Home Habari MKOA WA SHINYANGA NI KAA LA MOTO

MKOA WA SHINYANGA NI KAA LA MOTO

1860
0
SHARE

NA JOHANES RESPICHIUS


MKOA wa Shinyanga unaonekana kuwa  kaa la moto kwa baadhi ya wateule wa Rais hasa katika ngazi ya mkoa na wilaya.

Katika kipindi cha miaka miwili tayari viongozi watatu ndani ya mkoa huo wametumbuliwa wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Moto huo ulianzia kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Anna Kilango, ambaye aliitumikia nafasi hiyo kwa siku 29 tu na Katibu Tawala wa Mkoa huo Abdul Rashid Dachi.

Viongozi hao walitumbuliwa kwa sababu ya kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu sakata la watumishi hewa.

Rais alitengua uteuzi wa viongozi hao Aprili 11, mwaka 2016 mara baada ya hafla ya kupokea taarifa ya mwaka 2014/15 ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

MKUU WA WILAYA

Katika kudhihirisha kuwa mkoa huo ni kaa la moto kwa viongozi wa kuteuliwa, Julai 15, mwaka huu, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ta Kahama, Fadhili Nkurlu alitumbiliwa kwa kile kinachodaiwa kutoelewana na  Mkurugenzi wa Halimashauri.

Nkurlu alitumbuliwa akiwa kwenye ziara na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyokuwa akiifanya wilayani humo na nafasi yake kuchukuliwa na Anamringi Macha.

TATIZO SUGU

Inaelezwa kuwa tatizo kubwa ndani ya mkoa huo ni chuki, fitina na majungu hali inayosababisha baadhi ya viongozi kupelekewa taarifa za uongo na wakati mwingine kuundiwa mizengwe na baadhi ya watendaji ndani ya Serikali ya mkoa.

Hata katika ziara yake, Waziri mkuu, aliwapasha watumishi na viongozi wa halmashauri za wilaya za Ushetu, Msalala na Kahama Mji kuachana na uhusiano mbaya na kuwataka wabadilika mara mnoja.

“Migogoro niliyoisikia ambayo iko hapa ni kwa sababu ninyi mmeingia kwenye biashara na kuchukua upande, hapa Kahama, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Wilaya hamuelewani, Mkurugenzi na Wakuu wa Idara hamuelewani, Wakuu wa Idara na wasaidizi wao nao pia hawaelewani.

“Hali ya mahusiano hapa Kahama ni mbaya kuliko Kishapu na Shinyanga. Mnachapa kazi vizuri,  lakini tatizo kubwa kila mmoja anaenda kivyake, hakuna anayemsikiliza mkurugenzi wa halmashauri wala mkuu wake wa idara.

“Serikali haitavumilia kuona watumishi wakifanya mambo ya ovyo. Kahama ni wilaya yenye majaribu na Shinyanga nayo ni wilaya yenye majaribu makubwa. Kwa hiyo watumishi inabidi muwe makini, kuweni waangalifu msije mkaingia kichwakichwa kwenye majaribu haya,” alisema.

Aliwataka viongozi wanaopelekwa wilayani hapo kuwa makini kutokana na Kahama kuwa na fursa kubwa na nzuri kwenye kilimo, madini, mifugo na biashara.

“Kiongozi ukiletwa hapa inabidi uwe na kichwa kilichotulia. Inabidi uwe mwaminifu sana ili uweze kudumu kwenye wilaya kama hii. Kama kiongozi ulizoea kwenda disko inabidi uache, kama ulizoea kwenda baa inabidi ununue kreti uweke ndani kwako. Kama ulizoea kushabikia mpira kwa kujichora chaki, sasa basi. Kaa sebuleni kwako, angalia mpira kwenye luninga yako, ndiyo dhamana ya uongozi hiyo,” alisema.