Home kitaifa MPANGO WA KUINUA UBORA WA ELIMU UMESAIDIA JAMII

MPANGO WA KUINUA UBORA WA ELIMU UMESAIDIA JAMII

5852
0
SHARE
NA DERICK MILTON, BARIADI   |   

Katika Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, inabainishwa kuwa serikali na wadau mbalimbali wa elimu nchini wanao wajibu wa kushirikiana kuiletea maendeleo sekta ya elimu na kutatua changamoto zinazoikabili.

Madhumuni ya sera hiyo ni kuhakikisha elimu inayotolewa kwa watanzania inakuwa bora na yenye kiwango kinachokubalika kimataifa kwa kupata watanzania walioelimika watakaolifanya Taifa lipate maendeleo na kufikia  uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Licha ya sera hiyo kuonyesha majukumu ya kila mdau katika kuleta mafaniko hayo kwenye elimu, bado haijatoa ufafanuzi ulio wazi kwa jamii ni jinsi gani ina wajibu katika kufanikisha malengo hayo.

Changamoto kubwa ambayo imekuwa ikizikabili shule za msingi nchini ambazo ziko chini ya serikali, ni wananchi kushindwa kutambua kuwa shule hizo ni mali yao hivyo wanaowajibu wa kushiriki katika maendeleo yake.

Hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa migogoro kati ya walimu na wananchi, uongozi wa shule na wananchi ikiwa ni pamoja na uongozi wa serikali ngazi za vijiji, kati na wananchi.

Moja ya migogoro ni pale wananchi wanapogoma kushirikiana kuboresha miundombinu ya shule, ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, choo pamoja na utengenezaji wa madawati au meza.

Migogoro mingine ni kuwepo kwa  uvamizi wa ardhi iliyotengwa kwa ajili ya asasi za elimu na za Serikali ambazo zimekuwa zikihitaji kumiliki ardhi ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na maendeleo ya baadaye.

Lakini pia bado jamii imekuwa haitambui umuhimu wa kushirikia katika kuboresha taaluma kwa wanafunzi, hasa kuongeza ufaulu wa shule pamoja na kudhibiti utoro wa rejareja na ulio sugu.

Walimu kipigwa na jamii, kutozwa faini, kupewa adhabu na jamii kutokana na kuwaadhibu wanafunzi, ni baadhi ya matukio ambayo yanaonyesha kuwa bado jamii haitambui kuwa shule ni mali yao.

Halmashauri ya Bariadi Vijijini Mkoani Simiyu ni moja ya maeneo ambayo yamekuwa na mwamko duni wa wananchi wake kushiriki katika maendeleo ya shule zinazoanzishwa kwenye maeneo yao.

Hali ilivyokuwa vipi tangu mwaka 2015 

Matukio ya migogoro ya maeneo ya shule na wananchi, walimu kupigwa pamoja na wananchi kushindwa kutatua changamoto za miundombinu ya shule ni vitu ambavyo vimejitokeza katika Wilaya hii miaka ya nyuma.

Changamoto hizo zimekuwa zikisababisha walimu kufanya kazi katika mazingira magumu na kusababisha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kushuka kila mwaka kwenye mitihani ya kitaifa.

Henry Kitori ni Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Sapiwi ‘A’ iliyoko kijiji cha Mwandama anasema baadhi ya migogoro ilisababisha baadhi ya walimu kuhamishwa kutokana na kupigwa na wananchi.

Anasema kuwa moja ya mgogoro mkubwa uliokuwepo shuleni hapo ni wananchi kutumia eneo la shule kwa ajili ya kuchungia mifugo yao kwa madai kuwa hawana maeneo ya malisho.

“ Mwaka 2015 mmoja wa walimu katika shule yangu aliomba uhamisho baada ya kupigwa na wananchi, kutokana na kuzuia Ngo’mbe waliokuwa wanachungiwa katika eneo la shule.

“Tukio hilo lilisababisha shule kuingia kwenye matatizo makubwa na kufikiwa uamuzi wa wananchi waliohusika na kumpiga mwalimu huyo kupelekwa mahakamani”..

“ Hukumu ya kesi hiyo ilitoka mwaka 2017 na kati ya wananchi ambao walipelekwa mahakani mmoja ndiye alikutwa na hatia na kufungwa kifungo kwenda jela miaka mitatu na faini shilingi 150,000” anasema Kitori.

Waratibu elimu Kata

Nzumbi Elisha ni Afisa Elimu kata ya Sapiwi anasema kuwa katika kata yake yenye shule za msingi saba, mbali na changamoto ya wananchi kuvamia maeneo ya shule, anawatupia lawama viongozi wa kisiasa.

Anasema kuwa changamoto kubwa ambayo alikuwa anaipata ni viongozi wa kisiasa katika kata hiyo kuhamasisha wananchi wagome kuchangia maendeleo ya shule kwenye maeneo yao kwa madai kuwa wanalinda kura zao.

Elisha anaongeza kuwa mbali na hilo kamati za shule wengi wa viongozi na wajumbe wa kamati hizo walikuwa wanasiasa, ambapo vikao vyao vilikuwa kujadili mambo ya maendeleo kisiasa.

“ Kamati hizi zilikuwa hazina hata elimu ya kujua wapi mipaka yao kwenye shule wanayoongoza, walikuwa wakijiona wao ndiyo wenye mamlaka zaidi kwenye shule hivyo hakuna mtu mwingine kuwaingilia.

“ Mwalimu hakuwa hana uwezo wa kuweza kumwita mzazi au kumwadhibu mwanafunzi kwa sababu ya utoro, akifanya hivyo ugomvi unaanza kati ya walimu na kamati ya shule pamoja na wazazi” alisema Elisha.

Viongozi wa vijiji/kata

Viongozi wa vijiji na kata wanasema kuwa elimu ndiyo tatizo kubwa kwao, lakini viongozi wengi walikuwa hawajui shule kama ni mali yao hivyo wanatakiwa kushirikia katika kutatua changamoto.

James Kibuga ni Diwani kata ya Sapiwi (CCM) anasema kuwa kutokuwa na elimu kwa viongozi wa vitongoji, vijiji pamoja na kata ambao wamechaguliwa na wananchi ilisababisha maendeleo ya shule katika kata hiyo kudorora.

 “Tatizo kubwa hapa ni kulinda kura, hilo ndilo lilikuwa linatufanya sisi kufanya hivyo, lakini tulikuwa hatujui kuwa tunaendelea kuzorotesha hali ya elimu kwenye kijiji na kata yetu” anasema Kibuga.

Mwenyekiti wa kijiji Cha Mwandama, Sospiter Maduhu anasema kuwa mshikamo kati ya wazazi na walimu kipindi cha nyuma haukuwepo kwani kila mmoja alimuona mwenzie kama adui.

Anasema kuwa walikuwa wakianzisha migogoro bila ya kuangalia madhara kwao, kwa walimu pamoja na wanafunzi, wakidhani kuwa ndiyo wanafanya vizuri kumbe matatizo ndiyo yanazidi kuongezeka.

Hali ilivyokuwa mwaka 2016…

Pamoja na sera ya elimu ya mwaka 2014 kuwa na mapungufu ya kutoelezea wajibu wa mwananchi katika maendeleo ya shule, elimu ilionekana kuwa tatizo kubwa la kutambua wajibu huo.

Kutokana na hali hiyo Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wa elimu kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (Equip) wakaamua kutatua changamoto hiyo.

Fredrick Nyengela ni Kaimu Afisa Elimu Msingi wa halmashauri hiyo, anasema kuwa mpango huo ulianza kutekelezwa toka mwaka 2014, ambapo lengo lake ni kuboresha elimu nchini.

Nyengela anaeleza kuwa baada ya kugundua changamoto kubwa ya wananchi kutotambua kuwa shule ni mali yao, kupitia mpango huo iliandaliwa baadhi ya mikakati ya kutatua hali hiyo.

Anasema kuwa baadhi ya mikakati ni pamoja na kuletwa kwa muundo mpya wa kamati za shule, ambapo mabadiliko yaliyofanywa na serikali ni mwenyekiti wa kamati sharti anatakiwa kuwa na elimu ya kidato cha nne na kuendelea.

“ Kamati zilikuwa zinalaumiwa sana kwa viongozi wake na wajumbe kuanzisha migogoro kwenye shule, tukaona tatizo lipo kwa viongozi, ikiwa kiongozi atakuwa hana uwezo wa kusimamia pamoja na elimu lazima matatizo yatakuwepo” anasema.

Anasema mbali na hilo kupitia mpango huo kumeundwa chombo kinachoitwa Ushirikiano wa Wazazi na Walimu (U.W.W), chombo ambacho anaeleza kimeanzishwa katika kila shule kwenye halmashauri hiyo.

“ Chombo hiki kimepewa mafunzo ambalimbali ya kutambua kuwa shule ni mali ya jamii, na kinashirikiana na kamati ya shule pamoja na walimu, kupitia chombo hiki mafanikio makubwa zaidi ya asilimia 90 yamepatikana” anasema Nyengela.

Anasema U.W.W umekuwa mwarobaini wa kuondoa migogoro shuleni, kati ya walimu na wazazi, kuondoa utoro, wananchi kushirkia kwa asilimia 100 katika shughuli za maendeleo ya shule yao.

“ Kupitia chombo hiki mpaka sasa wananchi wamejenga vyumba vya madarasa 278 ambayo yamefikia usawa wa lenta ya mwisho, na mahitaji ni 2,2252, yaliyopo ni 601, na madarasa haya yamejengwa kwa muda wa miaka miwili” anasema Nyengela.

Naye Mratibu wa Mpango huo halmshauri Isaya Adamu anasema kuwa vyumba hivyo vya madarasa vimejengwa kwa nguvu za wananchi, kupitia ushawishi na elimu kubwa kutoka katika chombo hicho U.W.W.

Aidha, Mratibu huyo anasema kuwa kupitia chombo hicho wazazi wenyewe ndiyo wasimamizi wa shule, huku kila darasa likiwa na mlezi ambaye ni mwananchi kwa ajili ya kudhibi utoro na kuongeza nidhamu kwa wanafunzi.

Viongozi/wajumbe wa UWW

Baadhi ya viongozi na wajumbe wanasema kupitia mpango wa Equip wamepata elimu ya kutosha kutokana na mafunzo wanayopata kila mara na kufanikisha jamii kutambua kuwa shule ni mali yake.

Ng’wasi Masanja ni katibu wa U.W.W shule ya Msingi Mwasinasi kata ya Mwaumatondo, anasema kuwa wadhibiti wakuu wa utoro kwa wanafunzi ni wazazi pamoja na kuongeza nidhamu.

“Katika shule yangu kama kiongozi wa U.W.W, mzazi ninapambana kila mara kukomesha utoro, tumeweka adhabu kwa mzazi mwenye mtoto mtoro, faini Sh 200,000 na tumefanikiwa” anasema Masanja.

Anaongeza kuwa awali kulikuwepo na tabia ya baadhi ya wazazi hasa wanaume kuwataka watoto wao wa kike ambao ni wanafunzi kufanya vibaya katika mtihani wa darasa la saba ili kumwozesha.