Home Tukumbushane MJADALA WA KUJENGA TAASISI IMARA ZA UMMA UENDELEZWE

MJADALA WA KUJENGA TAASISI IMARA ZA UMMA UENDELEZWE

4575
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Tangu mwisho wa Vita Baridi mwishoni mwa miaka ya 80, suala la udhibiti wa mali asili limetokea kuwa muhimu katika somo zima la usalama, farakano na amani hapa duniani.

Wanazuoni na wataalamu wengine katika fani ya maendeleo wamekuwa wakiona kwamba katika nchi changa uendelezaji wa taasisi imara za umma unaolenga kudhibiti mamlaka za usimamizi za nchi za nje ambazo hukazania sana uwepo wa kanuni za kiliberali-mamboleo kama vile utandawazi, ubinafsishaji, uwazi na uwajibikaji kama vitu vya lazima katika kusuluhisha migogoro ya uvunaji wa maliasili katika nchi husika na pia kujaribu kutafuta suluhu na haki katika jamii.

Lakini katika nchi nyingi Barani Afrika malengo haya yamekuwa ni ndoto kwani watawala wamekuwa hawapendi uendelezwaji wa taasisi imara zinazojitegemea katika maamuzi na badala yake taasisi zozote zilizopo ama zenyewe hujisalimisha kwa watawala ambao ndiyo wateuzi wa wanazoziongoza, au wateuzi wenyewe wanazidhibiti, angalau kwa rimoti.

Kutokana na tabia hii viongozi kadha wamekuwa wanaziingilia taasisi hizo, hususan Bunge, kuzilazimisha kubadilisha katiba/sheria katika kujiongezea mihula ya kuendelea kukaa madarakani, au kujijengea ngome za kisiasa na kuwatenga wapinzani na wenye mawazo mbadala.

Hata katika uvunaji wa mali asili za nchi, taasisi zinazosimamia zinalazimishwa kuweka usiri mkubwa katika mikataba na wachimbaji kiasi kwamba wananchi hawajui wanapata kiasi gani kutokana na maliasili walizojaliwa na Mwenyezi Mungu. Kuna baadhi ya nchi hata taasisi za umma kama vile za ukaguzi wa mahesabu inayoweza kukagua mahesabu yanayohusu mapato ya mali asili zinazovunwa.

Kabla hajaondoka madarakani, mwaka 2016 Rais Barack Obama akihutubia kikao cha Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa alisema hivi kuhusu nchi yake: “Kuna mengi ambaye ningependa kuifanyia nchi yangu isonge mbele. Lakini sheria ni sheria, na hakuna mtu yuko juu ya sheria, hata rais.”

Obama alikuwa anamaananisha kwamba rais anapaswa kutenda kazi yake kwa kufuata sheria, na si vinginevyo. Rais anayetambua hivyo hawezi, kwa mfano akasema: “mimi lengo langu ni kuifikisha nchi iwe mithili ya pepo hapa duniani, na kama sheria zinanizuia, basi niko tayari kuzikiuka.”

Kwa ufupi, katika ujumbe wake kwa viongozi wa Afrika, Obama alikuwa anasisitiza uwepo wa taasisi imara zinazoheshimiwa na viongozi wake. Alitolea mfano uliohusu rais wa kwanza wa nchi yake, George Washington (1789-1797) ambaye alikataa kugombea muhula wa tatu mwaka 1798 pamoja na kwamba alikuwa shujaa na kupendwa sana na wananchi.

Aliondoka madarakani akisisitiza Katiba na misingi ya demokrasia waliojiwekea ufuatwe na iheshimiwe. Hata rais wa mzalendo wa kwanza wa Afrika ya Kusini Nelson Mandela alifanya hivyo hivyo.

Lakini mwaka 1940 Rais Franklin Roosevelt, katika hatua ya ambayo haikupata kutokea katika historia ya Marekani tangu George Washington aliomba na kuruhusiwa kugombea muhula wa tatu na akashinda.

Lakini hii ilitokea katika kipindi kigumu – wakati Vita ya Pili ya Dunia imeanza. Hata hivyo miaka michache baada tu ya Vita hiyo – mwaka 1947, na kabla nchi nyingi Barani Afrika hazijapata uhuru, Bunge la Marekani liliidhinisha mabadiliko ya Katiba yaliyosisitiza mihula miwili tu ya urais ya miaka minne minne. Ilichukua miaka minne kwa mabunge ya Majimbo yote 48 (wakati ule) kuidhinisha mabadiliko hayo.

Hiyo ni mifano tu ya wenzetu wanavyolipa umuhimu suala la kuheshimu mihula ya utawala kwa marais.

Na katika hotuba yake nchini Afrika ya Kusini ya kuadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Nelson Mandela mapema mwezi uliopita Obama huyo huyo alirudia uwepo wa taasisi imara katika nchi za Afrika, na kuwataka wananchi wajenge utamaduni wa kuwawajibisha viongozi wao.

Alisema hii ni muhimu kwa sababu viongozi na vyama vya siasa huja na kuondoka na iwapo kuna taasisi imara, basi maendeleo yanahakikishwa, achilia mbali amani na utulivu wa nchi. Hali ya amani na utulivu inahakikishwa iwapo kuna taasisi imara inayosimamia chaguzi – suala ambalo ndilo mara kwa mara huwa chimbuko la farakano katika nchi kadha barani humu na hata vita za wenyewe kwa wenyewe.

Uwepo wa taasisi huru na imara za umma na siyo viongozi wenye nguvu, pia linatajwa kama njia sahihi ya kupambana na ufisadi katika nchi zetu Barani Afrika. Hata hapa kwetu hivi karibuni suala hili limeanza kuzungumzwa na viongozi mbali mbali, akiwemo Mdhibiti na Mkaguzi wa Mahesabu ya Serikali (CAG), Pro Mussa Assad ambaye anaongoza taasisi hiyo muhimu katika kulinda fedha za serikali. Ni vyema mijadala ya aina hii iendelezwe.

Na katika kushughulikia ufisadi hakuna suala tete ambalo huibuka katika nchi mbali mbali kama ufisadi unaohusu wakuu wa nchi – waliopo madarakani na wale wa zamani.

Hili linatokana na msemo katika lugha ya Kiingereza unaosema “corruption of the best is the worst” – yaani ufisadi unaofanywa na watu wa juu ndiyo mbaya zaidi. Na ndiyo unaoangamiza nchi kimaendeleo kwa sababu ufisadi wa wakubwa, kama hakuna taasisi imara za kuzuia na kuchunguza, basin chi nzima inaweeza ikadhoofika kiuchumi.

Hata hivyo katiba na sheria za nchi mbali mbali zinatofautiana – kuna baadhi zinatoa kinga kwa viongozi hao – kwa mfano Tanzania, na nchi nyingine, lakini zipo nchi kadha hakuna kinga hiyo. Nchi kama Korea ya Kusini na Brazil hazina kinga kwa marais wa zamani na wa sasa.

Na tukiacha kinga kwa wakuu wa nchi kuna baadhi ya nchi ambako taasisi zake za  usimamizi wa sheria – kama vile taasisi za uchunguzi na za mashitaka huwa ni huru zaidi na vyenye nguvu na viko juu ya siasa – kitu anachosisitiza Obama – na hivyo huweza hata kumwita rais wa nchi kwa mahojiano.

Marais wawili wa zamani wa Korea ya Kusini, Chun Doo Hwan aliyeoongoza 1980-1988 na mrithi wake Roh Tae Woo (1988-93) walishitakiwa na kuhukumiwa vifungo gerezani katika kile kilichoitwa “Kesi ya Karne.” Na ni mwaka huu tu Rais Park Geun-hye aliyongoza tangu 2013 naye aliondolewa madarakani kutokana, pamoja na mambo mengine, ufisadi.

Mwaka 2001 aliyekuwa rais wa Ufilipino

Joseph Estrada aling’olewa madarakanani kwa maandamano ya wananchi kutokana na ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma na baadaye kushitakiwa. Alituhumiwa kupokea milungula kutoka makampuni ya kuchezesha kamari.

Aliyemfuatia Gloria Arroyo (2001-2010) alikamatwa mwaka 2011 kwa tuhuma za ufisadi na utumiaji madaraka vibaya na hadi sasa kesi inaendelea huku yeye akiwa amelazwa hospitali chini ya ulinzi mkali.

Miaka kadha iliyopita aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za miamala tata kuhusu kampuni zake katika miaka ya 90.

Na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan Benazir Bhutto (merehemu) mara mbili aliondolewa madarakani kutokana na tuhuma za ufisadi. Alishitakiwa na kuhukumiwa wakati akiwa nje ya nchi. Na aliyemrithi, Nawaz Shariff naye aliondolewa madarakani mapema mwaka huu kwa tuhuma za rushwa na hivi sasa anatumikia kifungo cha miaka 10 gerezani.

Lakini hakuna mfano mzuri wa namna wakuu wa nchi hujikuta kushawishika na kujiingiza katika ufisadi kama Brazil. Wanafanya hivyo wakijua fika kwamba nchi hiyo haina kinga ya kutoshitakiwa.

Na sasa hivi rais wa zamani wa nchi hiyo Luis Ignacio Lula da Silva ambaye alliongoza kuanzia 2003 hadi 2011 uko gerezani akitumikia kifungo cha miaka 12.