Home Latest News MIAKA 20 YA MAKUBALINO YA IJUMAA: UTULIVU WAANZA KUTOWEKA IRELAND YA KASKAZINI

MIAKA 20 YA MAKUBALINO YA IJUMAA: UTULIVU WAANZA KUTOWEKA IRELAND YA KASKAZINI

6287
0
SHARE
Kutoka kushoto: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Ireland Bertie Ahern, Seneta wa zamani wa Marekani George Mitchell, Seamus Mallon, David Trimble and Gerry Adams katika picha ya pamoja kuadhimisha miaka 20 ya Makubaliano ya Good Friday mjin Belfast mwezi ukipita.

 

NA HILAL K SUED   |

Wakati wa utawala wake, haikuwa siri kwa kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi kuvipa msaada wa kifedha vikundi/vyama mbali mbali vilivyokuwa vinapigania uhuru katika sehemu mbali mbali duniani.

Vilivyonufaika na misaada huo ni pamoja na Palestine Liberation Organisation (PLO) cha Mashariki ya Kati, Moro Liberation Front (MLF) cha jimbo la Mindanao la Ufilipino, na Irish Republican Army cha Ureland ya Kaskazini ambalo ni jimbo la Uingereza (UK). MLF ni kikundi cha wapiganaji Waisilamu wanaopigania kujitenga jimbo lao – kisiwa cha Mindanao kutoka utawala wa Ufilipino.

Lakini kilichowashangaza wengi ni msaada wake kwa IRA kwani wale si Waisilamu, bali ni Wakatoliki wanaotaka kujitenga kwa jimbo hilo na kujiunga na Jamhuri ya Ireland (Ureland ya Kusini. Hata huvyo jibu alikuja kulitoa mwenyewe Gaddafi.

Akiwa ziarani nchini Algeria aliwahi kuulizwa na wandishi wa habari kwa nini serikali yake ilikuwa inakisaidia kifedha kikundi hichi ili hali siyo Waisilamu? Alijibu: “Hawa wakoloni wamezoea kuleta chokochoko zao uwani kwetu, nami napeleka chokochoko uwani kwao. Kama wao wana haki ya kufanya hivyo nami pia ninayo haki hiyo.”

Nimeoma umuhimu kuweka utangulizi huu kutokana ukweli kwamba wengi hawakuwa wanafahamu kwamba pamoja na Uingereza kujiingiza kijeshi katika nchi kadha duniani – kama vile Iraq, Afghanistan, Visiwa vya Falklands, Sierra Leone na kwingineko, kwa lengo wanaloita “kuweka hali ya utulivu” katika nchi hizo, nchini kwake kwenyewe, kwa miongo mingi imekuwa ikihangaika kufanya hivyo hivyo katika jimbo lake moja, tena kwa ukatili mkubwa, iwapo ukiisoma vyema historia yake.

Jimbo la Ireland ya Kaskazini ambalo liko katika kisiwa cha Ireland, magharibi mwa Uingereza, lilimegwa na kubakizwa katika himaya ya Uingereza mwishoni mwa mwaka ya 1940 pale utawala wa London ulipotoa uhuru na kuundwa kwa Jamhuri ya Ireland kupitia sheria ya Bunge (la London) Republic of Ireland Act 1949.

Kisingizio kikubwa cha kulimega jimbo hilo ni kwamba eneo hilo lilikuwa na wakazi wengi wa madhehebu ya Kiprotestanti (madhehebu ya Malkia wa Uingereza) kuliko Wakatoliki ambao ndiyo wengi katika Jamhuri ya Ireland (Ireland ya Kusini).

Chama cha IRA ambacho kilikuwapo tangu miaka ya 1920 kimekuwa kikiendesha mapambano dhidi ya utawala wa London tangu wakati huo na kilizidisha harakati zake katika miaka ya 1960 na lengo lake kubwa ni kujiunga na Jamhuri ya Ireland. Utawala wa London umekuwa ukifanya kura ya maoni kwa wakazi wa jimbo hilo na kila mara matokeo ni kwamba wakazi wengi hupenda kuwa chini ya Uingereza iliyopo London.

Ghasia nyingi zimekuwa zikitokea, tangu zile kubwa za 1969 ambapo serikali ya London ilituma majeshi kulinda amani baina ya jamii mbili za huko (Wakatoliki na Waprotestanti) na wengi walipoteza maisha yao, na kupelekea kwa serikali hiyo kukipiga marufuku kikundi hicho cha IRA.

Ghasia hizo zilivuka mipaka na kuingia Uingereza kwenyewe ambako wapiganaji wa IRA walifanya vitendo vya kigaidi vya ulipuaji mabomu katika sehemu mbali mbali jijini London na katika miji mingine katika azma yao ya kutaka Uingereza iondoe majeshi yao kutoka jimbo hilo.

Na wakati huo huo jitihada mbali mbali za usuluhishi zimekuwa zikifanyika kumaliza mzozo huo wa muda mrefu na miaka 20 iliyopita (mwaka 1998) siku ya Ijumaa Kuu tarehe 10 Aprili kulitiwa sahihi makubaliano yanayoitwa “Good Friday Agreement” mjini Belfast.

Hivyo baada ya miaka 30 ya ghasia ambazo zaidi ya watu 4,000 waliuawa vikundi mbali mbali vya kisiasa vilikubaliana kuachana na ghasia na kufanya kazi pamoja ili kutatua mizozo yao kwa njia za kidemokrasia.

Makubaliano hayo yalitokana na mchakato wa kupatikana amani na ndiyo uliyozaa serikali ya ugatuzi ya sasa. Aidha makubaliano hayo yalianzisha taasisi kadha baina ya jimbo hilo na Jamhuri ya Ireland kwa upande mmoja na baina ya Jamhuri ya Ireland na Uingereza kwa upande mwingine.

Hata hivyo wakati makubaliano hayo yametimiza miaka 20 mwezi uliopita tangu kusainiwa, Ireland ya kaskazini bado imegawanyika, ingawa wachunguzi wa mambo wanaona kuna uwezekano mkubwa wa kuungana kwa kisiwa kizima cha Ireland kuwa na serikali moja.

Wanasema hili linatokana na hatua ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya (EU) mwaka 2016, hatua inayotajwa kwamba itayaathiri sana makubaliano yale ya 1998.

Makubakliano hayo yalianzisha Bunge la pamoja na wakati wale wanaopendelea kubakia chini ya utawala wa London (Unionists) walihakikishiwa utambuzi wao kwa Uingereza, wakati wale wanaotaka kujiunga na Jamhuri ya Ireland (Republicans) nao pia walihakikishiwa lengo hilo kama ni halali. Asilimia 71 ya wakazi wa Ireland ya Kaskazini walipiga kura ya maoni kuridhia makubaliano hayo katika kura ya maoni iliyofanyika.

Hata hivyo katika kipindi hiki cha miaka 20 hali ya utulivu bado haijapatikana na bado vipo vikundi vya wapiganaji vinavyoendesha mapambano ingawa kichinichini.

Hata upigaji kura katika uchaguzi wa jimbo hilo umebadilika katika kipindi hiki. Wakati wa kutiwa sahihi makubaliano hayo mwaka 1998 kiongozi wa chama cha Ulster Unionist Party (UUP) David Trimble mwenzake wa Social Democratic and Labour Party (SDLP) John Hume walitunukiwa tuzo ya Amani ya Nobel kwa jitihada zao za kufanikisha suluhu.

Hata hivyo wapigakura wamehama na kufuata siasa za msimamo mkali zaidi. Kiongozi wa DUP Mchungaji Ian Paisley na ambaye ni mtiifu wa kupindukia kwa utawala wa London alikipiku chama cha UUP, wakati chama cha Sin Fein (mkono wa kisisa wa IRA) na ambacho hakiyumbi katika azma ya kuungana na Jamhuri ya Ireland, kimekirithi chama cha SDLP.

Hata hivyo tangu miezi 12 iliyopita, jimbo hilo la Ireland ya Kaskazini lilijikuta halina serikali baada ya Naibu wa Kwanza Martin McGuinness kujiondoa pamoja na mawaziri wake kutoka serikali ya pamoja kutokana na sintofahamu kuhusu mradi mmoja wa nishati.

Kuvunjika kwa hali ya kuaminiana kati ya chama tawala cha Nationalist na kile cha Unionist kunaendelea kukosa ishara yoyote ya suluhu hadi sasa.

Kwa kuwa uungwaji mkono wa kambi zote mbili unahitajika ili sheria mpya ziweze kutungwa, hakuna shughuli yoyote za kibunge zinazoendelea ndani ya Bunge hilo – Stormont Assembly mjini Belfast

Hivyo bajeti ya jimbo hilo la Uingereza ililazimishwa kutoka serikali ya London, huku shughuli nyingine za kila siku za serikali zikifanywa na watumishi wa umma.

Hali ya namna hii inaonekana si ya kawaida lakini kutokuwepo kwa uongozi wa kisiasa hakujaweza kusababisha kuporomoka kwa huduma za jamii na wananchi wanaendelea kafanya shughuli zao kama kawaida.