Home Makala Miongo minne ya uhasama wa Marekani na Iran

Miongo minne ya uhasama wa Marekani na Iran

3058
0
SHARE

. Ukweli mradi wa nyuklia unavyopotoshwa

NA HILAL K SUEDJumatatu wiki hii Marekani ilirejesha rasmi vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran, vikwazo ambavyo vilikuwa vimeondolewa mwaka 2015 kufuatia maafikiano yaliyotiliwa sahihi baina ya nchi hiyo na mataifa sita ya Magharibi (likiwemo Marekani) wakati wa utawala wa Barack Obama).

 

Awali vikwazo dhidi ya Iran viliwekwa na mataifa hayo mwaka 2012 kutokana na suala la mradi wa nyuklia wa Iran ambao nchi hizo za magharibi zilidai unaweza kutengenezea zana hatari za nyuklia na hivyo kuhatarisha amani katika eneo hilo la Mashariki ya Kati ambalo hata hivyo ni eneo ambalo limekuwa halina amani tangu kumalizika kwa Vita ya Pili ya Dunia.

Urejeshwaji wa vikwazo hautuhusu nchi nyingine nne za Ulaya (Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Italia) ambazo zimesema zitaendelea kuheshimu mkataba wao na Iran wa 2012. Vikwazo vyenyewe vimelenga katika sekta ya mafuta na fedha – kuinyima Iran kuuza mafuta yake na mizunguko ya malipo ya fedha kimataifa kaetika biashara na Iran.

Iran imezoea vikwazo vinavyosukumwa na Marekani – suala linalosababishwa na uhasama kati yao uliodumu takriban miongo minne sasa. Wiki hii inaadhimisha miaka 39 kamili tangu kikundi kimoja cha wanafunzi kilipowateka maafisa 53 wa kibalozo wa Marekani katika ubalozi wao mjini Teheran.

Utekaji huo ulitokana na mapinduzi ya Kiisilamu yaliyofanyika nchini humo yaliyemng’oa Mfalme Shah Reza Pahlevi aliyekuwa swahiba na mteja mkubwa wa Marekani (pamoja na Israel) katika eneo hilo la Masdhariki ya Kati.

Mapinduzi hayo yaliletwa na maandamano tu, na yaliongozwa na kiongozi wa kidini – Ayatollah Rohulla Khomeini aliyekuwa uhamishoni Paris Ufaransa, na April 1 1979 Jamhuri ya Kiisilamu ya Iran ilitangazwa.

Baada ya Shah kukimbilia Marekani wanafunzi waliuteka ubalozi wa Marekani na kushikilia maafisa wake mateka kwa wiki kasha wakidai Shah arejeshwe Iran asimamishwe kizimbani kwa makosa mbali mbali yakiwemo ya mauaji ya wapinzani wake ulikuwa unafanywa na kikosi chake cha kijasusi cha SAVAK kikishiriana na kile cha Israel cha Mossad.

Taasisi mbili hizi zilitumika sana dhidi ya wapiganaji wa Kipalestina na hivyo baada ya Shah kung’olewa, Iran ilianzisha mahusiano na Palestina na aliyekuwa kiongozi wao, Yasser Arafat alipokelewa kwa shangwe mjini Teheran.

Kwa hiyo Marekani haikuwa inapendezwa na mabadiliko hayo na hivyo ikaanza kampeni kali dhidi ya Iran pamoja na kuitumia Iraq (chini ya Saddam Hussein) kuivamia Iran katika vita iliyodumu kwa miaka minane 1980-88.

Katika vita hiyo mamia ya maelfu walikufa kwa pande zote mbili na katika ilipofika mwaka 1984 Iraq ilikuwa inaelemewa sana na baada ya majeshi ya Revolutionary Guards ya Iran kuiangusha ngome kuu ya Iraq katika mji wa Khorromshahr magharbi mwa nchi hiyo, Marekani ikaanza kuingiwa hofu kwamba huenda Iran ingeingia na kuivamia Iraq na hivyo ikaamua kumpa Saddam Hussein zana za kemikali.

Hivyo miaka 20 baadaye mambo yalipogeuka na Marekan ikijiandaa kuishambulia Iraq hiyo hiyo hiyo ya Saddam Hussein, utawala wa George W Bush ulipokuwa unadai kwamba saddam alikuwa na zana za kemikali, ilikuwa inajua kile unachokisema ingawa hizo zana hazikuonekana. Ilidaiwa zilikimbizwa na kufichwa Syria.

Sasa hivi Rais Donald Trump amesema kwamba miongoni mwa tuhuma kadha dhidi ya Iran hadi kuirejeshea vikwazo, ni kwamba nchi hiyo inavisaidia vikundi vya madhehebu ya Shia dhidi ya utawala wa Baghdad ambao pia ni wa Kishia.

Na hili ndilo suala ambalo linaifanya Marekani isijue inachokifanya kule Mashariki ya Kati. Wakati ilipouondoa utawala wa Kisunni wa Saddam Hussein, ilijua wazi kwamba inaingiza utawala wa Kishia, utawala wa madhehebu kuu unaoiongoza Iran nchi ambayo ni hasimu wake mkubwa.

Isitoshe Marekani inashindwa kuelewa kwamba vikundi vingi anavyoviita vya kigaidi katika eneo la mashariki ya kati kama vile Al-Qaeda na ISIS ni vikundi vya Kisunni – madhehebu ya dini kuu ya Saudi Arabia na nchi nyingineza za eneo hilo.

Lakini turejee kwenye ukweli wa suala la mradi wa nyuklia wa Iran. Tofauti na miradi ya nyuklia ya nchi za India, Pakistan, Korea ya Kaskazini na Israel, ambayo hairatibiwi na Umoja wa Taifa chini ya taasisi yake ya kuratibu nguvu za atomiki (IAEA), mradi wa Iran, kama ili katika nchi za Magharibi na nyingine kama Urusi unaratibiwa na taasisi hiyo.

Na hapo ndipo nchi za magharibi zimekuwa zikipata mwanya wa kuibana Iran kutokana na uhasama uliopo baina yao, uhasama, kama nilivyotaja hapo mbele wa miaka mingi tangu mapinduzi ya Kiisilamu ya mwaka 1979.

Mradi wa Iran uliingizwa katika uratibu wa IAEA mwaka 1976 wakati wa utawala wa Rais Gerald Ford wa Marekani, wakati huo Iran ikitawaliwa na Mfalme Shah Reza, swahiba mkubwa wa Marekani (na wa Israel pia). Na lengo lilikuwa ni kuipa sapoti Israel dhidi ya harakati za nchi za Kiarabu dhidi ya taifa hilo la Kiyahudi.

Lakini baada ya mapinduzi ya Iran ya 1979, mradi huo wa Iran ukageuka kuwa chungu kubwa kwa Marekani na Israel, hasa wakati wa urais wa Mahmoud Ahmedinajad ambaye alionekana kuhoji: “Mbona Israel wana mradi huo, na pia zana za nyuklia na haiulizwi chochote?”

Propaganda za muda mrefu za nchi za Magharibi kupitia vyombo vyao vya habari zimekuwa mstari wa mbele kuuambia ulimwengu kwamba Israel ama haina zana za kinyuklia, na kama inazo basi zana hizo ziko katika mikono salama, kuliko zile ambazo Iran ingeachiwa kuzitengeneza.

Lakini kutokana na vyanzo vya kuaminika vya nchi hizo hizo za Magharibi, Israel inamiliki mabomu ya nyuklia kati 80 hadi 400 katika ghala yake iliyoko Dimona katika Jangwa la Negev. Nchi hiyo ilikuwa ya sita duniani katika kutengeneza zana hizo kwa ushirikiano na wanasayansi wa Ufaransa na zana ya kwanza ya nyuklia ilikamilishwa mwaka 1966.

Wachunguzi wa mambo wamekuwa wakisema iwapo Iran itatuma mabomu yake (yaani iwapo itakuwa nayo hapo baadaye) kulitekeleza taifa la Israel, nyambizi za kinyuklia za Israel zilizoko katika Bahari ya Mediterranean zina uwezo wa kuteketeza sehemu kubwa ya Iran.

Kuacha idadi ya mabomu ya nyuklia ambayo Israel inamiliki, mnyumbuliko huu wa mashambulizi ya kiangamizi ni wa kufikirika zaidi kuliko kiuhalisia.

Mahmoud Ahmedimanajd, aliyekuwa rais wa Iran kabla ya huyu wa sasa, aliwahi kusema anashangaa Israel na maswahiba wake wa Magharibi wanavyopaza propaganda kwamba Iran ina nia ya kuifuta kabisa Israel kutoka ramani ya dunia. Alihoji: “Mbona hampigi kelele taifa la Palestina ambalo tayari lilishafutwa kutoka ramani ya dunia?”

Lakini pia kuna uhasama baina ya India na Pakistan kuhusu jimbo la Kashmiri, uhasama ambao siyo tu uliibua nchi hizo mbili kupigana mara kadha, bali pia kuanzisha miradi yao nyuklia.

Pakistan kwa mfano ni nchi ya Kiisilamu na ambayo kuna harakati nyingi za wapiganaji wenye itikadi kali, lakini bado Marekani inasisitiza zana zake za nyuklia ziko katika mikono salama.

Kwa upande wao viongozi wa Israel wanawaona wale wa Iran kama siyo watu wa kawaida – ni machizi, wakereketwa wakubwa wa udini, na kwamba wanaweza kuiangamiza nchi yao wenyewe (Iran) kwa uchu wao wa kuliangamiza taifa la Israel. Mitazamo ya aina hii inatokana na miongo mingi ya chuki dhidi ya Iran, hususaan viongozi wao.

Lakini ukweli ni kinyume kabisa – kwamba viongozi wa Iran ni watulivu, na huyapima sana masuala ya kisiasa kabla ya kuchukuwa hatua. Si viongozi wanaokurupuka na kuliweka taifa lao rehani. Haya yamesemwa na mwandishi mmoja maarufu, raia wa Israel, Yuri Avnery katika makala yake katika gazeti la Jerusalem Post miezi kadha iliyopita.

Avnery ambaye pia ni mwanasiasa na mwanaharakati mkubwa wa upatanishi baina ya Israel na Wapalestina, aliwahi kuwa mwanachama wa kikundi cha Irgun katika miaka ya 1940 kilichokuwa kinadai taifa la Israel kutoka koloni la Palestina lililokuwa linakaliwa na Uingereza.

Alishiriki sana katika ulipuaji mabomu miundombinu, mahoteli na majengo mengine ya wakoloni hao katika vitendo ambavyo sasa hivi vingeitwa ugaidi tu.

Avnery anasema jazba za Iran za kimapinduzi za wakati wa Ayatollah Khomeini zimepungua nchini Iran, na hata Khomeini mwenyewe, angelikuwa bado hai, asingefanya mambo ya kuhatarisha taifa lake mwenyewe.

Pamoja na hayo, historia pia inatuambia kwamba kabla ya mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979 mahusiano baina ya Wayahudi na Wairani yalikuwa mzuri sana tena kwa miaka mingi. Wakati taifa la Israel lilipoanzishwa, Iran ilitambuliwa rasmi kama ni swahiba wa ki-asili wa Israel, kwani Waziri wake Mkuu wa kwanza, David Ben Gurion aliiona Iran kama ni nchi muhimu kwa usalama wake katika dunia ya nchi nyingi hasimu za Kiarabu.

Mfalme Shah wa Iran, aliyesimikwa na Wamarekani mwaka 1941 alizidisha biashara na Israel na pia shirika la makachero la Mossad la Israel na lile la Iran la Savak yalishirikiana na CIA ya Marekani kuratibu harakati za Wakurdi waliokuwa wakipambana na utawala wa Sadam Hussein wa Iraq.

Hata baada ya mapinduzi ya mwaka 1979, Israel iliiunga mkono Iran katika ile vita yake dhidi ya Iraq katika miaka ya 80.

Hivyo basi iwapo mambo yataharibika kabisa nchi hizi mbili zinaweza kujikuta zikivumiliana katika uwiano wa kutishiana. Hivyo ni vyema nchi hizo zikatumia muda uliopo kurekebisha mambo kupata muafaka katika mgogoro kati yao.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, katika kutafuta kura katika uchaguzi uliopita wa 2015, alitumia ubabe, lugha ya vitisho na kadhalika dhidi ya Iran wakati majadiliano ya mradi wake wa nyuklia yakiendelea huko Uswisi.

Aidha inafahamika wazi kwamba ‘uhasama’ wa Iran kwa Israel unatokana na hatima ya watu wa Palestina. Hali ya undugu iliyopo kupinga maonevu ya Wapalestina yamejikita ndani ya damu ya Waisilamu duniani kote, hivyo Iran haiko peke yake. Hivyo hakuna kitu kingine kinachochochea uhasama huu wa sasa isipokuwa suala la Wapalestina.

Yuri Avnery anasema iwapo suala la Wapalestina litatatuliwa, hakuna kiongozi yoyote wa Iran atakayeweza kuamsha uhasama wowote kwa wananchi wake dhidi ya Israel.