Home Habari MBIO ZA MWENGE ITILIMA, BARIADI ZILIVYOIBEBA SIMIYU

MBIO ZA MWENGE ITILIMA, BARIADI ZILIVYOIBEBA SIMIYU

4428
0
SHARE
Kiongozi wa Mwenge, Charles Kabeho akizindua baadhi ya miradi mkoani Simiyu

NA DERICK MILTON, SIMIYU


Katika makala ya wiki iliyopita, tulionyesha kwa kina halmashauri zilizofanya vibaya wakati wa mbio za Mwenge 2018 mkoani Simiyu na hatua za viongozi ambazo wameendelea kuchukua kwa watendaji.

Katika makala ya leo, tumeangazia Halmashauri mbili, ambazo miradi yake yote ilizinduliwa na kuwekewa jiwe la msingi, huku ikionyesha kutoa tabasafu la furaha kwa kiongozi wa Mwenge Charles Kabeho.

Ikiwa Mkoa wa Simiyu utafanya vizuri na kushika nafasi za juu katika tadhimini ya Mwenge inayoendelea kufanyika, au itakayofanyika basi Halmashauri za Wilaya ya Itilima na Bariadi, ndizo zitakuwa zimesababisha hali hiyo.

Lakini kama itakuwa kinyume chake, Mkoa wa Simiyu ukashika nafasi cha chini na kuonekana umefanya vibaya, basi lawama zote lazima watupiwe halmashauri ya Meatu pamoja na Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Sababu kubwa ya kutupiwa lawama kwa halmashauri hizo mbili, ni kukataliwa zaidi ya mradi mmoja kwenye maeneo yao, ikiwa pamoja na kuonekana kwa kasoro nyingi katika baadhi ya miradi iliyotembelewa kwa ajili ya kukaguliwa.

Wilaya ya Itilima.

Katika halmashauri za Wilaya ya Itilima pamoja na Bariadi, mambo kwao hayakwenda mrama kama ilivyokuwa kwa wenzao, baada ya miradi yote kuonekana imetekelezwa kwa kiwango cha hali ya juu.

Mwenge Uhuru ukiwa katika Itilima, ulizindua miradi mitatu ya huduma za kijamii, pamoja na kuweka jiwe la msingi mradi mmoja wa ujenzi wa miundombinu kwenye Kituo cha Afya Ikindilo.

Katika uzinduzi wa mradi wa Maji kijiji cha Lagangabili, pamoja na vyumba vinne vya madarasa Shule ya Msingi Lagangabilili, ni miradi ambayo Kiongozi wa Mwenge, Charles Kabeho, hakuweza kutilia shaka lolote.

Licha ya kuuliza maswali mbali mbali mara baada ya kufika kwenye miradi hiyo, bado haikuonyesha kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha kutokana na miradi yenyewe kujengwa katika ubora.

Katika mradi wa vyumba vinne vya Madarasa, taarifa ya mradi huo iliyosomwa na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Anna Mathew, alisema kuwa kiasi cha shilingi milioni 91, kimetumika kujenga vyumba hivyo.

Mwalimu Anna alieleza kuwa mbali na kujenga vyumba hivyo, kiasi hicho cha fedha kilitumika kujenga matundu nane ya choo cha wanafunzi na walimu, pamoja na kuweka madati katika kila darasa.

“Kiasi hiki cha fedha, mchango wa wananchi ni shilingi milioni 5.5 huku Serikali ikitoa shilingi milini 86.6 na kwenye choo matundu sita ni kwa ajili ya wanafunzi na matundu mawili ni kwa jili ya choo cha walimu,” alisema Mwalimu Anna.

Mchanganuo wa ghamara hizo haukuficha furaha ya kiongozi huyo mara baada ya kukagua mradi huo na kuweka jiwe la msingi, huku akiupongeza uongozi wa shule pamoja na halmashuari kwa ujumla.

Kabeho alizitaja halmashauri nyingine nchini kwenda katika shule kwa ajili ya kujifunza matumizi mazuri ya fedha za miradi ya maendeleo, pamoja na usimamizi wa kazi, ujumbe ambao uliwafikia moja kwa moja halmashuari ya wilaya ya Meatu.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Mwenge hakuishia hapo, aliwataka walimu wote wa shule hiyo kujipanga kwa ajili ya kushika Mwenge wa Uhuru ikiwa ni inshara ya pongezi kubwa kwa kazi nzuri walioifanya.

Katika mradi wa maji kiongozi huyo, wakati akitoa ujumbe wa Mwenge, aliwapongeza viongozi wa wilaya, Mbunge wa Jimbo hilo, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, kutokana na ushirikiano wao.

Alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni wa kiwango cha hali ya juu na kutumia gharama halisi, vinatokana na uwepo wa mahusiano mazuri kutoka kwa viongozi wa wilaya, halmashauri, watendaji pamoja na wananchi.

Pongezi za kiongozi huyo zilitokana na mradi huo wa maji ambao uligharimu kiasi cha shilingi milioni 967, huku akitarajia kuwahudumia wananchi zaidi ya 2000 wa kijiji hicho, ambao tangu uhuru walikuwa hawajawahi kupata maji safi na salama.

Alisema kuwa kupatikana kwa huduma ya hiyo kwa wananchi, ni moja ya huduma muhimu sana katika maisha ya binadamu, ambapo aliwapongeza kwa kufanya kuwa kipaumbele cha kwanza katika maendeleo ya kijiji hicho.

Kabeho aliwataka wananchi kushirikiana na viongozi wa halmashuari hiyo, wilaya, mbunge, pamoja na watendaji katika kuhakikisha wanalinda mradi huo wa maji ili uweze kutoa huduma kwa muda mrefu.

Katika mradi wa mwisho wa uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa miundombinu katika Kituo cha Afya Ikindilo, kiongozi huyo alilirizishwa na ukarabati huo ambao alisema matumizi ya fedha yanaendana na ukarabati wenyewe.

Ujenzi wa miundombinu hiyo ni pamoja na jengo la wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti pamoja na nyumba ya mganga, ambapo kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Kabeho aliwapongeza watendaji wa Idara ya Afya wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri, Dk. Anold Musiba, kwa kazi nzuri ya usimamizi katika ujenzi wa miundombinu hiyo.

Aliwataka viongozi na watalaamu hao, kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na ndani ya muda mfupi.

“ Tumeona ujenzi uko vizuri sana na niwapongeze halmashauri hii ni moja ya eneo la kuigwa katika matumizi mazuri ya fedha za umma, usimamizi wa miradi na kujengwa kwa kiwango, lazima wengine waje waige hapa Itilima,” alisema Kabeho.

Mkuu wa Wilaya.

Mkuu wa Wilaya, Benson Kilangi, anasema kuwa ushirikiano ulipo na viongozi wa kisiasa na serikali, umekuwa ni mkubwa sana na ndiyo siri ya mafanikio hayo kwao wakati wa Mwenge.

Kilangi amesema kuwa mbali na hilo, usimamizi ulipo kwenye ofisi yake, Ofisi ya Mkurugenzi pamoja na Madiwani ambao miradi inatekelezwa kwenye maeneo yao, umekuwa mkubwa na kushirikiana.

Mbunge.

Mbunge wa Jimbo hilo, Njalu Silanga, ambaye alishikiri mbio hizo mpaka mwisho, anatajwa kuwa ndiye kichocheo kikubwa cha mafaniko hayo ndani ya Wilaya hiyo.

Licha ya kuwa ni miongoni mwa wilaya mpya, uwepo wa Mbunge huyo unaiondoa wilaya kuwa miongoni mwa wilaya mpya kutokana na maendeleo ambayo yamepatikana katika kipindi kifupi.

Mbunge anasema kuwa silaha kubwa ni ushirikiano ulipo kati yake, wananchi, pamoja na uongozi wa wilaya katika kuhakikisha wanafanya kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Anasema kuwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, yeye kama Mbunge, amekuwa akifuatilia mara kwa mara utekelezaji wa miradi hiyo, ikiwa ni moja ya jukumu lake la kusimamia matumizi mazuri ya fedha za serikali.

Wilaya ya Bariadi.

Mwenge ukiwa katika Halmashauri Wilaya ya Bariadi uliweza kupitia miradi minne yenye thamani ya shilingi milioni 568 ukiwemo Mradi wa Maji Kasoli.

Miradi mingine ni ujenzi wa Shule ya Msingi Otto Busese, ambayo imejengwa kwa ufadhili wa kiwanda cha kuchambua pamba—Alliance  Ginnery Limited, kilichopo Kasoli Bariadi, pamoja na ujenzi wa daraja la Ikungulyabashashi.

Mambo yalienda vizuri kama ilivyokuwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, baada ya kiongozi wa mwenge kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, ambayo alisema imetekelezwa wa ubora.

Kiongozi huyo wa Mwenge alisema kuwa halmashauri za Itilima na Bariadi Vijijini, zinatakiwa kuwa halmashuari za kuingwa katika Mkoa wa Simiyu na nje katika kutekeleza miradi yao.