Home Habari Mishahara ya viongozi yatikisa Zanzibar

Mishahara ya viongozi yatikisa Zanzibar

1691
0
SHARE

OthmanMasoudOthmanNA MWANDISHI WETU , ZANZIBAR
MVUTANO wa kisheria umeibuka visiwani hapa juu ya uhalali wa viongozi wa juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kulipwa mshahara.

Vigogo wanaoguswa na mvutano huo ni Rais, Makamu wa kwanza na wa pili wa Rais, mawaziri, Spika na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Mvutano huo uliowagawa wanasheria katika pande mbili, umeibuka kutokana hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta matokeo ya uchaguzi wa Rais na wawakilishi.

Upande mmoja wa wanasheria wanasema si halali kwa vigogo hao kuendelea kuchukua mshahara unaotokana na kodi za wananchi na kwamba kwa sasa Zanzibar haina Serikali, huku upande mwingine ukihalalisha kwa madai kuwa ZEC imeufuta uchaguzi huo kwa mujibu wa sheria.

Wanasheria wanaotetea hoja hiyo wanasema kuwa Rais Dk. Ali Mohamed Shein na vigogo wengine wapo madarakani kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, lakini pia amepewa siku 90 za kuongoza kipindi cha mpito wakisubiri marudio ya uchaguzi, hivyo wanastahili kulipwa  mshahara.

Mwanasheria Mkuu wa zamani wa SMZ Othman Masoud Othman, anasema  kisheria hata Rais Dk. Shein kuendelea kubaki madarakani si halali hivyo na  makamu wake wa  kwamza na wa pili wa Rais spika, mawaziri na wajumbe pia uhai wao kikatiba kwa nafasi zao umekoma.
Masoud anaeleza kuwa uhai wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni miaka mitano na kwa sababu baraza halipo na muda wao kuisha hawana haki ya kulipwa mishahara na stahili nyingine.

“Anayepaswa kubeba  lawama ya jambo hilo  ni muajiri ambaye kama yeye anaamini yupo kihalali wakati yuko madarakani kinyume na Katiba ya Zanzibar, hataweza kuwanyooshea kidole waajiriwa na kuwaambia hawapo na hawastahili kulipwa kwa sababu wote ni wavunja sheria na  Katiba, “alisisitiza.

Aliyewahi kuwa Mwanasheria mkuu wa SMZ, Hamid Mbwezeleni anasema kwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi yupo madarakani na bado hajavunja Baraza la Mawaziri hivyo anastahili  kulipwa mishahara na stahili nyingine zote.

Mbwezeleni alisema  kusita kwa kazi za mawaziri ni pale Rais aliyewateua anapotangaza kuvunja Baraza la Mawaziri au akiamua wakati wowote  kumfukuza kazi waziri mhusika.
“Kwanza ninachoamini, Rais Dk. Shein yupo madarakani kihalali kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, wakati wowote anaweza kuitisha Baraza la wawakilishi ikiwa kuna jambo la dharura, “alisema Mwanasheria huyo.

Alisema ikiwa wapo wanasiasa wanaosema Rais hayupo madarakani kikatiba na kwamba hakuna serikali, wanakosea na kama wanaosema hivyo wanatoka upinzani, basi wanapaswa kurudisha magari ya Serikali.
Kwa upande wake mwanasheria wa kujitegemea Mohamed Ali Ahmed , anapingana na hoja hiyo huku akisema Katiba ya Zanzibar inataja mtu atakayebaki  madarakani kwa siku 90 ni Rais na Katiba haitaji uwapo wa  makamu wa kwanza na wa pili, mawaziri, spika au  wajumbe wa Baraza la wa wakiishi.

Mohamed anasema ukomo wa kazi za mawaziri, spika na wajumbe wa baraza la wawakilishi umegota kikatiba na kisheria hivyo kuendelea kulipwa si haki.

Alisema suala la kuwalipa mishahara watu hao si sahihi kwani uchaguzi umefutwa na utafanyika ndani ya siku 90, hivyo hawastahili chochote.

“Anayeteua mawaziri ni Rais ambaye sasa kuwepo kwake tu  madarakani ni ndani ya kipindi cha siku 90 ili uchaguzi mwingine uitishwe, Rais anaweza kuongoza nchi akiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu pamoja  makatibu wakuu wa wizara na watendaji wengine bila kuwepo mawaziri na kazi zikaenda kama kawaida ” Mohamed.
Akizungumzia uhalali wa kufutwa kwa uchaguzi mkuu, alijibu  kuwa ajuavyo yeye kisheria Mwenyekiti wa ZEC ana madaraka na mamlaka hayo pamoja na mengine bila ukomo.

 

Hata hivyo Waziri wa  nchi ofisi ya makamo wa pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed  amewahi kuthibitisha kuwa mawaziri wote wa SMZ wanaounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wanaendelea kulipwa mishahara yao na hakuna hata mmoja  aliyekataa kulipwa.