Home Uchambuzi MNYAA: Hakuna uchaguzi Zanzibar bali ni uchafuzi

MNYAA: Hakuna uchaguzi Zanzibar bali ni uchafuzi

3267
0
SHARE

DSCN4912NA GABRIEL MUSHI

MACHI 20, mwaka huu Wazanzibar wanatarajiwa kupiga kura ya kumchagua rais, wawakilishi na madiwani huku kukiwa na hali ya sintofahamu kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani hususani Chama Cha Wananchi (CUF) ambacho kimesusia kushiriki marudio ya uchaguzi huo.

Marudio ya uchaguzi Visiwani humo, yamekuja baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka jana, kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kwa madai kuwa ulikuwa na kasoro nyingi.

Uamuzi huo uliibua hasira na malumbano kutoka kwa vyama vikuu vya siasa kikiwamo CCM na CUF, pamoja na viongozi wake kukutana zaidi ya mara nane hapakuwapo na suluhu.

Kama ilivyo ada RAI katika safu hii lilipata fursa ya kuzungumza na mmoja wa wanasiasa machachari Mohammed Habib Mnyaa (CUF), ambaye ni Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mkanyageni huko Pemba na kuelezea mambo kadhaa kuhusu uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na madhila aliyokumbana nayo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mnyaa alianza kuelezea hisia zake kuhusu mgogoro huo wa Zanzibar na kusema ni dhahiri kuwa mambo ya Zanzibar yanatia aibu kwa Wazanzibari  kutokana na kitendo cha Jecha kufuta uchaguzi wa wawakilishi, madiwani na rais, lakini wabunge akawaacha kwa maana kuwa ni halali wakati uchaguzi umefanyika katika sehemu moja, chumba kimoja na mawakala ni walewale.

Anasema sasa haieleweki aliyevunja Katiba ya Zanzibar ni nani.

“Mgogoro wa uchaguzi Zanzibar watu wengi wanasema ni wa kihistoria, hili nalipinga kwa sababu huu unatokana na madaraka ya watu wa chache wanaotaka kutumia historia nafasi kujinufaisha, Kiujumla mapinduzi ya Zanzibar yamenikuta nikiwa na umri wa miaka saba, sasa walio wengi tumekua katika historia ya mapinduzi hayo, sasa nina miaka 60 na si kweli kuwa kulikuwa na mgogoro miaka yote hiyo. Hili ni tatizo ambalo linapandikizwa na watu.

“Mwaka 2010 Maalimu na Karume walikubaliana kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa, hili ni suala ambalo tulitakiwa kuendelea nalo ili kuondokana na migogoro kwa sababu wenzetu wanaendelea na kujiimarisha kiuchumi, lakini Zanzibar, hakuna viwanda, kila mtu ili aweze kuwa na kazi mpaka aajiriwe kwenye majeshi pekee, hali ya uchumi ni mbaya,” anasema.

Kwa mantiki hiyo anasema kuwa uamuzi wa ZEC ni kufuta uchaguzi huo ulikuwa ni shinikizo ambalo lilitokana na Wazanzibar ambao wanaungwa mkono na upande wa Jamhuri.

Aidha, akizungumzia marudio ya uchaguzi huo, Mnyaa anasema Jumapili hakuna uchaguzi bali kuna uchafuzi, kwa sababu katika ndoa upande wa mwanamke na mwanamume lazima pande zote zifikie makubaliano ndipo pawepo na ndoa.

“Uchaguzi lazima pawepo na makubaliano ya vyama ndipo ufanyike uchaguzi. Kwa sababu Shekhe au Padre wa kuozesha ndio ZEC au Jecha, sasa haaminiki na hata CCM waliwahi kusema hawamuamini sasa sijui kama hiyo ndio au uchaguzi upo. Vile vile lazima katika ndoa pawepo na mashahidi, sasa tukianngalia katika uchaguzi huu hakuna waangalizi, kwani wa nje na ndani wamekataa kutambua huu uchaguzi, hivyo ni dhahiri kuwa hakuna uchaguzi kuna uchafuzi,” anasema.

Changamoto katika Uchaguzi Mkuu 2015

Hata hivyo, Mnyaa hakusita kuzungumzia anguko lake katika kura za maoni mwaka jana, amekiri kuwa ulikuwa ni uchaguzi mgumu kuliko chaguzo zote.

“Mchakato wote wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ulikuwa na matatizo ambayo yanatofautiana kati ya sehemu na sehemu, kwa upande wangu nilipitwa na mwenzangu kwa kura nane kwenye kura za maoni,  ingawa katika kuteuliwa kuna sehemu tatu, ikiwamo kura za maoni, kuhojiwa na kupimwa kwa shughuli ulizozifanya jimboni, hivyo kwa upande wangu nilipitiwa kwa kura nane kwenye kura za maoni lakini katika shughuli jimboni na mahoajiano kote huko nilipita na Baraza Kuu lilipitisha jina langu.

“Kilichotendeka kulikuwa na mgawanyo wa majimbo, hivyo Jimbo la Mkanyageni likaingizwa Mkoani. Katika majimbo 18 ya Pemba walilitoa la Mkanyageni wakaongeza kule sehemu za Chakechake, hivyo Mkoani ilikuwa na majimbo matano ikawa na majimbo manne na Chakechake ikawa na majimbo matano. Tukakuta katika jimbo la Mkoani kuna wagombea wanne ambao walipitishwa kama wawakilishi, hivyo chama kikachukua maaamuzi ambapo wale wa zamani wakachaguliwa, mmoja mwakilishi na mwingine mbunge, sasa sijui sababu za kunitoa ni nini,” anasema.

Aidha, anasema mgawanyo huo wa majimbo huko Visiwani ulikuwa ni mpango wa CCM kupunguza majimbo Pemba na kuongeza Unguja.

“Tofauti inayoendelea kuongeza sasa ni hatari kwani nyakati za ukoloni haikuwa hivi… kwani mwaka 1963 kulikuwa na majimbo 31, kati ya hayo majimbo 17 yalikuwa Unguja na 14 Pemba, tofauti ilikuwa majimbo matatu. Baada ya mapinduzi hapakuwa na uchaguzi mpaka ilipofikia mwaka 1992 na mfumo wa vyama vingi kuanzia ambapo mwaka 1995  Zanzibar iligawanywa katika majimbo 50 ambapo Pemba ilikuwa na majimbo 21 na Unguja 29, hapo kukawa tofauti ya majimbo nane. Mwaka 2002 kulikuwa na sensa nyingine wakagawanya majimbo wakapunguza Pemba kutoka 21 mpaka 18 wakaongezea Unguja kutoka 29 mpaka 32 ikawa tofauti ya majimbo 14. Ilipofikia tena mwaka 2015 majimbo yakaongezwa manne Unguja na Pemba yakabaki yaleyale ambapo Unguja ilifikia majimbi 36 na Pemba 18, hivyo tunaona tofauti ni 18.

“Maana yake sasa ni sawa na kuwanyima maendeleo upande wa Pemba.  Kwa sababu kama jimbo moja ambapo Mwakilishi anapewa fedha za mfuko wa jimbo milioni 15 na Mbunge anapewa Sh milioni 24 kwa mwaka, maendeleo katika jimbo hilo yalikuwa ya uhakika kwani ukipunguza majimbo unapunguza hata fedha za maendeleo.

“Pia kigezo cha sensa ni kibovu kwa sababu Unguja yapo majimbo ambayo yana watu zaidi ya 4000 lakini Pemba wanapunguza kwa kuwa CCM hawapati kura huko. Ndipo sababu ya Maalim Seif kupata nguvu kwani anataka haki kwa pande zote,” anasema.

Anaongeza na kusema uchaguzi mkuu umezidi kuwa mgumu kwa sababu nafasi za ubunge na uwakilishi zimekuwa kama kimbilio na kusababisha idadi kubwa ya wagombe zaidi ya 20 katika nafasi moja.

“Hali hii inasababisha matumizi pia makubwa ya fedha kwa mfano kwa upande wa Tanzania bara ambapo majimbo ni makubwa. Nadhani tukiendelea na mfumo huu wa uchaguzi, tutakwama, ipo haja ya kutafuta njia nyingine ya kupata wabunge ambapo tunachagua Rais ambaye atakuwa anateua wabunge na wawakilishi wake. Hili nadhani linaweza kupunguza rushwa katika level ya kitaifa na kichama kiujumla.

Akifafanua sababu zilizosababisha Tanzania kutosaini Mkataba wa Afrika kuhusu mambo ya Uchaguzi, Demokraisia na utawala bora, Mnyaa anasema; Tunaona kuwa nchi ambazo hazijasaini na kuridhia ni 16 kati ya nchi 28 ambazo ziliandaa mkataba huu.

“Kiujumla katika mkataba huu kuna sehemu ya 2 (i-ii) ambayo ndio yenye mambo muhimu ambayo yamesababisha uchaguzi wa Zanzibar na Tanzania kuwa mbovu, hivyo ni dhahiri Tanzania inafanya makusudi, kwani iwapo nia ingekuwepo basi ingesaini huu mkataba, kwa hiyo hili nalo ni jipu vilevile. Tunamtaka Magufuli alitumbue.

“Lakini pia Tanzania imesaini mkataba wa masuala ya uchaguzi ule wa SADC lakini huu wa AU kwa sababu moja, ni kwamba huwezi kusaini huu wa AU bila kuwa na tume huru inayojitegemea, kwa kuwa kuna miongozo ambayo imetolewa na mkataba huo wa AU ndio maana hadi sasa imesuasua kusaini na kuridhia. Hiki ndicho kipengele ambacho Tanzania inashindwa kutekeleza,  iwapo Rasimu ile ya Jaji Warioba ingepita tungeweza kusaini kwa sababu ilitaka kuwepo na tume huru za uchaguzi,” anasema.

Pamoja na mambo mengine, Mnyaa anapongeza hatua anazochukua Rais Magufuli ila atekeleze kwa umakini bila kuvunja sheria.

“Nampongeza kwani ndio mambo ambayo nilikuwa napigia kelele kule Bungeni na wapinzani wenzangu, jambo muhimu isije kuwa ni nguvu ya soda, namshauri liwe ni jambo endelevu,” anasema