Home Habari MFANYABIASHARA ADAKWAKWA TUHUMA ZA KUGHUSHI

MFANYABIASHARA ADAKWAKWA TUHUMA ZA KUGHUSHI

1393
0
SHARE

NA CHARLES MULLINDA

MFANYABISHARA kigogo anayetajwa kuwa na  ukwasi mkubwa, Iqbal Baghdad ametiwa mbaroni kwa makosa ya uhalifu wa kifedha ikiwemo kughushi nyaraka za ardhi.

Taarifa za uhakika zilizolifikia RAI kutoka kwa watu walio karibu na Baghdad na kuthibitishwa na Jeshi la Polisi, zimeeleza kuwa mfanyabiashara huyo alikamatwa wiki mbili zilizopita na maofisa wa Polisi wa Kitengo cha Uhalifu wa Makosa ya Kifedha.

Vyanzo vya habari vilivyo karibu na Baghdad, vimelieleza RAI kuwa alikamatwa baada ya wafanyabiashara wenzake kutoa taarifa polisi kuwa ameuza kinyume cha taratibu eneo la Waislamu walilokuwa wameliendeleza kwa kujenga shule na nyumba za ibada.

Kwamba Baghdad aliliuza eneo hilo baada ya kutofautiana na wafanyabiashara wenzake aliokuwa akishirikiana nao kuendeleza eneo hilo kisha kuchukua fedha zote.

“Ni kweli amekamatwa, wafanyabiashara wenzake aliokuwa akishirikiana nao kuendeleza eneo kubwa kwa ajili ya shule na nyumba za ibada walimshtaki kwa kuwazunguka akauza eneo hilo kama mali yake wakati ni mali ya waislamu.

“Ukiacha hilo, lakini pia anatajwa kuhusika kwenye baadhi ya mambo ambayo yanawakera baadhi ya wafanyabiashara wenzake.

“Polisi walimchukua wakampeleka kwenye kituo chao cha Kamata wakamuhoji kisha wakampeleka Kituo cha Selander Bridge ambako alilala kwa siku tatu kisha akadhaminiwa. Hivi sasa anakwenda kuripoti kila siku asubuhi.

“Ruhusa rasmi ya kuliongelea suala hili haijatoka, lakini wiki ijayo njoo nitakueleza kwa undani kila kitu. Sasa hivi wewe labda watafute polisi watakuambia tuhuma zinazomkabili,” alisema mmoja wa watu wa karibu wa mfanyabiasha huyo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa Baghdad alisema hana taarifa.

“Niko safari, niko Dodoma, yupo aliyebaki nitakupa mawasiliano yake baadaye kidogo uzungumze naye hivi sasa niko kwenye position nyingine kabisa,” alisema Mambosasa.

Alipotafutwa baadaye kwa simu yake ya kiganjani, Kamanda Mambosasa alisema suala hilo linaweza kuzungumziwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Abdul.

“Hilo liko Ilala, ninakupa namba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Salum Abdul yeye anaweza kulizungumzia.

Alipoulizwa Kamanda Abdul kupitia simu yake ya kiganjani, alisema anayeweza kulizungumzia ni msemaji wa jeshi la polisi.

“Sikiliza nikuelekeza, kwanini nasema suala hilo linaweza kuzungumziwa na makao makuu. Kitengo cha Financial Crime Unit ambacho kiko pale Kamata ni kitengo kilicho chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ambacho ni sehemu ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

“Kwa hiyo mimi, Afande Mambosasa au kamanda yeyote wa zone hatuwezi kulizungumzia hilo, kwa hiyo mtafute msemaji wa jeshi, Barnabas Mwakalukwa ndiye anaweza kuwa na ufafanuzi au kulizungumzia hilo,” alisema Kamanda Abdul.

Msemaji wa Jeshi la polisi, Mwakalukwa alipoulizwa kupitia simu yake ya kiganjani alisema anayeweza kulizungumzia suala hilo ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.

“Kama alikuwa Selander basi wasiliana na DCI, na kama anaripoti Kamata wasiliana na huyo huyo au msaidizi wake, maana kama liko chini ya upelelezi wa makosa ya jinai, hayuko chini ya Kamanda wa Kanda Maalumu au Kamanda wa Polisi Ilala.

“Hilo moja kwa moja liko ngazi ya kitaifa kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai au Kamishna wa Upelelezi, yeye ndiye anajua na ndiye atakupa taarifa. Hawa wengine hata kama litakuwa chini ya himaya yao, lakini kwa maelekezo ya DCI ndiye anayeweza kukupa taarifa unazotaka hawa wengine hawawezi kuliongela hilo.

“Hata mimi siwezi kuliongelea kwa sababu lipo chini ya uchunguzi, na uchunguzi kama unafanyika na Mkuu wa Upelelezi Tanzania basi yeye ndiye ana jukumu hilo,” alisema Kamanda Mwakalukwa.

DCI Robert Boaz alipozungumza na RAI kuhusu kukamatwa kwa Baghdad, kwanza alisema yuko kwenye kikao atafutwe baadaye na alipotafutwa tena alielekeza atafutwe Jumanne, Agosti 28, asubuhi saa 2.00 ndiyo atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutoa taarifa.

Akizungumza na Rai juzi, Jumanne asubuhi, DCI Boaz, alisema mfanyabiashara huyo ni kweli amekamatwa kwa makosa ya kughushi nyaraka.

“Amekamatwa kwa makosa ya kughushi nyaraka, anatuhumiwa kughushi nyaraka mbalimbali zinazohusiana na mambo ya ardhi. Inatosha kusema kuwa tunaye, anatuhumiwa na watu walioleta malalamiko kwamba ameghushi nyaraka, sasa upelelezi ukikamilika kama atapelekwa mahakamani taarifa nyingine mtazipata huko.

“Sisi tukianza kueleza kila kitu sasa tutafungua milango ya watu wengine kuharibu upelelezi wetu,” alisema DCI Boaz.