Home Makala MIGOGORO YA WALIMU, WANAFUNZI IPATIWE UFUMBUZI

MIGOGORO YA WALIMU, WANAFUNZI IPATIWE UFUMBUZI

1979
0
SHARE
Baadhi ya walimu wakiandamana

NA NASHON KENNEDY


WAKATI nasoma shule ya msingi na sekondari, mimi na wanafunzi wenzangu tuliwaheshimu na kuwaogopa sana walimu kuliko hata wazazi wetu.

Kuna wakati mama alinizuia nisiende shule, na badala yake niende shambani kupalilia, lakini nilikataa na kutoroka kwenda shuleni. Hali hiyo haikuwa kwa upande wangu tu, hata pale nilipofanya kosa wazazi wangu walitishia kunishtakia kwa mwalimu wangu.

Nakumbuka kipindi hicho nilikuwa sipendi kukutana ana kwa ana na walimu wangu. Walimu wa miaka hiyo walikuwa wanafanyiwa kazi na wanafunzi bila ya kushurutishwa wala kusukumwa kuliko wazazi wa wanafunzi.

Walimu, tofauti na baadhi yao wachache ambao hawakuwa na maadili, walikuwa ni wenye nidhamu ya hali ya juu, walionekana kuwa kama wazazi wa uhusika wa kweli kwa wanafunzi na zaidi walijituma kufundisha na waliipenda kazi yao.

Hali hiyo ilitufanya miongoni mwetu tujenge uroho wa kutamani kuajiriwa katika kada ya ualimu baada ya kuhitimu elimu yetu. Si hilo tu, tuliiga hata mwenendo wa kuzungumza, kuvaa na mambo mazuri wanayofanya walimu, kwani tuliamini yapo kwao tu.

Jamii ilijenga utamaduni wa kuwasaidia walimu katika shughuli za shamba na nyingine, kwani iliamini mwalimu kutokana na umuhimu wake kwao alistahili kupata huduma hizo.

Ushahidi wa mambo haya ulidhihirika pale wazazi walipojitokeza kwa wingi kuhudhuria mikutano ya wazazi, walimu na wanafunzi kila mwisho wa mwaka, kila mtu alifahamu wajibu na majukumu yake kwa wakati huo.

Lakini kwa miaka ya hivi karibuni hali imekuwa tofauti kabisa. Jamii inaiona taaluma ya ualimu kama ajira mbadala baada ya mtu kukosa ajira muhimu aliyokuwa anaitaka kwa udi na uvumba.

Nikiwa kwenye daladala naelekea kwenye kituo changu cha kazi hivi karibuni jijini Mwanza, mwanamke mmoja alikuwa anaongea na ndugu yake kwa njia ya simu, akimlalamikia kwa kijana wake aliyehitimu chuo kikuu kukosa ajira.

Lakini kabla hajakata simu, mwanamke yule alisema, na hapa namnukuu “Yupo tu nyumbani, amekosa hata ka- ualimu”, mwisho wa kumnukuu. Mtazamo wa jamii kwa sasa unaiona taaluma ya ualimu kama ni ajira mbadala pale mtu anapokosa ajira muhimu anayoitaka.

Huu ni mtazamo hasi, hauna budi upigwe vita na kila mmoja wetu katika jamii yetu. Ninayeandika makala hii nimefikia hapo baada ya kupewa misingi mizuri ya elimu na walimu wangu kiasi cha kuwa na uwezo wa kufanya kazi hii ya uandishi wa habari.

Kuwajenga vijana wetu kisaiokolojia kwa kuwatafutia ajira ya ualimu kwa wanaofeli elimu ya sekondari au chuo ni kujenga mfumo mbovu wa elimu nchini na zaidi ni kujenga taifa mbumbumbu ambalo halitakuwa na watalaamu wa kutosha kwa siku za baadaye.

Mataifa makubwa duniani yenye uchumi mkubwa wa viwanda yamefanikiwa kufika hapo yalipo kutokana na kuwekeza zaidi katika elimu na kuwa na wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali.

Hali hiyo imeyafanya baadhi ya mataifa hayo kujiamini zaidi, hasa kwenye maeneo ya uendeshaji wa kisekta, sayansi na teknolojia, ukuaji uchumi kutokana na kuwa na wataalamu ambao si wa kutilia shaka.

Tofauti na hapa nchini, elimu bora katika mataifa hayo hupatikana kwenye shule na vyuo vya umma (Serikali) ambapo hapa nchini elimu bora hupatikana kwenye shule za msingi na sekondari za binafsi.

Hali hiyo imewafanya baadhi ya Watanzania na viongozi kuthamini zaidi kuwapeleka watoto wao kusoma nje ya nchi bila kutambua kuwafanya watoto kusoma huko kutasababisha wanakili mila na tamaduni za kigeni na kukosa uzalendo katika nchi yao kwa siku za baadaye.

Lakini pia wanaziboresha nchi hizo kiuchumi kupitia ada wanazowalipia watoto wao ambazo zingeingia kwenye pato la taifa na zikafanya maendeleo.

Kwa wakati huu ambao Serikali ya awamu ya tano inatoa elimu bure, uende sambamba na kujenga mazingira mazuri ya kufundisha kwa walimu wetu.

Matukio ya hivi karibuni na baadhi yaliyotokea mwaka jana imekuwa ajenda inayotangazwa karibu na vyombo vyote vya habari habari nchini.

Kutokana na kuongezeka kwa matukio ya walimu na wanafunzi kuwa katika ugomvi ambao hauishi, ndiyo sababu ya kuandika makala haya na hivyo kufanya walimu kutothaminiwa katika jamii.

Matukio haya yanadhalilisha walimu hapa nchini. Yanapotokea mamlaka zenye dhamana ya ualimu hazichukui hatua za haraka kuwasaidia walimu au wanafunzi wanaokuwa wamefanyiwa ukatili.

Baadhi ya walimu na wanafunzi wameathirika kisaikolojia na baadhi yao wanajuta kuajiriwa kwenye taaluma na wanafunzi nao wanashindwa kusoma kutokana na kuathirika pia.

Tukio la mwaka jana la wanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Usevya, iliyoko mkoani Katavi la kumshambulia Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Makonda Ng’oka, linaonyesha matatizo yanayowakumba walimu.

Aidha, tukio la hivi karibuni la wazazi katika Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa kumdhalalisha mwalimu Musa Mkalambosa wa Shule ya Msingi Kipanga kwa kumcharaza fimbo mbele ya wanafunzi, wakimtuhumu kuwaadhibu watoto kwa kuwabebesha matofali, ni tukio la udhalilishaji walimu.

Nimpongeze Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura, kwa kutoa agizo la kukamatwa kwa wazazi hao, ili wafikishwe mahakamani na kuagiza mwalimu aliyefanyiwa ukatili ahamishiwe kituo kingine cha kazi.

Kwa tukio la Mwalimu Makonda ambapo pia walimu wengine walijeruhiwa sana baada ya kuvamiwa na wanafunzi wao, tuliona mamlaka zinazohusika na elimu zilichelewa sana kuchukua hatua. Mwalimu Ng’oka alituhumiwa kwa kuwafanyia vitendo vya ukatili wanafunzi wa kiume katika shule hiyo.

Kwa walimu wanaopata matatizo yanayofanana na ya Mwalimu Ng’oka hapa nchini na wanafunzi wanaolawitiwa na kujamiiana na wanafunzi na wengine kuchapwa wakitembezwa uchi kwa wanafunzi wenzao, hili limekuwa ni tatizo kubwa hapa nchini.

Kushambuliwa kwa walimu na wanafunzi  kwa sasa kunatokana na sababu nyingi, kubwa ikiwa ni ya kimaadili na elimu anayoipata mwalimu.

Serikali iangalie upya muundo wa utoaji wa mafunzo kwa walimu ili kuona kama yanakidhi mazingira ya sasa, ili kumjenga mwalimu kimaadili na kutoa ajira kwa  walimu sawa na ikama ya wanafunzi.

Hata kama atakuwa amepata shahada ya juu katika fani ya ualimu na kujua kusoma lugha zote, mwalimu lazima atambue kuwa, yeye ni mzazi kwa watoto anaowaongoza.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Elimu kwa miaka saba iliyopita, inaonyesha kuwa uwiano kwa mwalimu na wanafunzi ulikuwa 1:37, ikiwa ni tofauti na uwiano wa miaka mitatu nyuma wa 1:53.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chama cha Walimu Tanzania ( CWT) wa mwaka jana, Tanzania ina shule za msingi 15,000 ambazo zina jumla ya walimu 200,000, wakati mahitaji yake halisi ni walimu 300,000, ikiwa na upungufu wa walimu 100,000.

Kwa mujibu wa utafiti huo, shule za sekondari zilizopo ni 4,650 zenye walimu 85,000, wakati mahitaji ya shule hizo ni walimu 135,000 na hivyo kuna upungufu wa walimu 50,000, yote haya yanachangia kuwapo kwa matatizo ya walimu nchini.

Pamoja na juhudi kubwa ambazo wamekuwa wanakabiliana nazo walimu, bado wanakosa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wazazi, watendaji na viongozi wa kisiasa, hali iliyodidimiza kuwapo kwa motisha na morali ya kufundisha kwa walimu katika kuleta mabadiliko chanya ndani ya shule na kijiji (jamii).

Mwalimu ni mzazi wa pili, ndiye anayekaa kwa muda mrefu na mwanafunzi, tofauti na mzazi, hivyo tuhuma zinazotolewa na wanafunzi za baadhi ya walimu kuwataka mahusiano ya kimapenzi zisipuuzwe.

Aidha, bodi na kamati za shule ziongozwe  na watu wenye weledi, staha na uvumilivu wa kujua upana wa taaluma ya elimu na ile ya ualimu na namna ya kushughulikia matatizo ya walimu.

Wenyeviti wa bodi za shule za sekondari wawe ni watu wenye kiwango cha elimu cha kuanzia shahada ya kwanza ili waweze kuziongoza vyema shule hizo na kutoa maamuzi ya haki na stahiki kwenye migogoro inayowapata walimu na wanafunzi wao.

Nasema hivyo kwa sababu, kuna baadhi ya maeneo hapa nchini, baadhi ya wenyeviti wanaochaguliwa kuongoza bodi za shule za sekondari huchaguliwa kutokana na sifa ambazo hazikidhi vigezo vya kitaaluma.

Wengine huchaguliwa (hasa kwa upande wa sekondari za kata) kutokana na umaarufu wao katika jamii, uwezo wa kifedha na baadhi yao ni wahitimu wa darasa, na hawa baadaye hushindwa kutatua migogoro inayoendelea kwa hivi sasa.

Kama Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya sekondari ni mhitimu wa darasa la VII, atakuwa na uwezo gani wa kutatua tatizo la kitaaluma baina ya walimu na wanafunzi, au mwalimu na uongozi wa shule?

Maana migogoro mingi ya walimu na wanafunzi katika shule zetu na vyuo ni ya kitaaluma zaidi. Imefikia wakati baadhi ya wanachuo kugomea mitihani ya majaribio kwa madai kuwa iko nje ya mitaala ya elimu!

Je, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya sekondari ambaye ni mhitimu wa darasa la saba atakuwa na uwezo gani wa kusuluhisha migogoro ya aina hiyo ya kitaaluma?

Taaluma ya ualimu ni taaluma nyeti ambayo haina mbadala wake. Mwasisi wa taifa hili, Hayati Mwl Julius Nyerere, kitaaluma alisomea ualimu, ambapo alifundisha Shule ya Sekondari Pugu na Rais wa awamu ya pili Ally Hassan Mwinyi naye ni Mwalimu na viongozi wengine wa juu wa kitaifa, akiwamo Rais John Magufuli, ni walimu kitaaluma.

Upatikanaji wa elimu bora unategemea mambo mengi sana, mitaala bora, miundombinu imara, ikama inayotosheleza ya walimu, wanafunzi na utayari wa jamii wa kumruhusu mtoto kupata elimu, lakini pia ufumbuzi wa kudumu wa migogoro iliyopo kwa sasa, kubwa likiwa ni kuwajenga wasomi wetu katika misingi ya weledi ya kuthamini utu na uzalendo ili baadaye wawe wafanyakazi bora wa nchi yetu.

MWISHO

0756 823 420/0784 822 407