Home Makala MAWIGI YA MAJAJI NA MASHUSHUSHU WA CIA

MAWIGI YA MAJAJI NA MASHUSHUSHU WA CIA

1198
0
SHARE

SEPTEMBA 18 mwaka huu nilikuwa nasoma makala iitwayo, “Why African Judges Still wear wigs” katika gazeti la The Independent la Uingereza.

Mwandishi wa makala hayo ni Kevin Sieff akiwa jijini Nairobi, ambaye amefanya rejea kuhusiana na uvaaji wa Majaji wa Mahakama ya Juu nchini Kenya wakati ikitoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa na kiongozi wa muungano wa upinzani NASA, Raila Odinga kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC iliyomtanagza Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee kuwa mshindi.

Mwandishi wa makala hayo alijenga hoja kuu moja iliyogawanyika katika maeneo mawili. Mosi, mwandishi wa makala hayo analaumu tabia za viongozi wa Afrika na watu wake kupuuza au kuacha kuheshimu misingi yao badala yake wanakimbilia mambo yaliyofanywa na wakoloni na kuyaona kama ndio msingi wa kuendesha maisha na nchi zao.

Pili, mwandishi anasema inashangaza kuanzia nyakati za ukoloni hadi wakati huu Majaji wa Mahakama wanavaa mawigi ambayo kimsingi yalianzishwa katika utawala wa kikoloni. Anasema mtindo wa uvaaji wa mawigi unaachwa katika mahakama za Uingereza na kwamba haoni kwanini mhimili huo barani Afrika unadumisha ukoloni.

Yeye (nakubaliana naye) anatafsiri kuwa ili kukiri kuachana na ukoloni ni vyema kuachana na mambo yao yote ikiwemo mawigi ya majaji, pamoja na majina ya miji na maeneo ambayo kwa namna moja au nyingine yanadhihirisha tunavyodumisha ukoloni.

Katika hoja hizo zinalengwa nchi zote zilizowahi kutawaliwa na Mwingereza (Anglophones). Anazitaja nchi za Malawi, Uganda, Zimbabwe, Kenya na kwingineko ambako majaji wanavaa mawigi. Anataja maeneo kama Victoria Falls, Ziwa Victoria na kadhalika. Msingi wake ni uleule kwanini bara afrika linaendeleza na kudumisha ukoloni? Swali hilo linajibiwa kwa kuweka wazi kuwa hata bei ya Wigi moja ni dola 6,500.

Tuanzie hapo, kisha tuendelee mbele. Kuna mjadala mwingine umewahi kutokea miaka ya nyuma. Tuliona mjadala mkali na ushauri wa kualikwa kwa vyombo ya kijasusi kutoka nje ya nchi ili vije kuchunguza masuala mbalimbali hapa nchini.

Vyombo vya ujasusi vinavyozungumzwa zaidi ni CIA (Central Intelligence Agency) la Marekani na SDcotland Yard la Uingereza. Na zaidi chombo kingine kinachotajwa tajwa ni Shirika la Upelelezi la Marekani pia FBI.

Vyombo vyote hivyo vinaendeshwa kwa kodi ya wananchi wa Marekani na Uingereza kama ilivyo kwa vyombo vyetu vya dola hapa nchini. Hata hivyo ninalo swali linalonisumbua, kama ninavyokubaliana na mwandishi Kevin Sieff kwenye majaji juu ya kuendekeza ukoloni.

Kwamba mapendekezo ya kualika vyombo vya nje kuchunguza masuala mbalimbali hapa nchini yanatokana kuviamini sana vyombo hivyo au kasumba ileile kwamba “Kitu chochote cha Mzungu ndio kizuri zaidi”?

Mathalani kwenye kanuni za upelelezi ninaona zitakuwa zilezile, licha ya kuafiki kuwa tunazidiwa masuala ya teknolojia na mengine. Lakini tunavisifu vyombo vya nje kutokana na kasumba tuliyomeza kwamba “cha mzungu” ndicho hufanya kazi nzuri zaidi na hakijawahi kufeli kokote.

Tumesahau takwimu zinazojieleza dhahiri, kuwa kutoka mwaka 2010 hadi sasa asilimia 68 ya mauaji ya Marekani yalifanywa kwa kutumia moto. Kesi nyingi za mauaji zinategemea maabara kuanzia vinasaba hadi alama za vidole.

Licha ya Shirika la upelelezi la FBI kuwa na kikosi cha kurekodi takwimu za vinasababu juu ya kesi kiitwacho Combined DNA Index System (CODIS) ambapo raia wote vinasaba vyao vinahifadhiwa ili kufanyiwa ulinganifu. Pamoja na kuwa na kikosi cha CODIS bado FBI wameshindwa kumaliza kabisa kesi wanazokutana nazo ili kukamilisha ushahidi.

Ukweli mwingine ni huu; Tangu mwaka 1968 (karne ya 20) hadi mwaka 2011(karne ya 21) kuna mauaji milioni 1.4, lakini kesi zilizofanikiwa na kutolewa hukumu ni chini ya milioni 1.2. kuna deni la kesi 200,000 halijaisha.

Hapo ndipo ninapojiulzia katika mihangaiko yetu yote huku na huko tumeshindwa kuviamini vikosi au vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya upelelezi juu ya masuala yoyote yaliyotukabili? Ni kweli kwamba vyombo hivyo vimeshindwa kufanya kazi yake na badala yake vinahitajika kutoka nje?

Kila kukicha tunasikia huyu anamtuhumu yule, na yule anamtuhumu huyu. Hakuna kuaminiana tena. Hakuna weledi tena. Hakuna ile hali ya viongozi kupeana muda wa kukamilisha majuku myao bali kila mtu anataka kumpa presha mwenzake.

Jambo baya zaidi ni kwamba katika mapendekezo yanayotolewa juu ya kuletwa mashirika ya upelelezi ni kwa sababu ya kutatua mambo kwa muda mfupi. Kwamba faida inayotafutwa ni muda mfupi kuliko ile ambayo kama taifa ingelipata kwa muda mrefu.

Tunaweza kuvialika vikosi vya usalama kutoka Marekani au Uingereza, lakini tunajikuta tuko palepale kwamba tunaimba na kupiga filimbi za ukoloni huku tukishutumiana kwanini hatujitegemei. Binafsi sipendi kabisa kauli ya kusema nchi yetu ni changa wakati tuna miaka 50 ambayo tunaweza kufanya lolote lenye manufaa kwa nchi yetu.

Kutokamilika kwa jambo tunalopigania haina maana kwamba taifa letu ni change bali hatukufikia malengo, lakini angalau kumekuwa na kujaribu na kufanikisha machache kuliko mengi yanayotafsiri umwamba wa taifa.

Hivi leo tunawaruhusu watoto wetu wawe maofisa usalama, wanajeshi, mashushushu na kadhalika lakini linapokuja suala linalowahusu na lenye kuhitaji uwezo wao wa kikazi tunakosa imani kwao na kutaka tuwaalike mashushushu wa Scotland Yard FBI au CIA. Haya ni maajabu ambayo baadhi yetu tunaona hayana tofauti na mawigi ya majaji wanayotamba nayo mahakamani ilhali ni kuendekeza na kudumisha ukoloni kwa njia nyingine.

Nitihimishe kwa kusema tunavihitaji vyombo vyetu vya usalama visafishe ‘wingu’ kutoaminiwa kama linavyoonekana nyakati hizi. Na ‘kutoaminiwa’ haina maana vimekosa uwezo bali hisia hasi kutokana na matukio mbalimbali. Nimekuwa na mawazo hayo kwa leo, naweza kuwa sahihi au kukosea lakini nimefikiri hivi leo, ila napinga kuwaendekeza wakoloni. Wakati mwingine tutajadiliana matatizo yanayovikabili vyombo vyetu.