Home Makala Mihadarati, viroba sumu inayoangamiza taifa  polepole

Mihadarati, viroba sumu inayoangamiza taifa  polepole

1035
0
SHARE

Na Balinagwe Mwambungu

VIROBA na mihadarati ni kama mapacha. Hupatikana kila mahali, ingawaje mihadarati huapatikana kwa kificho. Lakini viroba, huhitaji kwenda dukani au kwenye baa—vipo kila kona, hata kwenye vituo vya daladala, stendi kuu zote na kwenye vichochoro.

Jina kiroba limetokana na mfuko wa unga wa kilo hamsini wenye ujazo wa kilogramu 50. Viroba sasa ni vifungashio vya vitu mbali mbali ikiwemo sukari, maharage, mahindi, karanga, njegere na bidha nyingine za viwandani.

Lakini vifungashio vidogo ya plastiki vyenye mils kati ya 100 na 50 za pombe kali kama vile Konyagi na Kiroba Original, vimebadili matumizi ya neno kiroba. Labda imetokana na ukweli kwamba wanywaji wa ‘viroba’ huchoka haraka kana kwamba walikuwa wanabeba mizigo katika viroba.

Hii ni  kwa sababu wanavyonza pombe hizo kali bila kuchanganya na kitu chochote. Wanywaji wengine hupenda kunywa viroba vya konyagi, kwa sababu bei yake ni nafuu ukilinganisha na bia, na wengine ndio kinywa murua kwao. Lakini wanakunywa kwa ustaarabu.

Baadhi ya wanywaji wanasema ni vizuri kunywa vinywaji vikali baada ya kula. Wengine wanasema hawanywi konyagi kavu kavu. Lazima wachanganye na soda au maji ili kupooza makali. Lakini vijana wengi wanakunywa viroba bila kula na bila kuchanganya na kitu chochote na wanaonekana kuathirika kiafya—wamedhoofu, mabega yao yamepanda na nywele ambazo rangi yake ni nyeusi, zinaonekana kupoteza uasilia. Pombe kwa ujumla wake zina madhara kwa afya ya binadamu na si nia ya makala haya kutaja zote, lakini kubwa ni kwamba hata madaktari wanaonya wateja wao kwamba wanywe kwa umakini ili kulinda afya zao.

Lakini inaeleweka kwamba kunywa pombe kali bila kuipooza, mwili hupungukiwa maji unakuwa ‘dehydrated’—unapoteza maji.

Mbali na madhara hayo, viroba sasa limekuwa janga la kitaifa—vinapatikana kila mahali na kwa bei rahisi sana—kama ilivyo upatikanaji wa sigara ambazo pia zinauzwa na vijana popote. Zamani sigara na pombe viliuzwa grosari na kwenye bar tu, kwa sababu wauzaji wanatakiwa kukata leseni.

Lakini baada ya viwanda vinavyotengeneza vileo kubuni vifungashio vya karatasi ya plastiki, imekuwa rahisi kwa yeyote anayetaka kununua. Vijana wananunua na kunywa viroba hapo hapo wakiwa wima, au huweka mfukoni na kufyonza taratibu, kimoja baada ya kimoja.

Viroba havijapangiwa muda maalumu wa kunywa, iwe alfajiri, alasiri au usiku wa manane, anayetaka kunywa atakunywa. Baadhi ya madreva wanaoamsha daladala alfajiri, hununua viroba na kuvipiga hapo hapo eti apate kile wanachokiita kukata ‘stimu’—eti kuchangamsha mwili.

Lakini hii haiko kwa madereva tu, hata vijana wanaofanya vibarua, hasa wajenzi na wanaofanya kazi za shruba, huwa wanaanza na viroba. Madereva wanaoendesha malori na mabasi ya masafa marefu, hujaza pombe kali kwenye chupa za maji na kubughia konyagi huku wanaendesha.

Matokeo yake, pombe ikiingia nyingi kichwani, madereva wanakosa umakini na kuendesha kwa mwendo mkali hata sehemu wanazotakiwa kupunguza mwendo. Ajali nyingi zinatokana na madereva kupoteza umakini na kutozingatia alama za barabarani.

Upatikanaji wa viroba kwa urahisi, umeathiri kundi kubwa la vijana wengi mitaani ikiwa ni pamoja na wanafunzi, hasa wa shule za sekondari zilizopo mijini.

Ukitafiti kidogo, utagundua kwamba, baadhi ya wanafunzi wanapokwenda shule, au wakati wa mapumziko, huchepuka pembeni na kufyonza viroba—hii inawafanya kutokuwa makini darasani, pombe huwapa jeuri ya kutowatii walimu—wanatenda lolote wanalotaka na kama hakuna udhibiti, nidhamu ya shule hushuka.

Matokeo yake, shule hizo hazifanyi vizuri katika mitihani ya kitaifa kwa vile wanafunzi huwa watoro, hata wanapohudhuria madarasani, wanakuwa wapo wapo tu—badala ya kujazwa elimu na maarifa, wanabeba ‘viroba’ vichwani!

Kwa vijana waliokatika mahusiano ya unyumba, wanashindwa kuyamudu majukumu—kila siku wanarudi nyumbani wakiwa wamelewa—hufikia kitandani na kulala—hawataki usumbufu. Katika baadhi ya maeneo hapa nchini, inaripotiwa kwamba hata uzalishaji—hasa mashambani, umekuwa ukishuka—wanaume huamkia viroba wakidhani vinawapa nguvu, kumbe ni kinyume chake. Akili ikichoshwa na kilevi, mwili hauwezi kuwa na nguvu ya kufanya kazi ngumu.

Tatizo la viroba linaweza kudhibitiwa, lakini kuna tatizo linguine sugu linalowasibu vijana hapa Tanzania—dawa za kulevya. Dawa hizi zimeingia hata shuleni na vyuoni. Hili ni tatizo sio tu kwa walimu, walezi na wazazi, ni tatizo la kitaifa.

Kuna mtaalamu moja anasema kwamba tofauti na risasi ambazo zinaua mara moja, dawa za kulevya na pombe kali vinaua taratibu, bila mtu kujijua—ndio maana watengenezaji wa pombe wameweka umri wa miaka 18 kwenda juu ndio wanaoruhusiwa kuuziwa pombe.

Wanasema—drink responsibly, kunywa kwa wangalifu na sheria ya mojawapo ya Usalama Barabarani inakataza kuendesha chombo cha moto ukiwa umelewa pombe.

Biashara ya dawa za kulevya ni vigumu kuidhibiti kwa kuwa mtandao wake ni mpana na wa kificho. Ugumu wake umeongezeka zaidi baada ya kuingia mfumo wa soko huria na utandawazi. Na maendeleo ya teknojia yameifanya dunia kuwa kama kijiji.

Taifa linapoteza nguvu kazi kwa kuwa vijana wakibobea kwenye ulevi na dawa za kulevya, wanakuwa legelege, hawana msaada kwa familia zao na taifa kwa jumla.

Kwa kuwa mwisho wa siku, hata kama walikuwa na kazi, huwa wanapoteza ufanisi. Jamii yetu imeshuhudia kutoweka kwa haraka vijana walioinukia kwenye sanaa, wamegeuka kuwa mazombi.

Kijana huwa anabadilika tabia, na kama alikuwa na uwezo wa kifedha, huziharibu na kugeuka kuwa mdokozi, au akimzoea mtu fulani, anakuwa  tegemezi—ombaomba ili apate fedha kidogo za kununua kete.

Wengine huanza kuuza mali na vitu vyake kidogo kidogo, mwishowe anauza hata nguo zake. Inakuwa vigumu kumgundua mlevi wa dawa za kulevya kwa sababu anakuwa msiri. Lakini jinsi siku zinavyokwenda, na asipopata dozi, utamgundua. Anakuwa hana utulivu na anakuwa na wasi wasi.

Hivi sasa vijana wengine wako katika vituo maalumu vya kuwarekebisha—‘rehabilitation centres’ ambako wanafundishwa njia mbadala ya kuachana na dawa za kulevya.

Sisi kama taifa tunachukua hatua gani kuzuia upatikanaji rahisi wa viroba na matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana? Njia moja wapo ni Serkali kupiga marufuku vifungashio vya plastiki vya Konyagi na Kiroba Original, lakini pia Sheria ya Vileo (1968) pamoja na maboresho yake, iweke mkazo kwa kuziba mianya ya upatikanaji wa vileo .

Aidha, mtu akikamatwa anauza pombe mahali ambapo si rasmi, na wala hana leseni, akamatwe kama anavyofuatiliwa muuza mihadarati na apelekwe mahakamani.

Hili la dawa za kulevya ni ‘pasua kichwa’ dunia nzima. Tanzania imejaribu njia mbali mbali, kupambana na uingizaji na uuzwaji wa dawa za kulevya—ikiwa ni pamoja na kuunda kikosi maalumu cha kupambana na ‘wazungu wa unga’—bila mafanikio.

Rais aliyepita, Jakaya Kikwete, aliwahi kutamka kwamba alikuwa na orodha ya watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, lakini akaondoka madarakani kimya kimya bila kuwataja na kuwachukulia hatua. Kwa nini na orodha ya majina alimwachia nani?

Tunaweza kuhisi tu kwamba suala hili linawagusa vigogo wengi na huenda baadhi yao ni maswahiba wa viongozi, au ni watoto wao. Labda viongozi wetu wachukue hatua kama anazochukua Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, ambaye ametoa amri kwa vigogo wote serkalini na wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya wajisalimishe, vinginevyo vigilante—sungusungu na polisi, wawashughulikie.

Hadi mwishoni mwa mwezi uliopita, imeripotiwa kwamba watu 1,900 ambao wanahusishwa na biashara ya dawa za kulevya, wameuwawa tangu rais huyo aingie madarakani mwezi Mei, 2016.

Kuna vijana wa Kitanzania zaidi ya 200, ambao wanatumika kama punda wa kubeba mihadarati,  wanasota kwenye magereza ya Hong Kong pekee. Hadi Machi, 2015, vijana 185 walikuwa wamefungwa nchini China adi na wengine wamenyongwa huko ughaibuni kwa kosa hilo!

Wakati umefika sasa,  Bunge litunge sheria kali zaidi ili watu waogope. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, alisema mara baada ya kuapishwa Juni, 2016 kuwa ataipa kipaumbele vita dhidi ya dawa za kulevya.

Waziri Nchemba apelike muswada bungeni wenye vipengere vikali zaidi ikiwa ni pamoja na kifungo  cha maisha, na kuwafilisi vigogo watakaopatikana na hatia, ikiwa ni pamoja na wake na ndugu zao wa karibu na watoto wao—maana hawa hufaidika kwa njia moja au nyingine na matunda ya biashara hii haramu.