Home Makala Kimataifa MOROCCO KUINGIA ECOWAS KUTABADILI HALI YA KISIASA?

MOROCCO KUINGIA ECOWAS KUTABADILI HALI YA KISIASA?

546
0
SHARE

NA MOSES NTANDU

WIKI iliyopita nilijadili na kuzungumzia Morocco ilivyojikita katika kuhuisha Afrika kuwa moja na kuwa Taifa hilo liliomba kujiunga na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas).

Katika hali ambayo imeonesha kuleta mabadiliko chanya makubwa ni kwamba wiki hii nimefanikiwa kupata taarifa za moja kwa moja kutoka Serikali ya Morocco kutoka jijini Rabat kuwa: “Miezi mitatu tu toka Morocco kuwa na makubaliano ya awali ya kujiunga na Ecowas, Serikali imepokea ujumbe wa ukanda huo na kukaribishwa Waziri wa Mambo ya Nje, Nasser Bourita, ili kukagua maombi ya Morocco kujiunga na jumuiya hiyo.”

Pia imeelezwa kuwa masuala yote ya kisheria na kiufundi ambayo yataiwezesha Morocco kujiunga na jumuiya hiyo tayari yameshafanyiwa kazi ipasavyo na hivyo kuna imani kubwa kuwa Taifa hilo litafanikiwa kupewa uanachama wa moja kwa moja.

Marcel Alain De Souza, ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Jumuiya hiyo, anathibitisha haya mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kusema: “Juhudi zinazofanywa na Morocco kupata uanachama katika jumuiya hii zipo katika njia sahihi na unakidhi haja zote hivyo tutathibitisha haya katika kikao chetu kijacho cha kawaida kitakachofanyika jijini Lomé, Desemba 16, mwaka huu.”

De Souza pia anasema kuwa vigezo vikuu vya kuikubali Morocco katika jumuiya hii vyote vimezingatiwa na kuheshimiwa na taifa la Morocco, ikiwa ni kwamba hadi sasa Taifa la Morocco limeruhusu biashara huru katika taifa hilo.

Pia Taifa la Morocco limekuwa na siasa safi zinazozingatia demokrasia na utawala bora, pia suala la usafirishaji wa bidhaa, huduma za kijamii na pia suala la udhibiti wa biashara za kikanda.

Kwa upande wa uenyekiti wa Ecowas, hii inaelezwa kuwa ni suala la kisheria na kidiplomasia ambalo litatekelewa pale ambapo Taifa la Morocco litakapokuwa mwanachama kamili wa jumuiya hiyo, ambapo pia watakuwa na haki ya kuwa na nafasi ya kupata uenyekiti wa jumuiya hiyo.

Katika suala la kiuchumi, Morocco inalenga kuimarisha jumuiya hiyo na baadaye kuimarisha bara zima la Afrika ili kuwa na Taifa moja imara la Afrika, Morocco inalenga kuwa na sarafu moja katika ukanda huo wa Ecowas na baadaye kuendelea na harakati hizo katika kuelekea katika Taifa moja la Afrika lenye uchumi imara.

Katika mkutano wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Bourita na ujumbe maalumu ulioongozwa na Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, De Souza, ujumbe wa Serikali ya Morocco ulisema kwamba Mfalme Mohammed VI ameandika barua rasmi akieleza dhana yake rasmi kwa Morocco kuwa radhi na kuomba jumuiya hiyo iwe na sarafu moja, ikiwa Morocco itaingia rasmi katika jumuiya hiyo.

Katika kujibu hoja hiyo, De Souza alisema ombi hilo linaweza kuchukua takribani muongo mmoja. Mfalme Mohamed VI alisema Taifa lake liko tayari katika historia hii ya kiuchumi na mahusiano barani Afrika ikianza na mataifa 15 ya Magharibi mwa Afrika.

Halikadhalika Morocco ipo tayari kufanya ukombozi wa kiuchumi na biashara katika jumuiya hiyo ya Ecowas ambayo inaelezwa kuwa na walaji wapatao milioni 340.

Katika malengo ya muda mrefu katika jumuiya hiyo, De Souza alisema wanatarajia kwamba watahamasisha na kupitia ushuru mbalimbali katika jumuiya hiyo ili kuwapunguzia ushuru huo, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uchumi wa jumuiya hiyo, kwani hadi sasa kuna takribani njia 6,000 za ushuru na Taifa la Morocco lina njia 17,800 za ushuru.

Pengine kwa sasa ni jambo gani linaelezwa kuwa ni njia thabiti za Morocco kukamilisha harakati zake kujiunga na jumuiya hii ya kimaendeleo kwa nchi za Magharibu mwa Afrika?

Kwa upande wa Bourita, anasema: “Ni lazima tuzingatie nyanja kuu tatu; ya kwanza njia ya majadiliano na mazingatio ya kiufundi, pili ni kujitambua na kuelewa malengo yetu ndani ya jumuiya hii na tatu ni kuzingatia matakwa ya jumuiya hii ya Ecowas.”

Kujiunga kwa Morocco katika Jumuiya hii ya Ecowas, De Souza anaeleza kuwa kunaonekana kubadili kabisa hali ya kisiasa katika ukanda huo na kuonekana kwa sasa kuwa na hali njema na tulivu kabisa.

“Tupo katika hali bora sana kisiasa kwa sasa bila kujali kwamba kila Taifa lina aina yake ya siasa, hivyo tunajitahidi kubadilika ili kuwa na siasa ya aina moja katika ukanda wetu huu ili iendane na mipango yetu ya muda mfupi na muda mrefu katika kujenga uchumi bora na mahusiano mema katika jumuiya yetu,” anasema De Souza.

Hali hii ya maelezo yanayotolewa na mwenyekiti wa jumuiya hii inaonesha kuwa kuna uwezekano mkubwa na Taifa la Morocco kupewa uanachama wa moja kwa moja, kwani Taifa hilo linaonekana kukidhi kila vigezo na kuwa limelenga kuboresha jumuiya hiyo kiuchumi, kisiasa, kimaendeleo na kidiplomasia.

De Souza pia alieleza kwamba:“Katika kipindi hiki ambacho imekuwa na jumuiya takribani tano ambazo zinaonesha kugawanyika, lakini Mfalme Mohamed VI wa Morocco anasema ukanda wa magharibi unapaswa kujitanua hadi kufika Kaskazini.”

Hii maana yake ni kwamba lengo la Mfalme Mohamed VI wa Morocco ni kuwa na jumuiya moja ya Afrika iliyo imara na yenye nguvu kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia na hii maana yake ni kuvunja ukanda na kuwa na Afrika moja badala ya kuendelea kuwa na kanda hizi tano tulizonazo.

Matakwa haya ya kuwa na Afrika moja yanaelezwa kuwa pamoja na changamoto zilizopo katika kanda tano zilizopo barani Afrika, bara la Afrika bado linaweza kuzingatia mahusiano na maono ya viongozi waliopita wa baadhi ya nchi za Afrika, wakiwa na lengo la kuunganisha mataifa yote ya Afrika na kuwa Taifa moja.

Mwandishi wa Makala hii anapatikana kwa namba ya simu 0714 840656 na baruapepe mosesjohn08@yahoo.om