Home Makala Mnyika anaweza kuvaa viatu vya Dk. Slaa?

Mnyika anaweza kuvaa viatu vya Dk. Slaa?

534
0
SHARE

Na JUVIUS KAIJAGE

Desemba 19, mwaka huu Mwenyekiti wa Chama cha Demokraia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amemteua mbunge wa Kibamba, John Mnyika, kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Mnyika ameteuliwa kuchukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Dk. Vicent Mashinji, ambaye ametumikia nafasi hiyo kwa muda wa miaka minne tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo Machi mwaka 2016.

Baada ya uteuzi huo  wa Mnyika na taarifa kutangazwa kwa wajumbe wa chama hicho katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam,  zilianza kuibuka hisia, mitazamo ambayo hatimaye ilizaa mijadala mbalimbali.

Kimsingi mijadala hiyo imekuwa ikilenga sababu za Mnyika kuteuliwa na uwezo alionao katika kukijenga chama ambacho inasemekana baada ya Dk. Wilbroad Slaa kuvua viatu vyake vya ukatibu mkuu nafasi hiyo ilikuwa haijapata mtendaji sahihi wa kuvivaa vyake. 

Nasema nafasi hiyo ilikuwa haijapata mtu sahihi wa kuvivaa viatu hivyo  kwa maana kwamba tangu Dk. Mashinji ateuliwe kuwa katibu mkuu mwaka 2016, chama kimeendelea kuwa na ubaridi baada ya kukosa msisimuko uliokuwa umezoeleka.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanadai kuwa Dk. Mashinji ni msomi mwenye kujiamini kulingana na historia yake lakini siyo mwanasiasa kama alivyokuwa Dk. Slaa na ndiyo maana hata hotuba zake hazikuwa na mvuto wala ushawishi. 

Ni ukweli usiopingika ukimsikiliza Dk. Slaa anapokuwa anahutubia hakika unatamani aendelee kuongea kwani hotuba zake zina mvuto wa hali ya juu na mara nyingi ni za kiutafiti na takwimu. 

Ni mwanasiasa anayeongea kwa hisia kali na uchungu hasa pale anapokuwa anazungumzia masuala ya nchi ambayo kimsingi yanakwenda kombo wakati wenye mamlaka ya kuyashughulikia wapo. 

Dk. Slaa ni mwanasiasa ambaye hapendi majungu, fitina na masengenyo kwani kutokana na uwazi wake huwa anaongea bila kificho ilimradi ana ushahidi kwa kile anachokizungumzia. 

Ni mwanasiasa mwenye kujiamini katika viwango vya hali ya  juu kwani hata kama ungetumia vitisho ili kumziba mdomo kamwe huwezi kufanikiwa kwa sababu yuko tayari kufa kwa ajili ya kuutetea ukweli. 

Dk. Slaa aliyeingia Cahadema mwaka 1995 baada ya kufanyiwa ulaghai na chama chake CCM  katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini alikuwa na vitu vingine vya ziada ikiwamo mapambano makali dhidi ya  vitendo vya ufisadi na rushwa. 

Kwa wananchi wanaokumbuka  ufujaji wa pesa Benki Kuu Ya Tanzania (BoT) , kupitia mfuko wa madeni ya nje EPA, kashfa za Alex stewart, Mwananchi Gold na Deep Green Finance  bila kusahau  kashfa  ya Richmond watakubaliana na ninachokisema. 

Dk. Slaa ni mpinzani halisi wa kujilimbikizia mali kwani akiwa mjengoni aliwahi kupinga hadharani kitendo cha wabunge walafi na makupe kutaka kujiongezea mishahara kwa kiwango kikubwa, kujiongezea  marupurupu na kununua magari ya kifahari yanayotumia mafuta mengi  ilhali  mamilioni ya wananchi ni fukara. 

Akitumia karata ya rushwa na ufisadi ambao kimsingi ulikuwa umeota mizizi katika taifa letu, Dk. Slaa alifanikiwa kwa kiwango kikubwa kuiongezea Chadema idadi kubwa ya wabunge na wanachama. 

Kutokana na msimamo mkali wa mwanasiasa huyu ni dhahiri katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 alikataa chama chake kumpitisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa mgombea urais na hivyo kuamua kutoa talaka hadharani kwa Chadema huku akitangaza kuachana na kujihusisha na masuala ya siasa. 

Kilichosababisha Dk. Slaa kumkataa kabisa Lowassa kuwania  kuingia katika jumba la kifalme ni kichefuchefu cha kula matapishi yake. 

Ikumbukwe kuwa kwa miaka kadhaa kabla ya uchaguzi huo Dk. Slaa alikuwa akimtuhumu Lowassa kuwa ni fisadi na hivyo kama angemkubali basi Watanzania wangemweka katika orodha ya wanasiasa vigeugeu na wasio na msimamo. 

Hizo zikiwa ni miongoni mwa sifa za Dk. Slaa, inasemekana kuwa sifa hizo zilipwaya katika ukatibu mkuu wa Dk. Mashinji licha ya mazingira magumu ya kufanyia siasa. 

La kujiuliza ni je, John Myika aliyeaminiwa na bosi wake hadi akamteua,  anao uwezo wa kuyafanya matendo aliyokuwa akiyafanya Dk. Slaa ili kukifanya chama kiendelee kupaa na kuwa hai hasa tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani? 

Wataalamu wa masuala ya ustawi wa jamii wanadai kuwa kila binadamu ana upekee na ni wa aina yake kwani kila mtu kuna namna alivyoumbwa. 

Kwa mantiki hii ya upekee katika maumbile ambayo ni kwa mujibu wa tafiti za wanataaluma bado swali linaendelea kuulizwa je, Mnyika ataweza kuvivaa viatu vya Dk. Slaa? 

Wakati Mbowe akimtangaza kumteua Mnyika na viongozi wengine katika nafasi mbalimbali, alisema amefanya hivyo kutokana na sababu za wanasiasa hao kukulia ndani ya chama hicho. 

‘‘Huyo mtu hajui, nasikitika hata kamati kuu haijui. Ninaowateua ni watu mnaowaamini wamekulia ndani ya chama,” kauli ya Mbowe wakati akitangaza uteuzi wa Mnyika. 

Kauli hii inaibua swali jingine kwamba, Mnyika kukulia ndani ya Chadema inatosha kumfanya awe mtu sahihi wa kuvaa viatu vya Dk. Slaa ambavyo kimsingi vilionekana kumpwaya Dk. Mashinji au kuna sababu nyingine za ziada? 

Wanaomfahamu vizuri Mnyika wanadai kuwa ni mwanasiasa shupavu anayejiamini hasa kwa kitu anachoamini kuwa yuko sahihi. Anao uwezo mkubwa wa kujenga hoja anapokuwa anahutubia hadhira kitu ambacho kilikosekana kwa Dk. Mashinji. 

Licha ya uwezo wake katika  kujenga hoja na kujiamini pia anatajwa kuwa ni mwanasiasa ambaye si rahisi kununuliwa na chama kingine kwa urahisi na ndiyo maana amekaa ndani ya Chadema kwa muda mrefu ukilinganisha na wanasiasa wengine.

Mnyika ana historia ya kuwa mtetezi wa watu tangu akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na hata akiwa mbunge kwa nyakati tofauti amekuwa akisimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya maji hususan maji.

Hata hivyo historia ya kujiamini, uwezo wa kujenga hoja na kuwa mtetezi wa watu si kipimo tosha cha kumfanya atoshe kuvaa viatu vya Dk. Slaa kwani hata mtangulizi wake Dk. Mashinji kabla ya kuteuliwa kuwa kwa nafasi hiyo alikuwa na historia iliyombemba ya kuwatetea madaktari wenzake lakini alipopewa zigo la ukatibu wa chama, kilichotegemewa kutoka kwake hakikuonekana.

Inawezekana matarajio kutoka kwa Dk. Mashinji hayakuonekana kutokana na sababu ya kwamba kuwa mtetezi wa watu katika taasisi fulani ni jukumu tofauti kabisa na lile la kuwa mtendaji mkuu wa chama.

Kimsingi nyika tayari ameaminiwa na chama na kuungwa mkono na wajumbe wengi kuwa anafaa kuwa katibu mkuu hivyo  kupimwa kwake kama anaweza kuvivaa viatu vya Dk. Slaa au la ni baada ya kuingia uwanjani na kucheza na kipimo kimojawapo itakuwa ni harakati za kuelekea katika Uchaguzi Mkuu 2020.

Simu: 0756521119, barua pepe: javiusikaijage@yahoo.com