Home Michezo Kimataifa MIGUU YAO ITAZIBEBA TIMU ZAO EPL

MIGUU YAO ITAZIBEBA TIMU ZAO EPL

1047
0
SHARE

KELVIN LYAMUYA NA MITANDAO

MSIMU mpya wa Ligi Kuu England umeanza kwa kasi sana ambapo timu ya Manchester United imeonesha nguvu yao katika kipindi hiki cha awali kabisa kwa kushinda mechi mbili mfululizo.

United ilianza harakati zao za kusaka taji la ligi hiyo kwa kutoa vichapo vya mabao manne-manne dhidi ya West Ham na Swansea. Hiyo ni jumla ya pointi sita na mabao nane bila nyavu zao kutikiswa.

Kucheza ni jambo la kwanza lakini kutafuta ushindi ni jambo lingine. Ushindi huo unapatikanaje bila ushirikiano wa wachezaji uwanjani? Hilo ni swali la msingi sana.

United isingeweza kushinda michezo yao miwili bila ushirikiano wa wachezaji, na sio wachezaji tu, bali wachezaji bora.

Moja ya kitu muhimu kwenye mchezo wa soka ni kombinesheni ya wachezaji uwanjani. Sio mbaya pia tukisema ni roho ya timu nyingi za soka. Kuongezeka kwa idadi ya nyota wanaoelewana uwanjani kumezidi na kufanya timu hizo kufanya mambo makubwa.

Kiungo Paul Pogba na straika Romelu Lukaku wameshaonesha wazi kuwa watakuwa ni wachezaji muhimu sana kwa United msimu huu kutokana na kiwango kikali wanachokionesha uwanjani sambamba na uelewano mzuri.

Ndani ya uwanja, Lukaku ndiye mchezaji bora ambaye Pogba alikuwa akimuota ndani ya jezi ya United. Anapambana na mabeki, anashirikiana vizuri sana na viungo, soka lake ni la mbele kwa mbele na zile pasi za Pogba sasa zimeshapata mtumiaji mzuri.

Lukaku sio mchezaji mwenye chenga za maudhi lakini nguvu, uwezo wa kujipanga vizuri katika eneo la hatari litamfanya afunge mabao mengi sana, na Pogba huenda akamaliza msimu kwa na idadi nzuri ya pasi za mwisho zilizozaa mabao.

Hadi sasa, Lukaku ana jumla ya mabao matatu, huku Pogba akiwa nayo mawili. Ndio kwanza mechi mbili zimeshachezwa lakini kuna mengi ya kuyasubiri kutoka kwa wawili hao.

Kwa upande wa mahasimu wao, klabu ya Liverpool ambayo ilishinda bao 1-0 dhidi ya Crystal Palace mapema wiki iliyopita, ina nyota wawili ambao bila shaka watakuwa msaada mkubwa kwao msimu huu.

Liverpool ilitarajiwa kurudiana na Hoffenheim ya Ujerumani wiki hii, hivyo kutokana na changamoto ya kushiriki michuano hiyo ilibidi wasajili wachezaji bora, mmojawapo akiwa ni Mohamed Salah.

Winga huyo tayari ameshaunda ushirikiano safi na mshambuliaji mwingine wa Liverpool, Sadio Mane ambaye alikuwa akitegemewa na klabu hiyo kutokana na upungufu wa mchezaji mwingine mwenye kasi zaidi yake.

Wachezaji hao ndiyo silaha kubwa za Liverpool kwa sasa. Wamezoeana haraka kuanzia ‘pre season’ na wanategemewa kufanya makubwa msimu huu katika mfumo wa Jurgen Klopp unaotumia washambuliaji watatu. Hadi sasa wameshafunga jumla ya mabao manne, Mane akifunga matatu na Salah moja.

Upande mwingine wa washika mitutu wa London, Arsenal, hali inaonena kuwa tete kidogo lakini ujio wa straika Alexandre Lacazette unahitaji muda hadi kuja kuwa na faida.

Straika huyo anatajwa kama mtu muhimu sana kwa kiungo Mesut Ozil ambaye ni mbunifu bora wa Arsenal katika miaka yote aliyoichezea klabu hiyo.

Ozil anasifika kwa upigaji wa pasi maridadi za mwisho na alikosa kuivunja rekodi yake ya kutoa pasi nyingi za mabao katika msimu wa 2015/16 kutokana na ubovu wa Olivier Giroud katika umaliziaji.

Lakini kwa Lacazette ambaye anaongoza kwa kuwa na wastani mzuri wa kufunga mabao katika mashuti aliyopiga, akiwa na asilimia 39 za mashuti yenye faida zaidi ya mastraika wa ligi tano kubwa za Ulaya, Arsenal itakuwa na safu nzuri ya wachezaji wawili wenye ushirikiano bora ndani ya miaka miwili au mitatu ijayo.

Msimu uliopita Chelsea ilinyakua ubingwa kutokana na uhakika wa ulinzi kutoka kwa N’Golo Kante na Nemanja Matic kwenye kiungo cha kukaba.

Na sasa wameziba pengo la Matic kwa kumnasa kiungo kinda, mwenye kasi na nguvu, Bakayoko ambaye ataunda ukuta mgumu katikati na Kante. Kutokana pia na uwezo wa Bakayoko wa kusogea mbele na mipira, Chelsea itaendelea kuwa na nguvu kuanzia nyuma.

Man City haikuwa na mabeki wazuri sana wa pembeni hasa upande wa kulia lakini walifanikiwa kutumia zaidi ya pauni milioni 100 kutatua changamoto hiyo huku wakiongeza nguvu upande wa kulia wa mashambulizi.

Beki wa kulia, Kyle Walker na winga ya Kireno, Silva ambaye alikuwa aking’ara na Monaco watakuwa silaha ya siri kwa Pep Guardiola katika kuifungua minyororo ya wapinzani kutokea upande wao huo wakitumia kasi na akili nyingi.