Home Michezo Kimataifa Messi kufuta mkosi Copa America?

Messi kufuta mkosi Copa America?

1307
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

NI kweli Lionel Messi amekuwa kwenye kiwango cha juu kwa miaka zaidi ya 10 sasa akiwa na Barcelona lakini changamoto ya muda mrefu ni kushindwa kuipa taji timu yake ya taifa, Argentina.

Hiyo imekuwa ikimfanya apoteze mvuto kwa mashabiki wa soka nchini humo, wakifia hatua ya kumzomea mara kadhaa.

Safari hii, Messi na wenzake watakwenda nchini Brazil itakakofanyika michuano ya Copa Amerika. Ni mashindano ambayo wakati Argentina ikitwaa ubingwa kwa mara ya mwisho (1993), Messi alikuwa na umri wa miaka sita.

Kwa misimu miwili iliyopita ya mashindano hayo ya Kusini mwa Bara la Amerika, Argentina ilitinga fainali mara mbili lakini walipoteza zote.

Wakiwa wamepangwa Kundi B, Argentina watakuwa na kibarua kizito cha kuvuka viunzi vya Columbia, Paraguay na Qatar waliolikwa kushiriki.

Mtihani wa kwanza kwa Messi ni Juni 15, siku atakayoshuka dimbani kumenyana na Colombia, akiwa na kumbukumbu ya kufanya vibaya katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka jana.

Itakumbukwa kuwa hiyo ilisababisha kocha Jorge Sampaoli apoteze kibarua chake, nafasi ikichukuliwa na Lionel Scaloni, beki wa zamani wa kikosi hicho.

Baada ya kuvurunda katika fainali hioz za Kombe la Dunia, safari hii macho na masikio ya mashabiki wa kandanda kule Argentina yatasubiri kwa hamu kuona atakavyowaokoa.

Wengi watasubiri kuona mkali huyo atakavyoweza kuwabeba, ikizingatiwa kuwa aliumalia msimu uliopita akiwa ameipachikia Barca mabao 51 katika mechi 50.

Zaidi ya hapo, si tu aliibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha mfungaji bora wa La Liga, pia ndiye aliyekuwa kinara wa mabao kwa ligi zote kubwa barani Ulaya, ingawa aliambulia taji moja tu (Ligi Kuu).

Akiwa ndiye mchezaji alioyewafungia mabao mengi katika historia ya soka la Argentina, bila shaka mashabiki timu hiyo wanataka kuona atakavyokuwa daraja kwao kulibeba taji la Copa America, ambalo wamelisubiri kwa miaka 26.

Wakati hayo yakiwa kwa Messi, pia Sergio Aguero atambue kuwa haendi Brazil kutembea, bali kufanya kile ambacho amekuwa akikifanya akiwa na jezi za Manchester City.

Mashabiki wa Argentina wanajua wazi kuwa msimu uliopita ulikuwa mzuri kwake, akiingia wavuni mara 32 na kutoa ‘asisti’ tisa katika mechi 46 katika mechi za michuano mbalimbali.

Aguero aliipa Man City taji la Ligi Kuu kwa mara ya pili mfululizo, Kombe la Ligi, Kombe la FA, hivyo anatakiwa kuhamishia makali hayo akiwa mbele ya mashabiki wa Argentina kule Copa America.

Uzuri ni kwamba Messi na Aguero wanakwenda Brazil wakiwa na huduma nzuri ya kiungo aliye kwenye ubora wa juu kwa sasa, Giovani Lo Celso.

Kiungo huyo wa Real Betis aling’ara msimu uliokwisha hivi karibuni, ambapo licha ya umri wake mdogo wa miaka 23, alicheza mechi 45, akifunga mabao 16 na kutoa ‘asisti’ tano.

Sifa za mido wa kati huyo anayependa kushambulia, ni uwezo mkubwa wa kukokota mpira, akiwa pia ni mzuri wa kuwatoa mchezoni viungo wengine kwa rafu zake za kiufundi.

Lo Celso alikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa Betis msimu uliopita kutokana na uwezo wake wa kupiga mashuti ya mbali, hivyo huenda akaitikisa Copa America atakapokutana na Leandro Paredes katika eneo la kiungo.

Nyota wengine wanaoweza kuwa msaada kwa Messi kutimiza ndoto yake ya kuipa Argentina taji la mashindano hayo ni wazoefu Nicolas Otamendi, Angel Di Maria na Paulo Dybala.