Home Latest News MIAKA 56 YA UHURU, TUFANYE MAPINDUZI YA FIKRA

MIAKA 56 YA UHURU, TUFANYE MAPINDUZI YA FIKRA

1013
0
SHARE
Rais John Magufuli akipokea heshima kutoka kwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama kuadhimisha miaka 56 ya Uhuru

NA VICTOR MAKINDA


Naomba radhi, sitaendelea na mfululizo wa makala ya ‘Natamani kukutana na Rais, nimweleze Ukweli’.Nimelazimika kufanya hivyo ili kuyafanyia kazi baadhi ya mambo panapo maajaliwa nitaendelea na mfululizo wa makala hayo.

Leo nijadili miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika na umuhimu wa kufanya mapinduzi ya fikra. Ndiyo, Miaka 56 ya Uhuru, tufanye mapinduzi ya fikra. Kwa nini nasema hivyo…tuendelee.

Binadamu ni  fikra. Binadamu asiye na fikra sahihi na matendo sahihi kwa wakati na kuzingatia vipaumbele, kamwe hawezi kupiga hatua katika lolote hususani maendeleo. Ifahamike kuwa msingi wa matendo yetu ni fikra zetu.  Wanaotenda vibaya ni wale wanaofikiri vibaya. Wanaotenda mazuri ni wale wanaofikiri vizuri. Unaweza kufikiri vibaya lakini ukashauriwa na kutenda vizuri. Fikra sahihi zinaweza zisizalishwe na mtu mmoja lakini mtu huyo akapokea ushauri uliotokana na fikra sahihi za watu wengine. Waswahili wana msemo wao kuwa ‘Mtu ni Mtu mwingine wakimaanisha kuwa ukamilifu wa mtu hutokana na mtu mwingine.

Nchi yetu bado inakabiliwa na ufukara katika nyanja nyingi. Pamoja na kuwa tumejaaliwa rasilimali nyingi lakini bado tungali na mafukara wengi na wengi wetu tunaishi maisha ya chini ya Dola moja kwa siku. Hii ni hatari sana kwa hatima ya maendeleo ya nchi na watu wake.

Na tujiulize sasa kwanini tangu tumepata uhuru  miaka 56 bado tunashambuliwa na maadui wale wale ambao tuliwatangazia vita na kuahidi kuwa tutapambana nao kufa au kupona ili tuwashinde?

Maadui wetu si wengine bali ni ujinga, maradhi na umaskini. Miaka 56 bado tunapambana na maadui hawa licha ya nchi yetu Tanzania kujaaliwa rasilimali ambazo ni wazi kuwa kama tungekuwa tunezitumia vizuri leo hii maadui hawa wangebaki historia kwetu. Je, nini tatizo, kwa nini katika kipindi cha miaka 56  tangia tumejitawala tumeshindwa kuwashinda maadui hawa. Nani aliyeturoga?

Izingatiwe kuwa mika 56 ni umri mkubwa. Ni umri  wa mtu aliyemaliza ujana na ameingia katika umri wa uzee.  Ni umri ambao tayari mtu anakuwa amejukuu na baadhi hata vitukuu. Miaka 56 ndio umri wa akina Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na wengine wengi. Miaka 56 ni mingi mno katika kufanya mtu au taasisi kuwa imejiimarisha vizuri na kuwa imeondokana na baadhi ya kero ambazo kimsingi zinaweza kutatulika kiurahisi kwa kuwa na fikra sahihi za kimapinduzi. Nini kimetukwaza mpaka tumekwama?

Nieleweke kuwa sibezi mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hiki cha miaka 56. Yapo mafanikio ambayo kama Taifa tumeyafikia. Kuyaorodhesha ni mengi mno. Lakini tunapolinganisha rasilimali tulizonazo kama Taifa na hatua za maendeleo tulizofikia, sambamba na umri tuliojitawala, ni wazi kuwa tuko nyuma. Na endapo kama tungetumia rasilimali zetu kikamilifu kwa ajili ya kutuendeleza basi leo hii  tusingekuwa tunaendelea kuimba wimbo ambao tumeuimba tangu mwaka 1961, wimbo wa kupambana na maadui Ujinga, Maradhi na Umaskini. Nini Chanzo cha kupata matokeo yasiyolingana na utajiri wa rasilimali tulizonazo? Tupanue mjadala.

 UJINGA

Ni ukweli usiofichika kuwa Serikali ya awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, haikutilia mkazo elimu ambayo ni msingi wa kupambana na ujinga. Ukitaka kuwaudhi Watanzania mseme vibaya Mwalimu Nyerere. Katika nukuu zake mwenyewe Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa katika kipindi cha utawala wake, yapo mazuri aliyoyafanya na pia yapo mabaya aliyoyafanya. Ndiyo, Nyerere hakuwa malaika. Alikuwa ni biniadamu mwenye mazuri na mapungufu pia kama alivyo binadamu yeyote mwingine. Tunakubali kuwa alikuwa na kipaji kikubwa cha uongozi.  Muungano na ujamaa wa kitaifa ni miongoni mwa mambo ambayo Mwalimu Nyerere alijaaliwa mno. Katika kipindi cha uongozi wake, alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuliunganisha Taifa na wananchi wake kuwa kitu kimoja. Hili alifanikiwa kwa kuwa hapakuwa na matabaka makubwa nchini kwetu. Ilimuwia urahisi kwa kuwa tulishakuwa na msingi wa umoja na mshikamano miongoni mwa Watanganyika.

Mwalimu Nyerere na Serikali yake waliendeleza misingi hiyo sambamba na kuisimika zaidi. Amani iliyokuwepo pamoja na kupata uhuru bila mtutu wa bunduki ilikuwa ni tija ya kufanya tuendelee haraka.

Lakini ni ukweli usiopingika kuwa Mwalimu Nyerere hakuipa Elimu Kipaumbele kama njia ya ukombozi wa Mtanzania. Hii ndiyo sababu hasa ya wasomi wa enzi za Mwalimu kuwa wachache. Shule mpya za msingi na za upili sambamba na vyuo vikuu zilizoanzishwa wakati wa Mwalimu, ni chache mno. Nasema bila kupepesa macho kuwa Mwalimu Nyerere kwa miaka 23-24 ya utawala wake hakutoa kipaumbele sana kwa elimu. Alifanikiwa kuusimika uzalendo wa Watanzania kwa nchi yao kwa asilimia kubwa.

Mwalimu alijikita katika ujamaa wenye chembechembe za ufukara. Ujamaa wake hakuupa sura ya utajirisho. Aliutaja kuwa ubepari ni unyama tafsiri ambayo binafsi sidhani kama ni sahihi sana. Kuna wakati nawaza pengine alifanya kosa kuwafukuza wazungu haraka. Lakini hatuwezi kuacha kumpongeza kwa elimu kiduchu iliyotolewa ambayo haikuwa na tabaka.

Wote waliostahili kuipata waliipata japo ni kwa uchache. Ni ukweli kuwa elimu ni moyo wa Taifa. Taifa lisilo na watu wengi walioelimishwa vizuri wakaelimika maendeleo lazima yatakuwa ni yenye kusua sua. Ukuaji wa maendeleo lazima utakuwa  wa taratibu mno. Rejea kuhamishwa kwa wakurugenzi na mameneja wa viwanda pindi wanapovurunda maeneo yao ya kazi. Hii ilikuwa ni kwa sababu hatukuwa na wasomi wengi. Nipo tayari kusahihishwa.

Nikiusawiri kidogo utawala wa Mwalimu Nyerere  ninauona kama ni utawala uliotumia muda mwingi  na rasilimali nyingi  miaka ya Mwanzo wa Uhuru, kupigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika. Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Bostwana na Afrika Kusini ni mifano michache katika mingi.

Nionavyo huo haukuwa muda wa kupigana kwa ajili ya wengine. Huo ulikuwa muda mwafaka wa kujenga Taifa la watu walioelimika kwa wingi na kujenga uchumi imara wenye kusimamiwa na wasomi wa nyanja tofauti.

Makala haya hayana lengo la kuukosoa utawala wa Mwalimu Nyerere lah hasha. Lengo la makala haya ni kuhamasisha mapinduzi makubwa ya fikra ambayo tunatakiwa kuyafanya. UKweli ulivyo, kamwe huwezi kufanya Mapinduzi ya fikra pasipo kubaini kuwa fikra zilizokuwepo na zilizopo haziwezi kufanya mabadiliko. Kung’amua hayo na kujipanga upya ni jambo lisiloepukika.

AWAMU YA PILI

Utawala uliofuata baada ya Mwalimu Nyerere ni miongoni mwa tawala zilizofanya mapinduzi makubwa ya fikra. Ndiyo, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, utawala wake ulifanya mapinduzi makubwa ya fikra. Aliuacha ujamaa na walau akakumbatia sera za kibepari na kuruhusu  soko huria na utandawazi. Watanzania wote kwa ujumla walioishi kipindi cha utawala wa Mwinyi 1985-1995, wanakiri wazi kuwa kipindi hiki mtindo wa maisha ya Watanzania ulibadilika mno.

Nchi yetu kwa mara ya kwanza iliingia katika soko huria na kuruhusu bidhaa za nje kuingia nchini sambamba na kushamiri biashara ya kimataifa. Uhuru wa vyombo vya habari na kuondoshwa urasimu katika nyanja za kiuchumi kulisaidia sana kuyasukuma maendeleo ya watu. Mwinyi anapongezwa kwa hilo na mengine mengi japo naye kwa upande wa elimu hakujenga misingi mizuri sana ya elimu hasa elimu ya upili.

Lakini hakuna anayethubutu kupinga kuwa kipindi cha utawala wa Mwainyi maendeleo yalitafsiriwa kuwa ni maendeleo ya watu na sio vitu. Watu walipiga hatua za haraka sana za maendeleo. Mzunguko wa fedha ulikuwa mikononi mwa wananchi na upatikanaji wa bidhaa na ulikuwa ni mzuri. Huu ni wakati ambao uchumi wa Tanzania ulichangamka mno. Ujenzi imara wa taasisi za kiserikali ulikuwa wa kiwango cha chini.

 AWAMU YA TATU

Rais Benjamini William Makapa alifuata baada ya Mwinyi. Huyu alikuwa ni mjenzi wa taasisi imara. Mkapa aliyatafsiri maendeleo kama ujenzi wa taasisi imara zenye nguvu. Hiki ndicho kipindi ambacho Watanzania walilalamika kama ambavyo wanalalamika katika utawala huu, kuwa fedha imeadimika. Rais Mkapa alifanyia marekebisho makubwa sera za kiuchumi za mtangulizi wake. Alijikita katika kuimarisha taasisi za Elimu ya Msingi na Sekondari, rejea MEM NA MEMSI ubinafishaji wa Mashirika ya Umma,  ambayo mengi yalikuwa mahututi kama sio kufa kabisa… Iatendelea wiki ijayo….