Home Makala ‘MOTO WA ESCROW’ UMEREJEA KWA NGUVU

‘MOTO WA ESCROW’ UMEREJEA KWA NGUVU

675
0
SHARE
Mtambo wa kufua umeme wa IPTL, Tegeta, Dar es Salaam.

NA HILAL K. SUED


 

“Ni bora kukaa kimya hata kama utaonekana mjinga, kuliko kuzungumza na kuondoa shaka yoyote ya ujinga.”

Nukuu hiyo inayohusishwa na Maurice Switzer, mtunzi vitabu vya riwaya Mmarekani wa Karne ya 19 inaweza kupingwa na wengi, lakini wengi pia watakubaliana nayo – kwamba mara nyingi ukimya unaweza ukawa dawa nzuri katika mazingira tete ambayo mtu hujikuta nayo.

Aidha ni nukuu iliyonijia kichwani baada ya kuona ule moto wa kashfa kubwa zaidi ya wizi wa fedha za umma kuikumba Tanzania katika historia yake ghafla umeanza kuwaka tena kwa nguvu baada ya kupotea kwa karibu miaka mitatu.

Pengine si sahihi kusema moto ule ulipotea, bali ni kwamba haukupata mtu sahihi wa kuushughulikia hadi mwisho wake kwa njia stahiki na ya haki – bila kuonea mtu au kupendelea mtu.

Katika sakata hilo kulikuwapo mambo yaliyojiri ambayo ni vigumu katika hali ya kawaida kuyaelezea bila ya mtu kupandwa na hasira. Aidha kuna mengine yaliyotolewa kauli za kushtua ingawa sasa hivi siamini iwapo hawa wanaweza kuzirejea kauli zao kwa msisitizo, achilia mbali kuzipigania zifanyiwe kazi.

Kwa mfano siamini iwapo Christopher Ole Sendeka, aliyekuwa Mbunge wa Simanjiro katika Bunge lililopita anaweza tena kuibuka na kusema kwa kujiamini: “Serikali lazima ifanye uchunguzi wa kina kuwabaini na kuwachukulia hatua wale waliochukua mabilioni ya fedha taslim kutoka Benki ya Stanbic na kubeba katika mifuko ya sulfate kwa siku mbili…kinyume na taratibu zote za kibenki.”

Serikali haikuwahi kuipinga kauli hii, na kama ilifanyiwa kazi matokeo yake bado hayajawekwa hadharani, ingawa sasa hivi kuna kila dalili kwamba hili linaweza kuwekwa hadharani, pengine muda si mrefu – kutokana na jitihada zinazoendelea chini ya utawala wa Rais John Magufuli.

Lakini hakuna suala lililoshtua zaidi wananchi kama ile kauli ya Jakaya Kikwete, rais wa Awamu ya Nne katika mkutano na wazee wa Dar es Salaam aliposema fedha zile zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow hazikuwa fedha za umma, na hivyo kuamini kwamba alikuwa amelizika kabisa suala hilo – achilia mbali kuliondolea makali yake.

Naye pia siamini iwapo ataweza kuirejea kauli hiyo. Kingine ninachokumbuka katika hotuba ile ni kwamba hata mara moja hakutaja kwa majina Harbinder Singh Sethi au hata neno ‘Stanbic.’ Haidhuru basi angeyataja hayo kwa kusema suala zima la uchotaji fedha zile zilikuwa ni uzushi tu ulioibuliwa na kusambazwa na Chadema. Lakini ni Mbunge mwandamizi wa chama chake aliyotamka hayo Bungeni, naye alikuwa akirejea tu yaliokuwamo katika ripoti ya CAG.

Lakini katika mkutano ule kikwete angeweza kuyasoma ‘maoni’ ya wasikilizaji wake, namna walivyoonekana kutoridhishwa pale alipokuwa ‘akiwahukumu’ wale ambao yeye aliwaona ni wahusika wa kashfa ile – tofauti na hukumu (na orodha ya wahusika) iliyotolewa na Muhimili mwenza – Bunge.

Kwa mfano alipotangaza kumtimua Waziri wa Ardhi na Makazi Prof Anna Tibaijuka, wasikilizaji walishangilia, lakini aliposema analiweka kiporo suala la Prof Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini wengi walisikika wakiguna, kama ishara ya kutokubaliana naye katika uamuzi huo. Ujumbe wao kwake ulikuwa wazi kabisa.

Walionekana wakimwambia kwamba Watanzania, hawakuridhishwa na namna sakata hilo lilivyokuwa likihitimishwa. Na inashangaza kwamba Kikwete hakulijali hili hasa pale, wiki moja kabla, chama chake kilipoteza viti vingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

Wengi waliona kwamba matokeo hayo mabaya yalikuwa ni ishara kutoka kwa wananchi namna walivokuwa wakichukizwa na ufisadi ulioshamiri nchini, na kwa ujumla namna utawala wake ulivyokuwa unalishughulikia.

Hakuna wakati katika historia ya nchi hii ambapo kashfa moja ya ufisadi iliibua mjadala mkubwa katika jamii na kukaa vichwani mwa mamilioni ya wananchi katika muda mfupi.

Katika kipindi cha takriban miezi sita hadi kufikia mkutano na wazee, maneno ‘Tegeta’ na ‘IPTL’ yametajwa au kuchapishwa mara nyingi zaidi kuliko hata katika kipindi chote cha miaka 20 cha uwepo wa mtambo huo tata wa kufua umeme.

Aidha kuna baadhi walitaja kwamba kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi 10 tu Kikwete alitinga hadharani kutoa hotuba ambayo ilikinzana na matokeo rasmi kuhusu suala muhimu la kitaifa, matokeo yaliyoibuliwa na taasisi rasmi za utawala wake.

Mwezi Februari 2014 wakati akizindua Bunge la Katiba (Constituent Assembly) aliyashambulia matokeo muhimu ya Tume aliyoiunda kutafuta maoni ya wananchi kuhusu uandikaji wa katiba mpya – iliyoongozwa na jaji Joseph Warioba.

Na Novemba mwaka huo huo alifanya hivyo hivyo kuhusu matokeo muhimu ya Bunge – hasa kamati yake ya Fedha (Public Accounts Committee (PAC) na ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) ambayo ilichunguza wizi huo kutokana na maagizo ya PAC, aliposema, pamoja na mengine, kwamba fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow hazikuwa za umma.

Kamati ya Bunge iliyoongozwa na Wabunge Deo Filinkunjombe (sasa marehemu) na Zitto Kabwe ilihuzunika sana kwani kwa sababu ndiyo iliyotoa hadidu za rejea kwa CAG kufanya uchunguzi wa kina kuhusu kashfa. Hivyo PAC ndiyo ilikuwa chombo sahihi kutafsiri matokeo ya CAG na si mtu mwingine.

Isitoshe ‘harufu’ ya kashfa hiyo kwa mara ya kwanza ilinuswa na Mbunge mmoja, na si Muhimili wa Dola, pamoja na muhimili huo kumiliki vyombo kadha kwa kazi hii – kama vile TAKUKURU, Polisi na hata idara ya usalama wa taifa. Ni kama vile vyombo hivi vilikuwa havipo.

Lakini cha ajabu zaidi ni kwamba baada tu ya Bunge kuanza kuishughulikia kashfa hiyo, Muhimili wa Dola ukaanza kuingilia kati, na si kwa namna ya kuchimbua kila kitu, bali ni kwa kuvuruga ili ukweli halisi usipatikane. Kiingereza wanaita “throwing spanners into the works.”