Home Makala Miaka 21 ilitosha Mfalme Alexander kuitawala dunia

Miaka 21 ilitosha Mfalme Alexander kuitawala dunia

1394
0
SHARE


NA GAMANYWA LAITON

AFYA yake ilikuwa imezorota ndani ya wiki mbili, mwili wake ulikuwa katika maumivu, kulikuwa na mkanganyiko juu ya ugonjwa wake na kile kilichokuwa kikimsumbua kwa muda mfupi huo. Homa kali iliyokuwa na dalili zote za ugonjwa wa maralia ilikuwa imemdhohofisha, japo baadaye kuna wengine walikuja kugundua kuwa mfalme alikuwa amepewa sumu iliyokuwa imechanganywa katika kikombe cha mvinyo.

Baada ya homa kuzidi, mfalme akafariki dunia katika umri mdogo wa miaka 32, lakini akiwa tayari ameshinda kila miliki duniani, kila jemedari wa jeshi, kila pigano na vikwazo vilivyowashinda watangulizi wake. Huyo hakuwa mwingine ila Alexander maarufu kwa jina la Alexander Mkuu (Alexander the Great).

Mmoja kati ya Mfalme kijana, Jemedari wa Vita na Kiongozi wa kisiasa aliyeacha alama na historia ambayo haijapatwa kufananishwa na mtu mwingine yeyote ambaye anaweza kulingana naye kwa aina ya yale aliyoyafanya kwa muda mfupi alioishi duniani.

Ili kumwelewa Alexander ni muhimu kwanza kuwaelewa watu watatu waliochangia kumtengeneza Alexander, watu hao muhimu ni baba yake Mfalme Philip, mama yake aliyekuwa akiitwa Olympasi na mwalimu wake aliyekuwa akiitwa Aristoto.

Mtu wa kwanza ambaye tutamwangalia ili kumfahamu Alexander Mkuu ni Baba yake mzazi ambaye alikuwa ni  Mfalme Philip wa pili.

Kama wahenga wasemavyo kuwa maji hufuata mkondo na mtoto wa nyoka ni nyoka, njia ya kutukuka ya Alexander mkuu iliandaliwa na baba yake aliyekuwa akiitwa Mfalme Philip wa ukoo wa ‘Argeadi’ koo ya kipekee iliyotoa wafalme kadhaa walioiongoza miliki ya Macedonia kwa vipindi tofauti tofauti, Mfalme Philip, alizaliwa mwaka 382 na kufa 336, kama mtoto wake Alexander, mfalme Phillip alikuwa mtu wa vurugu na huruma, mpenda mapigano na mtu wa vinywaji vikali.

Tofauti ndogo iliyomtofautisha Mfalme Philip na mtoto wake, Alexander, ilikuwa ni tabia ya kupenda vimwana. Mfalme Philip alikuwa akipenda vimwana lakini mtoto wake Alexander katika maisha yake alikaa mbalimbali na vimwana, inasemekana baada ya kumpata mama yake Alexander (Olympus), Mfalme Philips kwa kuwa alikuwa akimpenda sana Olympus, alijaribu kufichaficha na kujizuia dhidi ya tabia ya kupenda vimwana lakini alishindwa baada ya muda na kujikuta akiirudia.

Mfalme Philip alikuwa mpenda ushindi  kwa namna yoyote ile, mfalme Philip alikuwa na intelijensia ya pekee iliyomsaidia katika utawala wake na katika medani za kivita, inasemekana kuwa Mfalme Philip alikuwa ni mtu mwenye moyo mzito aliyependa kuzungukwa na wapiganaji na majemedari wa kivita ambao wako radhi kujidhabihu hata ikibidi uhai wao kwa ajili ya ushindi wa kivita.

Tamaa yake ya kupenda ushindi kwa namna zote na kutanua miliki yake ilikuwa imemwacha na kilema cha bega, jicho moja lenye kovu na mguu mmoja uliokuwa na matatizo. Kiufupi Mfalme Philip hakuwa mtu wa kawaida.

 Mtu mwingine muhimu tutakayemwangalia ili kumfahamu vizuri Alexander Mkuu ni mama yake mzazi ambaye alikuwa akiitwa Olympus.

Olympus alikuwa ni mwanamke mrembo, mwenye nguvu na katili, katika kitabu cha ‘The Story of Civilization, mwandishi wa historia, Will Durant, anatumia neno ‘Barbaric’ kueleza sifa ya pekee aliyokuwa nayo Olympus, kulingana na kamusi ya Kiingereza ya Oxford toleo la 10 neno Barbaric lina maana ya ‘savagely and cruel’ (anayefanya mambo kwa nguvu na bila kumwogopa mtu na katili). Neno lingine linaloendana na neno Barbaric ni neno la Kiingereza ‘Primitive’ lenye maana ya isiyostaarabika au tabia ya kufanya mambo bila kuzingatia ustaarabu, ovyo ovyo nk.

Inasemekana kisasi cha Olympus ndicho kilichomdhohofisha Mfalme Philip katika utawala wake, baada ya Mfalme kuanza kutoka nje ya ndoa, Malikia Olympus alianza kutoa siri za mfalme Philips ili kulipa kisasi na hatimaye siri za utawala wa mfalme Philips zikazagaa mitaani na ikawa kama vile mfalme alikuwa uchi kila mtu akijua alifanyalo katika jumba lake la kifalme.

Kwa miaka mingi Malkia Olympus alikuwa amedai kuwa yeye ni zao la Achilles shujaa wa Kigiriki aliyesemekana kuwa na nguvu za kutoweza kudhurika kwa namna yoyote ile, habari za shujaa huyo zipo katika mashairi ya maarufu ya Iliad, mashairi ambayo Alexander alikuja kujifunza baadaye na kuyakariri.

Hivyo, katika fikra moja kwa moja Alexander toka anafundishwa habari za Achilles, alikuwa akitambua kuwa Achilles ni babu yake na hivyo yeye ni zao la mashujaa na alikuwa na jukumu la kufuata hatua za babu yake huyo shujaa na kumaliza kazi aliyokuwa ameianza ya kutafuta ushindi kupitia mapigano. Itaendelea wiki ijayo