Home Habari Miaka 25 ya harakati za haki za binadamu, kuna kinachodaiwa?

Miaka 25 ya harakati za haki za binadamu, kuna kinachodaiwa?

847
0
SHARE

DK. KIJO BISIMBA

JUMA lililopita nilibahatika kuhudhuria shughuli tatu muhimu sana katika kuangalia hatua tulizopiga katika harakati za haki za binadamu na hususan haki za wanawake  na masuala ya jinsia hapa nchini.

Kwanza nilishiriki katika Tamasha la 14 la Jinsia linaloandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), kisha nilihudhuria  ufunguzi wa ofisi ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dodoma na hatimaye ufunguzi wa warsha iliyotanguliwa  na Mkutano Mkuu wa Shirika la Wanawake  Katika Sheria na Maendeleo (WiLDAF).

Shughuli zote hizi zilikuwa muhimu sana kwangu nikiwa mstaafu kwani baada ya mwaka mmoja nikiwa nje ya harakati nilikuwa nina hamu ya kuangalia hatua zinazoendelea kupigwa na wenzetu waliopo kwenye harakati wakati huu. 

TGNP walikuwa wanasherehekea miaka 25 ya uwepo wa shirika hilo na tamasha hilo lilitumika kuangalia tulikotoka na tunakoelekea miaka 25 ya shirika na kufikia miaka 25 tangu uwepo wa mkutano mkuu wa wanawake ulimwenguni uliofanyika Beijing.

LHRC nao walikuwa wanasherehekea miaka 24 ya uwepo wa shirika huku wakizindua maadhimisho ya miaka 25 ya shirika yatakayofikia kilele mwakani 2020 na uzinduzi wa ofisi hiyo ya Dodoma.

WiLDAF wao walikuwa na warsha ambayo ilijikita katika kujadili sheria za mirathi nchini na muswada waliokuwa wameuandaa wakishirikiana na wadau mbalimbali ambao ulipelekwa kwa Waziri wa Sheria.

Katika matukio yote matatu jambo kubwa nililojifunza ni kuwa bado kazi ni pevu. Pamoja na juhudi nyingi mno ambazo hadi sasa zimefanyika haya mashirika yana kazi sana kuhakikisha yale yaliyokuwa yanajadiliwa wakati mashirika yanaanza miaka 24/25 iliyopita yamekamilika kwani yako mengi bado yanayohitaji kufanyiwa kazi.

Huko Dodoma mgeni rasmi wa tukio lile alisema kuwa hafurahishwi sana na watu au mashirika yanayosema kuwa serikali haijafanya kitu, aliwashangaa sana watu wa aina hiyo kwani ukweli ni kuwa serikali imefanya mengi na katika mengi aliyoyataja ni miundombinu, elimu bure na vitu vya aina hiyo. Wakati akisema hivyo alikwishapokea sifa kutoka kwa watendaji wa kituo kuwa yeye amekuwa mstari wa mbele kukemea uvunjifu wa haki hasa zinazohusu watu wanaotuhumiwa kuwekwa mahabusu siku ya Ijumaa na kutodhaminiwa hadi Jumatatu au Jumanne, jambo ambalo ni uvunjifu wa haki ya mtu kupata dhamana.

Hata mimi nisingekubaliana na mtu ambaye angesema Serikali haijafanya kitu, kwa vile Serikali inafanya vitu vingi sana ila watetezi wa haki za binadamu macho yetu huwa katika yale ambayo Serikali haijaweza kuyafanya kwa kutotoa kipaumbele, kwa makusudi au kwa kupitiwa na kwa yale iliyoyafanya kinyume na matarajio.

Kwenye shughuli ile nilikuwa mwalikwa na hivyo sikuwa na fursa ya kuongea pamoja na tulipata habari kuhusu hali ya wafungwa magerezani na hasa mahabusu kwa vile magereza yana watu wengi kuzidi uwezo wake.

Hili likanikumbusha alichosema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu huruma anayowaonea watu walio magerezani kwa muda mrefu na kuwataka waliokuwa na kesi za uhujumu uchumi , utakatishaji wa fedha wakiri kosa na kisha warudishe fedha.

Tuliarifiwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa LHRC naye yuko mahabusu kwa muda mrefu sasa na ameshuhudia hali halisi ya magereza na jinsi watu wanavyotaabika huko kiasi cha kulishauri shirika kuona umuhimu wa kuwa na mpango wa kushughulikia haki jinai.  Ikumbukwe kuwa ndugu huyo aliye mahabusu wakati yeye na wenzake wanaanzisha LHRC walikuwa wameona uonevu mkubwa katika mashauri ya daawa na hususan haki ardhi na haki za kisiasa na zaidi uelewa wa wananchi wa haki zao.

Miaka 25 baadaye ameshuhudia hali halisi ya haki jinai na kwa njia ambayo naye ni muathirika na kuona ni eneo ambalo shirika inabidi lijielekeze. Waathirika wa haki hizi wapo pia wanaotokana na mafanikio ya kupata haki za kisiasa hasa mfumo wa vyama vingi vya siasa ambao sasa wamejikuta matatani.

TGNP mgeni rasmi alizungumzia hali ya haki za wanawake na haki za kijinsia kuanzia kipindi cha kabla ya Beijing hadi tulipo na alionesha hatua kubwa zilizopigwa, kwani zipo sheria nzuri zilizotungwa na hali ya wanawake kuweza kushiriki mambo mbalimbali kama elimu na hata siasa.

Wengine waliozungumza katika ufunguzi huo walionyesha jinsi ambavyo bado hatujaweza kuifikia ndoto ya hamsini kwa hamsini katika uongozi na utawala wa nchi na umuhimu wa kuanza upya mkakati huo.  

Wapo walioshangazwa, hasa wageni kutoka nchi za nje kuwa Tanzania bado tunaivumilia sheria inayoruhusu mtoto  mdogo wa miaka 14/15 aolewe kiasi cha Serikali kukata rufaa hata baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi unaomlinda mtoto.

Katika warsha ya WiLDAF sauti ilikuwa ni suala la sheria ya mirathi. Hili ni suala ambalo limefanyiwa kazi kwa zaidi ya miaka 30 sasa. Mgeni rasmi hapa yeye alikuwa mkweli sana. Alisema suala hilo si jepesi na hawezi kutoa ahadi kuwa atapeleka muswada na utapita kwani kwa kupokea rasimu tu alishaanza kutahadharishwa na  baadhi ya wabunge kuwa hilo suala ni ‘kaa la moto’.

Katika kuzungumza na mgeni rasmi huyu,  ilikuwa ni maumivu sana aliposema watu waanze kuwashawishi na kuwaelimisha wabunge kama kweli hili suala inabidi lipite. Yaani baada ya miaka 25 tuanze tena ushawishi upya.

Nilikumbuka jinsi ambavyo kama wanaharakati tulivyokutana na karibu kila Waziri wa Sheria na wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Jinsia aliyeteuliwa katika miaka 25 ya harakati.

Yupo aliyetuambia atalipeleka bungeni ila tujitahidi kufanya uchechemuzi kwa wabunge, yupo aliyetuambia alifikia hatua ya kupeleka kwenye baraza la mawaziri lakini akakwama hakupata kuungwa mkono katika ngazi hiyo.

Na mgeni rasmi huyu wa mkutano wa WiLDAF alitoa rai kuwa haki haipatikani  katika sahani bali hutafutwa, akimaanisha kuwa wanaokiuka haki hizo wapambane kuzitafuta haki hizo. Wapo waliotuambia wanalifanyia kazi na kadhalika.

Hoja inayonipa tabu katika suala hili ni kuwa ni nani katika hao wabunge au mawaziri anayefurahia kuona hali ya kibaguzi na kunyanyaswa wanakonyanyaswa  wanawake kwa sheria hizi za mirathi tulizo nazo?

Pia la kujiuliza ni nani katika watunga sheria na hata viongozi wetu aliye tayari kumuoza binti yake wa miaka 14? Na kwanini? Tukiangalia mfumo na haki jinai je ni nani  ambaye anajihakikishia kuwa yeye hatafika kuitafuta haki hiyo au kama si yeye jamaa yake?

Bila kuyaangalia haya kibinafsi tuyaangalie kimrengo wa haki. Haki za binadamu ni haki zinazopaswa kufaidiwa na kila mtu bila ubaguzi.

Mchakato wa Katiba ulianza kuleta nuru ya mabadiliko makubwa ya kimfumo ambayo yangeweza kuwa majibu ya harakati zetu za miaka hiyo 25, lakini bahati mbaya mchakato umekwama.

Nadhani tuna sababu bado kuwakumbusha  kiasi gani mchakato ule ulitugharimu kifedha na hata kimuda na kihisia kuwa pamoja na jitihada zote za kutengeneza miundombinu, haikuwa haki kuufifisha mchakato ule ambao ungetuletea mabadiliko chanya kwa wote.

Bado ninabaki na swali kichwani iwapo pamoja na mengi yaliyofikiwa tuna ujasiri wa kutoka kifua mbele, kuwa harakati zetu zote zimetuzalia matunda tuliyoyataraji na changamoto zilizopo ni mpya kabisa? Tusikilize aliyetushauri kuwa haki inatafutwa haitolewi tu.