Home Makala Kimataifa MKAKATI WA SADC KUDHIBITI UGAIDI UNAHITAJI MBINU MPYA

MKAKATI WA SADC KUDHIBITI UGAIDI UNAHITAJI MBINU MPYA

539
0
SHARE

NA AMINA OMARI, MUHEZA

VITENDO vya uharamia na ugaidi vimekuwa vikitikisa duniani kwa sasa na kuchangia kuleta machafuko na madhara ikiwemo vifo pamoja na ulemavu.

Mataifa mengi duniani yamekuwa yakichukua hatua mbalimbali za kudhibiti vitendo hivyo viovu, kwani vimekuwa vikichangia kuyumbisha uchumi wa wananchi na nchi kwa ujumla.

Hapo awali vitendo hivyo vilikuwa vinasikika sana katika bara la Ulaya lakini katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa kukitokea matukio hayo katika mabara ya Asia pamoja na Afrika.

Hivyo vitendo hivyo vimechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza majukumu ya majeshi kwa nchi mbalimbali duniani kuanza kubadilika kiutendaji na kimbinu ili kukabiliana  na matukio hayo.

Hivyo, kutokana na kuwepo kwa matishio ya matukio hayo, nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa bara la Afrika (SADC) zilipoamua kwa pamoja kuja na mpango wa kushirikiana katika kulinda pamoja na kupambana na vitendo hivyo.

Hivi karibuni Mkoa wa Tanga ulikuwa mwenyeji wa majeshi ya SADC kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kupambana na matukio ya ugaidi

pamoja na uharamia  yatakayotokea katika nchi hizo.

Mafunzo hayo yaliyodumu kwa takribani mwezi mmoja, yalijulikana kwa  jina la Operesheni Matumbawe ambayo iliweza kufanyika katika

maeneo ya nchi kavu na majini katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, anasema

mazoezi ya ugaidi na uharamia yaliyofanywa na vikosi vya SADC yatasaidia kuibua mbinu mpya ya upambanaji wa matishio ya uvunjifu wa amani na usalama kwa nchi washirika.

Kutokana na wahusika wa matukio ya ugaidi na uharamia kubadili mbinu za matukio hayo mara kwa mara, hivyo hali hiyo imechangia kutolewa kwa mafunzo hayo ili kuwapa uwezo wanajeshi wa nchi za SADC kupambana na uhalifu huo.

Anasema matukio ya uharamia ama ugaidi hayana mipaka na hivyo ni lazima yakapigwa vita kwa pamoja kwa kushirikiana baina ya nchi washirika wa umoja huo.

Anasema kwa sasa nchi za SADC ni kama  bara moja ambalo linashirikiana katika kutunza amani pamoja na kudhibiti na kuzuia vitendo vyovyote vitokanavyo na  kuvuruga amani.

“Mazoezi hayo ni sehemu ya uthibitisho wa ushirikiano uliokuwepo baina

ya nchi washirika katika kupambana na matishio ya ugaidi na uharamia katika nchi za SADC pale ambapo yanatokea,” anasema Waziri Mwinyi.

Vilevile Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, anasema operesheni hiyo ilikuwa imelenga katika malengo makuu matatu ambayo ni kujenga uzoefu baina ya majeshi na kuweka ushirikiano wa kindugu na ukaribu, kutengeneza mkakati wa kulinda amani kwa pamoja hasa katika kukabiliana na  matishio ya ugaidi, uharamia na biashara za madawa ya kulevya na binadamu.

“Operesheni hiyo ililenga katika kuandaa vikosi hivyo kuweza kushiriki katika jeshi la pamoja la Afrika, kwani nchi za SADC majeshi yake huwa yanashiriki katika  kanda tano za Afrika.

Aidha, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, anasema

kama wanajeshi wameweza kupiga hatua moja mbele kwani vitisho vinavyotokea sasa havina mipaka, hivyo tunahitaji ushirikiano.

Huku akikumbushia namna ambavyo mwaka 2012 matukio ya uharamia yalivyoweza kuleta athari kwa nchi ya Tanzania yalihusisha  utekaji wa meli za mizigo ambayo ilikuwa imebeba bidhaa za wafanyabiashara kwa ajili ya kuleta katika soko la Tanzania.

Hivyo hali hiyo iliweza kusababisha matishio ya hali ya uchumi wa nchi, kwani  wafanyabiashara walilazimika kutishia kusitisha kuleta bidhaa

kutokana na watekaji hao kudai fidia kubwa  ili kuachia mizigo hiyo. Na kusababisha majeshi ya kimataifa kuingilia katika kukabiliana na matishio hayo yaliyokuwa yakiukabili ukanda huyo, ambapo kutokana na matukio hayo ndipo majeshi ya nchi za SADC yaliweza kujiimarisha.

“Kama mnakumbuka vizuri matishio yaliyoweza kutokea katika maeneo ya

Amboni jijini Tanga na Kibiti namna ambavyo yalivyoweza kuleta athari kwa wananchi na mali zao,” anasema Mabeyo.

Matukio ya Amboni majeshi yetu yaliweza kupambana na ugaidi vizuri, hivyo tukaona tuwalete wenzetu nao waweze kushuhudia kama mapango hayo yanaweza kuingilika.

Hivyo ameongeza kuwa kuja kwa Operesheni hiyo ni kuongezeana nguvu ili kukabiliana na matishio ya aina hiyo  pamoja na kubadilishana uzoefu wa kimiundombinu  pamoja na vifaa vya utaalamu katika kukabiliana na matukio hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Operesheni hiyo, Meja Jenerali Harison Masebo, anasema licha ya vikosi hivyo kufanya kazi iliyokusudiwa pia vimeweza  kushiriki katika shughuli za maendeleo zilizoko jirani na eneo hilo la Mlingano.

“Pia niwahakikishie kuwa tupo tayari kwa muda wote kupambana na majangili pamoja na maharamia ambao wataweza kuvamia nchi mojawapo na kujaribu kufanya matukio tutaweza kupambana mara mmoja kwani sasa tupo kama jeshi moja,” anasema mkuu huyo.