Home Makala miaka 19 bila nyerere

miaka 19 bila nyerere

1703
0
SHARE

 *Hakuna kiongozi wa kulinganishwa naye

 Na HILAL K. SUED

Jumapili ijayo – Oktoba 14, itatimia miaka 19 kamili tangu kututoka muasisi wa taifa hili na rais wake wa kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere – aliyefariki katika hospitali moja mjini London, Uingereza.

Daima siishiwi kushangazwa – kwamba kwa nini Mungu Mwenyezi anakuwa mbahili kwenye uzalishaji wa watu wazuri ili wawe viongozi katika Bara hili, watu wenye busara na uadilifu mkubwa, badala ya majambazi ambao kazi yao kuu baada ya kuingia madarakani ni kujilimbikizia mali, wao, wanafamilia wake na maswahiba.

Kweli kabisa ule usemi wa “Penye miti hukosa wajenzi.” Baada ya kulipa Bara letu utajiri mkubwa wa madini na maliasili nyingi, Mwenyezi Mungu akalikabidhi kwa maharamia wa Kimafia kuliongoza.

Pamoja na mapungufu yake mengi tu aliyokuwa nayo, mengine yakitokana na udhaifu wa kibinadamu, kitu kimoja kikubwa Nyerere alichowapatia Watanzania, ukiacha ukombozi wao kutoka kwa makucha ya ukoloni, ni heshima ya nchi yao mbele ya dunia. Sote tunakumbuka alivyokuwa anachukia udhalililashi wa aina yoyote dhidi ya wananchi wake.

Si mara moja au mbili amewahi kuwatimua wageni waliokuja kufanya kazi hapa au kuwekeza (yaani kufanya biashara — kama ilivyokuwa ikiitwa siku hizo) ilipobainika kwamba mgeni huyo alitukana, au kunyanyasa wanachi wazalendo. Mara kadha alifanya hivyo kwa kuwapa muda mchache – masaa 24 tu kuondoka.

Leo hii kitu kama hicho nadra sana, mgeni anayenyanyasa wananchi, mara chache hufanyiwa kitu chochote, sana sana wale wanaomtuhumu ndiyo huandamwa na pengine kufukuzwa kazi, iwapo ni wafanyakazi wa umma. Maelezo ni kwamba tusikimbize wawekezaji.

ALISISITIZA MAADILI YA UONGOZI NA YEYE KUWA MFANO

Lakini Mwalimu aliweza kulinda heshima ya mwananchi na kwa kiasi kikubwa aliweza kufanya hivyo kwa sababu yeye mwenyewe aliwaongoza wananchi wake kwa uadilifu mkubwa – hakuwa na, na wala hakutaka makuu, hasa katika kujilimbikizia mali.

Alifanya hivyo ili kutoa mfano kwa viongozi wenzake, na hata kusisitiza kwa kuwawekea miiko mikali ya uongozi chini ya Azimio la Arusha. Alijua kuwa mamilioni ya Watanzania bado walikuwa katika umasikini mkubwa na hivyo viongozi wakijiingiza katika kujilimbikizia mali, basi kuna uwezakano mkubwa kuwasahau hao wananchi.

Watanzania wengi bado wanayafahamu yote hayo, kwa wanaomkumbuka hakuna anayeweza sasa hivi kusema bila kutafuna maneno kwamba katika utawala wake Mwalimu alijilimbikizia mali. Hakuna. Kama wapo, ni waongo wakubwa, wanafiki waliokubuhu, wenye ajenda zao za siri. Yeye na familia yake waliishi maisha ya kawaida tu.

Binafsi nakumbuka kwa mara ya kwanza kabisa nilifika nyumbani kwa Mwalimu Msasani mwaka 1992 – wakati akiwa anaishi kama rais mstahafu. Wakati huo nilikuwa mwandishi katika gazeti la Kiingereza la Family Mirror, miongoni mwa magazeti ya kwanza yaliyoanzishwa baada ya tasnia ya upashaji habari kuruhusiwa kwa magazeti binafsi. Hivyo nilikuwa katika kundi la waandishi wa habari aliowaita kuzungumzia suala la hoja ya kuwepo kwa serikali ya Tanganyika ilioanzishwa na kikundi cha Wabunge kilichoitwa G55.

Baada ya kuandikisha majina yetu kwa mlinzi getini tulitembea kuelekea jumba la ghorofa moja umbali kama kama mita mia moja hivi. Lilikuwa jumba la kawaida tu — kama jumba lolote lile katika maeneo ya Magomeni, Ilala au Mwanayamala ambapo mpita njia hana sababu ya kulitupia macho mara mbili.

Wengi tulishtushwa kukuta hadhi ya nyumba ile – baadhi ya viyoo vya madirisha ya luva (louvre) vimevunjika, nyavu zake za kuzuia mbu zimechanika, huku rangi za kuta imepauka. Binafsi nikafikiri labda jengo hili ni la walinzi na wafanyakazi wa Mwalimu na kudhani kuwa makazi yake halisi yalikuwa nyuma ya jengo.

Fikra hizi zilifutika muda mfupi baada ya kukaribishwa kwenye veranda iliyotazamana na Bahari ya Hindi kwa mbali na kutokana na picha nilizokuwa nikiziona katika magazeti ya Daily News na Uhuru miaka ya nyuma, hapa ndipo ilikuwa sehemu alipokuwa akikutana na kuongea na viongozi mashuhuri duniani wakati wa uongozi wake.

Baada ya muda tukatangaziwa ujio wa Mwalimu. Punde tukamuona anateremka ngazi (stairs) kutoka ghorofa ya juu akifuatana na katibu muhtasi wake wa miaka mingi, Bi Joan Wickens, aliyekuwa na asili ya Uingereza, na msaidizi wake mwingine wa kiume.

Akatupa mikono wote, nami ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kupeana naye mkono na akatuashiria kuketi. Viti havikutosha na wengine kati yetu ilibidi tusimame. Aliketi katika kiti chake cha bembea (rocking chair) akiipa mgongo Bahari ya Hindi. Kuna baadhi yetu walipata bahati ya kukaa katika viti vya sofa kama vitatu hivi, viti ambavyo, pamoja na kile kiti chake cha bembea, vilikuwa vimechoka, na hali ilionyesha kulipaswa kuwepo kwa samani mpya.

Miaka ya nyuma watu mashuhuri duniani kama Henry Kissinger, Kenneth Kaunda, Gamal Abdel Nasser, Indira Gandhi na Fidel Castro waliwahi kukaa katika sofa hizo.

Baada ya kuketi mkutano ukaanza lakini mawazo yangu yalikuwa kwingine kabisa – nikijaribu kuyatuliza akilini yale niliyoyaona: Ilikuwaje mtu huyu maarufu, shujaa wa ukombozi wa Bara la Afrika, na ambaye hata baada ya kustaafu uongozi, tena kwa hiari yake mwenyewe aliendelea na umaarufu wake kwa kushikilia msimamo wake wa uongozi wa kimaadili na visheni yake ya ujamaa, kuridhika kuishi katika mazingira duni kama haya?

Na bila shaka mazingira kama haya ndiyo alikuwa akiishi hata wakati akiwa Rais, tabia inayoeleza jinsi Mwalimu alivyowapiku viongozi wengi sana duniani katika uadilifu na kujinyima. Kwa vipi alikataa maisha ya anasa, kitu ambacho angeweza kukipata wakati wowote kwa ishara ya vidole tu?

Wakati nikimsikiliza Mwalimu akitoa mashambulizi yake dhidi ya kikundi cha G55 ambao alisema walikuwa wanadhamiria kuuvunja Muungano (alisema labda hiyo itokee juu ya kaburi lake), mimi nilikuwa napandwa na hasira – kwa nini viongozi aliowakabidhi madaraka waliamua kuyatelekeza makazi ya Mwalimu katika hali hii?

Siku ya pili yake habari kubwa katika magazeti mengi haikuwa kuhusu kile Mwalimu alichokieleza kuhusu hoja ya “Tanganyika” bali ilikuwa ni kuhusu hali mbaya ya makazi yake. Ilikuwa ni aibu kwa serikali kuiacha nyumba ya rais mstahafu katika hali ile. Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi iliitikia kilio hicho na mara moja ikapeleka mafundi na vifaa kukarabati nyumba ya Mwalimu.

Matokeo ya ukarabati huo yalionekana mwezi mmoja hivi baadaye nilipotumwa na Mhariri wangu kwenda tena kumhoji Mama Wickens iwapo Mwalimu anakubaliana na uamuzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuipa Barabara ya Pugu (Pugu Road) jina lake — yaani ‘Julius Kambarage Nyerere Road.’

Mwalimu alikuwa Butiama lakini baada ya muda Mama Wickens (bila shaka baada ya kuwasiliana na Mwalimu kwa simu) akanijibu kwa kusema Rais mstaafu hataki jina lake lipewe jina la barabara au kitu chochote kile wakati akiwa bado hai.

Hivyo Halmashauri ya Jiji wakaondoa “Julius Kambarage” kwenye alama za barabara na kubakia “Nyerere Road” kwani wapo akina ‘Nyerere, wengine waliozaliwa hapa duniani. Aidha baada ya kukamilisha ujenzi wa wanja mpya wa ndege wa Dar es Salaam (Terminal 2) katikati ya miaka ya 80 kulikuwapo wazo kuupa jina lake. Alikataa kwa sababu hiyo hiyo, lakini baada ya kufa kwake hatimaye uwanja huo ulipewa jina lake.

Ukarabati huo wa makazi ya Mwalimu Msasani ndiyo ulikuwa wa mwisho kwani waombolezaji waliofika nyumbani kwake mara tu baada ya kufariki kwake mwaka 1999 walishangaa kuona nyumba ikiwa katika hali mbaya, mapazia yamechanika, rangi za kuta zimepauka n.k. na hapo hapo kuwaona mafundi wakiirekebisha hali hiyo.

Leo hii baadhi ya wakuu wetu wa nchi wanaishi katika maisha ya pepo na anasa kubwa – tofauti kabisa na hayo ya Mwalimu. Kuna baadhi wamejenga mabwawa ya kuogelea karibu na vyumba vyao vya kulala.

WANAFAMILIA WAKE WALIISHI KAMA WATANZANIA WENGINE

Aidha mapema miaka ya 70 nilipokuwa nafanya kazi Arusha kuna mtoto mmoja wa Mwalimu (sikumbuki vizuri ni yupi baina ya Makongoro na Madaraka) alikuwa akisoma shule moja ya hapo – Arusha School. Shule hiyo ilikuwa ya bweni na Mkuu wa Mkoa, wakati huo Abdul-Nuru Suleman (sasa marehemu) alihisi mtoto huyo anapata adha kuishi shuleni.

Aliamua kumhamisha na kumweka nyumbani kwake huku gari la serikali likimpeleka shuleni na kumrudisha kila siku. Mwalimu Nyerere alikuja kupata habari hizo na akamkaripia sana Mkuu huyo wa Mkoa na kumuamrisha kumrudisha bwenini mara moja kijana huyo.

Hivi ndivyo Mwalimu alivyokuwa – watoto wake walipata elimu humu humu nchini, kama watoto wa wananchi wengine. Leo hii, sababu kubwa inayotajwa ya kuzorota kwa elimu hapa nchini ni kwa wakubwa kuwapeleka watoto wao kusoma katika shule na vyuo binafsi vya gharama kubwa vikiwamo vya nje ya nchi. Katika hali hii wakubwa hawa hawajali sana matatizo yanayoikumba sekta ya elimu hapa na hivyo hawaoni umuhimu wa kuiboresha.

Mambo ni vivyo hivyo katika hospitali zetu na huduma za afya kwa ujumla. Hata wakati Mwalimu alipoanza kuugua, inasemekana alikuwa anapinga sana kupelekwa nchi za nje kutibiwa. Ingekuwa kuna uwezekano kwa Mwalimu kurudi katika uhai – ingawa kwa muda mchache tu, angeweza kuwakemea sana akina Mkapa kwa kumwachia kwenda kufia katika nchi ya Wazungu – tena wale wale aliopambana nao katika kudai uhuru wa wananchi wake ili wajikomboe kutoka katika ujinga umasikini na maradhi.

Angeona Wazungu hao wangemsuta kwa kumwambia: “Baada ya miaka karibu 40 ya uhuru, mmeshindwa kujikomboa katika maradhi hadi wewe mwenyewe unaletwa kufia huku kwetu?”

Manyerere Jackton, mwanafamilia mmoja wa Mwalimu ambaye sasa ni mwanahabari, na aliyewahi kuishi katika makazi ya Mwalimu ya Msasani miaka ya mwisho mwisho kabla ya kustaafu kwake aliwahi kunihadithia jinsi Mwalimua alivyokuwa hapendi makuu.

Manyerere alisema kwamba baada ya watu wengi kuanza kujenga majumba karibu ya eneo hilo, pressure ya maji ya bomba majumbani ilikuwa inapungua, kwa hivyo mara kadha maji yalikuwa hayapandi juu ghorofani. Mapema asubuhi moja Manyerere alikuwa jikoni akitayarisha chai na mara alimuona Mwalimu amesimama mlangoni ameshika ndoo huku amevalia bukta ndefu na singleti.

“Ee bwana eeh, leo tena maji hakuna kule juu na naona Waswahili wangu (akimaananisha wahudumu wake wa makazi yake juu ghorofani) bado hawajafika.”

Manyerere (alivyonihadithia) alimpokea ndoo na kumwambia arudi tu juu na kwamba atampandishia maji. Akamkingia maji katika ile ndoo na kumpandishia juu huku Mwalimu akimsubiri juu ya ngazi (stairs) ambapo alimpokea ndoo hiyo na kuingia nayo ndani. Mwalimu huyo!

INGEKUWAPO WAKAT WAKE ANGEIKWAA TUZO YA MO IBRAHIM

Miaka 12 iliyopita, mfanyabiashara maarufu wa Sudan, Mohamed Ibrahim, alianzisha Tuzo ya kila mwaka kwa viongozi wastahafu wa Barani Afrika waliojitokeza katika kusimamia (wakati wakiwa madarakani) uongozi uliotukuka na wa uadilifu, kudumisha utawala bora, kuwaendeleza wananchi wake, kutokumbatia ufisadi na kung’atuka kwa hiari na bila mizengwe kipindi chake cha utawala kilipomalizika.

Tuzo hiyo, yenye kiambatanisho cha pesa taslimu dola za Kimarekani milioni 5 ni tuzo kubwa kuliko zote zinazopewa mtu binafsi hapa duniani – kuliko hata ile Tuzo ya Nobel. Lengo lake ni kusisitiza utawala bora katika bara la Afrika, bara ambalo, kwa maneno yake mwenyewe Ibrahim, “limejaliwa kuwa na madini mengi ya kila aina kuliko mabara mengine yote, lakini zaidi ya wakazi wake bilioni 1.2 wanaishi maisha duni sana — chini ya dola moja ya Kimarekani kwa siku.”

Kwa tafsiri yoyote ile, Tuzo ya Mo Ibrahim ni ya heshima kubwa kwa kiongozi mstaafu katika Bara hili lakini kwa bahati mbaya wanaoonekana kutimiza vigezo na sifa za kupata tuzo hiyo ni wachache sana na ni viongozi wa zamani watano tu ndiyo wametunukiwa hadi sasa.

Tuzo hii ingekuwapo enzi zile Mwalimu angeikwaa bila pingamizi yoyote.

Kutokana na uchache huu tangu ianzishwe tuzo hiyo, ni viongozi wa zamani watano tu tu ndiyo walipata. Hii ni kwa sababu wengi wa viongozi siku hizi wanaweka masilahi yao na yale ya wanafamilia wao na maswahiba wao mbele kuliko masilahi ya wananchi waliowachagua.

Kuhusu ufisadi, hakika ulikuwapo tangu enzi za utawala wa Mwalimu lakini siyo katika kiwango cha miaka hii – na hasa tangu kufariki kwake. Kashfa kubwa za ufisadi kama vile EPA, Escrow na nyinginezo zilitokea mara baada tu ya kufariki Mwalimu.

Sote tunaikumbuka hotuba moja ya Mwalimu Nyerere kuhusu Ikulu na biashara. Na katika kuzingatia hilo, ndiyo maana Mwalimu, kimaadili, hawezi kulinganishwa na kiongozi yoyote mwingine baada yake.