Home Makala Kimataifa MISHAHARA YA WAFANYAKAZI YAWEKWA HADHARANI

MISHAHARA YA WAFANYAKAZI YAWEKWA HADHARANI

743
0
SHARE

OSLO, NORWAY

NCHINI Norway mishahara ya watu si kitu cha siri. Mtu yeyote anaweza kujua mshahara gani mtu yeyote anapata na hili halileti matatizo yoyote.

Huko nyuma mishahara ya watu ilikuwa ikichapishwa katika kitabu. Orodha ya mapato ya mtu yeyote, mali zake na kodi anayolipam vyote hivi vilikuwa vinapatikana katika maktaba za umma. Lakini siku hizi habari zote hizi hupatikana kupitia tovuti kwa kubofya kwa sekunde chache tu.

Mabadiliko haya yalikuja mwaka 2001 na ghafla yaliibua mwamko mkubwa. Likawa suala la burudani kwa wengi, kwani mtu anaweza kufahamu mara moja mapato ya marafiki zake wa mtandao wa Facebook. Na hapo likaanza kuwa suala la dhihaka.

Wachunguzi wa mambo wanasema uwazi ni kitu muhimu kwa sababu Wanorway hulipa viwango vya juu sana vya kodi ya mapato; vya wastani wa asilimia 40.2 ya mapato ukilinganisha na asilimia 33.3 vya Uingereza, kwa mujibu wa taasisi ya Eurostat. Wastani wa viwango katika nchi za Umoja wa Ulaya (EU) ni asilimia 30.1.

Wachambuzi wa masuala ya kodi nchini Norway wanasema iwapo mtu analipa kiasi kikubwa cha kodi namna hiyo, ana haki ya kujua wengine wanalipa kiasi gani na kwamba kodi hiyo inatumika katika mambo mema.

Kwa mfano ukiingia katika tovuti utakuta kipato cha Waziri Mkuu wa Norway Erna Solberg kwa mwaka 2015 kilikuwa NKroner 1,573,544 (sawasawa na Pauni za Uingereza 151,001. Mali zake zilikadiriwa kuwa NKroner 2,054,896 (Pauni 197,179) na alilipa kodi NKroner 677,459 (Pauni 65,011).

Wachunguzi wanasema taarifa kama hizi huondoa matatizo yanayoweza kujitokeza kutokana na masuala ya wivu.

Katika sehemu nyingi za kazini nchini humo wengi huwa wana ufahamu wa kutosha mishahara ya wenzao bila hata kuangalia kwenye tovuti.

Mishahara katika taasisi nyingi hupangwa kutokana na mikataba ya kipamoja na tofauti za viwango huwa ni ndogo sana.

Hata tofauti ya mapato kufuata jinsia huwa ni ndogo ukilinganisha na viwango vya kimataifa. Taasisi ya World Economic Forum (WEF) inaianisha Norway kuwa ni ya tatu miongoni mwa nchi 144 duniani katika usawa wa kimapato katika ajira za aina moja.

Lakini Tom Staavi na wenzake katika taasisi ya moja ya kiharakati kuhusu masuala ya ajira na mishahara nchini Norway wamekuwa wakiitaka Serikali kuweka kanuni ambazo zitawashawishi watu kufikiria mara mbili kabla ya kuingia kwenye tovuti kuangalia taarisa za kipato cha rafiki yake, jirani yake hata mwanafamilia mwenzake.

Sasa hivi Wanorway wanalazimika kutumia namba zao za vitambulisho vya kitaifa ili kuingia katika tovuti ya mamlaka ya kodi ya mapato.

“Kuanzia 2014 imekuwa rahisi kujua ni nani amekuwa akisaka taarifa zako za kodi kupitia tovuti,” anaeleza Hans Christian Holte, Mkuu wa mamlaka ya mapato nchini Norway.

Norway ina walipa kodi milioni tatu kati ya idadi ya watu milioni 5.2. Mwaka mmoja kabla ya kuweka kanuni mpya mamlaka ya mapato iliruhusu bila pingamizi chunguzi za milioni 16.5 za taarifa za watu mbali mbali. Sasa hivi kuna chunguzi milioni mbili tu kwa mwaka.