Home Afrika Mashariki MGOGORO MKUBWA WA KIKATIBA WAINYEMELEA KENYA

MGOGORO MKUBWA WA KIKATIBA WAINYEMELEA KENYA

2757
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Kenya polepole inaelekea kwenye mgogoro mkubwa wa kikatiba baada ya kuzidi kuzorota kwa hali ya sintofahamu ilyopo baina ya wagombea wawili wa urais kuhusu namna ya kufanikisha uchaguzi wa marudio.

Mahakama ya juu ya nchi hiyo iliagiza kurudiwa kwa uchaguzi baada ya kugundua dosari kubwa kutokana na ukiukwaji wa kanuni na sheria katika uendeshaji wake uchaguzi wa mwezi uliopita.

Pande zote mbili zimekuwa zikishikilia misimamo yao bila kuyumba. Kuanzia mapema wiki hii Raila Odinga (NASA) aliitisha mandamano makubwa akidai kufumuliwa kwa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kabla ya uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao Oktoba 26.

Kwa upande wake chama cha rais Uhuru Kenyatta (Jubilee) kinapinga mabadiliko yoyote kwenye Tume hiyo kikisema upigaji kura lazima ufanyike chini ya watendaji hao hao wa Tume.

Msuguano huu unapandisha hatari ya uwezekano wa uchaguzi wa marudio kutofanyika, hali ambayo kufuatana na Katiba siyo tarajiwa kwani itakuwa haina maelezo ya cha kufanya.

Wadadisi wa mambo ya siasa wanasema iwapo pande mbili hizo sitashikilia misimamo yao mikali, kutazuka mgogoro wa kikatiba, kwani ni muhimu kwa wadau wote wa siasa waonyeshe utulivu kwa kutambua kwamba Kenya haitakubali michezo hii ya wanasiasa kuathiri amani iliyopo.

Hali ya sintofahamu kuhusu uchaguzi wa marudio umewatia wasiwasi wawekezaji kuhusu mali zao zilizopo nchini huku sarafu ya nchi hiyo ikipoteza thamani yake kwa asilimia 0.3 dhidi ya Dola ya Kimarekani katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja.

Migogoro kadha iliyopita wakati wa uchaguzi ilikuwa inaibua ghasia, na kubwa zilikuwa zile ghasia baada ya uchaguzi wa 2007 ambao ulisababisha vifo vya watu zaidi ya 1,100 na zaidi ya 350,000 wengine kuyakimbia makazi yao.

Uchaguzi wa marudio unazidi kuweka wingu kwenye muonekano wa uchumi ambao hata hivyo ulikuwa unapungua na unahatarisha sifa ya nchi kama ni nchi yenye matarajio makubwa kwa wawekezaji katika Bara la Afrika. Kenya ni kitovu katika ukanda huu kwa makampuni kadha makubwa ya duniani yakiwemo CocaCola na General Electric.

Hata hivyo Tume ya Uchaguzi bado haijatangaza namna ya kujibu madai ya upinzani ya kuifumua tume, hasa watendaji wake waliohusika katika kuvuruga matokeo.

Vile vile tume hiyo bado haijajibu yale yaliyoandikwa katika hukumu ya kesi ile ya kupinga matokeo ambayo ilisomwa rasmi na Majaji wa Mahakama ya Juu wiki iliyopita. Hukumu hii iliitia hatiani Tume kwa kutangaza matokeo ya uchaguzi bila ya kuwapo kwa nyaraka sahihi.

Hivyo kuna wasiwasi kwamba maandamano ambayo upinzani wa NASA umeyaandaa yanaweza kuzidisha hai ya msuguano uliopo iwapo chama cha Jubilee kitatimiza vitisho vyake vya kuyapinguza mamlaka ya Mhimili wa Sheria.

Wakati Kenyatta amesema atatii uamuzi wa Mahakama ya Juu, aliilalamikia hukumu yake, na kuwafananisha Majaji wake kama ni watu “wahuni” na hukumu yao kuwa ni “mapinduzi ya mahakama.”

Wabunge wa Jubilee katika baraza la Senate wanapanga kufanya mabadiliko ambayo yakipita itakuwa vigumu kwa mahakama hiyo kubatilisha matokeo ya chaguzi.