Home Habari Misingi ya amani na utulivu inapaswa kulindwa

Misingi ya amani na utulivu inapaswa kulindwa

614
0
SHARE

Na JOSEPH MIHANGWA

“Wameiponya jeraha ya watu wangu kwa juu juu tu, wakisema, Amani, Amani wala hapana amani” [Yer. 6:14]

TUNAITWA Watanzania, wenyeji wa nchi nzuri, yenye jina tamu sana – Tanzania. Ni nchi kamili yenye wimbo wake wa Taifa, Bendera ya Taifa na Ngao ya Taifa.

Lakini Mwanafalsafa mmoja wa kale, Gordon Lewis, aliwahi kusema, “yahitaji kitu zaidi ya wimbo wa Taifa, hata uwe mtamu vipi; bendera ya Taifa, hata iwe ya kuvutia vipi; ngao ya Taifa hata iwe ya kufaa vipi, kuunda Taifa hai”. Ni kipi hicho “kitu” kinachounda Taifa?, unaweza kuuliza. Jibu utalipata baadae.

Nchi imepita njia na hatua za maendeleo ya kiuchumi na kijamii kama zilivyofanya nchi zote za sayari hii iitwayo “Dunia” kufikia hapa ilipo: kutoka Umajumui na Ujima hadi tawala za kivikundi vya kikabila [tribal States]; Utaifa wa nchi kwa kutawaliwa [Colonial National State] na uhuru, hadi utandawazi unaotunyemelea.

Lakini tofauti na nchi zote za dunia, Tanzania ina sifa moja isiyohojika wala kuwa na mshindani:  ni chimbuko na makao ya binadamu wa kwanza kutembea juu ya uso wa nchi, pale “Oldupai” [Kimasai, korongo lenye mkonge], neno lililokuja kuitwa kwa kukosewa “Olduvai Gorge” baada ya kurekodiwa na Mtafiti, Mjiolojia wa Kijerumani, Profesa Wilhelm Kattwinkel mwaka 1911, kama “Oldoways” kwa Kijerumani.

Kwa yeyote yule awaye; awe muumini wa nadharia inayodai kwamba binadamu wa sasa alitokana na mageuko/mabadiliko [evolution], au wa nadharia ya uumbaji [creation], ukweli huu unabaki ulivyo. Hatuna sababu ya kutoamini kwamba Olduvai Gorge ndiyo Bustani ya Eden ya Babu yetu mkuu Adam, na Bibi yetu mkuu Hawa, badala ya Eden ya Mashariki ya Kati tuliyoaminishwa.

Na kwa nini tusiamini pia kwamba wanyama alioingiza Babu Nuhu kwenye Safina kuepuka kifo kwa Gharika kuu, ndio hao waliopo Shimo la Ngorongoro karibu na Olduvai; na mlima Kilimanjaro kuwa ndio mlima Ararat ambao juu yake iligota Safina ya Nuhu?.

Tena, kama ilivyokuwa kwa nchi zingine, Tanzania imetawaliwa na Mataifa ya kigeni [Wajerumani/Waingereza]; imepata uhuru wa bendera na kufuatiwa na kipindi cha kuuimarisha na kuulinda.

Tulipopata uhuru mwaka 1961, tulirithi mfumo wa kikoloni kwa misingi ya uhusiano wa “Mabwana” na “Watwana” katika nyanja zote za maisha; na mwaka 1962, tulianza kuzungumzia uhusiano kwa misingi ya “usawa” chini ya itikadi ya “Ujamaa” kama mhimili wa amani na maendeleo.

Maendeleo hayaji bila usawa na maridhiano, bali chuki, mifarakano na utengano kwa misingi ya “Wao” na “Sisi”. Wala matumizi ya nguvu hayaleti tija kwa shinikizo katika nchi iliyo huru, ila kuzua mitafaruku. Nchi haitawaliki pale wananchi wanapokosa matumaini; hupoteza subira na mitafaruku kujengeka na pengine kusababisha ghasia na amani kutoweka. Inapofikia hapo, hata kama ni kwa nchi “huru”, watu wataanzisha vuguvugu la harakati za “ukombozi wa pili” [second liberation] ili kuyapata matumaini wayatakayo.

Watanzania, kupitia Kiongozi wao mwenye maono, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, waliliona hilo mapema, wakabuni “Usoshalisti” unaoitwa “Ujamaa”, kama msingi wa usawa, maendeleo na amani.

Kitu gani hiki kiitwacho amani ya nchi?. Je, ina maana ya watu wakomavu kisiasa, kijamii, kiuchumi na kisaikolojia wenye kutambua kwamba ghasia [violence] siku zote hazina ushindi mkubwa; kwamba iwavyo, kwenye vita hakuna mshindi wa kweli?.

Au “amani” maana yake ni kuwanyamazisha wananchi wenye uelewa, wasomi wenye maono wanapodai haki zao, iaminike kwamba kuna amani wakati hapana amani?.

Hapa yafaa tutahadharishe mapema kwamba, dhana ya “amani na utulivu” yaweza kutumiwa vibaya na wenye hila, wanasiasa na wakwasi kwa jasho la umma, kuwafunga midomo wananchi ili kulinda maslahi ya kitabaka na kuendeleza “yale yale” [status quo] yanayokera jamii, na kwa “Viongozi” wabovu kujiponya huku wananchi wakizidi kupoteza matumaini.

Hadi lini Wananchi watakubali kuendelea hivyo wasipige kelele kutaka wasikilizwe bila kuzua mitafaruku?. Nini dawa ya mitafaruku;  kichapo kwa nguvu ya vyombo vya dola; au kuwanyamazisha, kuwafunga midomo na uhuru wa vyombo vya habari kwa Sheria kandamizi?.

Mahatma Gandhi [1869 – 1942] anaelezea mitafaruku ambayo yeye anaiita kwa usahihi -“Uasi wa raia” [Civil disobedience], kuwa ni “haki asilia ya raia ambayo hawezi kuiacha bila kujiumbua utu wake”.

Anasema, “Uasi wa raia hausababishi wala kuambatana na vurugu ila uasi wa raia wa kijinai unaweza kusababisha vurugu. Kila Serikali hutumia nguvu kuzima uasi wa kijinai; lakini kuzima uasi wa raia ni kujaribu kuiteka roho, dhamiri na uhuru wa mawazo wa raia”.

Kwa mujibu wa Gandhi na kwa mantiki tu ya kidemokrasia, haki za kiraia na utawala bora ni kwamba, wananchi wana haki asilia ya kuhoji utendaji kazi wa Serikali waliyoiweka madarakani kwa lugha na ujasiri wa kiraia, nayo Serikali inapaswa kuheshimu na kutoa majibu sahihi kwa maswali yanayoelekezwa kwake hata kama ni ya ukakasi kwake au yenye kuumbua mradi tu ni hoja za msingi.

Ni kuwakosea adabu wananchi, kwa Kiongozi kuwatuhumu kubeza au kuwachukulia kama waasi, wahaini au wapinzani wa Serikali na kuwanyamazisha kwa nguvu ya viwango mbali mbali wanapotumia haki yao hiyo. Kufanya hivyo kunajenga hasira ya mlipuko mithili ya boila ambalo siku moja laweza kulipuka kwa madhara makubwa ikiwamo amani kutoweka.

Katika “Tujisahihishe”, Mwalimu Nyerere anakemea tabia ya kuwasifia na kuwaambia Viongozi mambo yale tu wanayopenda kusikia na kuwaficha ukweli mchungu; na kwamba pasipo na ukosoaji na kujikosoa, maana yake ni kujifanya kutoona makosa hata kama ni yenye kuathiri maadili na maslahi ya Taifa na hivyo kukaribisha mitafaruku.

Tiba ya mitafaruku ni kwa Viongozi kuwa wawazi kwa wananchi, wasikivu na wavumilivu wa hoja na kukosolewa, badala ya matumizi ya nguvu kuzima maoni mithili ya enzi za ukoloni.  Huko ni kudhalilisha demokrasia. Hivi, ni wangapi wanajua kwamba “amani” tunayojivunia ni zao la Siasa ya Ujamaa ambao sasa baadhi yetu hatupendi kuusikia ila kutamani matunda yake – Amani?. 

Uongozi, kama anavyofafanua Mwalimu katika “Uhuru na Maendeleo”, “maana yake si kukemea watu wala kutukana au kudhalilisha mtu au kikundi cha watu unaotokea kutokubaliana nao. Wala Uongozi si kuamuru watu kufanya hili na lile; Uongozi maana yake ni kuongea na kujadiliana na watu na kuwashawishi”.

[identity]

Mwalimu anaendelea kufafanua; “Uongozi ni kutoa mapendekezo yenye tija, kufanya kazi na watu na kuonesha kwa vitendo kile unachowahimiza wafanye;  maana yake ni kuwa sehemu ya watu kwa kuwa mmoja wao na kutambua usawa wako na wao”.

Misingi ya haya yenye kuzaa amani na utulivu katika nchi yetu ni “Usoshalisti” ambao sisi tuliupa jina “Ujamaa”.

Kuna tofauti kati ya “Usoshalisti” wa ki-mapokeo na “Ujamaa”.  “Usoshalisti” ulioasisiwa Ulaya karne ya 19, ni kusanyiko la nadharia za kiuchumi zenye kutetea uchumi na vitendea kazi vya uzalishaji, ugawaji mali na huduma kumilikiwa na umma au Serikali katika jamii yenye usawa.

Ujamaa au Usoshalisti wa Kiafrika kwa upande wa pili, ni imani katika kugawana rasilimali za Taifa kwa misingi ya jadi za Kiafrika [udugu], tofauti na Usoshalisti.

Tofauti ya falsafa mbili hizi ni kwamba, wakati Usoshalisti ni matokeo ya mapambano ya Kitabaka, Ujamaa ni matokeo ya mahusiano mapana ya kifamilia kwa familia pana.

Ujamaa ulijizolea sifa na ushawishi mkubwa kwa misingi mikuu mitatu:  kwanza, uliwakilisha hatua ya kupiga teke utamaduni wa utawala wa kikoloni/kibeberu; pili, ulikuwa mfumo wa Kiafrika katika mazingira ya Kiafrika wenye kutambua na kutetea heshima ya Uafrika

, dhana iliyokuwa na nguvu kuzidi hata upinzani dhidi ya ubepari; na tatu, ulilenga kurejesha/kufufua moyo na maadili ya Kiafrika.

Sababu zingine ni Afrika/Tanzania ilikuwa mbali nyuma ya nchi za kibepari kuelekea kwenye Usoshalisti kama mfumo wa uzalishaji mali kuweza kushindana kikamilifu na kwa haki.  Mwalimu aliwahi kusema, hakuwa tayari kujenga na kuimarisha kwanza ubepari ili afikie Usoshalisti kwa sababu tu ni lazima nchi ipite njia hiyo kimfumo.  Alisema, hakutaka “kugeuka jiwe” au nguzo ya chumvi ya Kibiblia.  China ilipita njia hiyo kwa kurukia Ubepari kwenda Usoshalisti kwa mruko mkuu [The Great Leap Forward] mwaka 1949.

Pili, palitakiwa moyo wa umoja na ushirikiano ambao haupatikani kwenye ushindani wa kibepari ila kwa njia ya “Ujamaa” pekee. Mwisho, Maendeleo ya Afrika/Tanzania yalipaswa kupangwa kimkakati kuzuia utapanyaji rasilimali zetu kuepuka migongano ya kitabaka baadaye.

Utambulisho wa Kiafrika na Ujamaa mara nyingi vilitizamwa kwa pamoja; wengine wakidai kuwa tangu kale Afrika ilikuwa ya Kisoshalisti kabla hata ya Usoshalisti wa Kiulaya, wakiuona Ujamaa kama kiunganishi cha Mwafrika kiutamaduni hivi kwamba, Mapinduzi ya kijamii yenye tija yalipaswa kufuata mkondo huo.

Falsafa ya Ujamaa inasimama juu ya mafiga matatu – Usawa, Uhuru na Umoja: Usawa kwa sababu bila usawa watu hawawezi kufanya kazi kwa ushirikiano; Uhuru kwa sababu mtu hawezi kuhudumiwa na jamii isiyo yake; na Umoja kwa sababu ni jamii yenye umoja pekee itakayowezesha wananchi wake kuishi na kufanya kazi katika hali ya amani, usalama na ustawi. 

Tumedumu katika falsafa ya “Ujamaa” kwa miaka 30 kwa awamu mbili, kuanzia mwaka 1962 hadi 1966 Ujamaa ulipotumika kinadharia bila programu; na kuanzia 1967 Ujamaa ulipotumika kivitendo kupitia Azimio la Arusha na Kujitegemea hadi mwaka 1992 lilipopigwa ngwara kwa Azimio la Zanzibar na nchi kutupwa kwenye Sera za kinyang’au za Soko huria na Utandawazi kwa shinikizo la ubepari wa kimataifa. Hivyo unaposema nchi inajivunia “amani na utulivu”, tunamaanisha mtaji uliojengwa kwa miaka 30 chini ya falsafa ya “Ujamaa” na Kujitegemea na si vinginevyo.

Lakini tulivyo sasa, sisi ni Taifa la watu waliochanganyikiwa kisera, kati ya Ujamaa na ubepari.  Wakati sote, Viongozi kwa wananchi kwa pamoja, tunataka tutendewe na jamii ki-ujamaa [kupendwa, kupewa ushirikiano], wakati huo huo tunataka kutenda kibinafsi kwa kukwea juu ya vichwa vya wengine kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni kana vile kusema, “Aliye na kingi ataongezewa, lakini asiye nacho hata kile kidogo alicho nacho atapokonywa”.  Hapo “amani na utulivu” vitatoka wapi?.

Je, amani itadumu vipi kwa mazingira ya kitabaka yanayoibukia, kati ya walio nacho na wasio nacho; kati ya “watawaliwa” na watawala wakwasi, wanajiona wapo kutumikiwa badala ya kutumikia; kati ya “Walala hoi” na “Walala heri” na kwa nchi kupungukiwa Viongozi na kujaa Watawala wenye kutumia nguvu za dola kusukuma mambo?.

Watanzania wamelelewa na kuishi kwa matumaini yenye kuzaa “Amani na Utulivu”. Ni kwa matumaini kwamba hadi leo, licha ya ubepari na ubeberu kutunyemelea, uwezekano wa kutoweka kwa amani kwao ni jambo lisiloingia akilini, wakisema “hakuna taabu” kwa kufa na tai shingoni. 

Wabaya wa nchi na wa wananchi wasiuchukulie “upole” huu kama ujinga, wakajaribu kuwatemea mate usoni wakitarajia wataendelea kukaa kimya. Lakini watavuta subira hadi lini kuiona heri, nyuma ya bango la “Amani na Utulivu”?.

Tunapojilinganisha na majirani zetu Kenya, kwamba licha ya uchumi wao kukua kwa kasi kwa mfumo wa kibepari, kukua huko siku zote kumeambatana na mitafaruku na machafuko kwa sababu ya mgawanyo wa rasilimali usio sawa.  Kipi bora, kukua kwa uchumi kwa kasi kwa wachache ndani ya machafuko; au kukua kwa uchumi kwa wote kwa amani na utulivu?.

Je, ni “amani na utulivu” tunapokaa vibarazani tukipiga soga juu ya namna mafisadi yaliyokubuhu yanavyopora rasilimali za Taifa bila kuguswa; hatupigi kelele kwa sababu tu sisi ni nchi ya “amani na utulivu”?.  Wachochezi wa vita ya baadaye ni hawa Mafisadi wa leo.

Je, tunapaswa kushangilia Bunge linapotunga Sheria kandamizi zenye kuweka mikononi mwa wachache uchumi wa nchi; au linapowakingia kifua “kambale” wenye tuhuma kubwa kubwa za ufisadi; hatuandamani kwa amani kwa “kuwaheshimu” wakubwa hao kwa sababu tu sisi ni nchi yenye “amani na utulivu”?.

Je, ni demokrasia kuangalia matajiri wakizidi kutajirika siku kwa siku; masikini wakiserereka chini ya mstari wa ufukara, tukitikisa vichwa kupinga kimya kimya; hatudai haki kwa kuwa tu sisi ni nchi yenye “amani na utulivu”?.

Tangu tuulaki ubepari kwa pupa, umoja wa kitaifa umeparanganyika; tunatumia bango la “amani na utulivu” ambalo msingi wake ni “Ujamaa” kukingia kifua maovu ya ubepari uzaao ubeberu kuua fikra na kiu ya haki kwa wananchi na pengine kwa matumizi ya nguvu za dola.

Tunadhalilisha utu kwa kufikiri kwamba ubepari kama mfumo wa kutengeneza pesa, ndio altare na maana ya maisha yenyewe. Tunaona kwa kukatika kichwa, kwamba pesa ya haraka haraka, pesa nyingi kwa njia halali na haramu; za rushwa, ufisadi na “shinikizo”, lazima zitengenezwe ili maisha yatunyookee. Je, Mwalimu hakuonya kwamba “Fedha si Msingi wa Maendeleo”, bali Watu, Ardhi na Uongozi bora?.

Kuna ukweli katika usemi kwamba, “Ukiona vinaelea vimeundwa”. Amani na utulivu tunaojivunia kuwa kivutio cha wawekezaji wa kigeni, lazima vionekane na kuenziwa kwa misingi ya sera za “Ujamaa” bila kujali tofauti zetu za kiitikadi. Je, si uhayawani kupenda yai lakini ukamchukia kuku?.

Ikitokea mwangwi wa “Ujamaa” kuanza kufifia na watu kupoteza matumaini, subira ya “Walala hoi” dhidi ya “Walala heri” na wakeketaji wa demokrasia itapotea, mitafaruku itazuka; Edeni ya Tanzania itachafuka.  Hapo Amani itatoka wapi?.