Home Makala Kimataifa MIAKA 73 YA UMOJA WA MATAIFA:

MIAKA 73 YA UMOJA WA MATAIFA:

3859
0
SHARE

*Lengo la dunia ya amani kizungumkuti

* Mabadiliko ya mfumo lazima kudumisha amani ya kweli

 NA HILAL K. SUED

Jana, Oktoba 24 Umoja wa Mataifa (UN) ulifikisha miaka 73 tangu kuundwa kwake kutokana na majivu ya Vita Kuu ya Pili, vita ambayo ilileta madhara makubwa zaidi katika historia ya dunia – kwani hadi kwisha kwake ilisababisha vifo zaidi ya 50 milioni – wapiganaji na raia.

Nchi zilizokuwa huru za dunia – zipatazo 50 tu wakati ule, zilikutana San Francisco, Marekani na kutia mktaba uanzishwaji wa Umoja huo (UN Charter) ambao sasa hivi una wanachama 192. Kimsingi Umoja huo ulirithi Muungano wa Mataifa (League of Nations) ulioundwa baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914 – 1918), muungano ambao hata hivyo ulishindwa kuzuia vita kubwa kuibuka tena duniani baada ya miaka 20 tu.

 

Nchi wanachama wote wa umoja wa mataifa huchangia fedha kufanikisha shuhuli zake, ambazo ni pamoja na ile ya awali ya kulinda amani ya dunia, lakini sasa inajumuisha pia kulkinda haki za binadamu, kutilia mkazo maendeleo ya kijamii nay a kiuchumi, na kutoa misaada duniani kote kutokana na majanga kama vile ya njaa na yale ya kiasili na mapigano ya kutumia silaha.

Kwa mfano sasa hivi Umoja wa Mataifa unagawa misaada ya chakula kwa nchi zipatazo 80 duniani, unatoa chanjo kwa asilimia 45 ya watoto hivyo kuweza kuokoa maisha ya watoto milioni 3 kila mwaka duniani kote. Umoja wa mataifa pia hutoa hifadhi ya kibinadamu wakimbizi milioni 63 wanaokimbia vita, majanga ya njaa na ukandamizaji na mamlaka zao za utawala. Lakini kikubwa kabisa Umoja wa mataifa una askari wake 117,000 katika operesheni 15 katika nchi nne tofauti.

Lakini hata hivyo bado Umoja wa Mataifa hauko imara – kimuundo na kiutekelezaji, kama nitakavyoeleza hapo mbele – unahitaji marekebisho makubwa.

Kwanza kabisa si kila nchi mwanachama huuangalia Umoja wa Mataifa kwa jicho chanya. Nchi Mataifa yenye nguvu kubwa za kijeshi duniani, Marekani na Urusi (tangu enzi za Urusi ya Kisovieti), zimekuwa katika mstari wa mbele katika kukiuka maazimio kadha ya Umoja huo kupitia Baraza lake la Usalama (UN Security Council).

Lakini Marekani, nchi ambayo makao makuu ya Umoja huo uko katika ardhi yake (mji wa New York) ndiyo inaongoza katika hili na hasa katika maamizimio yanayohusu mzozo wa muda mrefu wa Mashariki ya Kati – wa Israel na Wapalestina.

Ukitaka kufahamu namna Marekani inavyoutazama Umoja wa Mataifa angalia idadi ya watalii wanaozuru majengo ya taasisi hiyo yaliyopo jijini New York, na hasa watoto na wanafunzi wa shule.

Wakati wa majira ya joto (summer) mtiririko wa mabasi ya watalii huteremsha wanafunzi na watu wengine kutoka nchi mbali mbali hususan kutoa Afrika, Asia, Ulaya na Amerika ya Kusini.

Ni mabasi machache sana huteremsha wanafunzi wa Kimarekani. Marekani hujifanya kama vile Umoja wa Mataifa haupo, na kama upo basi hauna maana kubwa kwa watoto wake.

Kwa mfano, ni Wamarekani wachache sana wanaufahamu kwa undani mkataba uliounda Umoja huo (UN Charter) au ambao wamelisoma Azimio la Haki za Binadamu la mwaka 1948 (Universal Declaration of Human Rights).

Katika makala yake iliyochapishwa katika gazeti maarufu la New York Times miaka mitatu iliyopita Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter alikumbusha kwamba azimio hilo ndilo limekuwa mwongozo kwa wanaharakati wa haki za binadamu duniani kote ambao wamekuwa wakipambana na tawala za kidikteta na kusimika tawala za sheria.

Alisema: “Inasikitisha kuona kwamba badala ya kuiimarisha misingi hii, sera za serikali yetu (wakati huo serikali ya Obama) katika kupambana na ugaidi inakiuka moja kwa moja vifungu 10 kati ya 30 vya Azimio hilo, vikiwemo vile vinavyokataza utesaji wa binadamu.”

Lakini ukweli ni kwamba ni wanasiasa na wanahabari wachache sana wa Marekani wanaoweza kuvitaja angalau vifungu vitano tu kati ya 30 vya Azimio la Haki za Binadamu.

Na tukizungumzia masuala hayo ya haki za binadamu, ukiukwaji wake umekuwa ukiongezeka duniani na hivyo kuibua mifarakano pamoja na vita vya wenyewe wenyewe au baina ya mataifa.

Katika mingi ya mifarakano na vita hizo Marekani yenyewe imekuwa inatuhumiwa kuwa ni chanzo au mshiriki mkuu – mshiriki wa moja kwa moja au kwa uwakala (proxy). Hapa tunazungumzia vita zinazoendelea sasa hivi kama vile Afghanistan, Iraq, Yemen na Syria, vita ambazo zilitakiwa kutokuwepo iwapo Umoja wa Mataifa ungekuwa imara – kimuundo na kiutekelezaji.

Croesus, aliyekuwa Mfalme wa taifa la Wayunani katika karne ya tano alinukuliwa akisema: “Wakati wa amani vijana huwazika wazazi wao, lakini wakati wa vita wazee huwazika vijana wao.”

Hivyo ndivyo ukweli kuhusu vita, ingawa amani nayo ina mapungufu yake kwani imekuwa ikileta hisia kwamba vita haisuluhishi chochote – na kwamba mara nyingi kushinda vita kuna athari sawasawa na kushindwa. Lakini wengi wanaafiki kwamba hali ya amani ni bora kuliko vita.

VITA DHIDI YA UGAIDI

Katika miaka ya karibuni, na hasa baada ya tukio la kigaidi la ulipuaji mabomu majengo mjini New York Septemba 11 2001, nchi za magharibi zikaanzisha vita dhidi ya ugaidi. Ugaidi ni hali ambayo haikuwapo wakati Umoja wa Mataifa unaanzishwa hivyo kushughulikiwa kwake kumeleta changamoto kubwa. Bush, alisema anapambana na ugaidi alipoanzisha vita Afghanistan mwishoni mwa 2001 kwa kile kilichoelezwa kumsaka Osama bin Laden, kiongozi wa Al-qaeda aliyetajwa kuwa ni mhusika mkuu wa tukio la York Septemba 2011.

>>>>>Hivyo dunia iliaminishwa na akina George W Bush na Tony Blair kwamba vita ya namna hiyo – ya ugaidi – ni vita halali – kwa ajili ya kuleta haki na amani duiani.

Hata hivyo wachunguzi wengine wa mambo wana mtazamo kwamba hata vita ya kawaida nayo ni ugaidi tu. Na Bush, katika kuhalalisha vita yake hiyo alitoa tafsiri ya ugaidi kwamba ni vitendo vyote vya mauaji ya watu wasio na hatia vinavyofanywa na mtu au kikundi cha watu kwa malengo ya kisiasa.

Lakini ukweli ni kwamba uvamizi wa Iraq uliofanywa na Marekani nao pia ulikuwa ni ugaidi kwani walikufa watu wasiokuwa na hatia na kwamba malengo yake yalikuwa ni ya kisiasa pia.

Kama nia ya magaidi ni kufikia malengo kisiasa kwa kutumia njia ya kuua watu wasio na hatia, vivyo hivyo kwa wanaoendesha vita za kawaida katika nchi mbali mbali ambako raia wasio na hatia wanauawawa kwa kudondoshea mabomu kutoka angani – katika kuyafikia malengo yao ya kisiasa.

Tofauti iliyopo na kwamba “magaidi” hutumia zana ambazo nchi za magaharibi zinataka dunia izione kwamba ni za kishenzi, na huua watu kwa njia ya kikatili yenye kukosa ustaarabu. Swali hapa ni je, kuna ustaarabu wowote katika uendeshaji vita? Hivi kweli kuna kuua kistaarabu na kusiko kistaarabu?

Hivyo dunia inapoadhimisha miaka 73 ya uwepo wa Umoja wa Mataifa, dunia hiyo hiyo imetapakaa maeneo ya migogoro na vita ambako watu wasio na hatia wanauawa kila siku bila ya sababu yoyote ya msingi.

Na inasikitisha kuona kwamba mataifa makubwa yenye nguvu ambayo mataifa madogo na yaliyo dhaifu yangetarajia kupata miongozo ya kuepukana na migogoro, hayatoi miongozo hiyo kwa dhati, na badala yake yenyewe ndiyo yanaonekana “wakorogaji” wakubwa.

Dunia ina historia inayoonyesha kwamba wakati mataifa yanapokuwa na nguvu, yanajikuta hayatendi haki, na pale yanapotaka kutenda haki yanajikuta ni dhaifu.

Ni hali inayosikitisha, lakini ndiyo iliyo halisi – kutoweka kwa dunia yenye kusimamia haki, na pia ni kumbusho kwamba amani haitenganishwi na haki, kwani ziku zote amani ni zao linalotokana na haki.

BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA

Hata hivyo Umoja huo umeshindwa kwa sababu chombo chake kinachosimamia amani duniani – Baraza lake la Usalama – linadhibitiwa na mataifa makubwa ambayo, kama ilivyo tija, kwanza huangalia masilahi yao.

Ili kuhakikisha dunia ya amani Umoja wa Mataifa sharti ukubali kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wake ambao haujabadilishwa tangu uanzishwe. Mabadiliko yanatakiwa yatoe sauti kwa mataifa mengine katika maamuzi yake – kuhusu masuala ya vita na amani.

Lakini kila mara suala hili (la mabadiliko) linapoibuliwa ndani ya Umoja huo kwa majadiliano, mataifa makubwa yanapinga vikali. Mwaka huu pia suala hilo linatarajiwa kuibuliwa katika vikao vya Umoja huo vinavyoendelea.

Mapema 2009 wakati George W Bush anaondoka Ikulu ya nchi na hivyo kuondoka kutoka medani nzima ya dunia aliyokuwa akitamba nayo kwa miaka minane – aliushangaza ulimwengu alipokiri kwamba ile vita yake ya “kushtua na kupumbaza” (shock anda awe) dhidi ya Iraq ilikuwa ya kimakosa.

Alikiri hivyo bila aibu yoyote katika mahojiano na chaneli ya ABC, mwezi mmoja tu kabla ya mrithi wake, Barack Obama kuapishwa kuwa rais wa 44 wa nchi hiyo. Alianzisha vita dhidi ya Saddam Hussein baada ya kuyapuuza maoni ya Umoja wa Mataifa na ya dunia nzima kwa kuzikubali ripoti za kintellijensia zisizokuwa sahihi – kwamba nchi hiyo ya Mashariki ya Kati ilikuwa inamiliki silaha za maangamizi.

Kwa maneno mengine Bush alikumbatia tetesi tu katika kupeleka askari wake Iraq ambako kati yao zaidi ya 4,000 waliuawa pamoja na malaki ya Wairaq. Tusisahau kwamba Bush alipuuza maoni ya Umoja wa Mataifa na ya dunia nzima katika uamuzi wake dhidi ya Iraq.

Na alichoanzisha kule Iraq hadi leo kinaendelea, nchi haijatulia kabisa – maelfu ya watu wamekuwa wakiteketea katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, pamoja na kusababisha kuibuka kwa makundi mengine ya kigaidi hususan lile la Kiisilamu la ISIS ambalo nalo limesababisha mauaji makubwa – si ndani ya Iraq pekee, lakini sehemu nyingine pia na linaendelea kufanya hivyo. Umwagaji damu ambao chimbuko lake ni hatua ya Bush kuivamia Iraq pia yanaendelea Yemen, Syria, Mali na Nigeria.

Matokeo yake ni kuendelea kuwepo kwa dunia isiyokuwa na haki na mauaji. Na mataifa makubwa haya yana jeuri ya hata ya kufanya harakati za kuwaonesha viongozi wao kuwa ndiyo machampioni wakubwa wa kuleta amani aduniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres

OBAMA NA TUZO YA AMANI YA NOBEL

Chukua mfano wa Marekani. Madai yake ya kuwa championi wa amani unakinzana na hoja moja: kwamba katika miaka 72 tangu kuundwa kwa Umoja wa Mataifa, kipindi ambacho kiliiweka nchi hiyo kuwa mbele katika masuala ya dunia, ni rais mmoja tu wa nchi hiyo aliyetunukiwa Tuzo ya ya Amani ya Nobel (Nobel Peace Prize) akiwa madarakani. Mtu huyo ni Barack Hussein Obama ambaye alipata Tuzo hiyo mwaka 2009, hata hajamaliza mwaka mmoja tangu aingie madarakani.

Uamuzi wa Kamati ya Nobel ya kumpa Obama Tuzo uliibua utata mkubwa kwani ilidaiwa alitunukiwa kutokana na ahadi zake za kuanzisha ukurasa mpya wa maelewano baina ya mataifa duniani. Hivyo alitunukiwa kutokana na ahadi tu.

Na bila kukawia aliwasuta waliomtunuku Tuzo hiyo, kwani mwezi mmoja kabla ya kwenda Oslo, Norway, kuichukua (mwishoni mwa 2009) alitangaza azma yake ya kuongeza askari zaidi kule Afghanistan kupambana na wapiganaji wa kikundi cha Taliban — kwa maneno mengi alikuwa anapanga kufanya mauaji zaidi nchini kule – kilomita 10,000 nje ya mipaka ya nchi yake.

Hivyo alipokwenda Oslo alipata tabu sana mbele ya waandish wa habari alipoulizwa: “Umekuja hapa (Oslo) kuendeleza vita katika hafla inayohusu amani?”

Na mapema mwaka 2014 pale Obama alipokuwa anatarajiwa kutoa uamuzi wa kuwashambulia wapiganaji wa ISIS waliokuwa wametwaa maeneo kadha ya Iraq, mwandishi mmoja Peter Lee katika makala yake katika gazeti la Washington Post aliweka dhihaka; “Je Obama atakuwa amevalia T-shirt ya “Nobel Peace Prize” wakati anatia saini amri ya kufanya mashambulizi hayo?”

UTATA MAHAKAMA YA ICC

Utata mwingine unaoiweka Marekani katika azma ya kusimika amani duniani unajionyesha katika jukwaa jingine – Makama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (International Criminal Court -ICC). Hii ni mahakama ya dunia chini ya udhamini wa Umoja wa Mataifa, iliyoanzishwa maalum kuwafungulia mashitaka viongozi wa mataifa duniani na watu wengine kuhusu uhalifu wa kivita na dhidi ya binadamu kupitia vita na utesaji.

Marekani yenyewe haina imani na mahakama hiyo ingawa ilikuwa mmoja wa waliotia saini mkataba ulioianzisha (The Rome Statute). Kwa kusisitiza tu, aliyekuwa rais wa Marekani wakati huo, George W Bush alitoa onyo kali kwa nchi yoyote duniani ambaye itamkamata raia wake yoyote, popote pale na kumpeleka katika mahakama hiyo – kwamba itaona cha mtema kuni.

Na hivi majuzi tu Utawala wa sasa wa Donald Trump umeibua vita ya maneno dhidi ya Mahakama ya ICC kwa kuwatishia kuwawekea vikwazo majaji wake, na hata kuwafungulia mshitaka nchini humo iwapo wataendelea na uchunguzi wao dhidi ya makosa ya kivita yanayodaiwa kufanywa na askari wa Marekani nchini Afghanistan.

Lakini ajabu ni kwamba Marekani hiyo hiyo, kupitia kiti chake cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imekuwa ikishiriki vikao vyote vya chombo hicho vilivyotoa maagizo kwa ICC kutoa hati za kukamatwa viongozi wa mataifa wanaotuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita. Mfano mmoja ni utoaji hati ya kukamatwa kwa rais wa Sudam Hassan Al-Bashir.

Utata wa aina hii hauwezi kuifanya Marekani kuwa ni championi wa dhati wa kuhimiza amani duniani. Isitoshe watu wengi wamekuwa wakihoji: kwa yale waliyotenda nchini Iraq, kwa nini George W Bush na Tony Blair hawakamatwi na kufikishwa kwenye Mahakama hiyo?