Home Makala MIAKA 30 YA HUDUMA KH BILA SIASA

MIAKA 30 YA HUDUMA KH BILA SIASA

847
0
SHARE

NA SIDI MGUMIA,

MACHI 17, mwaka huu Hospitali ya Kairuki (KH) ambayo iko chini ya Mtandao wa Afya na Elimu wa Kairuki imetimiza miaka 30 ya kuanzishwa kwake, huku ikiwa katika kiwango cha juu cha huduma bora nchini.

Ubora wa hospitali hiyo kwa miaka yote hiyo, umeifanya kuingia kwenye orodha ya Hospitali zenye hadhi kubwa nchini na katika kuhakikisha kiwango hicho cha ubora hakishuki, badala yake kinapanda zaidi, uongozi wa Hospitali hiyo umekuwa ukifanya maboresho ya huduma zake kila mara.

Aidha kumekuwa na ongezeko la vifaa tiba vya kisasa vinavyoendana na mabadiliko ya teknolojia duniani. Hatua hiyo inafanyika kutokana na uongozi wa KH kujali zaidi afya za Watanzania.

Historia, Malengo na dira ya Hospitali hiyo kwa miaka ijayo yanazungumziwa na Mkurugenzi mkuu wake, Dk. Asser Mchomvu, ambaye anasema kuanzishwa kwa Hospitali hiyo mwaka 1987, ilikuwa ni kutimiza nia njema ya waasisi wa hospitali hiyo,yaani Hayati Profesa Hubert Kairuki na mke wake Bi Kokushubila Kairuki, kwa Watazania.

Dk. Mchomvu anasema wakati wa uhai wake, Prof. Kairuki pamoja na mke wake walifanikiwa kuanzisha Hospitali, Shule ya Wauguzi na Chuo Kikuu cha Tiba. Anasema taasisi hizo zimeendelea kukua siku hadi siku na sasa ni msaada mkubwa kwa jamii kubwa ya Watanzania na hata watu wengine kutoka nje ya Tanzania.

Anasema wanafamilia hawa waliweka kipaumbele kwenye afya ya Mtanzania wa kipato cha chini na ndio maana waliweka msukumo kwenye eneo hilo, lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora ya afya inamfikia Mtanzania.

Dk. Mchomvu anaeleza kuwa dhamira ya KH kutoa huduma za afya nchini imejikita katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania yenye dhamira ya kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya afya.

Katika muktadha huo, huduma za KH kwa Tanzania zinaenda sanjari na dira za maendeleo ya Taifa kwa miaka hiyo 30 ya utaoji wa huduma.

“Matarajio yetu ni kuwa watanzania  wataendelea kutupatia ushirikiano stahiki katika shughuli zetu ambazo kwa hakika zinalenga kuboresha afya za watanzania wenyewe,” alisema.

Dk. Mchomvu anasisitiza kuwa katika kuboresha huduma kwa mwaka huu, kuna maboresho makubwa yamefanyika na yataendelea kufanyika kwa lengo la kuliweka shirika karibu zaidi na Watanzania.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, KH  katika kuboresha huduma zake kwa Watanzania,   imeanza kutumia kitengo kipya kitakachokuwa na jukumu la kuwahudumia wagonjwa wa kutwa,   hususan wanachama wa mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).

Kitengo hicho kipya (OPD 3)  kilichopo nyuma ya Jengo kuu la hospitali mkabala na kitengo cha magonjwa ya viungo ( Physiotherapy Unit) kina sehemu kubwa ya mapokezi, vyumba 10 vya  madaktari, maabara, duka la dawa, sehemu ya sindano na kufunga vidonda, chumba cha vipimo vya Ultrasound, mapokezi , huduma za chanjo ya watoto (RCH) na chumba cha wauguzi.

“Kitengo hicho kitaiwezesha hospitali  kutoa huduma kwa haraka na ufanisi zaidi,hivyo kupunguza foleni kwa wagonjwa na kwamba kitazinduliwa hivi karibuni pamoja na vitengo viwili vinginevipya, kimoja kikiwa cha  kusafishia figo ( Dialysis Unit) na kingine cha kutoleahuduma za dharula ( Emergency Unit).

Zaidi ya hapo, imekuwa ni hospitali ya kwanza kuanzisha huduma za upimaji kutumia mashine za  CT scan tangu mwaka 1996.

Pia ni hospitali ya kwanza ya binafsi kuanza kutoa huduma za kufanya upasuaji kwa njia ya matobo (Laparoscopic service-1996)

Na kuwa hospitali ya kwanza mnamo mwaka 1998 kuanzisha shule ya binafsi ya udaktari nchini.

Aidha alisema KH inaendelea kufanya upasuaji wa njia ya matobo(Laparoscopic surgery), na wanaelekea kuanza kutoa huduma kwa kutumia teknolojia ya IVF (upandikizaji) lengo likiwa ni kuwasaidia wanandoa wenye matatizo ya uzazi kupata watoto kwa njia salama, lakini pia kuhifadhi mbegu za kiume na mayai kwa matumizi ya baadae watakapozihitaji (sperm bank or Cryobank). Huduma hii hutolewa kwa watu kama vile wagonjwa wa kansa ambao wanatibiwa kwa mionzi kwani mionzi huharibu mbegu hizo.

k1
Madaktari wa Hospitali ya Kairuki wakimfanyia mgonjwa upasuaji kwa njia ya matobo

Pia  kuna Mipango ya kuanzisha idara kamili ya magonjwa ya saratani itakayokuwa uwezo wa kutoa dawa na mionzi ya magonjwa hayo.

Mbali na kutoa huduma za kitabibu, hospitali ya Kairuki imekuwa ikijihusisha na utoaji wa huduma za kijamii kwa taasisi, makundi na watu mbali mbali, ikiwa ni mchango wake wa uwajibikaji kwa jamii (Corporate Social Responsibility), tangu kuanzishwa kwake miaka thelathini iliyopita.  Mathalan, KH imekuwa ikitoa misaada mbali mbali kwa shule ya msingi Mikocheni ambapo hospitali ilifanikiwa kujenga vyumba vya madarasa kadhaa, kuviwekea madawati na kuvikarabati vinapochakaa.  Lakini pia, KH imekuwa ikitoa huduma ya kwanza kwa wanafunzi wa shule hiyo bila malipo kwa miongo kadhaa sasa.

Aidha, KH iliingia makubaliano na serikali ili kutoa huduma mbali mbali kwa wananchi bila malipo ikiwamo huduma ya chanjo kwa wanawake, huduma ambayo hutolewa mara mbili kwa wiki, huduma ya Kifua kikuu  TB,  huduma ugonjwa wa ukimwi.

Lakini pia, katika wiki ya kumbukizi ya Marehemu Profesa Kairuki inayofanyika kila mwaka, KH hutoa huduma ya kupima afya za wananchi  na kutoa ushauri bila malipo.  Baadhi ya huduma zitolewazo ni vipimo vya afya za kinywa na meno, macho, saratani ya matiti, tezi dume, afya ya uzazi, kisukari, shinikizo la damu n.k.  Shughuli nyingine za uwajibikaji kwa jamii ambazo KH imewahi kuzifanya ni kutoa misaada ya vitanda vya hospitali na magodoro katika vituo vya afya na kwa makundi maalumu, kutoa elimu ya afya kwa jamii kupitia vipindi vya redio na runinga, kutoa misaada kwa wahanga wa maafa kama ajali ya treni, mafuriko, tetemeko la ardhi nk.

KUANZISHWA KWA KH

Profesa Kairuki, akiwa ni mwandishi wa majarida, makala mbalimbali za afya na mtaalamu wa magonjwa ya wanawake alianzisha KH kwa jina la T.A.G Mikocheni, huku ikiwa na vitanda 30 tu na wafanyakazi wapatao 60. Hata hivyo,hakukata tama kwa sababu aliamini iko siku Hospitali hiyo ingekuwa msaada mkubwa kwa Taifa.

CHANGAMOTO 

Akizungumzia changamoto walizokutana nazo tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, Dk. Mchomvu anasema tatizo kubwa ni ukosefu wa rasilimali watu kwa maana ya wataalamu wa magonjwa mbalimbali nchini hivyo kuufanya utoaji wa huduma mwanzoni kuwa mgumu.

Pili, anasema pamoja na kuingiza mashine nyingi za kisasa kwa ajili yakusaidia vipimo na matibabu, bado kuna changamoto ya vifaa hivyo kuwa bei ghali kuviagiza kutoka nje ya nchi.

Kama ilivyo katika kukosa waatalamu wa magonjwa, uendeshaji, utunzaji na ukarabati wa mashine hizo zinazonunuliwa kutoka nchi za nje bado ni changamoto yenye gharama kubwa kwa hospitali..