Home kitaifa MIAKA 20 BILA NYERERE: Matishio 14 kiusalama yatajwa

MIAKA 20 BILA NYERERE: Matishio 14 kiusalama yatajwa

950
0
SHARE

MWANDISHI WETU

MIAKA 20 bila Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, taifa limepita katika changamoto kadhaa za kiusalama, ambazo vyombo vya ulinzi na usalama vimekabiliana nazo kulingana na wakati.

Akizungumzia suala la amani, ulinzi na usalama wa taifa letu, miaka 20 baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Kamanda wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi na Usalama wa Anga katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremi, amesema taifa linakabiliwa na matishio 14 makubwa ya usalama.

Mkeremi aliyekuwa akiwasilisha mada ya ulinzi wa taifa katika kumbukizi ya Mwalimu Nyerere, Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Oktoba 11 mwaka huu, alisema ni wazi kuwa miaka 20 baada ya kifo cha Nyerere, changamoto na matishio ya usalama yamebadilika tofauti na hapo awali, na kwamba hata dhana ya usalama nayo imepanuka zaidi, ambapo sasa inahusisha usalama wa watu.

Alizitaja changamoto za kiusalama kuwa ni kutokuwapo kwa Mwalimu, ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa na mambo mengine ndani ya nchi, ikiwamo uanzishaji wa ushindani wa vyama vingi, mwelekeo wa Muungano na uteuzi wa wagombea wa urais.

“Katika Afrika na dunia, aliheshimika kutokana na msimamo wake imara katika masuala yanayohusu Afrika. Baada ya kustaafu uongozi, alikuwa ni kisima cha busara, hasa tulipokuwa na agenda kubwa ya kitaifa.

“Ni wazi kifo chake kimeacha ombwe kubwa la kiuongozi, baba, mshauri na mwongoza njia wa taifa letu na dunia kwa ujumla,” alisema.

Mkeremi alisema kizazi kipya ni changamoto nyingine ya kiusalama katika taifa, kwa kuwa wale waliozaliwa baada ya kifo chake mwaka 1999 ambao sasa wana umri wa miaka 20, wale waliokuwa na miaka 10 ambao kwa sasa wana miaka 30 ambalo ni asilimia 66 ya Watanznaia wote hawajayaishi mawazo ya Mwalimu.

Alisema kizazi hicho ambacho kinaathiriwa zaidi na utandawazi, bado hakijui historia ya kweli ya taifa na wengi wamekuwa wakijijenga wenyewe, wakiwa na mashujaa wao, viongozi wao, historia yao na njozi yao ya taifa, kwa hiyo lisipoangaliwa vizuri ni tishio la usalama.

Mkeremi alisema changamoto ya tatu ni Muungano kutokana na mijadala inayotishia Muungano, ambayo si migeni kwa kuwa ilikuwapo hata wakati wa Mwalimu, ambapo kupanda na kushuka kwa joto la mijadala hiyo kunaonekana wazi kupitia hotuba na maandiko ya wanasiasa, wanaharakati, waandishi wa habari na wananchi wa kawaida.

Alisema suala hilo la mjadala kuhusu Muungano ambalo lilionekana kupata joto zaidi wakati wa mchakato wa Katiba Mpya, ni moja ya changamoto za usalama zinazoikabili nchi.

Mkeremi alisema mfumo wa vyama vingi vya siasa uliopitishwa mwaka 1992 umepanua wigo wa demokrasia nchini, na kwamba pamoja na uzuri wake, migogoro ya kisiasa katika nchi imeongezeka, hasa nyakati za uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali.

“Dhana ya uadui unaotokana na kutofautiana kiitikadi inazidi kuota mizizi. Kuna dalili za kupungua kwa uzalendo tokea mfumo wa vyama vingi kuanza. Hili nalo ni moja ya changamoto za kiusalama kwa nchi yetu,” alisema.

Alisema changamoto ya tano ni hisia za ukabila, rangi, udini na ukanda ambapo pamoja na juhudi zinazofanywa kumaliza hisia hizo, bado zinaweka mizizi katika taifa.

Alisema kwa upande wa dini, migogoro kati ya Wakristo na Waislamu imeongezeka kuliko ilivyokuwa awali, hivyo kuleta wasiwasi juu ya hali ya baadaye ya mahusiano ya kidini nchini.

Mkeremi ambaye alikuwa akimwakilisha Mkuu wa JWTZ, Jenerali Venance Mabeyo, alisema changamoto ya sita ni uharaka wa upashanaji habari unaochochewa na utandawazi, hasa matumizi ya intaneti.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka jana, asilimia 43 ya Watanzania walikuwa wanatumia mtandao wa intaneti na asilimia 48.77 waliokuwa wanatumia simu za mkononi walikuwa wakitumia intaneti.

“Mtandao wa intaneti umekuwa kiwezeshi kikubwa cha mawasiliano kwa sasa, hasa kupitia mitandao ya kijamii. Mitandao hiyo imekuwa njia ya kuaminika ya kubadilishana habari hususani kwa vijana wa miaka 18-35, ambao ni asilimia 75 ya watumiaji wa mitandao ya kijamii.

“Bahati mbaya imekuwa ni vigumu kudhibiti au kuhariri habari zinazosambazwa na mitandao hiyo, hivyo kusababisha changamoto ya usalama dhidi ya nchi yetu. Mitandao ya kijamii imeua mipaka kati ya nchi yetu na dunia.

“Ikumbukwe kwamba mitandao hiyo ndiyo iliyochagiza mafanikio ya mapinduzi katika nchi za Kiarabu (Arab Spring). Hata vurugu zinazotokea maeneo mengi duniani hupangwa na kuratibiwa kupitia mitandao ya kijamii.

“Takwimu zinaonyesha mitandao ya kijamii inakuwa tishio kubwa katika nchi zenye vijana wengi, ukuaji wa haraka wa miji, uhaba wa ajira kwa vijana na nchi zenye ongezeko kubwa la vijana wenye elimu,” alisema.

Mkeremi alisema changamoto ya saba ni ukosefu wa ajira, ambapo kwa Tanzania kila mwaka zaidi ya watu 900,000 huingia katika soko la ajira, wakati fursa za ajira zikiwa ni kati ya 500,000 hadi 600,000 kwa mwaka.

Alisema viwango vya juu vya ukosefu wa ajira kwa vijana ambao wengi ni wenye elimu, huchochea ushiriki wao katika uhalifu na kuwafanya kuwa rahisi kujiunga na makundi ya uhalifu.

Changamoto ya nane, kwa mujibu wa Mkeremi ni migogoro ya ndani katika nchi jirani zinazopakana na Tanzania, ambazo kutokana na historia zao bado hazijapata amani ya kudumu hadi sasa.

“Kutokana na hali hiyo, Tanzania inakabiliwa na madhara yanayotokana na migogoro ya ndani ya jirani zetu. Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi kutoka katika nchi hizo wanaokimbia mapigano, ambao wamekuwa moja ya vyanzo vya uvunjifu wa amani,” alisema.

Alisema changamoto ya tisa ni ugaidi, siasa kali na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu kutokana na kuathiriwa na mashambulizi ya kigaidi ya mwaka 1998, wakati kundi la al-Qaeda lilipolipua ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, lakini pia uwepo wa biashara haramu unaendelea kuwa tishio kwa usalama wa nchi.

Mkeremi alisema tishio jingine ni changamoto zinazoletwa na maendeleo kutokana na miradi inayoendelea kujengwa nchini, kama ilivyo kwa kituo cha kuzalisha umeme wa maji huko Rufiji, bomba la mafuta la Tanga-Hoima, ujenzi wa miundombinu, ambayo inahitaji ulinzi unaohusisha watu, zana, vifaa vipya vya teknolojia na kwa kuwa baadhi ya mataifa makubwa hayafurahii miradi hiyo, inaleta wasiwasi wa kiusalama.

Alisema suala la ukuaji wa miji ni changamoto ya 11, ambapo tafiti zinaonyesha ukuaji wa miji na kuongezeka kwa taasisi za elimu ya juu ulikuwa ni moja ya kichocheo cha mapinduzi katika nchi za Kiarabu, na kwamba ukuaji wa miji una uhusiano wa moja kwa moja na kuongezeka kwa shughuli za kihalifu katika jamii, hivyo kuwa tishio kwa usalama.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni ongezeko la idadi ya watu, jambo ambalo husababisha changamoto katika utoaji wa huduma za jamii, lakini pia kuwapo kwa hali mbaya ya lishe, na kwamba watoto wanne kati ya 10 chini ya miaka mitano wamedumaa, hivyo kushindwa kukua na kuwa wazalishaji mali wa kutegemewa hapo baadaye, hivyo kutishia ukuaji wa uchumi na kuwa tishio la usalama.

Kwa mujibu wa Mkeremi, tishio la 13 ni changamoto za rasilimali za kuchangia zinazosababisha uwezekano wa kuzuka kwa migogoro baina ya Tanzania na nchi nyingine zinazochangia matumizi ya rasilimali, kama ilivyo matumizi ya Mto Nile, mpaka wa Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa na matumizi ya maji ya Ziwa Voctoria na Ziwa Tanganyika.

Alisema tishio la 14 linaweza kuwa magonjwa, hasa yale ya milipuko ikiwemo dengue, ebola na pia migogoro kati ya wakulima na wafungaji, wahamiaji haramu, mabadiliko ya tabia nchi na uhalifu wa kimtandao.

Mkeremi alisema kutokana na changamoto na matishio hayo, JWTZ ambayo imepewa dhamana ya kuhakikisha usalama wa mipaka, kulinda masilahi ya nchi, kulinda uhuru na usalama wa watu, linaendelea kuziainisha na kuongeza majukumu yake kutokana na misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa, Mwaliku Julius Nyerere kwa kuzingatia changamoto za wakati.