Home Uchambuzi Miaka 42 serikali imefeli mkakati wake Dodoma

Miaka 42 serikali imefeli mkakati wake Dodoma

2675
0
SHARE

Marais wastaafu(kushoto) Rais Ali Hassan Mwinyi (kulia) Benjamin MkapaNa Markus Mpangala

TAKRIBANI miaka 42 iliyopita Halimshauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ilipitisha azimio la kubadili makao makuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Jiji la Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Dodoma uliopo katikati ya nchi.

Dar es Salaam ni mji muhimu na wa kwanza kibiashara   nchini. Mwaka 1973 aliyekuwa Rais wa kwanza nchini Mwalimu Julius Nyerere alitangaza azimio la kuhamia Dodoma kama ilivyokubaliwa na chama cha CCM.

Azimio hilo lilisema kuwa makao makuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yatakuwa mji wa Dodoma ambao upo Kanda ya Kati (katikati) ya nchi yetu. Hiyo ilikuwa moja ya sababu za kutaka kuhamia mji huo.

Aidha, taarifa zinaonyesha kuwa uamuzi wa kuhamia Dodoma ulifikiriwa kabla ya uhuru. Baada ya kupitishwa kwa azimio hilo liliendana na kuanzisha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) mwaka 1976.

Maandalizi na hatua za awali zilikuwa kuhamisha shughuli mbalimbali za serikali kutoka uliokuwa mji mkuu wa Dar es Salaam kwenda Dodoma. Ni mji huo ndipo yalipo makao makuu ya CCM na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ilielezwa kuwa kati ya mwaka 1988  hadi ifikapo mwaka 1993 ilitakiwa baadhi ya wizara zihamie mjini Dodoma, ambazo ni Wizara ya Fedha, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Nidhati na Madini, pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani na Ulinzi.

Aidha,  ili kukamilisha azimio hilo kwa nyakati tofauti shughuli kadhaa zimehamia Dodoma. Tumeshuhudia hatua nyingine ni kuanzisha Ukumbi wa Mikutano (vikao) vya shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma na kuachana na matumizi ya ukumbi wa Karimjee uliopo jijini Dar es salaam.

Mabadiliko ya kuhama shughuli za Bunge yaliakisi hatua za kuufanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi kama ilivyokuwa imekusudiwa.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ni kwamba ilitakiwa hadi kufikia mwaka 1986  serikali iwe imehamia katika mji mkuu mpya wa Dodoama. Hata hivyo hadi sasa serikali haijatimiza mpango huo na hakuna inachoelezwa zaidi.

Awamu ya kwanza ya Rais Nyerere iliweka mikakati na miongozo yote muhimu, ingawa haikutekeleza mpango huo. Awamu ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi haikufanya jitihada mpya za kuhamia Dodoma zaidi ya shughuli ndogo ndogo za kiserikali. Aidha, awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa pia hapakuwepo na mikakati thabiti ya kuhamia mji wa Dodoma.

Kwanini serikali haijatimiza suala hilo kwa miaka takribani 42 hadi sasa? Je ulikuwa mpango madhubuti kwa serikali au kuiga kutoka mataifa mengine? Turejee historia.

Katika kipindi cha miaka 1960 historia ya Afrika inaonyesha mataifa mengi yalipata uhuru. Ni katika kipindi hicho pia mataifa mengi ya Afrika yalikumbwana mapinduzi ya kijeshi.

Ambapo serikali na vyama vilivyokuwa vinatawala baada ya kurithi kutoka kwa wakoloni vilijikuta vinakumbana na upinzani mkali ndani ya nchi zao.

Aidha, katika kipindi cha miaka hiyo hadi 1970 tulishuhudia mataifa kadhaa yakibadilisha miji ya makao ya nchi zao. Mathalani Malawi ambayo ilibadilisha mji mkuu kutoka Zomba kwenda jiji la Lilongwe.

Nigeria ilihama kutoka Lagos kwenda Abuja. Mji wa Lagos ulikuwa makao makuu ya serikali kuanzia mwaka 1914 hadi 1991. Uamuzi wa kuhamisha makao hayo ulifanywa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Jenerali Murtala Mohammed. Hata hivyo utekelezaji wa mpango huo ulifanywa katika kipindi cha utawala wa Rais Ibrahim Badamasi Babangida.

Kutokana na wimbi la mataifa kubadili miji mikuu liliingia pia hapa nchini, na Mwalimu Nyerere kama miongoni mwa wana watiifu wa Afrika alionyesha dhamira hiyo “kuhamia’ Dodoma kama njia ya kuunga mkono.

Sababu nyingine ni kwamba Nyerere alikuwa amenusurika maasi ya kijeshi mara mbili, kama ambavyo baadhi ya mataifa ambayo yalilazimika kubadili makao makuu.

Nigeria inafahamika kwa mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea kwa miaka mingi na hata uamuzi wa kuhamisha makao makuu ulitokana na sababu za kiusalama.

Inasemekana kuwa kuhamia Abuja kulilengwa kuiwezesha serikali kutawala na kudhibiti mbinu zozote za mapinduzi. Lakini wapinzani wa hoja hii wanasema ingeliwezekana pia kupinduliwa hata huko Abuja.

Aidha ilitajwa sababu ileile kama ya Mwalimu Nyerere kwamba Abuja ilikuwa katikati ya nchi kuliko ilivyokuwa Lagos ambayo ulikuwa magharibi zaidi.

Pia ilikuwa ni kuepuka mgongano wa kimadaraka kwakuwa Lagos lilikuwa jiji kubwa na kwa muundo wa utawala lilikuwa chini ya Gavana wake, lakini walipohamishia Abuja aliteuliwa waziri anayeshughulikia mji huo hivyo hakuwa na mgongano na kiutawala.

Tukija suala la Malawi tunaona kuwa ilibadilisha bila shinikizo lolote kwenda Lilongwe ingawaje walikuwa na sbabu ileile ‘aktiati ya nchi’. Kwamba Malawi haikuwa na dalili zozote za kupatwa na maasi ya kijeshi. Hata hivyo inakubalika kuwa ‘huenda’ ililazimika ufanya hivyo kama njia ya kujikinga na maasi ya kijeshi. Kukubalika huko ni dhana tu hadi sasa.

Kwetu Tanzania jambo la kuhamia Dodoma limekuwa tatizo sugu. Je Tatizo letu hasa ni nini? Kwa maoni yangu inawezekana kuhamia Dodoma. Lakini itawezekana kama serikali kupanga mikakati ya awmau zilizofuata za utawala.

Watetezi wa serikali wanaweza kusema hata mpango wa ujenzi wa Daraja la Kigamboni uliidhinishwa na serikali mwaka 1976 na umekamilika mwaka 2015. Hata hivyo bado inajionyesha Daraja hilo halikupewa mkakati dhabiti au kipaumbele ndiyo maana limechelewa.

Wakati tunaweka azimio la kuhamia Dodoma bado hatuna nyumba za mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine wa serikali. Wakati wa serikali ya Nigeria inaamua kutoka Lagos kwenda Abuja iliamua kwa vitendo hasa kubadili hali hiyo.

Ingawa ilionekana kuhama Lagos ni ngumu zaidi lakini iliwezekana kwa kusimamia kipaumbele hicho. Kwanini serikali imetumia miaka 42 katika suala moja ili limamilike na je hiyo si ishara ya kwamba tunafeli katika kutekeleza vipaumbele vyetu muhimu?

Na kama kuhamia Dodoma halikuwa jambo muhimu ni kwanini lilipitishwa haraka na kuruhusiwa kuanzisha mamlaka ya ustawishaji mji wa Dodoma?

Nini cha kufanya ili kutatua kero hii iliyodumu miaka 42? Tunafahamu kuwa mabadiliko ya miji kama haya yanaleta migongano miongoni mwa wanasiasa. Tumeshuhudia migongano hiyo kati ya wanasiasa na CDA, ambapo wamekimbizana hasa kwenye kuhujumiana maeneo mkoani  Dodoma.

Inahitajika miaka mitano hadi kumi kawa awamu ya kwanza ya mikakati ya kuhamia Dodoma, kisha utaratibu uendelee rasmi ili kabiliana na changamoto mbalimbali mjini humo.

Aidha, ikumbukwe Dodoma changamoto ya maji ni kubwa kwa wakazi wake, jambo ambalo hata serikali italazimika kuweka mkakati mwingine wa ziada kuhakikisha mji wa Dodoma unapatikana maji ya kutosha.

Tunafahamu mkakati huo utalazimika kutumia rasilimali fedha na watu, jambo ambalo linahitaji muda. Hata hivyo ni vema kujisaili, kwamba tuliamua kwa dhati kuhamia Dodoma au zilikuwa santuri za michapo ya Wanamajumuhi?

Ninaamini endapo Daraja la Kigamboni limesubiriwa kwa wakati wote huo basi vilevile kuhamia Dodoma uwe mpango endelevu kuliko tunachoshuhudia sasa ‘wahamiaji haramu’ kuishi Dodoma kwa zama.

Ninapotumia ‘wahamiaji haramu’ nina maana ya wakuu na watu wa idara mbalimbali za kiserikali wanaolazimika kuhamia Dodoma kwa muda katika kipindi cha vikao vya bunge. Tunaweza kuepuka hilo lisilo na utulivu kiutendaji.