Home Makala MRADI WA UMEME STIEGLER’S GORGE: SERIKALI IOKOE BONDE LA KILOMBERO

MRADI WA UMEME STIEGLER’S GORGE: SERIKALI IOKOE BONDE LA KILOMBERO

1132
0
SHARE
Sehemu ya Bonde la Kilombero lilivyoharibiwa na mifugo likionekana kutoa angani

Na Chrysostom Rweyemamu


OKTOBA 2006, takriban mwaka mmoja tu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani, lilitokea tukio ambalo si la kawaida kwa watumiaji wa mitandao ya kompyuta katika Tanzania.

Tukio hilo ni lile la kikundi cha Watanzania kuanzisha tovuti na kuitumia kukusanya saini za wananchi za kuishinikiza Serikali kuutekeleza mradi wa kuzalisha umeme wa maji kwenye maporomoko ya Stiegler’s  Gorge; kwa imani kwamba ndio suluhisho la kudumu la tatizo la upungufu wa umeme nchini.

Kampeni hiyo, ambayo ilianzishwa katika kipindi ambacho nchi ilikuwa katika mgawo mkubwa wa umeme iliishia hewani. Lakini lengo la wazo hilo lilikuwa ni kukusanya saini milioni moja na kuziwasilisha kwa Rais Kikwete.

Iwapo saini hizo milioni moja hatimaye ziliwasilishwa kwa  Kikwete, au la, ni jambo ambalo halina uhakika; lakini jambo ambalo linajulikana kwa watu wengi; ni kwamba mgawo mkubwa wa umeme uliokuwapo wakati huo, miaka sita tangu mkakati ubuniwe, ulikuwa unaendelea.

Kwa ufupi; Watanzania walio wengi, wakiwamo baadhi ya watendaji na wataalamu serikalini, bado walikuwa wanaamini kwamba, Stiegler’s  Gorge ndio ulikuwa ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la umeme nchini, na kwamba umeme wa dharura wa majenereta si tu kwamba ulikuwa ghali, lakini pia ulikuwa hauaminiki.

Matumaini ya Watanzania ya kupata umeme wa bei nafuu wa  Stiegler’s  Gorge yalipata msukumo mpya wakati wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, na maofisa kadhaa wa Tanzania, walipokwenda Sao Paolo, Brazil na kufanya mazungumzo na wenzao kuhusu uwezekano wa nchi hiyo kuisaidia Tanzania katika mradi huo.

Waliporejea nchini, umma ukatangaziwa kwamba, mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge ungeanza muda si mrefu, na kwamba ungetekelezwa na wataalamu kutoka Brazil. Umma uliambiwa pia kwamba, itakapofika mwaka 2015, Watanzania wangeanza kuufaidi umeme wa bei rahisi kutoka Stiegler’s Gorge!

Lakini mpaka wakati ninaandika makala haya, Serikali ilikuwa bado haijatoa tamko kwamba mradi wa umeme wa maji wa Stiegler’s Gorge utatekelezwa mwaka gani, tukiacha tamko la 2015.

Lakini Stiegler’s Gorge ni nini hasa, na kwa nini Watanzania wengi walikuwa na imani kwamba ni mradi ambao ungewakoboa kwa kuwapatia umeme wa bei nafuu?

Stiegler’s Gorge ni mpalio mwembamba unaopatikana kwenye Bonde la Mto Rufiji, kilomita zaidi ya 200 kutoka Dar es Salaam.

Utafiti uliofanywa miaka ya 70 na mwanzoni mwa miaka ya 80  (1978-1980)  na Rufiji Basin Development Authority  (RUBADA), kwa kushirikiana na kampuni ya kigeni ya M/s Norplan/Hafslund, ulionyesha kwamba, mradi huo una uwezo mkubwa wa kuzalisha umeme mwingi kuliko mahitaji ya nchi.

Matokeo ya utafiti huo pia yalionesha kwamba, mpalio wa Stiegler’s Gorge una uwezo wa kuhimili mitambo mitatu mikubwa ya kuzalisha umeme, mtambo wa kwanza ambao utafungwa upande wa Kaskazini ya bwawa, utafua megawati 400.

Mtambo wa pili ambao utafungwa upande wa chini ya bwawa, utakuwa na uwezo wa kufua megawati 800, na mtambo wa tatu  wenye uwezo wa kufua megawati 900, utafungwa upande wa Kusini.

Kwa ufupi, mradi wa Stiegler’s Gorge utazalisha jumla ya megawati 2,100 za umeme—kiasi ambacho ni karibu ya mara mbili ya kinachohitajiwa hapa nchini kwa sasa, na hiyo inaeleza kwa nini matumaini makubwa ya Watanzania yalikuwa yamewekwa katika utekelezaji wa mradi huo.

Lakini je; utafiti huo bado unasimama katika hali ya sasa, ambapo mazingira yametibuliwa mno na vyanzo vya maji vimeharibiwa kupita kiasi katika mabonde ya Mto Rufiji na Mto Kilombero?

Pengine kitu ambacho Watanzania wengi hawakifahamu ni kwamba, mradi wa umeme wa maji wa Stiegler’s  Gorge unategemea ustawi wa Mto Rufiji;  ambao nao pia unategemea (kwa asilimia 60)  ustawi wa Mto Kilombero; hususan Bonde la Mto Kilombero.

Ikumbukwe hapa kwamba, Mto Rufiji hupata maji yake mengi kutoka mito miwili mikuu—Kilombero na Ruaha Mkuu—na hasa Mto Kilombero, ambao huchangia theluthi mbili ya maji ya Mto Rufiji kabla hayajafika Stiegler’s Gorge.

Ni dhahiri, hivyo basi, kwamba uwezekano wa Watanzania kupata umeme wa maji wa bei nafuu kutoka Stiegler’s Gorge, ni ndoto inayokaribia kuwa ya kweli endapo Serikali itachukua hatua za kuhifadhi (conservation measures) Bonde la Mto Kilombero. Na hivyo ndivyo ilivyo; maana ustawi wa bonde hilo hivi sasa unasambaratishwa kwa kasi na wafugaji Wasukuma ambao wamevamia bonde hilo wakiwa na mamia ya mifugo.

Mara tatu ujumbe wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) ulilitembelea bonde hilo na kukuta picha ya kutisha ya uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji unaofanywa na wafugaji hao.

Wataalamu waliohojiwa na JET, wanakubaliana kuhusu jambo moja kubwa—kwamba ardhioevu (wetland) katika Bonde la Kilombero ipo katika hatari ya kupotea kutokana na uvamizi wa wafugaji wengi walioingia katika Bonde hilo baada ya kufukuzwa na Serikali kutoka ardhioevu ya Ihefu wilayani Mbarari, Mkoa wa Mbeya.

Wataalamu wanakubaliana kwamba, ukataji miti ovyo, na uvamizi wa mifugo katika vyanzo vya maji, ukiongeza na tatizo la sasa linaloikumba dunia nzima—mabadiliko  ya tabianchi (climate change), vinaashiria kuwa muda si mrefu Bonde la Kilombero linaweza kupoteza sifa yake ya kuwa bonde adhimu la maji baridi ambalo ni kubwa kuliko yote duniani, lililokuwa linajaa maji misimu yote.

Labda kitu pekee ambacho wataalamu hao wanatofautiana, ni muda uliobakia kabla Bonde hilo halijasambaratika kabisa, endapo Serikali ya awamu ya tano, kwavile imeamua kwamba mradi wa  Stiegler’s Gorge lazima utekelezwe, italazimika kufanya oparesheni maalumu ya kitaifa ya kuwaondoa wafugaji katika mabonde yote inakoanzia mito inayomwaga maji yake katika Bonde la Kilombero.

Baadhi ya wataalamu wanalipa Bonde la Kilombero uhai wa miaka 10 tu, wengine miaka mitano tu; lakini wengine wengi wanasema kwamba baada ya miaka mitatu ijayo, itakuwa ni “bye bye” Bonde la Mto Kilombero.

Katika ziara ya miaka minne iliyopita kwenye Bonde hilo, JET ilitembelea Bwawa la Ngapemba katika Kata ya Utengule na kujionea jinsi bwawa hilo kubwa la enzi na enzi, lilivyoathiriwa na wafugaji.

Ujumbe huo ulipolitembelea tena hivi karibuni, picha ilikuwa ni ya kutisha zaidi; kwani bwawa hilo limezidi kusinyaa; huku mifugo ikiendelea kutamba pembezoni.

Kwa maneno mengine, bwawa hilo lililokuwa na ukubwa wa eka za mraba 1,000 na lililokuwa na hekaheka nyingi za uvuvi, sasa limenyauka na kusinyaa na kubakia eka chache sana za mraba.

Wakati wavuvi wachache waliobakia bado katika eneo hilo, walikuwa wanatumia mitumbwi kuvua samaki, sasa hawahitaji tena mitumbwi kutokana na kina cha bwawa kuzidi kupungua.

“Bwawa limepungua maji kiasi kwamba sasa unaweza kukatisha upande mmoja hadi wa pili kwa miguu,” anasema Oscar Njoweka, ambaye amekuwa akivua samaki katika bwawa hilo kwa miaka tisa.

Mvuvi huyo, sawa na wakazi wengine wa Kata ya Utengule waliohojiwa, anarusha lawama zake kwa wafugaji na Serikali za kijiji na Wilaya kwa ‘kuwaendekeza’ wafugaji hao.

“Hapa bwana kuna mchezo mchafu unachezwa. Viongozi wa vijiji huchukua ‘kitu kidogo’ kutoka kwa wafugaji hawa wa Kisukuma, ili wafumbe macho wakati wanaingiza mifugo yao kwenye vyanzo vya maji,” alilalamika mvuvi huyo.

Zamani bwawa hilo lilikuwa likichukuliwa kuwa ni takatifu (sacred) kwa imani za makabila ya asili ya maeneo hayo. Ndani ya bwawa hilo kulikuwa na msitu mdogo ambako wanavijiji walikwenda kwa ajili ya kufanya matambiko yao.

Kwa sababu hiyo, ilijengwa imani kwamba mtu yeyote ambaye angetenda chochote dhidi ya ustawi wa bwawa hilo kama vile kuvua samaki wachanga na kuwatupa au kuziba mikondo ya maji yanayoingia katika bwawa hilo, angepotezwa kabisa duniani bila mwili wake kuonekana! Kuna hata simulizi za watu inaoaminika walipotea kwa kufanya vitendo kinyume cha ustawi wa bwawa hilo!

Imani hizo za kale, kwa kiasi kikubwa, zilichangia kulitunza bwawa hilo miaka hadi miaka. Lakini hali ilianza kubadilika kwa kasi mwaka 2006, wakati Wasukuma waliofukuzwa pamoja na mifugo yao kutoka Ihefu, wakavamia maeneo jirani na bwawa hilo.

Kwa wafugaji hao wageni, ‘vitisho’ vya imani za kale havikuwazuia kuyavamia maeneo ya pembeni ya Bwawa la Ngapemba, yaliyokuwa na nyasi mbichi kulisha ng’ombe wao. Na huo ndio ukawa mwanzo wa kusinyaa na kukauka kwa bwawav hilo.

Huhitaji kuwa mtaalamu wa mazingira kutabiri kwamba bwawa hilo ambalo maelfu ya wanavijiji wa Bonde la Kilombero walikuwa wakinufaika nalo, sasa lipo “ICU”, na muda si mrefu vyanzo vyake vya maji vitatoweka kabisa katika uso wa dunia.

Katika bwawa jingine maarufu la Kibasila, picha iliyoonekana huko ni mbaya kuliko ya Bwawa la Ngapemba. Kibasila na Ngapemba ni mabwawa mawili makubwa yaliyosalia katika Bonde la Kilombero.

Idadi ya mifugo iliyokutwa pembezoni mwa bwawa la Kibasila ambalo nalo limesinyaa na kubaki ‘kiduchu’ ni kubwa, na hakuna maji. Lakini jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, wafugaji hao pia wameteketeza mikoko mingi ya maji baridi (fresh water mangrooves) katika bwawa hilo, ambayo ni mazalio ya samaki wanaopatikana Mto Kilombero. Wafugaji wameikata miti kwa wingi na kujengea maboma yao, na hivyo kuliacha eneo kubwa sasa kuwa na uwazi mkubwa.

Ziara ya JET katika Bonde la Mto Kilombero imethibitisha pia kwamba idadi ya mito na vyanzo vya maji inazidi kutoweka katika Bonde hilo. Hata mito iliyokuwa inajaa maji, sasa yamepungua au kwisha kabisa, na inashiria kwamba Serikali isipochukua hatua, mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge, unaotarajia kutumia fedha nyingi sana, utakuwa wa shoo tu (white elephant).

Utafiti mdogo wa hali ya mito kati ya Kihansi na Ifakara, unaonyesha zamani kuwa kulikuwapo na mito 29, lakini sasa imebaki mito mitano tu, huku mito tisa ikiwa na maji yaliyotuama. Miongoni mwa mito hiyo mitano ambayo inatiririsha maji, ni Luipa, Mpanga na Mnyera nab ado ina maji ya kutosha mwaka mzima.

Kwa hiyo, hali ya mito katika Bonde la Kilombero ni mbaya, na chanzo kikubwa cha hali hiyo ni uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji unaofanywa na wafugaji.

Lakini jambo la kusikitisha, hakuna hatua yoyote kubwa na ya maana iliyochukuliwa na Serikali – iwe ngazi ya taifa, mkoa au wilaya, kuchukua hatua na kuwadhibiti wafugaji.

Kuna wakati Wilaya ilianzisha oparesheni kabambe ya kuwaondoa wafugaji katika Bonde la Kilombero, lakini katikati ya utekelezaji, Serikali ilitoa tamko la kuisitisha.

Baada ya tamko hilo, wafugaji waliokwisha ondolewa, walirejea kwa kasi na kufuatiwa na wengine wengi. Walilitafsiri tamko hilo la Serikali kama ruksa rasmi ya kuingiza mifugo yao katika Bonde hilo.

Hivi sasa yeyote anayetoa kauli ya kuondoa mifugo katika Bonde hilo, anapewa rejeo la tamko la Serikali.

Bonde la Kilombero linaweza tu kuokolewa ni Serikali kufuta tamko lake la kusitisha operesheni ya kuwaondoa wafugaji ndani ya Bonde la Kilombero, ili uongozi katika ngazi ya Wilaya uanze upya operesheni hiyo ya kuwahamisha wafugaji kwa wamu.

Pili ni kwa Serikali kuanzisha operesheni maalumu ya kitaifa ya kuwaondoa wafugaji katika Bonde hilo kama ile iliyoifanya kwa mafanikio makubwa kule Ihefu mwaka 2006. Vinginevyo, Serikali iachane kabisa na mradi wa kufua umeme Stiegler’s Gorge.

  • Haya ni makala ya mwisho aliyoandika Chrisostom Rwemamu (RIP), ambaye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo, New Habari.