Home Makala MITI YA MATUNDA……….Ukombozi kwa mwanamke

MITI YA MATUNDA……….Ukombozi kwa mwanamke

1432
0
SHARE
Evelyn Kahembe (wa pili kushoto) akielezea jambo juu ya mradi wa Green Voices na namna wanavyofanya kazi katika shamba lao lililopo katika Kijiji cha Mwamila, Wilayani Uvinza, Kigoma. Picha na Sidi Mgumia

Na Sidi Mgumia, aliyekuwa Kigoma

KUMEKUWA na jitihada mbalimbali za kumkomboa mwanamke kiuchumi. Lengo ni kumwondoa kwenye utegemezi kwa mwanaume.

Harakati na kampeni mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kusaka utu wa mwanamke mbele ya jamii kandamizi ya wanaume.

Katika kuhakikisha jitihada hizo zimafanikiwa mwaka 1995, uliitishwa mkutano mkubwa uliowahusu wanawake maarufu kama Mkutano wa Beijing.

Maelfu ya wanawake walikusanyika katika mkutano huo ambao uliibuka na maazimio kadha wa kadha, yote yakiwa na lengo la kumpa usawa mwanamke na mwanaume.

Ni miaka 21 sasa tangu mkutano huo ufanyike, pamoja na jitihada za kusaka usawa, lakini bado kuna kikwazo cha woga na kipato kutoka kwa wanawake wenyewe.

Kwa kulibaini hilo  Taasi ya Wanawake wa Afrika chini ya Rais wake Maria Teressa De La Vegas, imedhamiria kumwondoa mwanamke kwenye utegemezi.

De La Vegas ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Hispania, ameasisi mradi maalum wa Sauti za Kijani (Green Voices) ambao pamoja na mambo mengine umejikita kwenye kuboresha mazingira.

Mradi huo umesambaa katika maeneo mengi ya nchini, Kigoma ikiwemo. Jopo la wanahabri wanaoshughulikia mradi huo wiki iliyopita lilifanya ziara ya kikazi katika kijiji cha Mwamila, kilichopo wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Jopo hilo la wanahabari wanawake likiwa katika kijiji hicho kilichozungukwa na uoto wa asili, lilikutana na  Evelyn Kahembe ambaye ni mmoja wa wanawake 15, wanaonufaika na  mradi huo.

Kahembe anasema anajisikia fahari kuwa mmoja wa wanawake wachache wa Kitanzania aliyepata fursa hiyo na kwamba hatua hiyo kwake ni deni.

Anasema kwa sababu dhamira yake ni kumkomboa mwanamke wa Tanzania hasa wa mkoani Kigoma, ameanzisha mpango wa kupanda miti ya matunda, ambayo anaamini itakua ni suluhisho la uhakika la kipato cha mwanamke.

 

Alisema mafunzo ya namna yakukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi aliyoyapata nchini Hispania mapema mwaka huu yamemuongezea ujasiri na nguvu ya kumkomboa mwanamke wa Tanzania.

“Nimerudisha ujuzi huu katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ili kuhakikisha wanawake wanakuwa chachu ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na  kujipatia kipato,”alisema.

Kahembe anatekeleza mradi huo kwa kupanda  miti ya matunda chini ya kikundi cha wanawake wapatao 20.

Evelyn alisema mradi huo wa upandaji miti ya matunda umelenga katika kuwasaidia wanawake waweze kupata kipato lakini pia isaidie kutunza mazingira.

“Tuna shamba ambalo kwa kuanzia tumeshalima ekari tano na bado zipo nyingine 25 ambazo bado hazijalimwa. Tunatarajia kupanda miti 1080 na mpaka sasa tumeshapanda miti ya machungwa 580 na mingine 500 ya maembe tutapanda mwezi Novemba wakati wa masika.

“Kupitia akina mama hawa tuna hakika kuwa kilimo cha miti ni rahisi sana kwa sababu ukishapanda hakuhitaji uangalizi mkubwa sana na wala hauhitajiki uwe karibu na shamba muda wote. Kuna kazi chache za kufanya kabla na baada ya kupanda miti,”.

Akieleza juu ya faida za upandaji wa miti ya machungwa na maembe Evelyn alisema Maembe na machungwa yaliopo Tanzania yanaweza kumuongezea kipato mkulima wa Tanzania kama akielimishwa vizuri kuhusu ukulima bora na wa kisasa.

Helena Elias mmoja wa wanakikundi wanaonufaika na mradi huo alisema wanafurahishwa na hatua waliyoipiga kwani inawaondoa kwenye umasikini.

Kahembe aliwaambia wanahabari kuwa tatizo kubwa linalowakabili ni upatikanaji wa mbegu bora za miti ya matunda, na pale inapopatikana gharama ya mche mmoja huanza kuuzwa kwa kati ya Sh. 4,500 na 5,000  kwa mche.

Mbali na tatizo hilo, lakini pia tatizo la magonjwa ya mimea nalo limekuwa likiwarudisha nyuma.

“Pamoja na hilo bado tunajitahidi kuitunza sana na kimsingi katika kilimo chetu tunatumia mbegu za kisasa ambazo huchukua muda mfupi kutoa maua pia tumechagua eneo katika Kijiji cha Mwamila kwani ni sehemu ambayo ina rutuba na iko karibu na upatikanaji wa maji yakutosha,” alisema Evelyn

Kwa upande wake Bernard Rusomyo ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza anasema kama serikali mradi huo wamepokea vizuri kwasababu serikali inafanya kazi na wadau na walifurahia zaidi kuwa haikuwa tu miti bali miti ya matunda.

“Miti hii ina faida mara mbili kwa maana yakusaidia katika kukabiliana na Mabadiliko ya tabia nchi na pia kufaidika na matunda yanayotokana na miti hiyo. Tunaamini kuwa ekari hizo zote 25 zikipandwa miti ya matunda faida yake itakuwa kubwa ,” alisema Rusomyo

Akizungumzia changamoto zinazowakabili, Rusomyo alisema Uvinza iko kwenye ukanda ambao misitu mingi bado imehifadhiwa hivyo hawana shida sana ya chakula.

Akifafanua juu ya misitu iliyopo, Rusumyo anasema bado wana uhakika wa kuwa na misitu hai kwani wanasaidiwa na wadau kama Jane Goodall kupitia taasisi yake ya Jane Goodall Institute (JGI) pia wadau wengine wanajiita Wekeza na wengine wengi wanasaidia sana katika kuilinda misitu iliyopo wilayani Uvinza.

“Kwa upande wa mvua, bado tunapata mvua lakini pamoja na hilo bado tuna changamoto ya wavamizi wa maeneo wanaofanya kilimo cha kuhamahama pia ukataji wa miti jambo ambalo serikali inalishughulikia ipasavyo kuhakikisha kuwa miti haikatwi hovyo. Na kwa hilo basi tunapoona wadau kama hawa wa Green Voices tunafurahi kwani wanaongeza nguvu katika kuiokoa miti yetu pia kukabiliana na chanagamoto zote zinazotokana na kukatwa kwake,” anasema Rusumyo

Naye Jacqueline Sengano, Mwenyekiti wa kikundi cha Tumaini la Jamii (HCF) kinachotekeleza adhma ya mradi wa Green Voices anasisitiza kuwa wamechagua zao hasa la maembe kwakua linalimwa katika mikoa yote kwa sababu ya uwezo wake wa kustawi katika aina mbalimbali za udongo na kustahimili aina mbalimbali za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na ukame.

Deo Baribwegure Mkurugenzi wa Kigoma Community by Radio anayefanya kazi na wakina mama hao wa Kikundi cha HCF anaongeza kuwa mradi huo unamanufaa makubwa kwani jambo la uhakika ni kuwa hata kama bei ya miti itabadilika hawataweza kupoteza mtaji mkubwa uliotumia na wala hawatakosa kuzalisha faida kwa shamba wanalomiliki wanawake hao.

Kwa ujumla wakulima wengi hawajui kanuni bora za kilimo cha matunda na hivyo kuwafanya wakulima kutoyaona manufaa yake.

Kwa upande mwingine, ili kuondoa tatizo la upatikanaji wa miche bora ya matunda haswa miembe Wizara ya kilimo chakula na ushirika imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa miche hiyo na upatikanaji kwa wakulima.