Home Makala Miundombinu mibovu chanzo kinamama wajawazito kupoteza maisha

Miundombinu mibovu chanzo kinamama wajawazito kupoteza maisha

1104
0
SHARE

IBRAHIM YASSIN-MBEYA

SERIKALI na wadau mbalimbali wamekuwa na jitihada katika kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya afya na kuwahamasisha akina mama kujifungulia katika vituo vya afya.

Haya ni moja ya malengo 17 ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo yanatarajiwa kufikiwa mwaka 2030, yaani kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi hadi kufikia uwiano wa 70 kwa vizazi hai 100,000.

Kutokana na hali hiyo ya kuwepo kwa mwamko mkubwa kutoka kwa wanawake kufika kwenye vituo vya afya, hali hiyo inaonekana kuwa huko tuendako vifo vitokanavyo na uzazi vitapungua au kuisha endapo elimu itatolewa kwa jamii.

Kitu ambacho kinafanya wanawake waliopo pembezoni wajenge Imani, ni kutokana na baadhi yao kutumia miti shamba ambayo wanaamini kwamba ni salama kwao bila kufahamu kuwa inahatarisha maisha ya mama na mtoto.

Kwa upande wa wanawake waliopo mjini wao wamejenga imani zaidi kujifungulia hospitali kwa kuamini kuwa ndiyo salama zaidi licha ya kwamba baadhi yao hutumia mitishamba na baadhi yao kujifungulia nyumbani lakini suala la kufika kwenye vituo vya afya linakuwa bado linazingatiwa.

Akizungumza na gazeti hili, Mkazi wa Ijombe Wilaya ya Mbeya Mjini,Frola Mlowezi anasema kuwa zipo sababu mbalimbali zinazowafanya wanawake kujifungulia nyumbani.

Anataja sababu hizo kuwa ni umbali wa vituo vya afya na zahanati na kwamba serikali ikitekeleza kama ilivyotoa ahadi zake kwa wananchi kuwa kila kijiji kitakuwa na zahanati na kila kata kuwa na kituo cha afya itasaidia kupunguza vifo hivyo.

Kuhusu mwamko wa wanawake wajawazito wanaohudhuria kliniki, Mlowezi anasema kumekuwa na tofauti kubwa sana na zamani hivi sasa wanawake wajawazito wanafika na waume zao kliniki.

Anasema kuwa hali hiyo imeleta faraja kubwa kwa wanawake kuona kuwa wanaume sasa wameanza kuona umuhimu wa kuwapeleka kliniki wake zao, ili kujua maendeleo ya afya na changamoto zingine zinazohusu uzazi kwa wanawake .

Anasema huduma ya uzazi ya mama na mtoto, imekuwa ikitolewa kwa ubora na hakuna lugha za matusi au dharau tena kwa wagonjwa kama ilivyokuwa zamani.

“Tunashukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kuendelea kuboresha huduma hasa kwa mama na mtoto hili limeleta matumaini makubwa sana,lugha mbaya kwa wagonjwa zilikuwa zinaleta shida mpaka wengine kufikia hatua ya kutokwenda hospitali lakini sasa tunatembea kifua mbele Rais Dk. John Magufuli amefanya kazi kubwa,”anasema .

Kwa upande wake Felix Assey ambaye ni Mkazi wa Uyole jijini Mbeya, anasema kuwa amekuwa na utaratibu wa kumpeleka mke wake kliniki kila tarehe anayotakiwa kufika.

Assey anasema kuwa alimpeleka mke wake hospitali ya wazazi Meta na kupewa huduma nzuri na vipimo vyote kwa wakati huku akishiriki kupokea ushauri wa afya ya uzazi ambayo imewasaidia na kuongeza afya njema kwa mkewe na kuwa na uhakika wa uzazi salama.

Debora Mwanyanje mkazi wa Gombe jijini Mbeya, anasema huduma ya afya ya mama na mtoto imeboreshwa kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo hivi sasa kuna mabadiliko makubwa kwenye huduma ya mama na mtoto.

Akizungumzia afya ya mama na mtoto Diwani wa Kata ya Igurusi,Hawa Kihwele anasema huduma ya mama na mtoto imeboreshwa kwa kiasi kikubwa na walio jirani na hospitali,vituo vya afya na zahanati wanajiona jinsi huduma hizo zilivyoboreshwa.

Anazungumzia kuhusu wanaume wanaosindikiza wenza wao kliniki kuwa ni robo ya wanaume wanaofanya hivyo, ambapo pia kuna wanaume wengi bado ni wakaidi kuambatana na wake zao kliniki pamoja na ushauri kutolewa na wizara ya afya mara kwa mara.

“Kikubwa elimu iendelee kutolewa ili wanaume waweze kujitokeza kwa wingi kuwasindikiza wenza wao kliniki na wasione aibu wala kuona kuwa ni kitu cha ajabu kwao kwani kwa kufanya hivyo kutajenga utamaduni imara utakaosaidia kufuatilia kwa karibu mwendelezo wa afya ya mwenza wake na kushauriana vyema,”anasema.

Kihwele anasema wanawake wajawazito wanaojifungua kwa wakunga wa jadi ni wachache kutokana na mazoea waliyojenga katika jamii zao.

Anasema kuwa sababu zinazowafanya wanawake wajawazito kufika kwa wakunga wa jadi kujifungua ni woga na hofu ya kufanyiwa upasuaji.

Kihwele anasema sababu nyingine inayowafanya wanawake kufika kwa wakunga wa jadi ni nauli na gharama za wauguzaji wa nje pamoja na kujenga ujasiri na mazoea ya kuiamini dawa za asili huku wengine wakishindwa kumudu gharama za usafiri kutokana na vituo vya kutolea tiba kuwa mbali na makazi yao.

Akielezea zaidi diwani huyo wa kata ya Igurusi, anasema kwamba kwa Wilaya ya Mbarali kabila la Wasangu wamekuwa wakijifungulia nyumbani kutokana na tabia waliyojijengea.

Hata hivyo Kihwele anatoa wito kwa wanawake wajawazito kuwahi hospitali pale wanapoona dalili za hatari ili kupunguza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi pamoja na ugonjwa wa fistula.

Akizungumza na makundi ya wanawake na vijana Meneja mradi wa shirika la Marie Stopes, Emmanuel Mang’ana anasema kuwa shirika hilo limekuwa likitoa elimu kuhusu afya ya uzazi na miradi mingine ambayo inahusu wanawake na vijana.

Mang’ana anasema kuwa lengo kubwa ni kuelimisha afya ya uzazi kwa ujumla hasa vijana ili waachane na tabia ya kukimbilia kwa waganga wa kienjeji kwa matatizo ambayo yanatibika kwenye vituo vya kutolea tiba ili kupunguza vifo visivyokuwa vya lazima .

“Tumekuwa tukitoa elimu kwa wanawake na vijana waliopo vijijini kuhusiana na afya ya uzazi maana makundi haya ndio muhimu katika jamii kwani yana changamoto nyingi kwenye afya ya uzazi,”alisema.

Aidha meneja mradi huyo, anasema elimu ya afya uzazi kwa wanawake na vijana walianza kutoa mwaka jana na wanaendelea mpaka sasa huku akieleza kuwa wengi wameanza kufuata ushauri na mabadiliko yameanza kuonekana.

Kwa upande wake, Mama Mchungaji wa Kanisa la Anglican,Paulina Haule anasema kuwa kwenye afya ya uzazi inabidi watu waelimishwe kwani wanawake na vijana wamekuwa wakizaa bila mpangilio na kusababisha watoto kuwa na afya mbaya kutokana na kukosa lishe bora.

Nchini Ghana, wanawake wote wajawazito kwa sasa wapo chini ya mpango wa kupatiwa madini ya chuma na tiba za malaria na watoto wote wa umri kati ya miezi sita na miaka mitano wanachanjwa dhidi ya magonjwa ya utotoni kama vile surua na polio.

Nchini Malawi, serikali imeanzisha programu ya kutoa chanjo ikiwa ni pamoja na kutoa matone ya kuongeza lishe – kiasi kidogo cha madini kama vile ya chuma, cobalt, chromium na shaba, Serikali pia inajenga visima kuboresha upatikanaji wa maji kwa watu wanaoishi maeneo ya vijijini na miji ya ndanindani.

Kulingana na ripoti hiyo, nchi tano kaskazini mwa Afrika zimefanya jitihada kubwa katika kupunguza viwango vya vifo vya watoto. Nchini Algeria, Misri, Libya, Morocco na Tunisia takwimu zilishuka kwa uchache kufikia asilimia 45 kati ya mwaka 1990 na 2006.

Mataifa haya ambayo kwa kiasi fulani ni matajiri yako katika shabaha ya kufikia lengo la Nne la Maendeleo ya Milenia (MDG): kupunguza moja ya tatu ya vifo miongoni mwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.

Lakini Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara haina uwezekano wa kufikia lengo lolote lile kati ya haya yanayohusiana ifikapo mwaka 2015; bara hilo lipo nyuma katika jitihada za kukabiliana na umaskini na njaa, kuboresha afya ya wajawazito na kuondokana na athari za kuenea kwa VVU.

Ripoti ya UNICEF inatoa wito wa fedha za kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na chanjo kwa watoto, huduma za kabla na baada ya kujifungua kwa wanawake, unyonyeshaji unaopendekezwa wa angalau miezi sita na kujengwa kwa vituo vingi zaidi vya afya.

Pia ripoti ya Unicef ‘Watoto na Wanawake Tanzania’ (2010), inaonyesha kuwa wanawake wanaojifungua vijijini wako katika wakati mgumu zaidi ukilinganisha na wale walioko mijini bila kujali kama wanajifungua nyumbani au kwenye vituo vya matibabu.

Ripoti hiyo inaelezwa kuwa wanawake wanaojifungua vijijini ni wengi zaidi (asilimia 80 ya wote wanaojifungua), huduma za haraka kwaajili ya akina mama ni duni vijijini huku robo ya vituo vya vijijini vikiwa na huduma zote zinazohitajika wakati wa uzazi.

Shirika la ELIMISHA lenye makao yake jijini Mbeya ni miongoni mwa shirika ambalo linawawezesha makundi ya Wanawake na Vijana katika kuwajengea uwezo jumuishi kwa kuongeza thamani ya maarifa yao kwa kutumia fikra bunifu ili kuliwezesha kundi hilo kufikia malengo yenye kutimiza ndoto zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la ELIMISHA, Festo Sikagonamo anasema kwa mujibu wa mwongozo wa kitaifa wa mwaka 2013 wa ujumbe wa uzazi wa mpango, maana ya uzazi wa mpango ni uamuzi wa hiari unaofanywa na mtu binafsi, mke,mume, mwenzi au kijana katika kupanga ni lini wapate watoto, idadi ya watoto, baada ya muda gani na njia ipi ya uzazi wa mpango wangependa kutumia. 

Aidha mkurugenzi huyo, anasema uzazi wa mpango una mchango mkubwa katika kukuza uchumi, maendeleo ya familia na ya nchi kwa ujumla ili hupunguza idadi ya mimba zisizotarajiwa, kuharibika kwa mimba, huboresha afya ya mama, baba, watoto wachanga na familia kwa ujumla.