Home Makala MIMBA ZA UTOTONI KINYUME CHA HAKI ZA BINADAMU

MIMBA ZA UTOTONI KINYUME CHA HAKI ZA BINADAMU

4931
0
SHARE

NA FERDNANDA  MBAMILA

Tanzania ni ya tatu katika Afrika Mashariki kuwa na kiwango cha juu cha ndoa na mimba zautotoni, baada ya Uganda na Sudani Kusini.

Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) ya 2017, inaonesha kwamba Sudan Kusini ina asilimia 52 ya watoto chini ya miaka 18, wanalazimishwa kuolewa, wakati kwa Uganda ni asilimia 40, Tanzania asilimia 28 na Kenya, asilimia 23.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa Umoja wa Mataifa huchukulia ndoa za watoto chini ya miaka 18 kuwa ni ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Hii ni kwa sababu mimba za utotoni ni moja ya sababu zinazomnyima mtoto wa kike haki ya kupata elimu ya msingi.

Ripoti hiyo imeeleza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha watoto na wadau mbalimbali wakiwemo wazazi, walimu na wadau wengine juu ya mapambano dhidi ya mimba za utotoni.

Kwa kulitambua hilo Makumbusho ya Taifa, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza mradi wa mapambano dhidi ya mimba za utotoni kwa njia ya sanaa kupitia mradi wao maarufu ujulikanao kama Museum Art Explosion Against Adolescence Pregnancy.

Lengo kuu la mradi huo wenye kaulimbiu ya ‘Mtoto wa kike washa taa’, ni kutoa elimu kwa watoto walio chini ya miaka 18 husuani wanafunzi wa shule za msingi na sekondari dhidi ya kupambana na mimba za utotoni kwa kutumia sanaa mbalimbali zikiwemo za jukwaani na  ufindi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni,  Achiles Bufure anasema kuwa, mradi huu una lenga katika kutoa elimu kwa watoto, wazazi na wadau wengine juu ya mapambano dhidi ya mimba za utotoni.

Pia watoto wengi wamekuwa  wakijihusisha na ngono zembe kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukosa uelewa, mila potofu na vishawishi mbalimbali amabpo hili la uwelewa si kwa watoto tu bali hata kwa watu wazima ambao ndio wamekuwa chanzo kikubwa cha changamoto hii ndio maana tumeamua kuja na program hiyo ili tuweze kupambana na hili janga,” anasema Bufure.

Anasema kuwa kupitia mradi huo, umeweza  umeendesha mafunzo kwa wasanii, wanafunzi, walimu na wadau mbalimbali juu ya mapambano dhidi ya mimba za utotoni katika ngazi za familia hadi taifa ili kwa pamoja kuwe na nguvu moja ya kupambana na changamoto hiyo.

Akizungumza na RAI Afisa Maendeleo ya jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee  na watoto, katika mafunzo hayo, Dk. Nuru Kitara, anasema  kuwa, tatizo la mimba za utotoni ni changamoto kubwa katika nchi yetu kwa sababu watoto wa kike wamekuwa wakipata ujauzito au kuolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Aliitaja mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni kuwa ni Shinyanga kwa asilimia 59, Mara asilimia55, Dodoma asilimia 51 na Lindi asilimia 48,Mbeya kwa asilimia 45, Morogoro na Singida asilimia 42, Rukwa asilimia 40 na Ruvuma asilimia 39.

Dk. Kitara ameongeza kuwa, wasichana wa vijijini wana uwezekano wa karibu mara mbili ya wale wa mijini wa kupata watoto kabla hawajafikia umri wa miaka 19 na pia nusu ya wasichana ambao hawakupata elimu hupata watoto au mimba kabla ya kufikisha umri wa miaka 19, ikilinganishwa na asilimia 25 kwa wasichana waliomaliza elimu ya msingi.

“Watoto waliozaliwa na mama wa umri mdogo wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kupoteza maisha kuliko wale waliozaliwa na mama wa umri mkubwa, visababishi ni mimba za utotoni na kuolewa mapema ni pamoja na mila na desturi zenye madhara, uelewa mdogo wa watoto wa kike kuhusu muda na vipindi wanavyoweza kupata ujauzito na wazazi kutokutimiza majukumu yao ya malezi kwa watoto kikamilifu”. anasema Dk Kitara.

Dk. Kitara aliendelea kuzitaja sababu zingine kuwa ni baadhi ya wasichana hulazimishwa kuolewa au hukataliwa na familia zao jambo ambalo huwaweka katika hatari zaidi ya kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji na matatizo ya kiuchumi yanaweza kusababisha wasichana wadogo kujihusisha na biashara ya ngono.

“Tunahitaji kutoa elimu kwa watoto na wazazi juu ya madhara ya mimba za utotoni ili kuwaokoa watoto na janga hilo,” anasema Dk. Kitara.

Dk. Kitara anasema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kupamba na tatizo hili ikiwa ni pamoja na kusaini na kuridhia mikataba mbalimbali inayohusu haki za mtoto, kuandaa sera ya maendeleo ya mtoto na kutungwa kwa sheria ya mtoto Na.21 ya mwaka 2009.

Vile vile Serikali  imekuwa ikiendesha kampeni ya ‘Mimi msichana najitambua Elimu ndiyo mpango mzima’ iliyozinduliwa Octoba, 2017.

“Tunahitaji kutoa elimu kwa watoto na wazazi juu ya madhara ya mimba za utotoni ili kuwaokoa watoto na janga hilo.

Pia nitoe wito kwa wadau mbalimbali kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya mimba za utotoni ili kujenga Tanzania yenye maadili mema” Aliongezea Dk. Kitara.

Serikali za mitaa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zimeboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma nzuri za afya kwa vijana katika wilaya husika, kusimamia shule zote zifundishe stadi za maisha kwa kushirikiana na vyama vya kiraia.

Vile vile  kufuatilia mwenendo wa mahudhurio, ukatishaji wa masomo shuleni na kuhimiza shule zote zitilie mkazo katika kuhakikisha mahudhurio mazuri na wanafunzi wanasoma mpaka wahitimu.

Naye Amabilisi Batamula kutoka FEMINA anasema kuna haja ya kuwa na mkakati wa uhamasishaji na uelimishaji jamii wenye tija juu ya madhara ya mimba za utotoni, watoto bila kujali kuwa ni msichana au mvulana, aelewa matokeo ya mimba zisizotakiwa, wajifunze namna ya kuzuia mimba zisizotakiwa na waeleweshe marafiki zako pia wawatambua wasichana wanaopata ujauzito na kuwashawishi waendelee na masomo.

“Sanaa iwe ya jukwaani au ya maonesho ina mchango mkubwa katika kutoa elimu kwa wadau hivyo ni vyema wa sanii mliopata fursa hii, itumieni vyema katika kutoa mchango wenu kwa jamii juu ya mapambano haya ya mimba za utotoni maana Sanaa ni njia muafaka ya kufikisha ujumbe kwa jamii kwa haraka zaidi” anasema Bibi Batamula.

Mratibu wa Mradi wa Museum Art Explosion Against Adolesence Pregnancy, Edger Joel anasema katika mradi huu wa kutoa elimu kwa njia ya sanaa, aina zote za sanaa zitatumika ikiwa ni pamoja na sanaa za jukwaani na za ufundi ili kutoa nafasi kwa kila mwanajamii kujifunza kwa kupitia aina ya sanaa anayoipenda.

Anasema mwisho wa mwezi wa Septemba kutakuwa na onesho kubwa Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni ambapo wanafunzi, walimu, wazazi na wadau mbalimbali watashiriki katika onesho hilo.

“Mwishoni mwa mwezi Septemba, wakazi wa Dar es Salaam na viunga vyake watapata nafasi ya kuona maonesho makubwa ya sanaa kutoka kwa wasanii nguli hapa nchini, sanaa hizo ni pamoja na michoro, vinyago, ubunifu wa mavazi, maigizo, musiki, ngoma na majigambo mbali mbali kwenye kumbi zetu za kisasa zilizopo hapa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam, Posta,” anasema  Chatanda.

Chatanda aliongeza kuwa, baada ya maonesho ya jijini Dar es Salaam, yanatarajiwa kufanyika katika mikoa ya Shinyanga wilaya za Shinyanga vijijini, Kishapu na Kahama na Mkoa wa Tabora katika wilaya za Kaliua, Nzega na Igunga