Home Makala MGOGORO WA CUF UNAWEZA KUBADILISHA RAMANI YA KISIASA NCHINI

MGOGORO WA CUF UNAWEZA KUBADILISHA RAMANI YA KISIASA NCHINI

755
0
SHARE

NA HILAL K. SUED


IJUMAA iliyopita ya January 27, mwaka huu, ilitimia miaka 16 tangu historia ya nchi yetu kuinga doa kubwa kutokana na mauaji ya makumi ya wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), baada ya kupigwa risasi na polisi Chake Chake, Pemba wakiwa katika maandamano ya amani.

Kiukweli yalikuwa ni madoa mawili makubwa katika historia ya nchi yetu tangu uhuru – likijumlishwa na lile la nchi yetu kwa mara ya kwanza kuzalisha wakimbizi waliokwenda nchi jirani kukimbia vurugu za kisiasa.

Maandamano hayo ambayo yalidaiwa na mamlaka kuwa hayakuwa halali, yalikuwa na ujumbe wa kudai tume huru ya uchaguzi Visiwani humo baada ya utata uliojitokeza wakati na baada upigaji kura katika chaguzi zilizopita za 1995 na 2000.

Hakuna anayepinga kwamba CUF kimepitia katika misukosuko mikubwa, pengine kuliko vyama vyote tangu mfumo huu wa vyama vingi uanzishwe robo karne iliyopita.

Tangu awali kabisa chama hicho kilionekana kuwa tishio kubwa kwa utawala kwa sababu kilikuwa ni chama pekee cha upinzani kilichoweza kujigamba, wakati kinazaliwa, kuwa na mwonekano wa kitaifa wake; kufuatana na matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Kilikuwa ni muungano baina ya vyama viwili; Chama cha Wananchi kilichoasisiwa na James Mapalala kwa upande wa Bara na Kamati ya Kupigania Uhuru (KAMAHURU) cha Shaaban Khamis Mloo kwa upande wa Visiwani.

Hivyo vita kuu dhidi ya CUF ilikuwa ni upande wa visiwani ambako ndiyo ngome kuu yake na kutokana na mfumo wa muungano ulivyo, chama hicho katika kila chaguzi tangu 1995 kilikuwa kinajizolea viti vingi vya Bunge la Muungano kuliko chama kingine chohote cha upinzani.

Na vita hii dhidi ya chama hicho na madai ya kudhulumiwa katika chaguzi kilikuwa kinakiumiza sana chama hicho kwa upande wa bara, pia kupitia mbinu mbalimbali kama vile kukiita chama cha Kiisilamu, cha kigaidi na kadhalika, sifa ambazo chama hicho kilikuwa kinatumia muda mwingi kujisafisha nazo.

Na haya yalikuwa yanatokea baada ya kufifia nguvu za NCCR-Mageuzi ya Augustine Mrema kuwafanya wananchi wengi waliokuwa wakishabikia upinzani kuanza kuvutiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilichokuwa kinaanza kupata nguvu kubwa kwa upande wa bara.

Kama ilivyokuwa kwa NCCR-Mageuzi, Chadema nayo haikuwa na ufuasi wowote visiwani. Kama Waswahili wanavyosema: “Unapopanga yako, Mwenyezi Mungu naye hupanga yake.”

Kitu kikubwa kilichoibuka kutoka kwenye ‘majivu’ ya mchakato wa Bunge la Katiba mwaka 2014, badala ya Katiba yenyewe kupatikana ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ulioundwa baina ya vyama vinne vya upinzani – CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.

Kwa kiasi kikubwa mchakato wa Bunge la Katiba kiliirudishia chati chama hicho hasa pale kilipohusika sana katika kuanzisha UKAWA. Muungano huo ukageuka kuwa mateso makubwa kwa chama tawala.

Ni kitu kikubwa ambacho hakikutarajiwa kabisa na utawala wa CCM na hasa baada ya umoja huo kusema utaweka nguvu za pamoja katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuikabili CCM.

Na ndivyo ilivyokuwa na hivyo utawala wa CCM ulibidi urekebishe mikakati yake kwani sasa unapambana na umoja wa upinzani wenye nguvu bila kutarajia, pamoja na kuwepo kwa vizingiti kem kem chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa kuhusu kuungana kwa vyama katika chaguzi, vizingiti ambavyo vyama hivyo vilivizunguka angalau kwa gharama kubwa hasa katika kupoteza utambulisho (identity) wa baadhi ya vyama ndani ya umoja huo.

Na kikubwa zaidi kilichofanikishwa na UKAWA ni kuweza ‘kumteka’ kada maarufu wa CCM ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu ambaye alijiunga Chadema na kutangazwa na umoja huo kuwa mgombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Hii ilikuwa na maana kwamba vyama vingine katika umoja huo hawakuweka wagombea. Na mbinu hii ya kuachiana nafasi za kugombea pia zilihusu ngazi nyingine kama vile ubunge na udiwani.

Kampeni zilizotokea kufuatia hali hiyo zilikuwa za mtikisiko mkubwa sana na kuna wakati ilikuwa vigumu kujua ni mgombea wa chama kipi, baina ya yule wa CCM (John Magufuli) na yule wa Chadema.

Kila kitu kilikuwa kinaenda vizuri kwa upande wa upinzani lakini ghafla tu na wiki chache kabla ya uchaguzi, dhoruba kubwa ikaikumba umoja huo na kujiengua ghafla kwa viongozi mashuhuri wa umoja huo wakiwamo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye pia alikuwa mwenyekiti mwenza wa umoja huo. Wote wawili hao walitaja kutoridhishwa na ujio wa Lowassa ndani ya umoja huo na hapo hapo kupewa nafasi ya kugombea urais.

Na ni Profesa Lipumba huyu huyu ndiye aliyebuni jina hilo la UKAWA na baadaye kushiriki kikamilifu katika mikutano yote iliyolenga kwa vyama vinavyounda umoja huo kuingia katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Na kwa upande wa vyama husika hakuna kilichoumiza zaidi kama CUF kwa sababu Lipumba hakujiengua tu na kuishia (kama vile Dk. Slaa), bali aliamua kubadili msimamo huo na kutaka arejeshwe, kitu ambacho kimekivuruga chama hicho hadi kutishia uhai wake.

Kilichovuruga mambo zaidi ni pale Msajili wa Vyama alipoingilia kati mzozo huo na kumtambua Prof. Lipumba kama ndiye mwenyekiti halali pamoja na kujiuzulu kwake awali.

Profesa Ibrahim Lipumba ni mwanasiasa maarufu nchini na msomi aliyebobea katika masuala ya uchumi. Amekiongoza Chama cha Wananchi (CUF) kwa zaidi ya miaka 20 tangu 1995. Aidha, amegombea urais kupitia chama hicho mara nne; kuanzia uchaguzi wa mwanzo chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.

Na katika mara zote hizo ni uchaguzi wa mwaka 2000 na 2005 ndiyo alifanya vizuri kwa kuwa wa pili nyuma ya CCM baina ya wagombea kadhaa waliokuwamo katika kinyang’anyiro katika nafasi hiyo.

Kwa ujumla katika kipindi cha uongozi wake, CUF ilifika kileleni kiufuasi na kiumaarufu kati ya 2000 na 2005 na baada ya hapo, kama nilivyosema, kikaanza kupokonywa umaarufu na Chadema, ingawa kule visiwani CUF iliendelea kuwa chama tishio kwa chama tawala.

Hakuna haja ya kusema kwamba kitendo cha kujitoa dakika hizo za mwisho kilikifurahisha chama tawala na sitakosea iwapo nitasema viongozi wa chama hicho walikuwa wanaambizana: “Si unaona, wameanza kusambaratika.”

Hatua ya Profesa Lipumba kujiondoa katika uongozi wa chama hicho katika dakika za mwisho, ambapo uwepo wake ulikuwa muhimu na kuhitajika sana kupita wakati wowote wa harakati za upinzani hapa nchini, ulionekana na wengi kuwa ni usaliti.

Nasema hivi kwa sababu ya ile ‘timing’ kwani kwa namna chama tawala kilivyokuwa kinabanwa jinsi uchaguzi ulivyokuwa unakaribia, ilitakiwa ‘msukumo’ mmoja tu wa mwisho (one final heave) wa kipamoja kukiondoa chama hicho madarakani kupitia sanduku la kura.

Ni vigumu kufahamu kuondoka kwa Prof. Lipumba kutoka UKAWA kuliuumiza umoja huo kwa kiwango gani katika Uchaguzi Mkuu wa 2015; bara na visiwani.

Wiki iliyopita Prof. Lipumba alionekana kutaka suluhu na upande anaozozana nao unaoongozwa na Katibu Mkuu Seif Shariff, lakini alimjibu kwamba katu hakuna suluhu kwani alishajiuzulu.

Wachunguzi wa mambo wanasema kama kweli kuna mkono wa utawala nyuma ya mgogoro huu kwa lengo la kukidhoofisha chama hicho, basi huenda nalo likawageukia. Ramani ya siasa nchini inaweza kubadilika kwa kasi kubwa iwapo CUF itakufa kwa faida ya upinzani.

Kwanza wengi wanasema bila ya Maalim Seif hakuna CUF. Baada ya Lipumba kujiengua, Maalim Seif aliweza si tu kutuliza mambo, bali aliweza kuwaunganisha wana-CUF katika kuukabili vyema uchaguzi uliokuwa mbele yao.

Akaweka imani yake kubwa kwa UKAWA na hivyo CUF ikaweka historia nchini katika chaguzi za wabunge kwa kupata wabunge 10 Bara. Mwaka 2010 chini ya uenyekiti wa Lipumba, CUF ilipata mbunge mmoja tu Bara.

Na hata kule Unguja, safari hii CUF ilipata wabunge 9, kawaida yao miaka yote hupata wabunge wasiozidi watatu.

Hivyo basi kisiasa, inawezekana kabisa kwa Maalim Seif kuhama chama chake na kuhamia Chadema na kuwaambia wafuasi wake visiwani nao wafanye hivyo. Iwapo Edward Lowassa aliweza kuhama CCM na kuingia Chadema, Maalim Seifa anaweza pia kufanya hivyo. Hakuna kisichowezekana katika siasa.

Hii itamaanisha kwamba Chadema rasmi itakuwa imeingia Visiwani na inaweza ikawa kwa kishindo na hivyo kwa mara ya kwanza kinaweza kuwa chama halisi cha kitaifa (pan-territorial) kama ilivyokuwa kwa CCM na CUF huko nyuma.

Siasa ndiyo zilivyo, huwa hazina kile unachoweza kuita maajabu.