikasema mimi rais?

“Nikamwambia hebu kasome sheria, mimi najua wa kutengua ni wewe waziri, nikamwambia ninakupa dakika 15 ukikuta mimi ndiye ninayestahili natengua na wewe nakutengua, lakini kama unaweza wewe katengue. Baada ya kama dakika 10 tu nikaona ameshatenguliwa, kumbe mamlaka ya kutengua ni ya huyo waziri,” alisema.

Alisema alikutana na hilo baada ya mmoja wa wasaidizi wake kufanya mambo ya hovyo hadi Sweden ikataka kuacha kutoa misaada kwa Tanzania kwa sababu ya mambo aliyoyafanya.

Aliwataka mawaziri wakafanye kazi, kila mmoja akaielewe wizara yake kwa kuwa anaona wapo watu ambao hawajazielewa vizuri wizara zao, hivyo wakafanye jitihada kuzielewa na wakayashughulikie yanayohusu wizara zao na wakayatatue.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli ni mwendelezo wa kutoridhishwa kwake na baadhi ya mawaziri na wasaidizi wake wengine, ambao wanashindwa kuchukua hatua za haraka kwenye baadhi ya maeneo yanayowahusu wao moja kwa moja.

Katika hotuba zake kadhaa Rais amekuwa akitoa kauli zilizobeba ukosoaji, maagizo na makatazo kwa wasaidizi wake hali inayoonesha kutoridhishwa na baadhi ya watu aliowateua.

Ukiachilia mbali kauli ya hivi karibuni, mwanzoni mwa mwezi Julai, Rais Magufuli alitoa kauli zilizowataka wateule wake wafanye kazi.

Tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015, Rais Magufuli ameonesha dhahiri kutowavumilia watendaji wazembe, hatua inayomfanya kuteua na kutumbua bila kujali jina la mtu.

Akiwa katika nusu ya kwanza ya utawala wake Julai 2, mwaka huu, akiwaapisha mawaziri na viongozi wengine 16 Ikulu jijini Dar es Salaam, alidhihirisha kuwa hafanyi mzaha katika yale anayoyasema baada ya kutoa maelekezo mazito kwa wateule wake, pamoja na kuwakosoa waziwazi baadhi ya viongozi bila kuwataja majina.

Katika kuonesha kuwa sasa amedhamiria kuona wateule wake wanatenda zaidi ya kusema, Rais Magufuli aliwaagiza mawaziri wake kuwa wakali na kuondoa mambo ya kubembelezana kwa  sababu mwaka 2020 wananchi hawatowabembeleza wagombea.

“Sasa tumebakiza miaka miwili na nusu, Kamwelwe ulikuwa maji umeshiriki miradi mbalimbali nafahamu umekuwa na ukali, ukali huu kaupeleke ujenzi ukaanze na wakandarasi,” alisema.

Aidha, alimtaka Waziri mpya wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, kutambua kwamba kuna matatizo makubwa kwenye maji, hivyo amempeleka katika wizara hiyo akiamini atakuwa mkali ili Watanzania wapate maji.

“Watanzania wanateseka sana, tunapeleka pesa nyingi, lakini hazitumiki, miradi mingi ya maji vijijini na wilayani haifanyi vizuri, kalisimamie hilo ili miradi ya maji ikatekelezwe,” alisema.

MAONI YA WADAU

Akizungumzia maagizo na uwezekano wa mawaziri zaidi kuendelea kutumbuliwa, Mhadhiri Mwandamizi wa kitivo cha siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana alisema aliyoyazungumza Rais yalikuwa yanatoa ujumbe kwa wale wote ambao wamepewa nyadhifa aidha kwa kuteuliwa au kwa kuchaguliwa.

Dk. Bana alisema ujumbe huo ulilenga kuwafahamisha Rais anataka nini na ilani ya chama chake inataka nini na kwamba rais anataka kuonesha kuwa ametekeleza ahadi zake na ilani ya chama chake kwa kiwango gani.

“Anataka kuwakumbusha kwamba wanao wajibu wa kusimamia majukumu ya wizara zote au taasisi alizowakabidhi waziongoze, wanao wajibu wa kuzisimamia na kufanya maamuzi bila kuanza kusubiri yeye kwanza afanye maamuzi au kutoa maelekezo.

“Wanayo dhamana kila mtu kwa wadhifa aliopewa na taasisi aliyopewa kufanya maamuzi magumu ambayo ndio dalili nzuri ya uwajibikaji, vilevile kusimamia na kufuatilia yale yanayotendeka katika maeneo ambayo wamekabidhiwa dhamana za kuongoza,. Huo ndio ujumbe kwa wale aliowaapisha na waliopo madarakani,” alisema Dk. Bana.

Hoja hiyo ya Dk. Bana ilipingwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji ambaye alisema ujumbe huo umeashiria kuwapo kwa tatizo la uongozi.

Tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015, Rais Magufuli amefanya mabadiliko ya mawaziri wake mara mbili.

Mara ya kwanza ilikuwa ni  Oktoba 7, 2017, ambapo aliwatema mawaziri wanne waliokuwepo kwenye baraza la awali.

Mawaziri walioachwa katika mabadiliko hayo ya kwanza ni  aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na nafasi yake ilichukuliwa na Hamis Kigwangwala aliyekuwa Naibu Waziri Wizara ya Afya.

Mwingine aliyeachwa ni aliyekuwa Waziri Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Mbunge wa Katavi,  Mhandisi Issack Kamwele ambaye awali alikuwa Naibu waziri wa wizara hiyo.

Pia alimtema aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Mbunge wa Viti Maalum CCM, Juliana Shonza wakati aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani nafasi yake ilichukuliwa na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga.

Julai mosi mwaka huu Rais Magufuli alifanya mabadiliko ya pili ya baraza la mawaziri na kumtupa nje aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, Dk. Mwigulu Nchemba ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM)

Aidha, katika mabadiliko hayo Magufuli aliwateua manaibu mawaziri  akiwamo Mbunge wa Singida Mjini, Musa Simma kuwa Naibu waziri  Ofisi ya Makamu wa Raisi – Muungano na Mazingira. Pia alimteua Mbunge wa Morogoro Kusini mashariki, Omarry Mgumba kuwa Naibu waziri wa kilimo.

Aliwabadilisha wizara, Profesa Makame Mbarawa ambaye alikuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuwa waziri wa Maji na Umgwailiaji huku  aliyekuwa  waziri wa wizara hiyo Mhandisi Isack Kamwelwe akihamishiwa Wizara ya Ujenzi.

Mabadiliko ya awali yalizidisha idadi ya wizara kutoka 19 hadi 21, ambapo wizara mbili alitenganishwa na kuzalisha wizara mbili zaidi.

Wizara zilizotengwanishwa ni Nishati na Madini, ambyo sasa Nishati inajitegemea na Madini inasimama yenyewe.

Nyingine ni wizara ya Kilimo na wizara ya Mifugo na Uvuvi ambazo kila moja  inaendesha shughuli zake yenyewe.