Home KIMATAIFA MIAKA 70 BAADA YA UHURU: INDIA,PAKISTAN BADO ZINAGOMBANA

MIAKA 70 BAADA YA UHURU: INDIA,PAKISTAN BADO ZINAGOMBANA

601
0
SHARE

DSC_4514

NA HILAL K SUED

August 15,mwaka huu India na Pakistan zinaadhimisha miaka 70 tangu zipate uhuru kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza. Kabla ya kujikomboa nchi zote hizo mbili zilikuwa moja – na iliitwa India (au British India) chini ya gavana mmoja.

Hata hivyo Waingereza waliona ni vyema zikagawanywa kutokana na misingi ya kidini kwani harakati za kudai uhuru zilijipambanua kati ya Waisilamu wa maeneo ya Kaskazini-Magharibi (sasa Pakistan) na wale wa Kaskazini-Mashariki ambayo sasa ni Bangladesh, na Wahindu katika eneo lililobaki ambalo ni ndiyo kubwa.

Baadaye mwanzoni mwa miaka ya 70 jimbo la Pakistan la Kaskazini-Mashariki lilijitenga na kuwa Bangladeshi baada mapambano ya wazalendo wa jimbo hilo dhidi ya utawala wa Islamabad.

Aliyeendesha harakati za kudai uhuru kutoka kwa wakoloni kwa upande wa Wahindu alikuwa Mohandas Mahatma Gandhi, mwanasheria machachari kutoka jimbo la Gujarat na ambaye aliwahi kuishi Afrika ya Kusini ambako alihusika katika harakati za kupinga ubaguzi wa rangi – hususan ubaguzi dhidi ya watu wa asili ya Asia.

Na kwa upande wa Waisilamu alikuwa Mohammed Ali Jinnnah ambaye pia alikuwa mwanasheria na mwanasiasa. Gandhi alikuwa anapinga India kugawanywa na alikuwa tayari hata kumwachia Jinnah kuongoza serikali ya kwanza baada ya uhuru. Aliwahi kukaa bila kula kwa miezi kadha kupigania kutogawanywa kwa nchi. Hata hivyo Wahindi wengi walimpinga katika azma yake ya kumwachia Muisilamu aongoze India.

Hivyo kuzaliwa kwa mataifa hayo mawili pacha kulikuwa kwa maumivu makubwa kutokana na kugawanywa kwani idadi kubwa ya watu walipoteza maisha kutokana na misingi ya imani za kidini.

Angalia: Ni kilometa 700 zinazotenganisha Delhi na Islamabad – miji  mikuu ya India na Pakistan mtawalia – ni kama vile kati ya Dar es Salaam na Kampala. Ni umbali mdogo sana kwa usafiri wa anga lakini mtu hawezi kusafiri baina ya miji hiyo miwili moja kwa moja. Hakuna kabisa safari za anga kati ya miji hiyo.

Na hali hii ni mojawapo ya uhasama uliodumu kati ya nchi hizo mbili kwa miaka 70 hadi sasa. Wananchi wa nchi zote hizo mbili ni mashabiki wakubwa wa mchezo wa cricket lakini hutumia viwanja vya nchi nyingine, hasa zilizo jirani kila zinapopambanishwa katika mashindano ya kimataifa.

Na katika miaka hiyo 70 nchi hizo zimepigana vita mara tatu, ingawa wengine wanasema ni mara nne, kwani mara ya mwisho majeshi yao yalipopambana mwaka 1999, hakukwapo tangazo la vita (declaration of war).

Aidha hali hii ya mahusiano mabaya imesababisha nchi zote mbili hizo kuendeleza miradi ya zana za nyuklia. Hivyo ingawa mzozo huo ni wa majirani tu, lakini umesheheni hofu kubwa kwa dunia mzima.

Sababu kubwa kwa Waisilamu kudai eneo la nchi yao ni kwamba kutokana na idadi yao kuwa ndogo walijiona wangekuwa wanabaguliwa na kunyanyaswa sana na Wahindu.

Hivyo Uingereza ilimteua gavana mpya (Viceroy) – Louis Mountbatten kufanya kazi ya kugawanya nchi hiyo, na hasa katika majimbo makubwa ya mipakani – Punjab upande wa Kaskazini-Magharibi na Bengal upande wa Kaskazini-Mashariki. Hata hivyo mchanganuo hasa wa wapi mpaka ungekuwapo haukujulikana hadi siku mbili baada ya kutangazwa kwa uhuru.

Mgawanyo huo wa mpaka ulifanywa kwa namna ya kupiga mstari kwa kutumia rula kwenye ramani na ulisababisha maafa makubwa katika Karne ya 20 ukiacha maafa ya Vita ya Pili ya Dunia iliyokuwa imeisha miaka miwili tu nyuma.

Hakuna anayejua idadi kamili lakini takriban watu 12 milioni walijikuta kuwa wakimbizi wakati walipokuwa wakihangaika kuhama kutoka upande mmoja wa mpaka mpya na kwenda upande mwingine.

Pia inakadiriwa kati ya watu laki tano na milioni moja waliuawa kutokana na ghasia za kidini na kikabila. Maelfu ya wanawake walitekwa na watu wa dini tofauti

Katika jimbo la Punjab ambapo Wahindu, Waisilamu na Makalasinga walikuwa wakiishi pamoja na kuongea lugha moja, uhasama wa kibaguzi wa ghafla uliibuka wakati wa Waisilamu wakihamia Pakistan na Wahindi kwenda India.