Home Makala MKASA WA MALKIA BESS NA UBABE WA VIONGOZI WETU

MKASA WA MALKIA BESS NA UBABE WA VIONGOZI WETU

409
0
SHARE

NA IGAMANYWA LAITON


MAMA yake Malkia Bess alinyongwa akiwa na umri wa miaka miwili na nusu tu. Baba yake alimkataa. Ndugu zake wakamtenga. Lakini akaja kuitawala dunia na kuacha alama kwenye historia ya mashujaa.

Mei 19, mwaka 1536 katika Jiji la London, mwili wa mwanamke mmoja ulikuwa ukining’inia katika mnara maarufu kwa kunyongea wahalifu jijini humo.

Kando kando ya Mto Thames, wakazi wa Jiji la Londoni walikuwa wamesimama wakitazama mwili wa Malkia wao, aliyenyongwa kwa amri ya mfalme baada ya kushindwa kumzalia mtoto wa kiume.

Ukiachana na kushindwa kumzalia mfalme mtoto wa kiume, maisha ya malkia huyo yalikuwa yamejaa misukosuko, jitihada zake kutaka kumpatia mfalme mtoto wa kiume zilikuwa zimekwama pamoja na kuzaa mtoto mmoja wa kike.

Kwa kipindi tofauti mimba zake tatu zilikuwa zimeharibika. Kwa kuwa mfalme alikuwa akitaka mrithi wa kiume, alikuwa amefanya mpango wa kuoa malkia mwingine, lakini ili kuondoa kikwazo kwa kuwa kidini ilikuwa si haki ya kumtaliki mke wake ambaye ni malkia mpaka kifo kiwatenganishe.

Mfalme alifanya njama na malkia huyo akakutwa na kosa la uhaini na hatimaye kuhukumiwa kunyongwa katika mnara huo maarufu uliokuwa kando ya mto maarufu wa Thames. Siku hiyo malkia huyo aliyekuwa akiitwa Anna Boleyn, akatundikwa na kufa akiacha mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa miaka miwili na nusu. Aliyekuwa akiitwa Elizabeth.

Kwa kuwa ndoa kati ya mfalme huyo aliyekuwa akiitwa Henry wa nane na Malikia Anna Boleyn ilikuwa imevunjwa, mtoto huyo wa kike aliyeachwa alikuwa akihesabika sasa kama si halali tena na haki zote za msingi katika utawala zilikuwa zimepotea moja kwa moja.

Mwaka mmoja baada ya Malkia Anna Boleyn kunyongwa, mfalme Henry wa Nane (Henry 8) alipata mtoto wa kiume kupitia Malkia Jane Seymour. Mtoto huyo aliyeitwa Edward wa Sita, ndiye aliyerithi kiti cha baba yake mwaka 1547 akiwa na umri wa miaka tisa tu.

Utawala wa Edward wa Sita ulikuwa mfupi sana kwani ulidumu kwa miaka 6, utawala wake ukikumbwa na misukosuko ya hali mbaya ya kiuchumi na maandamano ya wananchi na hali za kijamii zenye misukosuko, vita na Scotland na mengine mengi yaliyopunguza ufanisi wa utawala wake na kuonekana si kitu.

Februari mwaka 1553 akiwa na miaka 15, Edward alianza kuumwa, kwa kuwa ugonjwa wake ulionekana kuwa hautaweza kutibiwa, ilikuwa lazima yeye Edward kama mfalme ataje na kuidhinisha jina la atakayerithi kiti chake.

Edward hakutaka kutaja jina la dada yake Elizabeth na mwingine aliyekuwa akiitwa Mary (dada zake ambao walikuwa baba mmoja na yeye, sababu kuu hasa akiogopa Uingereza kurudi mikononi mwa Wakatoliki, kwa kuwa yeye alikuwa Mprotestanti), alichofanya akapendekeza jina la binamu yake aliyekuwa akiitwa Jane Grey.

Baada ya kifo cha Edward, wenye mamlaka ya kutangaza mrithi baada ya kifo cha mfalme kwa kutambua kuwa Edward hakuwa sahihi kutaja jina la binamu yake kama mrithi na kuacha dada zake, wakaamua kumpa ‘Mary’ madaraka ambaye baada ya siku tisa za kushika madaraka akaamuru haraka Jane Grey anyongwe.

Mary wa Kwanza alitawala kuanzia Julai mwaka 1553 hadi kifo chake mwaka 1558. Mary alikuwa binti pekee wa Mfalme Henry wa Nane kwa mke wake wa kwanza aliyekuwa akiitwa Catherine wa Aragon.

Mary baada ya kuamuru Jane Grey anyongwe, akairudisha Uingereza katika mamlaka ya Kanisa Katoliki, Mary anakumbukwa kwa kufunga ndoa na mfalme wa Hispania aliyekuwa akiitwa Phillips na hivyo kuunganisha tawala mbili za Uingereza na Hispania, wakati huo Hispania ikiwa ni ya Kikatoliki na moja ya tawala yenye nguvu kuwa kichumi na kisiasa Ulaya, Asia na duniani kwa ujumla.

Mwaka 1558, Malkia Mary alipatwa na kansa ya uzazi na afya yake kuanza kuzorota na hatimaye kufariki Novemba 11 mwaka 1558, akiwa na umri wa miaka 42. Alifariki na kuacha Uingereza imekumbwa na janga la ugonjwa wa kuambukiza (Influenza).

Kwa kuwa katika mlolongo wa vinasaba vya mfalme Henry wa Nane kulikuwa kumebaki mrithi mmoja Elizabeth (mtoto wa malkia aliyenyongwa katika mnara), Uingereza ikamtangaza kuwa malkia mpya.

Jiwe la pembeni likawa jiwe la msingi. Akipokea Uingereza kutoka mikononi mwa watawala wawili waliomtangulia ambao walikuwa hawajafanya chochote kikubwa, Uingereza ambayo ilikuwa imepiga magoti chini ya Hispania, Uingereza inayotafunwa na balaa la ugonjwa, hali ngumu za kiuchumi na mengineyo.
Akiwa mtawala wa mwisho wa koo za Tudor, Malkia Elizabeth aliwataka Uingereza kwa miaka 45 kuanzia Novemba 17 mwaka 1558 hadi kifo chake Machi 24, mwaka 1603.

Baada ya kushika mamlaka, Malkia Elizabeth au Bess jina lake jingine maarufu, alitafuta washauri wenye akili inasemekana Elizabeth wakati wote wa utawala wake, mashauri na maamuzi yake yalitegemea hawa washauri ambao walikuwa wenye akili na ujuzi mwingi katika utawala, hasa katika uchumi, vita na mambo mengine muhimu.

Akipingana na mtawala aliyepita, Malkia Mary ambaye alikuwa Mkatoliki, Malkia Elizabeth akairudisha Uingereza na kuwa ya Kiprostanti, jambo ambalo lilileta mgongano na uadui na mfalme wa Hispania ambaye alikuwa ni Mkatoliki, uadui ambao hatimaye ulizalisha vita muhimu kwa Malkia Elizabeth, vita ya kihistoria kati ya Hispania na Uingereza, vita kati ya Malkia Mprostanti na Mfalme Mkatoliki.

Mwaka 1585, Mfalme Philip wa Uhispania kwa kudhania Malkia Elizabeth ni wa mchezo mchezo kwa kuwa ni mwanamke, akakusanya jeshi lake na merikebu maarufu kama ‘Armada’(ambazo zilikuwa zikiogopwa kwa mashambulizi yake ya kushtukiza na masafa marefu) zake za kivita kwenda kuishambulia Uingereza.

Vita hiyo ilimwacha Malkia Elizabeth na ushindi baada ya majeshi yake yaliyopangwa kiustadi kuzishambulia na kuzichakaza vibaya merikebu za Mfalme Phillip.

Baada ya kuishinda Hispania, Uingereza ikaibuka kuwa miliki yenye kuogopeka barani Ulaya, Asia na duniani.
Utawala wa Malkia Elizabeth unajulikana kama utawala wa ufanisi na msingi wa Uingereza iliyokuja kuitawala dunia kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Ni katika utawala wa Malkia Elizabeth kulitokea mfumuko wa fikra katika sayansi na sanaa, ni kipindi cha utawala wake Uingereza ilitoa watu kama mwandishi mashuhuri William Shakespare, Christopher Marlowe na wavumbuzi maarufu kama vile Sir Francis Drake ambaye aliizunguka dunia kwa kupitia bahari.

Katika maisha yake yote Malkia Elizabeth alibaki bila kuolewa na hivyo kuwa mtawala asiye na mrithi na kupelekea kumaliza mlolongo wa vinasaba vya koo za Tudor katika utawala wa Uingereza. Inasemekana Malkia Elizabeth alibaki kuwa bikra miaka yake yote na ndiyo maana hujulikana kwa majina kama ‘Virgin Queen’ au ‘Malkia Bikra’.

“I know I have the body of a weak and feeble woman, but I have the heart and stomach of a King” (Ninajua nina mwili dhaifu na usio na nguvu kama ilivyo jinsi ya kike/mwanamke, lakini nimejaliwa moyo na tumbo kama Mfalme),” hayo yalikuwa maneno ya Malkia Elizabeth aliyoyatoa katika hotuba yake maarufu mbele ya wanajeshi wake 4000, Agosti 18, mwaka 1588.

Viongozi wababe kama mfalme aliyeamuru malkia kunyongwa wapo wengi. Ubabe mara nyingi hauambatani na busara. Tulilie busara itawale vinywa na vichwa vya viongozi wetu.