Home KIMATAIFA Mchango wa Cuba kuipindua Zanzibar ulivyoshindwa DRC

Mchango wa Cuba kuipindua Zanzibar ulivyoshindwa DRC

1623
0
SHARE

Na Joseph Mihangwa

JUHUDI za mmoja wa mashujaa wa Mapinduzi ya Cuba dhidi ya ubeberu wa Kimarekani, mzaliwa wa Argentina, “Ernesto” Che Guevara, za kujaribu kudidimiza ubeberu huo barani Afrika kwa staili ya Mapinduzi ya Cuba na yale ya Zanzibar mwaka 1964, ni mfano usioweza kusahaulika juu ya mshikamano wa “walalahoi” dhidi ya ubeberu.

Msaada wa Cuba ya Fidel Castro, iliotoa kwa harakati za ukombozi kwa nchi changa na zenye kuonewa Barani Afrika unazidi kipimo cha ukarimu, kisiasa na kijeshi kwa nchi za Algeria na Sahara Magharibi hadi Eritrea; Ethiopia, Zanzibar na kwa makoloni ya Kireno ya Guinea Bissau, Angola na Msumbiji.

Ushindi wa Cuba dhidi ya majeshi ya Makaburu wa Afrika Kusini nchini Angola mwaka 1975/76 na tena 1987/88 yalitia hamasa harakati za ukombozi na mafanikio nchini Namibia na hatimaye Afrika Kusini kwenyewe.

Juhudi za mwanzo kabisa za Cuba kutaka kusaidia harakati za Ukombozi Barani Afrika zilikwenda kwa Chama cha Ukombozi cha Algeria mwaka 1961, pale Fidel Castro alipotuma huko silaha nyingi na kubwa za kivita za Marekani zilizotekwa na wapiganaji wa Cuba nchini humo kufuatia uvamizi ulioshindwa wa “Bay of Pigs”.

Baada ya Algeria kujipatia uhuru mwaka 1962 kwa njia ya mapambano, ikarudisha hisani kwa kutoa mafunzo kwa vikundi vya “vita vya msituni” vya Ki-Argentina kutoka Algiers hadi Bolivia, Argentina mwaka 1963.

Miaka miwili baadaye, Cuba ilikuwa na vikosi tosha vya wapiganaji wa vita vya msituni kuweza kusaidia kwa njia ya kujitolea katika nchi zilizohitaji huduma hiyo. Che Guevara alikuwa mmoja wa waliojitoa mhanga kwa kazi hiyo na ambaye Novemba 7, mwaka huu [2018] anatimiza miaka 50 [nusu karne] tangu kuuawa kwake na mabeberu wa Kimarekani mwaka 1967 akitokea Congo baada ya jaribio la Mapinduzi lililoshindwa nchini humo.

Kipindi kufuatia kumalizika kwa vita ya pili ya Dunia hadi kushindwa kwa ubeberu wa Marekani kwenye vita ya miaka kumi nchini Vietnam mwaka 1975, kinajulikana kama zama za Mapinduzi na Ukombozi wa Mataifa.  Kilikuwa ni kipindi cha mitafaruku kutokana na kile ambacho Chama cha Kikomunisti cha China kilielezea kwa uhalisia kwa sentenso tatu fupi kuwa, “Nchi zinataka uhuru; mataifa yanataka ukombozi; watu wanataka Mapinduzi”.

Kipindi hicho kilishuhudia kuibuka kwa vijana wanaharakati wasomi na watetezi wa “mafukara wa dunia”, kwa maneno ya Franz Fanon katika kitabu chake “The Wretched of the Earth”, au kwa tafsiri ya Kiswahili cha Siasa za kiharakati, “Viumbe Waliolaaniwa”;  wakiuona ulimwengu umegawanyika katika dunia tatu, kwa maana ya dunia ya kwanza ya nchi tajiri zenye kukandamiza nchi masikini; dunia ya pili ya nchi zinazoendelea; na mwisho, dunia ya tatu ya nchi masikini za ukoloni mamboleo, zenye kunyonywa na kukandamizwa.  Muundo huu umedumu hadi leo, na ukatili wake umejionesha kwa upevu zaidi chini ya sera za “Utandawazi” ambazo dunia ya tatu imedakia bila kujielewa na kujikaanga kwa mafuta yake yenyewe.

Mapinduzi ya kiharakati nchini Cuba mwaka 1958, yaliyoongozwa na vijana wanaharakati wasomi, mashuhuri kati yao wakiwamo Fidel Castro na Che Guevara dhidi ya Serikali ya kibaraka wa Marekani, Fulgencio Batista kwa njia ya vita vya msituni yaliasisi mapambano ya ukombozi duniani kwa mtutu wa bunduki dhidi ya ukoloni na ubeberu wa nchi za dunia ya kwanza zikiongozwa na Marekani kuthibitisha usemi wa kimapambano kwamba, “Umma unapochoka na dhuluma, manyanyaso na kuonewa, hautishwi na nguvu ya majeshi”. 

Na ndivyo ilivyotokea Vietnam, kwamba, Marekani pamoja na nguvu zake za kijeshi kubwa kuliko za nchi yoyote duniani, haikufua dafu kwa dhamira ya Wavietnam ya kutaka kujikomboa.

Ni kwa dhamira hiyo ya Nchi kutaka uhuru, kwamba mwaka 1965, mkombozi na Kiongozi wa Cuba, Fidel Castro aliamua kupeleka Afrika kikosi cha wapambanaji kutoka Cuba kwenda kwenye eneo mojawapo tete na lenye kugubikwa na minyukano ya mataifa makubwa yaliyogombea utajiri na kielelezo cha ubeberu wa kimataifa barani Afrika wakati huo.

Eneo hilo liliitwa Congo (Leopoldville, sasa DRC), kwa lengo la kusaidia “Waasi” waliokuwa wakipambana na Serikali ya kibaraka wa Ubelgiji na Marekani, Joseph Kasavubu na baadaye dikteta, Jenerali Joseph Desire Mobutu ili kuupa somo ubeberu wa kimataifa.

Kikosi cha Guevara kilikusudiwa kuwa sehemu ya kile kilichoitwa “Jeshi la Ukombozi la Kimataifa la walalahoi” (International Proletarian Army), likiwa muungano wa vikundi vya kimapinduzi duniani kwa lengo la kukabiliana na ubeberu dunia nzima, na hasa ubeberu wa Kimarekani uliokuwa ukiibukia na kukomaza mizizi duniani katika kipindi hicho cha “vita baridi” kati ya nchi za kambi ya ubepari wa kimagharibi zikiongozwa na Taifa hilo, na nchi za kambi ya Usoshalisti/Ukomunisti za Mashariki, zikiongozwa na Urusi na China.

Kikosi hicho cha watu 120 kiliongozwa na yule shujaa wa Mapinduzi ya Cuba mzaliwa wa Argentina, Ernesto “Che Guevara”, baada ya kuchoka na maisha ya kivivu kama Waziri katika Serikali ya Castro na kutaka kutalii kunyoosha viungo katika ulimwengu wa harakati za mapambano.

Kabla ya kuongoza safari kuelekea Congo, Che Guevara alikwenda Algeria kupata ushauri wa Rais mwanaharakati wa nchi hiyo, Ahmed Benbella; China, kushauriana na Waziri Mkuu Chou En Lai; na Misri kupata ushauri wa Rais Mwanamapinduzi, Gamal Abdel Nasser, akasema, “Kwa vyo vyote vile lazima nitinge Congo kwa sababu ni eneo tete duniani kwa sasa… nadhani tutawanyuka mabeberu kwenye kitovu cha maslahi yao Jimboni Katanga”.

Kabla ya yote, Che Guevara, alitembelea nchi kadhaa za Kiafrika kimkakati, zikiwamo Algeria, Mali, Congo Brazaville, Senegal, Dahomey, Misri na Tanzania.

Mjini Dar es Salaam, alikutana na mmoja wa Viongozi wa waasi na mpiganaji, Laurenti Desire Kabila wakafanya mazungumzo. Kabila alitaka msaada kuimarisha ulinzi maeneo yaliyokombolewa ya Kongo Mashariki na Kongo Kusini Mashariki.

Mjini Cairo, alikutana na Gaston Soumialot aliyeomba msaada wa Askari na fedha kuimarisha mapambano; na mjini Brazaville alikutana na Agostinho Neto wa Chama cha Ukombozi wa Angola – The Peoples’ Movement for Liberation of Angola [MPLA] aliyemwomba msaada wa kuimarisha Jeshi la Chama hicho. Kwa ziara hiyo, Che alihamasika.

Februari 1965, Che alikwenda Beijing, China kuomba msaada kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kusaidia waasi wa Kongo. Alikutana na Waziri Mkuu Chou En Lai ambaye tayari alikuwa ametembelea nchi kadhaa za Kiafrika kati ya Desemba 1963 na Februari 1964. Baada ya hapo Chou alitembelea kwa mara ya pili Algiers [Algeria] na Cairo alikokutana na Viongozi wa wapigania uhuru wa Kongo.

Mkakati wa kuingia Kongo ulikuwa kama ifuatavyo: Vikosi vya wapiganaji wa Ki-Cuba vingesafiri kwa makundi madogo [small detachments] kwenda Tanzania na baadaye kuingia Kongo kwa kuvuka Ziwa Tanganyika na kuwasili Katanga Kaskazini kwa mapambano.

Kapteni Victor Dreke, Mcuba mwenye asili ya Kiafrika angeongoza kikundi cha wapiganaji wa msituni 120 akiwamo Guevara mwenyewe. Jorge Risquet Valdes Santana, mpiganaji na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha Cuba, alipangwa kuongoza “Batalioni” Patrice Lumumba Aprili 1, 1965.

Baada ya kikao cha mwisho na Fidel Castro mjini Havana, Cuba, Guevara aliondoka kwa ndege na kikosi kidogo tangulizi kwenda kwanza, Moscow, Urusi, kisha Cairo na baadaye Dar es Salaam.

Kwenye uwanja wa ndege wa Dar Es Salaam, alilakiwa na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Pablo Rivalta, Aprili 19, 1965. Akiwa Jijini Dar es Salaam, Guevara, alifanya mazungumzo ya mwisho na Kabila na Soumalioti kabla ya safari kuanza.

Jimbo la Katanga liligombewa na mataifa ya Ulaya kwa utajiri wake wa madini, ambapo mwaka 1961 lilifikia kujitenga kutoka Serikali ya Congo iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa kwanza, Patrice Emery Lumumba na kuwa chini ya kibaraka wa Wabelgiji, Moise Tshombe. Kuuawa kikatili kwa Lumumba mwaka 1961 kwa msaada wa Shirika la Kijasusi la Marekani [CIA] kulitokana na Kiongozi huyo mzalendo wa Afrika kujipambanua na upande wa nchi za Kikomunisti katika mgogoro huo wa Congo, na kibaraka wa nchi za Magharibi, Mobutu kuchukua madaraka.

Hata yule jasusi mkubwa wa CIA, kitanzi cha Wakomunisti Congo na nchini Portugal aliyepewa jina la “The Hangman of Portugal” – Mnyongaji wa wazalendo nchini Ureno”, Frank Carlucci, alipelekwa Zanzibar mwaka 1964 akitokea Congo yenye matata [baada ya Portugal] kwenda kuratibu na kusimamia mchakato wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar kwa shinikizo la Marekani na Uingereza zilizohofia Zanzibar ya Mapinduzi kuangukia kambi ya nchi za Kikomunisti.

Nasser, aliyetawala Misri kwa kumpindua Mfalme Farouk mwaka 1958, alimuonya Guevara na kumtahadharisha juu ya hatari kwa yeye kujigeuza “Tarzan” wa kingano asiyeshindwa, Mzungu mweupe kati ya watu weusi, akiwaongoza na kuwalinda badala ya kuwapa mafunzo na ujasiri waweze kupigania uhuru wenyewe dhidi ya adui.

Kuna tetesi na hisia zisizothibitishwa kwamba Che Guevara alishiriki ama kupanga au katika mapambano ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 kwa upande wa kikosi cha wanaharakati wa Kikomunisti wa Umma Party [UP] ambao wengi wao walipata mafunzo ya Kijeshi nchini Misri na Cuba. Uvumi wa aina hiyo ulikuwa hai siku ya Mapinduzi kwa duru za Kibalozi Visiwani, wageni na wapita njia walionukuliwa wakisema waliwaona Wacuba [wenye madevu]; au kwamba walisikia wapambanaji hao wakiongea Kihispaniola.  Kama hilo halikuwa kweli, basi bila shaka watu waliokuwa wakiongelewa ni wale vijana wa Abdulrahman Babu wa Umma Party, wahitimu wa mafunzo ya Kijeshi kutoka Cuba, waliorejea nchini Zanzibar wakiongea lugha ya Kihispaniola kwa ufasaha mkubwa.

Tukio lingine linalofanya watu wafikirie Che Guevara alikuwa na mkono wake katika Mapinduzi ya Zanzibar ni ziara yake mwaka mmoja baada ya Mapinduzi, Februari hadi Aprili 1965 wakati huo akijiandaa kuelekea Congo.

Uzito wa ziara yake Visiwani haukuwa wa kawaida kwani ingawa sherehe za kwanza za Mapinduzi Visiwani zilitakiwa kufanyika Januari 12, 1965,  ziliahirishwa hadi Februari 12, 1965 pengine kumsubiri awasili kwa ziara ya siri Visiwani Februari 11, 1965 ili ashiriki kwa siri siku inayofuata.

Rais Abeid Amani Karume alimpokea kwa bashasha kubwa na kumkabidhi kwa Ali Sultani [Mhitimu wa Mafunzo ya Kijeshi Cuba, 1962] akisema:  “Sikiliza Ali! Nakukabidhi mgeni huyu, “Comrade” mwenzenu uwe naye wakati wa ziara yake hapa Zanzibar na umhudumie vizuri”. Che alipewa kwa siri kubwa nyumba ya kulala na ulinzi madhubuti pale Beit-Ras hadi alipoondoka kwenda Dar Es Salaam akiwa njiani kuelekea Congo kwa mapambano.

Jambo ambalo Karume hakuelewa ni kwamba, Che na Ali Sultani walikuwa wanajuana tangu mwaka 1961 kule Cuba wakati Chama cha kiharakati cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kilipofungua Ofisi Havana, Cuba; na tena mwaka mmoja baadaye, pale Ali na wanaharakati wenzake wa ZNP walipokwenda mafunzoni nchini humo mwaka 1962 kabla ya kujiengua ZNP pamoja na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Babu mwaka 1963 kuunda Umma Party, kilichoshiriki Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Usiku wa Februari 12, 1965, Che alikutana na Makomredi waliokuwa Cuba 1962 katika karamu maalum iliyoandaliwa na kufanyika nyumbani kwa Ali Mahfoudh eneo la Migombani.  Waliokuwepo ni pamoja na Ali Mahfoudh mwenyewe, Mohamed Ali Foum, Ali Abdullah Bafaki, Salim Ali Ahmed Salim na wengine. Kanali Mahfoudh ndiye alikuwa Mkuu wa kwanza wa Jeshi la Ukombozi la Watu wa Zanzibar (Zanzibar People’s Liberation Army) – ZPLA kufuatia Mapinduzi.

Che alisikitika kuwakosa baadhi ya Makomredi, kama Amour Dugheish, Salim Saleh, Hashil Seif Hashil, Ali Mshangama na wengine ambao wakati huo walikuwa mafunzoni nchini Urusi na Indonesia.

Ziara ya Che Guevara Visiwani ndiyo iliyoibua tetesi zilizonaswa na “vyanzo” vya Ubalozi wa Marekani mjini Dar Es Salaam kwamba, mpiganaji huyo alikuwa pamoja na Babu nchini Tanzania; lakini Mwalimu Nyerere akakanusha na kujifanya hajui kitu.

Kikundi cha waasi ambacho Guevera alidhamiria kukiunga mkono nchini Congo kiliongozwa na Gaston Soumialot, na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Waasi hao, mwenye umri wa miaka 26 tu wakati huo, aliitwa Laurent Desire Kabila (baba mlezi na aliyekuwa Rais wa tatu wa DRC, Joseph Kabila), Mbunge kutoka Katanga Kaskazini na msomi mhitimu wa Paris na Belgrade, aliyetarajia kuanzisha Serikali ya Kijimbo kwa  maeneo yaliyokombolewa Congo Mashariki. 

Guevara kwa upande wake, alitarajia kuyatumia maeneo hayo kwa mafunzo ya kijeshi si kwa waasi wa Congo pekee, bali pia kwa Vikosi vya Ukombozi kwa nchi za Kusini za Barani Afrika na zaidi kama ingebidi, kufanya Congo kuwa kitovu cha Ukombozi mpana zaidi.

Aprili 20, msafara wa magari matatu aina ya Mercedez Benz nyeusi, uliondoka Dar Es Salaam na kuvuka ziwa Tanganyika kwa mtumbwi na kuingia Congo, Aprili 24, 1965.

Alichokiona Che kwa Waasi kilikuwa cha kusikitisha na kukatisha tamaa: Jeshi la Kabila halikufunzwa, lilikosa nidhamu na halikupangika vizuri kwa kazi ya kivita. Lilijaa uhasama wa kikabila na masengenyo miongoni mwa wapiganaji wake na liliongozwa na Makamanda wasio na ujuzi, wenye kupenda anasa, ufuska  na maisha ya utulivu na salama kwenye nyumba za vileo, dansi na “vimwana” mjini Kigoma, badala ya kuwa mstari wa mbele kwenye uwanja wa mapambano!.

Muonekano wa Jeshi hilo, kwa jina la “Jeshi la Ukombozi la Wananchi” [People’s Liberation Army] – PLA, ulikuwa wa kukatisha tamaa pia:  lilikuwa jeshi tegemezi na la kinyonyaji, lisilotaka wala kupenda kufanya kazi, mafunzo na mazoezi; halikupigana ila kudai mahitaji na kufanyiwa kazi na wananchi jirani, wakati mwingine kwa shuruti na kwa ukatili mkubwa.

Kabila mwenyewe alionekana mara moja tu akifika na shehena ya pombe kali [whisky] na kuondoka kurejea Kigoma baada ya siku tano; vinginevyo alitumia muda mwingi kwa ziara za nje au kwenye makazi yake, Dar Es Salaam.

Akielezea kutofurahishwa na haiba na muonekano wa Kabila, Che Guevara alisema: “Amejaa umbeya wa kisiasa; ni mlevi kupindukia na dhaifu kwa wanawake, hana umakini wala ujasiri wa kimapinduzi”. Na pale kikosi cha Guevara kilipojitupa uwanjani kuwasaidia waasi hao, kilijikuta kikibakia pekee kwa Jeshi la Kabila kutimua mbio, Maafisa wao wakitangulia kwa woga na hofu; wakatelekeza silaha zao na kuwaacha majeruhi wajiokoe wenyewe. 

Kwa jinsi hii, Jeshi la Mobutu, lililojumuisha Askari wa kukodiwa, lilizidi kupata ushindi siku hadi siku kwa kuwanyuka Jeshi la “walevi” la Kabila.

Miezi saba ya mapambano nchini Congo haikuweza kumpa Che Guevara na kikosi chake matumaini ya ushindi ili kutimiza ndoto yake. Hivyo, kwa uchovu na kukata tamaa, alianzisha safari kurudi nyuma kuvuka Ziwa Tanganyika hadi Kigoma na kuwasili Dar es Salaam Novemba 1965 alikopumzika kwa miezi minne hadi Februari 1966.

Ndani ya chumba kidogo kwenye Ubalozi wa Cuba alikofikia, Che aliandika maneno yafuatayo kuelezea hisia zake: “Hii ni historia chungu ya kushindwa inayoumiza”. Aliondoka Dar es Salaam, Machi, 1966 kurejea Cuba kabla ya kwenda Bolivia kuongoza mapambano kama yale ya Cuba, ambako aliuawa vitani, Novemba 7, 1967.