Home Latest News MBATIA: MZIGO WA KODI UNAKATISHA TAMAA WAWEKEZAJI WAZAWA

MBATIA: MZIGO WA KODI UNAKATISHA TAMAA WAWEKEZAJI WAZAWA

5014
0
SHARE
Mkurugenzi wa kiwanda Himo Tanaries, Saba's Woisso akimuelezea Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega kuhusu ubora wa ngozi inayozalishwa kiwandani hapo.

NA SAFINA SARWATT, MOSHI


LICHA ya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa wingi wa mifugo barani Afrika baada ya Ethiopia, bado kuna changamoto katika uzalishaji wa bidhaa za ngozi.

Ni sekta chache tu ndizo zinazoonekana kuwa na uwezo wa kiushindani hapa nchini, lakini zipo tafiti nyingi zinaonyesha kwamba Sekta ya Ngozi, inaonekana kuwa na uwezo wa kiushindani kwa viwango vya kimataifa.

Wanazuoni na wachumi mbali mbali, wamekaririwa wakisema kuwa bidhaa nyingi zimekuwa zikiingizwa nchini kutoka nje, huku zikiwa chini ya ubora lakini kwa kuwa huuzwa kwa bei rahisi hukimbiliwa mithili ya pipi.

Haya yanasababisha baadhi viwanda vyetu vinavyomilikiwa na wazawa kushindwa kujiendesha huku hata mitaji yao ya kibiashara ikipungua na hatimaye kuondoka kwenye soko la ushindani.

Kama haitoshi wajasiriamali wadogo nao wanaelekea kukata tamaa kutokana na wimbi la uzalishaji wa mali zinavyozidi kughubikwa na gharama kubwa za uendeshaji hii ikichangiwa na mlolongo wa kodi za serikali.

Sabas Woisso ni mmoja wa wawekezaji wazawa ambaye anamiliki wa kiwanda cha ngozi Himo Tanaries (Hita), kichopo mji mdogo wa Himo wilayani Moshi vijijini.

Hata hivyo, kiwanda cha Himo Tanaries ni mojawapo ya viwanda vinavyozalisha  bidhaa za ngozi, ikiwemo viatu, mikanda, mikoba.

Kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 1895 katika karne 19 kikiwa chini ya wakoloni wa Waingereza na mwaka 1966 kilimilikiwa na wahindi kwa kupitia leseni ya serikali ya viwanda kama Himo Tanners and Planters Limited.

Aidha, mwaka 1997 kiwanda kilikufa kutokana na mashine zake kuwa za zamani na kukosa malighafi pia wamilimiki hao kushindwa kukiendesha. Hata hivyo mwaka 2002 kilifunguliwa chini ya usimamizi wa wawekezaji wazawa.

Kiwanda hicho baada ya kufunguliwa kiliendelea kuzalisha chini ya viwango kutokana na mtaji na miundombinu ya kiwanda kuwa ya kizamani.

Akizungumza na RAI wiki hii Mkurugenzi huyo wa Himo Tanaries(Hita) anasema serikali inapaswa kupunguza mlolongo wa kodi kwa wawekezaji wa wazawa.

Woisso anasema punguzo hilo litasaidia kukuza uwekezaji kwani wawekezaji wazawa hutengeneza bidhaa mbalimbali za ngizo kwa kutumia ngozi asilia wanazozalisha wenyewe katika kituo chao.

Anasema shughuli za uendeshaji wa kiwanda zinahitaji ushirikiano  mkubwa wa serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kufanikisha lengo la Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

“Kuendesha viwanda kunahitaji fedha nyingi pamoja na mazingira bora ya uwekezaji, hasa kwa wawezaji wazawa ili kutela maendeleo katika nchi yetu.

“Kiwanda chetu kinaendelea kufanya vizuri lakini tatizo kubwa ni upatikanaji wa ngozi ghafi nzuri za kutosha kwa ajili uzalishaji, kwani ngozi nyingi zinazoletwa sokoni zimekuwa na matatizo ya uchunaji na kuwa na matobo wakati wa uchunaji pia moto yaani ‘brand mark,” anasema.

Anasema hali hiyo inachangia ngozi nyingi kutofaa kwa matumzi ya nje na ndani na kutokana na kukosa ubora.

Anasema kutokuwa na ruzuku serikalini na misamaha ya baadhi ya kodi kama ya inavyofanyika kwa wageni wanaowekeza nchini, pia ushuru mkubwa wa usafirishaji ngozi nje ya nchi pia vimechangia wawekezaji wazawa kushindwa kuwekeza kwenye viwanda.

Anasema serikali inatakiwa kuliangalia hili suala kwa haraka ili kuwalinda wawekezaji wazawa wenye nia ya dhati ya kufufua viwanda nchini.

Anasema kitendo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutosikiliza wadau hasa kwenye masuala ya  uhakiki wa nyaraka hadi kuwapeleka kwenye mabaraza ya kodi, huondoa morali ya uwekezaji nchini.

“Kwa mfano baadhi ya tozo hizo  ni service levy, export permit, business license, water use fee, water right fee, worker compensation fund (WCF), kodi ya majengo, Bili za Tanesco, Chemical permits fee, chemical inspection fee, medical examination fee, income tax.

“Hizo ni baadhi tu za tozo na vitu vingi vinajirudia rudi unakuta mwisho wa siku unashindwa kuendesha kiwanda kwani unajikuta fedha zote umelipa kodi za serikali,sisi hatukatai kodi Ila ombi kwa serikali ipunguze huo mlolongo,” anasema.

Mbali na hayo pia ameiomba serikali kuandaa utaratibu wa kupunguza muda wa kutoa haraka mizigo yaani malighafi za viwandani kama vile kemikali, na mashine bandarini ili kupunguza gharama za tozo.

Anasema hadi sasa kiwanda hicho anasema kimechangia kuzalisha ajira ya kudumu  kwa watanzanja zaidi  87, pia kina malengo ya kupanua wigo wa ajira.

Anasema kutokana na hali hiyo, uwapo wa kiwanda hicho pia umesaidia kufufua viwanda vingine vinavyotegemea malighafi ya ngozi kutokana kiwandani.

Anasema kuwa miongoni mwa viwanda hivyo ni pamoja na Shah Industries, Katanga  Foot wear na Italy shoes. Viwanda hivyo hutegemea malighafi kutoka Himo Tanaries, badala ya kuagiza nchi za jirani kama walivyokuwa wanafanya awali.

Aidha, Woisso alitoa angalizo kwa serikali kujaribu kuthibiti mfumuko huu wa bei ili kuweza kunusuru masoko ya ndani ya nchi kwa kuacha kukumbatia bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi.

Aidha, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR Mageuzi) anasema serikali inapaswa kuweka sera nzuri za uwekezaji katika sekta ya viwanda na kuondoa vikwazo vya mlolongo wa kodi.

“Hao wawekezaji wazawa wametusaidia sana katika kuongeza uchumi wa nchi na kuzalisha ajira kwa wananchi wetu sijaona sababu za mlolongo wa kodi nyingi ambazo nyingi ukiangalia zimejirudia rudia,” anasema.

“Hiki kiwanda kipo katika jimbo langu nimeona jinsi gani kinavyoisadia, hivyo tusipoangalia njia yakuisaidia kiwanda hiki tutakuwa tunawavunja moyo wawekazaji hao wazawa ambao wamethubutu,” amesema.

Naibu waziri wa mifungo na uvuvi Abdallah Ulega, naye anasema mwekazaji huyo mzawa anapaswa kupewa upendeleo wa kipekee kutokana na kuzalisha ajira pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa zetu za ngozi zinazozalishwa nchi.

“Binafsi nimefurahishwa na uwekezaji huo kwani itasaidia kuongeza thamani ya ngozi na wafungaji wetu wanapata soko la uhakika ya ngozi, ni kiwanda ambacho sisi kama serikali tunatakiwa kulitanzama kwa haraka,” anasema.

Anasema suala la kodi ataliwasilisha kwa haraka ili kuangalia ni ninamna gani litapunguzwa ili kuimarisha viwanda vyetu.

Naibu waziri huyo akiwa mkoani Kilimanjaro alifanya ziara katika viwanda vya kutengeneza chakula cha mifungo na unga sembe cha Maranga, kiwanda cha Ngozi cha Himo tanaries, Moshi leather, Kituo cha Utafiti wa Mifugo kilichopo wilayani Siha (Talri).