Home Makala Mradi unaoondoa umbumbumbu kwa watoto wa kike

Mradi unaoondoa umbumbumbu kwa watoto wa kike

775
0
SHARE

NA ALLAN VICENT-TABORA

SERIKALI imelipa kipaumbele kikubwa suala la elimu ndio maana iliamua kutangaza sera ya elimu bure kwa watoto wote kuanzia shule za msingi hadi kidato cha nne.

Katika kuhakikisha sera hiyo inatelekezwa ipasavyo imekuwa ikitenga bajeti ili kuwezesha utekelezwaji wake kwa shule zote na kuagiza mikoa na halmashauri kusimamia ipasavyo fedha hizo.

Tunashuhudia serikali ikipeleka fedha nyingi katika halmashauri kwa ajili ya uboreshwaji wa miundombinu ya elimu kuanzia msingi, sekondari hadi vyuo, hili ni jambo kubwa linalopaswa kuungwa mkono.

Kama ilivyo ada, mashirika, taasisi na wadau mbalimbali wa maendeleo ya elimu hapa nchini wamekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za serikali kwa kutoa mchango wa vifaa, kuboresha miundombinu na kusaidia baadhi ya wanafunzi wanaotoka katika familia zisizo na uwezo.

Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya elimu (CAMFED) ni miongoni mwa wadau ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa kuwezesha kielimu wanafunzi wa kike walioko katika mazingira hatarishi. 

Shirika hilo limepongezwa na Serikali ya Mkoa wa Tabora kwa kufadhili watoto wa kike 1,119 wanaosoma shule za sekondari za serikali kwa kuwawezesha mahitaji yao yote ya kielimu ili waweze kufikia ndoto zao.

Ofisa Elimu Taaluma wa Mkoa huo, Aron Vedasto, anasema shirika hilo limeunga mkono kwa vitendo jitihada zinazofanywa na serikali hii.

“Kitendo cha shirika hili kuwafadhili wanafunzi wa halmashauri mbili za Tabora Manispaa na Nzega ni heshima kubwa kwa serikali ya mkoa huo na mchango wao ni wa thamani kwa watoto hao na Taifa kwa ujumla,” anasema Vedasto.

Anasema mradi wa CAMFED umekuwa mkombozi kwao kwani watoto wengi wa kike licha ya kufaulu darasa la saba na kuchaguliwa kwenda sekondari baadhi yao hushindwa kuendelea na masomo.

Anataja sababu kubwa inayochangia baadhi ya watoto kushindwa kufikia ndoto zao kuwa ni ukosefu wa elimu unaochangiwa na hali duni ya maisha ya wazazi au walezi na mwamko mdogo wa kielimu.

Anasema ufadhili wa shirika hilo umesaidia kuondoa unyanyapaa na kuwapa fursa ya elimu ambayo imewasaidia kujitambua, kujua wajibu wao wawapo shuleni na hata baada ya kumaliza masomo yao.

Vedasto anaeleza kuwa shirika hilo mbali na kutoa gharama zote za mahitaji ya watoto hao shuleni ambazo ni takribani Sh 250,000 kwa kila mmoja pia limechochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya elimu kwa wilaya hizo.

Kwa mwaka 2018/19 CAMFED wametoa Sh milioni 252 kwa halmashauri hizo ili kuboresha miundombinu ya kusomea na kuwezesha watoto hao kupata mahitaji yao yote.

Naye Ofisa Elimu wa Manispaa ya Tabora, Chatta Luleka, anasema mradi huo umewezesha kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi walio wengi wakiwemo watoto wa kike.

Mwanafunzi Nicodemu Fidelis wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Bulunde wilayani Nzega, anaipongeza CAMFED kwa kuwapa mbinu za kufaulu masomo yao na kuwasaidia kutimiza ndoto zao.

Naye Silvester Severin kutoka Shule ya Sekondari Ipuli anasema kuwa mradi huo umekuwa msaada mkubwa kwani wamefundisha umuhimu wa elimu katika maisha yao, hivyo watatumia vizuri fursa hiyo na kuwa washauri wazuri.

Anasema ufadhili wa shirika hilo utawainua kimaisha watoto wa kike na kuwafanya kuwa msaada mkubwa kwa wasichana wenzao, hivyo akaomba wapanue wigo wa ufadhili huo hadi vijijini na utolewe kwa watoto wote wa kiume na kike.

Mnufaika mwingine Mwanne Said kutoka Shule ya Sekondari Isevya anasema shirika hilo limempa mwanga mpya wa maisha kwani asingeweza kumudu mahitaji yote ya shule.

Mratibu wa Miradi ya CAMFED mkoani hapa, Shida Athuman, anasema shirika hilo limekuwa likiandaa makongamano kama hayo kwa lengo la kuwapa uelewa wanafunzi juu ya namna ya kuongeza ufaulu na maarifa ya kujitegemea.

Anasema wanamwezesha kila mtoto kujua haki zake na umuhimu wa elimu anayopata katika maisha yake.

Anatoa ushauri kwa wadau wengine wa elimu kuendelea kujitokeza kusaidia watoto hao ili wafike mbali.

Naye Mwalimu Mlezi wa wanafunzi walioko katika mradi huo kutoka Shule ya Sekondari Sikanda, Zabibu Gregory, anasema umewezesha watoto wanaotoka katika mazingira hatarishi kujengewa uwezo na kuendelea na shule.

Anafafanua kuwa kongamano la elimu kwa watoto hao ni fursa muhimu ya kuwajengea uwezo ili waweze kujiamini katika masomo yao na kuwapa mbinu za uzalishaji mali baada ya kumaliza shule.

Anasema vikundi vya kijamii vilivyoanzishwa na shirika hilo katika halmashauri hizo vipo kwa ajili ya kuhamasisha jamii kulea watoto wao katika njia nzuri ikiwemo kuwapeleka shule.

Shule zilizonufaika

Zabibu anataja shule za sekondari za Manispaa ya Tabora zinazonufaika na mradi huo kuwa ni Sikanda, Isevya, Kazehill, Kariakoo, Lwanzari, Cheyo, Ipuli, Fundikira, Bombamzinga, Kanyenye na Nyamwezi.

Zilizoko katika Wilaya ya Nzega ni Nzega day, Bulunde, Miguwa, Bubwandege, Ndono, Itilo, Ijanija na Chifu Ntinginya. 

Muelimishaji wa masuala ya jamii ambaye ni Ofisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Manispaa Tabora, Irene Mpangala, anasema mtoto akielimishwa atajitambua na kujilinda. 

Anasema shirika hilo limekuwa chachu kubwa ya watoto wa kike kufanya vizuri katika masomo yao, hivyo akaomba waangalie uwezekano wa kusaidia hata watoto wa kiume wanaotoka katika familia duni.