Home Makala Mbivu, mbichi zao la pamba linavyotafsiriwa na wadau

Mbivu, mbichi zao la pamba linavyotafsiriwa na wadau

287
0
SHARE

Na YOHANA PAUL-MWANZA

PAMBA ni miongoni mwa mazao makubwa ya biashara yanayouzwa nje ya nchi huku zaidi ya asilimia 90 ya pamba ikizalishwa kusini mwa Ziwa Victoria hasa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Tabora, Kigoma na Singida, ambapo Mwanza na Shinyanga ikitajwa kuzalisha asilimia 80 ya pamba hiyo.

Zao la pamba linakadiriwa kuchangia takribani dola milioni 90 kwa mauzo ya nje ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, pato la pamba nchini linatajwa kuwa limeongezeka kwa kiasi cha tani 60,000, sawa na asilimia 0.3 ya pato la dunia la tani milioni 20.

Ikumbukwe kuwa ili kuhakikisha maendeleo mazuri ya kilimo cha zao la pamba, Serikali iliamua kuunda chombo kitakachosimamia zao hilo ambapo mwaka 1976 usimamizi wa zao la pamba ulikuwa chini ya Mamlaka ya Pamba na kuanzia mwaka 1984 ulikuwa chini ya Bodi ya Pamba (TCMB).

Aidha, mwaka 1991; usimamizi wa pamba ulikuwa chini ya Tanzania Cotton Lint & Seed Board (TCL & SB) na ilipofika mwaka 1993 ulifanywa kuwa chini ya Bodi ya Pamba (TCB).

Mbali na kuwekwa chini ya usimamizi wa TCB, bado tumeendelea kushuhudia changamoto nyingi zinazolikumba zao hilo ikiwemo changamoto ya soko la uhakika, kuyumba kwa bei na usambazwaji wa pembejeo zisizokidhi viwango kwa wakulima hasa mbegu na viuadudu.

Changamoto ambazo pia zilijidhihirisha katika msimu wa mavuno wa mwaka jana na kushuhudia idadi kubwa ya wakulima wakilalamika kuuza pamba yao kwa mkopo kwa mawakala na hata kucheleweshewa malipo yao.

Ili kupata ufafanuzi wa mipango na mikakati ya jinsi ambavyo bodi ya pamba kwa msimu wa kilimo 2019/2020, imejipanga kupunguza changamoto kwa wakulima wa zao hilo Desemba mwaka jana, tulitembelea ofisi za bodi ya pamba zilizopo Mwanza na kuacha baadhi ya maswali ambayo yalitolewa ufafanuzi na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala TCB, Gabriel Mwalo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu.

Akizungumuzia juu ya mwenendo wa hali ya malipo ya wakulima wa pamba msimu uliopita, Mwalo anasema kutokana na changamoto ya kushuka kwa bei katika soko la dunia anakiri kwamba ununuzi ulianza kwa kusuasua sana, hata hivyo serikali ilisimamia kwa ukaribu changamoto zilizokuwa zinawakabili wanunuzi hususani kukosa mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha.

Anasema kwa kuwa wakati benki zinaanza kutoa mikopo kwa kampuni za ununuzi tayari wakulima walishakusanya pamba nyingi kwenye vyama vya ushirika Amcos na hivyo wakulima wote hawakuweza kulipwa kwa wakati mmoja ingawa bodi kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa na wilaya imeendelea kusimamia ili kuhakikisha madeni yote ya wakulima yanalipwa.

Anaeleza ingawa kulikuwa na changamoto kadhaa lakini hadi kufikia mwisho wa msimu wa ununuzi wa pamba jumla ya tani 350,832 za pamba zilinunuliwa katika mikoa ya kanda ya ziwa ambapo mkoa wa mwanza pekee ulizalisha kiasi cha tani 33,243 za pamba mbegu kiwango ambacho hakikufikia lengo hasa kutokana na ukame ambao uliathiri sehemu kubwa ya maeneo inakozalishwa pamba.

Akizungumzia jinsi ambavyo TCB imejipanga kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa kwenye zao la pamba na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha, Mwalo anasema mabadiliko ya hali ya hewa ni jambo ambalo hakuna mtu mwenye majibu ya uhakika hivyo mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mengi nchini ni matokeo ya mabadiliko ya tabia ya nchi na kama ukame unavyoathiri mazao ndivyo mvua nazo zinaweza kuathiri mazao yote ikiwemo pamba pale zinapozidi kiwango, hivyo hakuna njia rahisi ya kukabiliana na mvua hizo tofauti na kuomba Mwenyezi Mungu zinyeshe kwa kiwango.

Kuhusu changamoto za mbegu na pembejeo kwa wakulima, Mwalo anasema ili kuondoa uhaba wa mbegu kwa wakulima, kwa msimu huu wa kilimo wakulima wamepatiwa mbegu za kupanda kwa mkopo kupitia vyama vyao vya ushirika Amcos lakini mchakato wa kupata viuadudu vizuri bado unaendelea ili kuhakikisha mazao ua wakulima yanakua katika kiwango chenye ubora pasipo kushambuliwa na viwavi na wadudu waharibifu.

Anasema ili kukabiliana na malalamiko ya tatizo la baadhi ya viuadudu kutofanya kazi bodi ya pamba kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Madawa (TPRI), inafanya majaribio ya viuadudu kwenye mashamba ya wakulima kabla ya kuvisambaza ili kujiridhisha na utendaji kazi wa kiuadudu husika.

Aidha anaongeza kuwa bodi ya pamba kwa kushirikiana na taasisisi ya utafiti ya ukiriguru, imeweka mpango endelevu wa kutoa mafunzo ya matumizi ya viuadudu na vinyunyizi kwa wakulima kila msimu wa kilimo kwani kutofanya kazi kwa kiuadudu pia kunachangiwa na sababu nyingi ikiwa ni pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya kiuadudu chenyewe au udhaifu wa kiuadudu.

Mwalo anaongeza kuwa ili kuondoa mbegu zisizofaa, katika msimu wa kilimo wa 2019/2020 bodi ya pamba imesambaza mbegu aina ya UKM08 kwa wakulima wote wa pamba nchini kama ilivyokuwa kwa msimu uliopita na kusisitiza kuwa wakulima wanapaswa kuelewa hakuna aina tofauti za mbegu za pamba kwa sababu mbegu kabla haijapelekwa kwa wakulima, inakuwa imeshafanyiwa utafiti na kujiridhisha kuwa inafaa kwa hali ya hewa ya maeneo yote nchini.

Anasema hapa nchini hakuna aina tofauti tofauti za mbegu za pamba kwa sababu mbegu kabla haijapelekwa kwa wakulima, inakuwa imeshafanyiwa utafiti na kujiridhisha kuwa inafaa kwa hali ya hewa ya maeneo yote nchini.

Akitolea tathimini juu ya maendeleo ya sekta ya kilimo cha pamba na mwenendo wa uzalishaji wa zao hilo, kama unaendana na uwepo wa sera ya viwanda nchini, Mwalo anasema katika sera hii ya Tanzania ya viwanda kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa pamba ambapo pamba ya mbegu tani 112,362 iliyozalishwa katika msimu wa 2016/2017 umeongezeka hadi kufikia tani 350,485 kwa msimu wa kilimo 2019/2020.

Kuhusu mwendelezo wa kuyumba kwa bei ya pamba nchini kila mwaka, Mwalo anasema kuyumba kwa bei hiyo ni kwa sababu bei ya pamba nchini inaongozwa na mwenendo wa bei katika soko la dunia kwa sababu Tanzania ni mpokeaji wa bei na haina nguvu ya ushawishi katika suala la bei duniani. 

Aidha pamba yetu nyingi inauzwa nje ya nchi kama pamba ghafi, hivyo kuathiriwa sana na hali ya kushuka kwa bei ya pamba katika soko la dunia.

Alipoulizwa juu ya ushauri wake kwa wakulima ambao wengi wao wameonekana kukatishwa tamaa na kilimo cha zao la pamba kutokana na uchache wa wanunuzi na wengi wao kutokuwa na pesa ya kutosha kuwalipa wakulima wote.

Anasema tatizo kubwa lililojitokeza msimu uliopita si uchache wa wanunuzi bali kushuka kwa bei katika soko la dunia ambako pamba nyingi inayozalishwa nchini inauzwa.

Mwalo anasema kutokana na bei ya mkulima kuwa kubwa kuliko hali ilivyokuwa katika soko, benki zilisita kutoa mikopo kwa kampuni za ununuzi, hata hivyo bodi ya pamba haimlazimishi mkulima kuzalisha pamba, iwapo anaona mpunga ndiyo utakaommupa faida zaidi anao uhuru wa kuachana na pamba na kulima mpunga.