Home Makala MIAKA 42 YA CCM: ‘Chama kinatikisika hakianguki’

MIAKA 42 YA CCM: ‘Chama kinatikisika hakianguki’

1567
0
SHARE

MWANDISHI WETU

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimo ndani ya shamra shamra na heka heka za kusheherekea miaka 42 ya tangu kuasisiwa kwake Februari 5, 1977.

Chama hiki ni zao la muungano wa vyama viwili vya Afro Shiraz Party (ASP) na Tanganyika African National Union (TANU).

Msingi mkuu wa CCM ni mapinduzi salama ya Zanzibar yaliyotekelezwa mwaka 1964 na chama cha ASP yaliyomng’oa aliyekuwa mtawala wa visiwa hivyo Sultan Jamshid.

Jambo la kufurahisha  ingawa halizungumzwi sana ni kwamba ASP nayo iliasisiwa Februari 5, 1957 eneo la Raha Leo, Unguja, hivyo kama kingekuwa kimesimama chenyewe nacho kingekuwa kinasheherekea kuasisiwa kwake.

ASP ambacho ndio kimefanikisha mapinduzi ya Zanzibar, kilitazamwa kama chama kikuu cha upinzani mbele ya kilichokuwa chama tawala cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) ambacho  kilikaa madarakani kwa miaka mitatu tu (1961-1964).

Katika kipindi cha mkiaka 42 ya umri wake Chama Cha Mapinduzi kimepita kwenye misuko suko mingi na mizito, ambayo ilihitaji uimara na uthubutu wa viongozi wake katika kuamua, vinginevyo kingeshaanguka kama vilivyoanguka baadhi ya vyama vya ukombozi barani Afrika.

Mwanasiasa mkongwe nchini Mudhihir Mudhihir katika mzungumzo yake na RAI ametaja baadhi ya misuko suko iliyokikumba chama hicho tangu kuasisiwa kwa ke hadi sasa.

RAI: Miaka 42 ya CCM, inakukumbusha magumu yapi yaliyowahi kukikumba chama hicho?

MUDHIHIR: Chama kimekumbana na changamoto nyingi ndogo na kubwa, lakini nadhani naweza kuziainisha chache kubwa ambazo kama viongozi wetu wasingekuwa imara basi kisingekuwepo leo.

Mwaka 1978 ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuasisiwa kwake, chama kiliamkia kwenye viota ya Kagera, fikiria ni mwaka mmoja tu wa kuasisiwa, hata viongozi hawajatulia na kukiimarisha chama, kinaangukia kwenye vita.

Jambo la kufurahisha, wtu waliisahau siasa na kujikita kwenye kuipigania nchi, hatimae tukavuka salama katika kipindi hicho.

Tukiwa hatujakaa sawa, mwaka 1979-80 mara baada ya vita ya Kagera, nchi ikaingia kwenye hali mbaya ya kiuchumi, hadi aliyekuwa Rais wakati huo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliwataka Watanzania kufunga mikanda baada ya nchi kuingia gharama kubwa kwenye vita.

Na hapo ndipo ilipoibuka misamiati ya uhujumu uchumi na ulanguzi, ilifikia mahali hata ukikutwa na mche wa sabuni ulikuwa unaulizwa umipata wapi.

Ilikuwa ndugu yako akienda Ulaya unamuagiza akuletee Colgate kwa sababu ilikuwa ni bidhaa adimu, muhimu na adhimu.

Mwaka 1983 mambo bado yakiwa hayajakaa sawa likaibuka suala la baadhi ya watu huko Zanzibar kutaka kujitenga.

Msimamo thabiti wa viongozi wa chama wakati huo ukasaidia kuwashughulikia wale wote waliokuwa wakiongoza harakati hizo.

Huu ulikuwa ni mtihani mgumu kwa nchi na chama, lakini ulivukwa salama bila kumwaga damu wala kutandikana.

RAI: Mara baada ya heka heka hizo ambazo bila shaka ni kama ziligusa mboni ya nchi moja kwa moja, ni changamoto zipi hasa unazozikumbuka ambazo zimekigusa chama?

MUDHIHIR: Mwaka 1995 chama kilipata mtihani mzito ambao kama isingekuwa juhudi na jitihada za Mwalimu Nyerere huenda kingeshafutika kwenye ramani ya siasa nchini.

Ikumbukwe kuwa mwaka huu ndio ulikuwa mwaka uliorejesha uchaguzi wa vyama vingi.Haikuwa rahisi kupenya kwenye mwaka huu.

Tukiwa katika safari ya kuelekea kwenye uchaguzi huo, mwenzetu tuliyekuwa nae ndani ya CCM tena waziri mwenye ushawishi mkubwa, Augustino Mrema, alikiasi chama na kukimbilia upinzani.

Wakati huo chama cha upinzani chenye nguvu kikiwa ni NCCR Mageuzi, tulihitaji kumpa mtu mwenye nguvu ya kisiasa hasa kupambana na Mrema, ambaye kwa wakati huo alikuwa akikubalika sana.

Hatimae kwa uimara wa hali ya juu chama kikaibuka na Benjamin Mkapa ambaye hakuna aliyemtegemea na kweli tukashinda.

Moja ya mambo muhimu kwa CCM ni kufanya uamuzi wake kupitia vikao, hakitegemei utashi wa mtu bali ni uamuzi wa wengi unaopatikana kwenye vikao.

Utamaduni huo umekifanya chama kuwa imara tangu kuasisiwa kwake hadi sasa, viongozi wanaopatikana hupatikana baada ya kujadiliwa vikaoni si kama wenzetu ambao mtu mmoja anakaa na kuibuka na uamuzi.

RAI: Baada ya 1995?

MUDHIHIR: Baada ya mwaka huo tukakutana na hali kama hiyo tena mwaka 2015, kama unakumbuka vizuri, wengi walijua sasa CCM inaanguka.

Ukweli ni kwamba chama kiligawanyika vipande vipande, hakuna aliyeamini kama tutavuka salama wakati ule.

Watu wachache walikuwa na nguvu kuliko chama chenyewe, lakini jambo la kushukuru mfumo mzuri wa kuteua viongozi uliowekwa ndani ya chama ulisaidia kumpata mtu sahihi kama ilivyokuwa mwaka 1995.

Hakuna aliyemtegemea Dk. John Magufuli kama angepenya kwenye kundi la wanasiasa wale ambao tayari walikuwa wameshajijengea himaya kubwa ndani ya chama.

Yapo mambo mengi yaliyotokea, lakini itoshe kusema kuwa kwa miaka yote hiyo 42 nimekishuhudia chama kikitikisika tu, lakini hakianguki na siuoni uwezekano wa kuanguka leo ama kesho, maana hata baada ya Magufuli naamini tutampata mtu sahihi na chama kitaendelea kuwepo madarakani.

Nina uhakika na hili kwa sababu bado sijakiona chama cha siasa chenye mikakati na mbinu zitakazowasaidia kuing’oa CCM madarakani.